Bunge legelege linachochea migogoro na migomo nchini; linasababisha nchi itisawalike! | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Bunge legelege linachochea migogoro na migomo nchini; linasababisha nchi itisawalike!

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Mzee Mwanakijiji, Jul 4, 2012.

 1. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #1
  Jul 4, 2012
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,362
  Likes Received: 6,393
  Trophy Points: 280
  [​IMG]
  Na. M. M. Mwanakijiji


  Migomo na migogoro mingi ambayo tumeiona ikitokea nchini kwa miaka kadhaa sasa hivi inachochewa na naweza kusema inasababishwa na Bunge letu. Wakati watu wengi walitilia mkazo kauli ya Mbunge wa Ubungo John Mnyika kuwa tumefikishwa hapa kwa sababu ya “udhaifu wa Rais Kikwete” mimi binafsi naamini uzito ulitakiwa kuwa kwenye “ulegelege wa Bunge”. Na bila yashaka hoja inaweza kujengwa kuwa “upuuzi wa CCM” nao umechangia sana kufika hapa. Hilo la upuuzi nitaliachia siku nyingine.


  Bunge letu ndicho chombo cha juu kabisa ambacho wananchi wa Tanzania wanacho kuweza kusimamia watawala wao. Wananchi wanapoenda kupiga kura kuchagua mbunge hawaendi kumchagua “mpiga porojo” wa jimbo au “bishoo” wa Bunge. Hawaendi kuchagua mtu ambaye ataweza kuwachachafya wengine Bungeni au atakayeenda kulumbana kwa mipasho Bungeni na wabunge wa kambi nyingine. Wanapochagua wabunge wananchi wanachagua “wawakilishi” wao. Dhana hii ya wawakilishi nadhani inapotea sana hasa pale watu wanapoitwa “wabunge”.  Mtu anapoitwa “Mbunge” anakuwa na hisia kuwa kazi yake kubwa ni “Bungeni” wakati “Mwakilishi” anajitambua kuwa yupo pale mjengoni kwa sababu anawakilisha watu au kundi fulani. Mbunge anayejitambua kuwa ni “mwakilishi” anaposimama Bungeni anasimama akijua kabisa kuwa ni maslahi ya wale waliomtuma ndio anahitaji kuyatetea. Kusimamishwa kwake na chama cha siasa hakumfanyi Mbunge huyo kujifikiria ni “mwakilishi” wa chama kile cha siasa. Ni mwakilishi wa jimbo la uchaguzi.


  Tukielewa hili upande mmoja tunaweza kuelewa kwanini sisi wengine hatuamini kabisa mantiki ya kuwa na viti maalum au wabunge ambao wanaingia Bungeni ati kwa vile “wameshinda bila kushindanishwa”! Wabunge wa viti maalum hawana mtu wanayemuwakilisha ambaye hawakilishwi tyayari na mbunge wa jimbo aliyechaguliwa. Siyo wanawake, vijana, au walemavu ambao wanahitaji MBunge wa kuwawakilisha zaidi ya wale wa Bunge. Lakini cha kuudhi zaidi ni watu ambao kwa kutumia mbinu mbalimbali au udhaifu wa washindani wao waliweza kujipatia ubunge “wa jimbo” bila kupigiwa kura hata moja na wengine wakaenda kushika nafasi za juu za nchi (Makinda na Pinda ni mifano ya viongozi wasio halali ambao wanawakilisha majimbo ambayo hawakuchaguliwa kwa mujibu wa katiba!)


  Haya yote hata hivyo yanadokeza kitu ambacho naamini tatizo kubwa zaidi ukiondoa udhaifu huo wa muundo – wabunge wameshindwa kusimamia serikali, kuliongoza taifa na sasa wananchi wetu wanalipa gharama ya ulegelege wao, uzembe na kwa kwa kila kipimo kuweka mbali vyama vyao kuliko majimbo wanayowakilisha. Migogoro yote ambayo tunaiona leo hii – mgomo wa madaktari, tishio la mgomo wa wafanyakazi na ule wawalimu n.k ni matokeo ya kushindwa huku kwa bunge! Siyo tatizo la Kikwete peke yake!


