Bunge laipa Serikali siku 4 kukomesha mauaji ya watoto Njombe

johnthebaptist

JF-Expert Member
May 27, 2014
83,902
141,842
Bunge limetoa siku 4 kwa Serikali kukomesha mauaji ya watoto mkoani Njombe vinginevyo.........!

Chanzo: Gazeti la Nipashe

=======


Mauaji Njombe yatikisa Bunge
MAUAJI ya kikatili ya watoto yanayoendelea kuripotiwa mkoani Njombe, yamechukua sura mpya baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai, kuiagiza serikali kuwasilisha taarifa kamili bungeni jijini Dodoma kabla ya kumalizika kwa mkutano wa sasa wa Bunge.


Chombo hicho cha kutunga sheria, kimetoa agizo hilo baada ya kuelezwa kuwa shughuli za kiuchumi katika miji ya Makambako na Njombe zimesimama kwa siku nne, huku wafanyabiashara wakubwa 10 wakidaiwa kukamatwa wakihusishwa na mauaji ya kikatili ya watoto yanayoendelea mkoani humo.

Zaidi ya watoto 10 wameripotiwa kuuawa kikatili na kunyofolewa viungo vyao, zikiwamo sehemu za siri na masikio. Ilielezwa bungeni jana na wabunge wanaotoka Mkoa wa Njombe kuwa, kwa sasa wakazi wa mkoa huo wanalazimika kujifungia kwenye nyumba zao kabla ya saa mbili usiku kutokana na hofu iliyoko.

Vilevile, wabunge hao walisema wazazi na walezi wamepata kibarua kipya cha kuwapeleka shuleni na kuwarudisha nyumbani watoto wao ili kuhakikisha usalama wao.

Mbunge wa Makambako, Deo Sanga na Mbunge wa Lupembe, Joram Hongoli (wote CCM), walisimama na kutoa hoja bungeni jana asubuhi, wakiomba Bunge lisitishe shughuli zake na kujadili hoja ya dharura kuhusu mauaji yanayoendelea mkoani Njombe.

“Hao wafanyabiashara wakubwa wana siku nne ndani, na hivi sasa hatujui nini kinachoendelea," Sanga alisema na kuongeza kuwa: "Wafanyabiashara wengine walikuwa wakazi wa Makambako na walikuwa Dar es Salaam, ni wawekezaji wakubwa katika mji wa Makambako wamekamatwa.

“Watu waliokamatwa mpaka sasa ni takribani 10 ambao ni wafanyabiashara wakubwa, kuna baadhi yao wana viwanda na wana watumishi zaidi ya 200. Shughuli sasa zimesimama kabisa." Sanga, maarufu kama Jah People, alisema taharuki iliyoko katika mkoa huo inachochewa na baadhi ya watu.

Alisema hali ya miji ya Makambako na Njombe kwa sasa si nzuri kutokana na shughuli mbalimbali kusimama. "Ukienda kule Lupembe aliposema Mheshimiwa Hongoli, Mji wa Lupembe katika Wilaya ya Njombe ndio unaozalisha mbao kwa wingi sana.

Watu wamekwenda na pikipiki (bodaboda), walipofika mahali wamesimama, watu wakasema hee, hao hao watu huko na huko na bahati nzuri wakampigia simu Mheshimiwa Mbunge, Mbunge akawaambia msiwaue, kwa hiyo hali ni tete," alisema.

Sanga alisema ni vyema kuwe na tamko la serikali kuhusu kinachoendelea Njombe na hatua ambazo zinachukuliwa na serikali kuhakikisha hali ya utulivu inarejea mkoani humo.

Awali, akijenga hoja ya kuliomba Bunge kujadili hoja hiyo ya dharura, Hongoli alisema kuna taharuki kubwa mkoani Njombe na watu wamekuwa na hasira kutokana na shughuli zote za kiuchumi kusimama na wanalazimika kuwasindikiza watoto kwenda shuleni na kuwachukua kuwarudisha nyumbani baada ya masomo.

Hongoli alisema: “Lakini kama vile haitoshi, Mheshimiwa Spika, kutokana na hiyo hasira, tayari kuna mauaji yameshajitokeza katika baadhi ya halmashauri kwa mfano juzi, kule Ludewa wameshaua mtu mmoja ambaye anadhaniwa kuwa kati ya watu wanaotafuta hao watoto wadogo chini ya miaka 10, lakini kumbe alikuwa si mtu anayeshughulika na shughuli hizo.

“Sasa niombe Mheshimiwa Spika, angalau kwa dakika 20 kwa idhini ya kiti chako, niombe Bunge lako liweze kujadili juu ya hali inayoendelea katika mkoa wa Njombe, maana leo iko Njombe, kesho inaweza ikaendelea na mikoa mingine na nchi nzima ikawa iko kwenye taharuki.

