Baraza la Kiswahili lashutumu wabunge kwa uchafuzi wa Kiswahili
From http://mwananchi.co.tz/newsre.asp?id=3171
Na Salim Said, MUM
MWENYEKITI wa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), Suleiman Hega amesema Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linaogoza kuchafua lugha ya kiswahili nchini.
Kauli hiyo aliitoa jana katika mjadala juu a lugha ya Kiswahili ulioendesha na Televisheni ya Chanel Ten kupitia kipindi chake cha 'je, tutafika' kinachorushwa kila siku ya Jumaatano usiku.
Hega, alisema bunge hilo, limetia fora kwa kuchanganya na kuharibu lugha ya kiswahili bila ya kiongozi wake kuchukua hatua yoyote.
Alisema katika Bunge, Spika ana nguvu katika kauli zake, lakini hata siku moja hajasimama kuwakemea wabunge kuhusu kuchanganya kiswahili na kiingereza katika mazungumzo yao badala yake anasimama na kupiga marufuku matumizi ya neno 'kazana' bungeni.
Naye Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Dk Ana Kishe aliitaka serikali kuongeza bajeti ya BAKITA ili kufanya kazi zake kwa urahisi zaidi na kutoa kipaumbele kwa matumizi ya Kiswahili.