  Kikwete ameshindwa

  Kwamba Rais Kikwete ameshindwa kuonesha uongozi wa kutatua matatizo haya zaidi ya kuwa na vikao visivyoisha na matumizi ya mikwara halina shaka. Kushindwa kwake huku wengine tulishakutarajia na kwa kweli kama wengine tulivyojenga hoja kabla ya uchaguzi uliopita ni bora wananchi tukubali tu yaishe. Lakini kama yeye kashindwa ina maana lazima na wengine nao washindwe? Rais Kikwete ni wazi anasubiri matukio ilia je nyuma yake badala yay eye kuyatangulia matukio na kuonesha uongozi. Nimewahi kusema zamani kwenye maandishi yangu kuwa “usipoongoza utajikuta unafuata” ni wazi kuwa sasa hivi serikali yetu hasa upande wa utendaji (executive) iko inafuata. Matukio yanatokea na wao wanakuja nyuma na kuzungumza kwa jazba zote!


  Bunge limeshindwa zaidi

  Hata hivyo kumlaumu Kikwete kuwa kashindwa kutatua mgogoro wa madaktari na masuala mengine kwa kiasi ni kumuonea. Kikwete kama Rais wa Kikatiba anafungwa na sheria ambazo Bunge linapitisha na anaweza kufanya yale tu ambayo Katiba na sheria inamruhusu kufanya. Hawezi kufanya zaidi ya vile kwani akifanya hivyo atashtakiwa na kuondolewa madarakani na Bunge kwa mashtaka ya kibunge (impeachment). Rais wetu – kama nilivyokataa aliposema ana uwezo wa kuamuru Dr. Slaa akamatwe na akakamatwa – hana nguvu zozote nje ya zile ambazo Katiba na sheria zetu zinampa. Hawezi kulazimisha kuingia ndani ya nyumba ya mtu, hawezi kuamuru mtu apigwe risasi au hata kuamuru boyfriend wa binti yake akamatwe na akakamatwa! Nguvu hizo hana! Ninachosema hapa ni kuwa anaweza kufanya kile tu ambacho wabunge wanamtaka afanye na wamemtengenezea sheria kufanyia.


  Zipo sheria ambazo zimeundwa zenye kusimamia sekta mbalimbali ikiwemo ile ya afya na elimu. Sheria hizi ndizo ambazo zimezaa mfumo huu wa afya ambao unatusumbua sana. Ni bunge liliopitisha sheria hizo na kutaka serikali izisimamie. Kitu kinachonishangaza mimi kama mdadisi wa masuala ya utawala na demokrasia ni kuwa ni lini Bunge litaamua kuangalia sheria zake na kuona jinsi gani zinachangia migogoro kwenye elimu na afya? NI nani mwenye akili timamu Bungeni – kama wote siyo legelege – ambaye anaweza kuwasema “sheria hii na hii ni mbaya tuzibadilishe”? Ni wazi kuwa wabunge wa aina hiyo hawapo ndani ya CCM kwani na wao ukiwasikliiza utaona wanaililia “serikali” ifanye jambo moja, hili na jingine.


  Wabunge hasa wa CCM (hata wa upinzani wako hivyo hivyo” hawachoki kusema “Miye naomba serikali…” au utawasikia “Serikali iamue kuanzia sasa…” au “Umefika wakati kwa serikali…” kufanya mambo elfu moja na moja. Wanachosahau ni kuwa ni wao bunge ndio wanaweza kusababisha kitu kifanyike ambacho hakifanyiki.


  Kwa mfano, kama wabunge wanataka muundo wa jeshi la polisi libadilishwe hawawezi kuitaka serikali wao kama watunga sheria wanatumia raslimali zao na kuandika muswada wa sheria wa kufanya mabadiliko wanayoyataka. Jambo baya sana katika Bunge letu ni kuwa ukiondoa michango, hoja, na hotuba mbalimbali wabunge wetu hawaleti miswada binafsi ya sheria. Kuna mifano michache sana ya baadhi ya wabunge kujaribu kuleta miswada ya sheria Bungeni. Mara nyingi wabunge hawachoki kuiomba serikali “ilete mswada Bungeni” kana kwamba wao kule Bungeni ni vilaza wa kutupwa.


