Bunge laibana mbavu serikali utekelezaji mazimio Mgodi wa Makaa Kiwira

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,789
288,011
Date::8/1/2009
Bunge laibana mbavu serikali utekelezaji mazimio Mgodi wa Makaa Kiwira
Na Habel Chidawali,Dodoma
Mwananchi


BUNGE limeitaka serikali kuhakikisha kwamba inatekeleza maazimio ya Kamati ya Nishati na Madini na maoni yaliyotolewa na wabunge kuhusu Mgodi wa Kiwira ifikapo Novemba mwaka huu.


Akitoa taarifa ya kamati hiyo bungeni mjini Dodoma jana kwa niaba ya mwenyekiti wa kamati hiyo, Mbunge wa Kibiti (CCM), Abdul Marombwa alisema kamati yao ilipokea taarifa mbili tofauti kuhusu mgodi huo na hivyo kushindwa kuelewa serikali inamiliki hisa ngapi katika mgodi huo.


Alisema pia kamati ilishangazwa na taarifa ya fedha zilizotumika kukarabati vifaa vilivyokuwa vimechakaa katika mgodi huo, wakati wafanyakazi wanasema hakuna ukarabati wowote uliofanyika.


"Uzalishaji umeshuka baada ya ubinafsishaji na wawekezaji wameuza vifaa kama chuma chakavu, serikali ifanye uchunguzi kuhusu hilo na ikibainika kuwa haya yamefanyika sheria ichukue mkondo wake," alisema Marombwa.

Hivi karibuni Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja aliwasilisha ripoti ya serikali kuhusu mgodi wa Kiwira ambapo alisema serikali itachukua mgodi huo na itamlipa mwekezaji fedha alizotumia kuwekeza kwenye mgodi huo.


Katika taarifa yao kamati hiyo ilibaini kuwa kulikuwa kuna upungufu makubwa ndani ya serikali na kwamba yalihitaji maelezo ya kutosha.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, William Shelukindo akichangia hoja alisema Kiwira bado serikali ina kazi ya kufanya hivyo ichukue maoni ya bunge na kuyafanyia kazi kama maazimio ya kamati.


Akichangia taarifa ya kamati hiyo, Mbunge wa Maswa, John Shibuda alimtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kama ameshindwa kuwawajibisha watendaji wakuu waliohusika na mgodi wa Kiwira ajiuzulu mara moja.

Shibuda alisema Waziri Mkuu ni sawa na baba wa kufikia ambaye sio mwenye mtoto hivyo akasema ni lazima akaze buti katika kuweka mikakati yake kuliko kurithi madhambi ya mtu mwingine na akayanyamazia na kwamba serikali itamke hadharani nani hasa mmiliki wa Kiwira.

Mbunge huyo alisema kuwa ndani ya serikali kuna watendaji na mawaziri ambao hawafai na kwamba hahawezi kuondoka, "hata mtoto si riziki huenda kuposa, hivyo serikali iwatimue mara moja,".


Kama ilivyo kawaida yake kutumia misemo na methali za Kiswahili, Shibuda alisema watuhumiwa wakubwa katika kupotosha mambo ya serikali ni makatibu wakuu katika wizara.


Bunge lilikuwa na furaha wakati Shibuda akiwa anachangia, alisema kuwa, "Udhaifu wa askofu si wa biblia hivyo uovu wa watu binafsi, haufai kulindwa na serikali,".

Alisema mswada wa kuiwajibisha serikali uletwe bungeni, ili tuwe tunawawajibisha kwa kuwa haitekelezi maazimio ya bunge.

"Kitengo cha sheria cha bunge kitengeneze sheria ya kuiwajibisha serikali," alisema Shibuda.

Alisema kuwa siku zote makatibu wakuu ndio ambao wamekuwa wakipotosha mambo ya serikali na kuwafanya wabunge kama watoto wadogo wasiojua kitu.

“Mimi nasema hivi serikali ya Kanu nchini Kenya ilianguka kutokana na watendaji wake kama hawa tulionao hivi sasa, kwa hiyo nasema kuwa iletwe sheria hapa tuwatimue kabla ya wao hawajatutimua,” alisema Shibuda na kuongeza:

“Wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya na hao makatibu wala sio wanasiasa ambao wanapanda majukwaani kama sisi, hivyo ndio maana umeibuka mtindo wa kusema kuwa mtu fulani akiwajibishwa serikali inaaibika,wafichuliwe haraka sana,” alisema.

Kwa upande wake Mbunge wa Kishapu,Fred Mpendazoe aliitaa serikali kumwajibisha kiongozi yeyote atakaekwenda kinyume bila ya kumwonea aibu na akasema kuwa Kampuni ya AnBen ilikuwa ndio mmiliki halali wa mgodi huo.

Bila ya kutaja hadharani mbunge huyo alimhusisha mmiliki wa kampuni hiyo na viongozi wa awamu ya tatu na kusema kuwa huenda walikuwa ni ndugu hivyo viongozi wa Tanzania wanajitajirisha wenyewe kwa kugawa rasilimali kwa ndugu zao.

“Kama ni hivyo, mmiliki wa Kiwira ajitokeze aombe msamaha kwa Watanzania, kwani serikali ya awamu hii imeapa kuilinda katiba hivyo hatutanyamaza kwani nimekuwa nikisema kila siku lakini naonekana kama mtu aliyechanganyikiwa,” alisema Mbunge huyo wa Kishapu.

Akitoa ufafanuzi kwa ufupi kabla ya spika kumtaka arejeshe mjadala huo katika mkutano ujao, Waziri wa Nishati na Madini William Ngeleja alisema kuwa mgodi huo unamilikiwa na wawekezaji kwa hisa za asilimia 70. Ngeleja na alisema kuwa lengo la serikali ya awau ya nne ni kuhakikisha kuwa mgodi huo unazalisha umeme kwa kiwango cha kutosha ndani ya miezi 18-20 na kwamba serikali inafanya tathimini ili kuhakikisha kuwa inaurudisha mgodi katika umiliki wake.
 
Back
Top Bottom