"Naomba nitoe hoja kwa dakika 20 tuweze kuijadili hoja hii, tuweze kuhakikisha kwamba serikali inaweza kuchukua jukumu la kuhakikisha kwamba mauaji haya yanatoweka." Hongoli alilieleza Bunge kuwa katika wilaya ya Wanging’ombe, watu wameshauawa na wengine kujeruhiwa wakidhaniwa kujihusisha na mauaji hayo.

“Kwenye jimbo langu (Lupembe), wiki iliyopita kuna mtu mmoja alinusurika kuuawa na juzi imetokea kwenye Kijiji cha Matembwe, mtu mmoja amenusurika kuuawa. Kwa hiyo, hali ni mbaya sana katika Mkoa wa Njombe," alisema.

PICHA MTANDAONI

Mbunge huyo aliongeza kuwa kuna watu wameongeza hasira kwa wakazi wa Njombe kutokana na kuweka picha kwenye mitandao zikionyesha watoto wameuawa.

Alisema kuwa Ijumaa iliyopita, walituma picha inayoonyesha watoto zaidi ya 20 wamerundikwa kwenye chumba kimoja na wote wamefariki dunia, na picha hizo kuwa na maelezo yanayoonyesha mauaji yametokea Njombe.

“Juzi na jana, wametuma kwenye mtandao wakionyesha watoto watano wameuawa na wametupwa kwenye shimo limechimbwa na wako tayari kufukiwa," alisema.

Mbunge huyo aliongeza: "Wanasema ni Mkoa wa Njombe na sisi wabunge wa Mkoa wa Njombe tumepeleleza kama kuna mauaji yametokea hivi karibuni ya idadi ya watu hao, taarifa zinaonyesha kwamba, hakuna idadi iliyotokea zaidi ya watoto watatu waliouawa Njombe Mjini na hao wawili waliouwa Lupembe,".

KAULI YA SERIKALI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama, akizungumza kwa niaba ya Waziri Mkuu, aliliambia Bunge kuwa jambo hilo ni zito na linachukua taswira nzito ndani ya taifa, hivyo ili serikali iweze kutoa maelezo ya kina, ni bora Kiti cha Spika kikaipa nafasi ya kutayarisha kauli yake kuhusu suala hilo.

“Mheshimiwa Spika, ili tuweze kuileta taarifa hiyo ndani ya Bunge lako haraka na Bunge liweze kujua hatua kubwa ambayo serikali tumechukua pia katika jambo hili, lakini itawapa 'comfort' (faraja) Watanzania na hasa wenzetu wananchi wa Mkoa wa Njombe ili waweze kuwa na amani na kuona kwamba serikali iko kazini, na Spika akiridhia, sisi kama serikali tuko tayari na tutatekeleza jambo lile," Mhagama alisema.

Kutokana na kauli hiyo, Spika Ndugai alikiri jambo hilo ni kubwa linalohuzunisha na kusikitisha, hivyo kukubaliana na ushauri uliotolewa na upande wa serikali, kwamba kabla Bunge halijaahirishwa Ijumaa, lipate maelezo toka serikalini ya nini kinachoendelea Njombe.

“Tukishapata maelezo hayo, sasa ndiyo kama kuna neno lingine tutaona namna ya kufanya. Kwa hiyo, serikali ijiandae, wakati tunamaliza shughuli zetu bungeni, tupate taarifa hiyo," Spika Ndugai alisema.

"Na tunawapa pole sana wazazi wote walioguswa na vifo vya watoto na tunaendelea kuihimiza serikali, kwa kweli iko haja kwa vyombo vyote vya ulinzi na usalama kuhamia huko Njombe ili kuhakikisha jambo hili linakomeshwa kabisa.



"Maana kama kuna jambo halikubaliki, halikubaliki kabisa, ni ukatili kwa watoto, ni jambo la kusikitisha sana, mtoto ambaye ni malaika wa Mungu, anauawa hivi hivi bila sababu za msingi, jambo hili linaipaka sana matope nchi yetu kimataifa, kwamba kuna watu nchi fulani wanaua watoto, ni jambo halipendezi hata kidogo."
 
Lipo tatizo,polisi wapo kila Kata, wanasubiri kutumika tu kwa mambo yasio ya msingi. Sehemu kubwa Usalama wa raia ni juhudi binafsi ,kudra za Muumba na Mahusiano raia. Polisi wetu ni reactive Sio proactive.

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Ni vizuri mleta uzi ungeleta habari iliyokamilika mfano, bunge la nchi gani?,kwa serikali ipi/ya nchi gani n.k?
 
Bunge hili hili la Ndugai Mkuu? au kuna bunge lingine unaliongelea hapa?

Katika vitu useless kwenye taifa hili nadhani bunge ni cha kwanza. I wish JPM angefutilia mbali hii kitu..after all he has proved that he can be a good bunge/judiciary and President!
 
Back
Top Bottom