  Hii ina maana kuwa kama wabunge wanaona kuna tatizo katika sekta ya afya – hususan mfumo wa utendwaji kazi wa madaktari na malipo yao basi wabunge wanaweza kuingilia kati na kuleta mswada wa mabadiliko ya sheria ili kuipa serikali nyenzo fulani ya kuweza kufanikisha hilo. Bahati mbaya sana tangu Machi hadi leo hii na kama ilivyokuwa tangu mgomo wa madaktari wa 2006 hadi leo hii wabunge wetu legelege hawajajaribu kuleta mabadiliko ya sheria ili kuongoza sekta na ajira za madaktari na badala yake wote wamekaa kama wachovu wakisubiri “Rais” na “Ikulu” iandae mikutano ya kunywa juisi ili mambo yamalizwe kiutuuzima. Safari hii madaktari wamegoma na kwa haki wanaendelea kugoma – na baadhii yetu tunawaunga mkono kwani wamefunua udhaifu mkubwa wa sekta hii. Sasa wabunge wanataka kujadili hotuba ya RAis, Waziri Mkuu au hali ya mgomo! Hawataki kuitana na kuandaa mswada wa dharura wa sheria ili kuokoa sekta hii na kuokoa maisha. Watu wamebakia kuwalaumu madaktari wakati ni wabunge ambao wametunga sheria ambazo serikali imezitumia dhidi ya madaktari! Hakuna mbunge wa CCM au wa upinzani ambaye amethubutu kuja na mswada wa sheria ya Afya ili kuleta mfumo mpya.

  Wabunge ndio wanagawa fedha
  Sasa inashangaza sana kuwa watu wamekaa na kumuangalia Rais kuhusu ongezeko la mishahara ya madaktari na maslahi ya watumishi wengine wa afya, elimu na kada nyingine. Wabunge wamekaa na kusubiri waziri alete bajeti yake ili waichambue. Bajeti nzima imeachwa iandaliwe na watu wa serikali kiasi kwamba wabunge wao wanakuwa “wachangiaji” bungeni. Hii inashangaza! Wabunge ndugu zangu ndio wanaamua fedha kiasi gani ziende wapi na kwanini! Serikali inakuja na mapendekezo na maombi. Labda nilieleze vizuri zaidi.


  Serikali ni mtumishi wa wananchi. Kinadharia haiwezi na haipaswi kutumia fedha yoyote ya umma bila kupewa au kugawiwa. Fikiria unataka kujenga nyumba na ukatafuta wajenzi. Wakaja wajenzi mbalimbali wakitafuta kazi na kati yao ukawachagua wale ambao unaamini wana uwezo wa kufanya kazi husika. Mkakubaliana ramani ya nyumba (itakuwaje), bajeti ya vitu mbalimbali, na gharama za ufundi. Katika kukamilisha kazi hiyo wewe kama mmiliki ulijua kabisa bajeti yako ni kiasi gani na mafundi walielewa bajeti hiyo.


  Sasa inakuja siku mafundi wanakuja na kusema wanahitaji fedha zaidi ya kununulia mchanga; unawauliza zile ulizowapangia kununulia mchanga wamezitumiaje wanakuambia ati wamenunua baskeli na viti vya kupumzikia! Na wewe kwa vile ni “tajiri sana” unawapa fedha nyingine za mchanga. Baadaye wanarudi tena na kusema wanahitaji fedha za kenchi! Unauliza vipi zile za kenchi ulizowapatia wanasema walijikuta wanapatwa sana na kiu wakaamua kununua mabox ya maji safi ya chupa! Utaendelea mpaka lini?


  Mwisho wa siku utatakiwa kuamua ama kuendelea na wajenzi wale wale ama kuanza kuwakatalia; itakupasa uamue kama unataka kuendelea kuwatengea fedha za Big G na Ice Cream au kuhakikisha wanatumia fedha kwa kujenga mabomba na kuinua nyumba. Wewe mwenye nyumba ndio mwenye uamuzi wa mwisho kuhusu nini kifanyike na kwa gharama gani.
  Sasa Bunge letu ndio wawakilishi wa sisi wananchi. Ndio maana Bunge linajadili bajeti, linapanga matumizi na hata kubadilisha vitu ambavyo serikali haijaviweka sawa. Bunge linafanya hivyo kwa sababu wao ndio wawakilishi wa sisi wananchi wote. Ni Bunge linalotakiwa kuamua nini kinafanyika nchini, kinafanywa na nani, na kwa gharama gani. Na ni hili hili Bunge linaloamua fedha hizo zinatoka wapi na kwa vipi! Siyo Rais Kikwete. Kwa mtindo wetu wa Kibunge, wabunge wanaweza kulazimisha serikali ibadili mipango yake au hata kutenga fedha (appropriate) zitumike vipi. Kama umefuatilia Bunge utaona kuna wakati Bunge “linakaa kama kamati” ambapo linapitia bajeti au mswada mstari kwa mstari (line items). Ni wakati huu bunge linafanya kazi yake hasa ya kutunga sheria na kupitisha bajeti.


  Hii ina maana ya kwamba, kama kweli tunaona kuna tatizo kwenye sekta ya afya na tumegundua kuwa Ikulu (chini ya Kikwete) hawana uwezo wa kutatua basi tumaini la mwisho ni Bunge. Bunge letu bahati mbaya ni legelege – siyo maneno yangu bali ya Mbunge mmojawapo na hayakutakiwa kufutwa! Ulegelege huu wa bunge ndio kweli umetufikisha hapa. Wabunge wa CCM wako makini kuona serikali na Rais wao hashambuliwi sana Bungeni. Tusiwategemee waamue kuingilia kati mgogoro tunaouoona sasa au ule mwingine (wa walimu). Wao wamelelewa katika fikra za chama kimoja ambapo wanaileza “serikali” na hawaishurutishi serikali yao. Hakuna mbunge wa CCM anayeweza kuleta mswada binafsi wa kuboresha sekta ya afya. HAKUNA!!! Wote wamekaa na kusubiria “Serikali” ilete mapendekezo au ilete mswada! Utasikia wanamuomba Mwanasheria Mkuu afanye hivyo. Kwanini kwa sababu wao wabunge ni legelege!


  Wabunge wa upinzani nao wameingia kwenye mtego huu huu. Wanajitahidi kuikosoa serikali sana ili itawale vizuri. Matokeo yake na wao hawafikirii kuleta mswada binafsi wa kubadilisha na kuboresha sekta ya afya na kama ni mswada mzuri kutafuta ushirikiano na wale wa CCM. Ni wazi ni rahisi zaidi kwa mbunge wa CCM kufanya hivyo kuliko wa upinzani kwa sababu hata kama mswada wa upinzani ni mzuri kiasi gani CCM hawatoukumbatia kwa kuogopa kuwapa ujio wapinzani! Matokeo yake wapinzani hata kujaribu hawajaribu.


  Lakini kutokujaribu kwao kunawaweka wao pabaya; kwani hadi hivi sasa hatujui ni sheria za namna gani upinzani wanaweza kuja nazo baadaye. Kwa mfano, je wanaweza kuandika sheria nzuri ya kusimamia sekta ya afya kuliko CCM? Je wanaweza kuandika sheria nzuri ya fedha kuliko ya serikali ya CCM? Ni bora wangekuwa wanajaribu na tuone miswada yao tuweze kupima kama itakuwa na unafuu kuliko kusubiri waingie madarakani ndio waanze kuhangaika na kuandika sheria. Lakini kwa mfano, wakiweza kuandika sheria mbalimbali (nzima au mabadiliko ya sheria za sasa) na zote zikakataliwa na CCM lakini zikapendwa na wananchi je siyo mtaji tosha kwao unapokuja uchaguzi mkuu kwani wananchi tayari wanajua ni sheria gani za kisekta ambazo zikutawepo chini ya chama cha upinzani!


  Sasa tuna matumaini? Swali hili sijui jibu lake. Lakini kama nilivyowahi kusema mwanzoni kila uchaguzi una matokeo (every election has its outcome) na uchaguzi wa wale waliowarudisha hawa madarakani una matokeo na matokeo yake mengine ni haya. Safari ijayo ukipewa michongoma na mahindi chagua sahihi; haiwezekani kwa miaka 50 bado unachagua michongoma na ikikuchoma unalalamika. Bunge la michongoma huchoma!


  Niandikie: mwanakijiji@jamiiforums.com
   
 2. Mohamedi Mtoi

  Mohamedi Mtoi R I P

  #2
  Jul 4, 2012
  Joined: Dec 11, 2010
  Messages: 3,326
  Likes Received: 44
  Trophy Points: 0
  Umenena kweli mwanakijiji, bunge limekuwa sehemu ya tatizo kwani limeonyesha dhahiri kuwa halina ubavu wa kuisimamia serikali kwa dhati ya kusimamia.

  Udhaifu wa bunge ni tumaini linalo kufa kwa upande wa wananchi.
   
 3. Nyani Ngabu

  Nyani Ngabu Platinum Member

  #3
  Jul 4, 2012
  Joined: May 15, 2006
  Messages: 73,655
  Likes Received: 35,416
  Trophy Points: 280
  Matawi yote matatu ya serikali ni legelege. Hakuna hata tawi moja linalotia matumaini.

  Hayo matawi mengine mawili (mahakama na bunge) ni kama vile yanamuogopa raisi.

  Wengine tulisema tokea 2005, Kikwete ni bomu lakini watu hawakutusikiliza.
   
 4. Edson

  Edson JF-Expert Member

  #4
  Jul 4, 2012
  Joined: Mar 7, 2009
  Messages: 9,202
  Likes Received: 722
  Trophy Points: 280
  kikwete kwa sasa anaongozwa na kufata
  bunge ndiobasi kabisa..hasa spika wa bunge kashindwa kuliongoza hoja za msingi zinazimwa na kusema ziko mahakaman
  wabunge wenyewe wamegawanyika sana...wapo wanaotetea maslahi ya nchi (hawa ni wachache) , wapo wengine wanaotete matumbo yao (hawa ni wengi kiasi) , wapo wanaotetea upuuzi wa chama tawala (hawa ni wengi sana)...sasa kwa kuwa walio wengi bungeni hawajui wanafanya nini ndio maana kila kitu unakiona shagala bagala.....

  ila kwa kifupi mpaka sasa kiti cha rais kimewekewa koti jeusi....
   
 5. mtotowamjini

  mtotowamjini JF-Expert Member

  #5
  Jul 4, 2012
  Joined: Apr 23, 2012
  Messages: 4,540
  Likes Received: 10
  Trophy Points: 0
  good analysis i hope wabunge wanaopiga chabo humu JF watachukua ushauri wako na kuufanyia kazi
   
 6. Adharusi

  Adharusi JF-Expert Member

  #6
  Jul 4, 2012
  Joined: Jan 22, 2012
  Messages: 10,635
  Likes Received: 3,017
  Trophy Points: 280
  Kazi hipo hapo,
  Vox populi,Vox dei
   
 7. F

  FJM JF-Expert Member

  #7
  Jul 4, 2012
  Joined: Apr 11, 2011
  Messages: 8,088
  Likes Received: 90
  Trophy Points: 145
  Bunge ndio chanzo cha umasikini wa hii nchi. Ni wapi uliona mwakilishi wa wananchi anasimama bungeni na kuanza kutafuta sifuri zimeandikwa wape, au spell checking? Hivi wapiga kura walimtuma kuangalia kuangalia tarakimu zinaandikwaje? Dakika 10 mtu anaongea kuhusu number zimekaaje?

  Na nikurudi kwenye uongozi wa bunge hasa Spika kwenye huu mgogoro wa madaktari hapo ndipo watanzania tumepata hasara kubwa sana. Spika amechochea sana huu mgogoro kwa kutoruhusu bunge kufanya kazi yake ya kuismamia serikali. Hata pale kamati ya bunge ilipofanya majadiliano na pande mbili za mgomo wa madaktari, spika ameamua kuficha report! Wawakilishi wa wananchi watafanye kazi kama spika anaficha taarifa?
   
 8. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #8
  Jul 4, 2012
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,362
  Likes Received: 6,393
  Trophy Points: 280
  Watanzania inabidi waanze kukasirishwa na Bunge; haiwezekani wenye nyumba wanabishana kuhusu mambo yasiyo na msingi wakati nyumba inabomoka. Bunge letu ni legelege!
   
 9. R

  RC. JF-Expert Member

  #9
  Jul 4, 2012
  Joined: May 24, 2012
  Messages: 446
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  kusema ukweli mh.mwanakijiji huwa unatoa vitu vya ukweli mimi nakukubali sana,siijui taaluma yako lkn unafaa sana kuwa mwanahabari!hongera sana mkuu!
   
 10. Nyakageni

  Nyakageni JF-Expert Member

  #10
  Jul 4, 2012
  Joined: Feb 1, 2011
  Messages: 13,959
  Likes Received: 1,284
  Trophy Points: 280
  Mkuu MM its true that we have a 'silly' Govt and Parliament. Lakini muhimili wa Mahakama unauonea. Ukweli ni kuwa muhimili huu haujaliwi
   
 11. segwanga

  segwanga JF-Expert Member

  #11
  Jul 4, 2012
  Joined: Mar 16, 2011
  Messages: 2,790
  Likes Received: 37
  Trophy Points: 145
  Serikal makini ingechukua vichwa kama MMJJ katika kitengo cha kutunga sera tungekuwa mbali.Genaro gattuso amewahi kusema kuwa anapomwangalia pirlo akicheza huwa anajiuliza ''je na mimi ni midfielder?'' hata mimi napoangalia makala za MMJJ HUWA NAJIULIZA NA MÍMÍ NI GREAT THINKER?
   
 12. Ndahani

  Ndahani JF-Expert Member

  #12
  Jul 4, 2012
  Joined: Jun 3, 2008
  Messages: 14,333
  Likes Received: 1,796
  Trophy Points: 280
  Kuna kina mama wako huko bungeni, yaani wacha kabisa.
   
 13. S

  Sometimes JF-Expert Member

  #13
  Jul 4, 2012
  Joined: Dec 28, 2010
  Messages: 4,567
  Likes Received: 361
  Trophy Points: 180
  Mkuu umeeleweka sana! Huitaji Masters kuelewa mada hii.
   
 14. Mbutunanga

  Mbutunanga Senior Member

  #14
  Jul 4, 2012
  Joined: Feb 15, 2011
  Messages: 183
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 35
  Hivi kama mwananchi, nifanyeje ili hili bunge hata livunhwe tu? Je nikipendekeza hili kwa katiba watanisikia, je nitahojiwa?
   
 15. B

  Bajabiri JF-Expert Member

  #15
  Jul 4, 2012
  Joined: Jan 1, 2011
  Messages: 9,755
  Likes Received: 27
  Trophy Points: 0
  me darasa la nne la mwinyi,,,na nimemuelewa
   
 16. mzamifu

  mzamifu JF-Expert Member

  #16
  Jul 4, 2012
  Joined: Mar 10, 2010
  Messages: 3,497
  Likes Received: 854
  Trophy Points: 280
  Ingawa mada yako ni ndefu, ina mabo mengi ambayo ni relevant na hali haliis kwa sasa hasa kwa wabunge serikali na wazalendo.
  Bila kurudia yale uliyosema nataka niongezee kuwa Wabunge na hata viongozi wa kitaifa wanashindwa kufanya uliyosema kwa sababu motives za walio wengi wakati wanaomba ubunge au uongozi hazikuwa kwa ajili ya kuleta mabadiliko kwa wanachi bali kujikimu wao binafsi. Matokeo yake wanaishia kupiga kelele na kutetea vyama vyao vilivyowasaidia kuwafikisha hapo bungeni badala ya kuwasemea wanachi.
  Wengi ni wanafiki na wapenda vyeo kwani hupenda kutoa sifa na pongezi kwa Rais, waziri n.k na kuishia kusema nanga mkono hoja.
  Mimi naona kuwa wabunge wa upinzani wametoa changamoto kubwa hasa katika kuikosoa serikali ili kuifanya iwajibike zaidi. matokeo ya kazi hii ni wabunge wa CCM kuungana na kujikuta kazi yao kubwa ni kutoa vijembe kwa wapinzani na kusahau wajibu wao wa msingi. wabunge wa CCM wamejenga hofu, woga, chuki na hata dharau dhidi ya wapinzani. Maanadalizi yao mengi ni kuandaa majibu ya kuwakatisaha tamaa wapinzani. Mawaziri naao wameingia katika mkumbo huo. hotuba za Vuai Nahodha na Werema wakijibu hoja leo ni ushahidi tosha
  Kwa kuzingatia maelezo yako nashauri Wabunge wote wawe kitu kimoja wenye lengo moja nalo ni kuwaletea wanachi maendeleo. wajue kuwa wanawakilisha majimbo yenye vyama tofauti hivo wawapo bungeni suala muhimu ni wanachi kwanza vyama baadae.
  Mimi naona kuwa rais si legelege kwa mantiki kwamba anautumikia mfumo uliomwezesha kufika hapo juu ya mti wenye matuda. Yeye anajaribu kwasaidia kufikia hayo matunda na wengine anawachumia na kuwarushia basi na wao hushangilia na kupiga vigelegele Baaaba! Baaaba! Wengine mtaishia kulalama rais, rais, rais, wengine wanasema big up JK. Kwa hivo kila wanapoanza hotuba zao hawaachi kusifu, kupongeza ... Nampongeza Mheshimiwa,... DOKTA, cjui ...kwa hotuba yake ya mwisho wa mwezi. Hii ndo sala yao kma vile Baba yetu uliye ...
  Mwisho nijibu swali lako; Je, kuna matumaini? Jibu ndio yapo kwa sababu mawazo yako ni sehemu ya kuanzia katika kuleta matumaini tatizo itabidi tusuburi watu wapate ufahamu, ni lini, hapo cijui lakini matumaini yapo. Hongera mwanakijiji
   
 17. jogi

  jogi JF-Expert Member

  #17
  Jul 4, 2012
  Joined: Sep 25, 2010
  Messages: 19,335
  Likes Received: 12,801
  Trophy Points: 280
  Katika hiyo hasira unayokusudia naanza kwa kuwashauri kuwa bunge liwe na mamlaka ya kujadili bajeti inayoishia kwanza ili kuibana serikali kama ilizembea popote kiutekelezaji, kuona kama fedha kusudiwa zilipatikana kama vyanzo vya mapato vinavyoeleza, distribution ya hizo fedha ilifanyika accodingly and timely then wabunge waipe serikali mapendekezo kutoka kwa wananchi majimboni wanataka nini ili serikali ikapange hiyo budget, itohoe vyanzo vya mapato kuendana na mahitaji ya miradi ya maendeleo na matumizi ya kawaida. Ili hatimaye itakapoletwa bungeni, wabunge watakuwa na nafasi ya kuirekebisha kusuit mwendokasi wa maendeleo na vipaumbele kuzingatia geographical location per priorities.
   
 18. k

  kitero JF-Expert Member

  #18
  Jul 4, 2012
  Joined: Feb 21, 2012
  Messages: 563
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Ninacho fahamu na ndiyo ilivyo kama baba akishindwa kuisimamia nyumba yake kila kitu kitayumba,Mama atafuata lake na watoto lao.Kwahiyo ni vizuri kila kitu kikawekwa upya vizuri na kufundishana jukumu la huyu ni nini na mipaka ya huyu ni nini .Na si kwaaliye pewa juku la kufanya hili kuja kuomba ruhusa ya kufanya hili kwa asiye na mamlaka hata kidogo ila uaweza kuomba ushauri,ila la muhimu ni kusimamia sheria na kutekeleza sheria.
   
 19. The Son of Man

  The Son of Man JF-Expert Member

  #19
  Jul 4, 2012
  Joined: Feb 9, 2010
  Messages: 12,124
  Likes Received: 1,709
  Trophy Points: 280
  Nshakata tamaa kwababu ya hawa watu! Mbunge anasimama badala ya kujadili hoja ya serikali, ye anajadili maoni ya kambi rasmi ya upinzani. Hivi bungeni watu hao wana akili kweli?
   
 20. E

  Elizabeth Dominic Platinum Member

  #20
  Jul 4, 2012
  Joined: Dec 7, 2007
  Messages: 4,547
  Likes Received: 53
  Trophy Points: 145
  Naamini kabisa John Mnyika angepewa nafasi ya kufafanua kauli yake Bungeni siku ile alipotolewa nje nadhani tungekuwa na mjadala mkubwa zaidi kuhusu Bunge legelege kwani watu walipata kuzungumzia hapa na pale kuhusu udhaifu wa Rais.
  Dhana iliyojengeka miongoni mwetu hasa katika kipindi hiki cha Upinzani kupamba moto na kuongeza viti kadhaa Bungeni ni kuwa kazi ya Wabunge ni kusemea matatizo ya Wananchi, hapo ndio utaona wanaposhindana kupaza sauti na hadi nime notice mirindimo ya sauti zao inafanana....its sickening kuwa Wabunge wengi wameingia Bungeni kwa mfumo mbovu wa Uchaguzi kuanzia kwenye hatua ya kura za maoni kwenye chama hadi kwenye Uchaguzi na sasa tunaona matokeo yake....... Mzee Mwanakijiji umesema vyema kuwa sasa ni wakati wa kuwa hold accountable hizi abracadabra zimetupoteza kabisa na sasa wakati mwingine tunashindwa kujua which is which
   
  Last edited by a moderator: Jan 4, 2016
Loading...