Bunge lageuziwa kibao

Kakke

JF-Expert Member
Dec 4, 2010
1,885
2,000
WAKATI wabunge wakiituhumu Mahakana Kuu ya Tanzania kwamba iliandika barua kwa Spika wa Bunge, kutaka kuzuia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kuhusu kashfa ya uchotwaji fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow isijadiliwe, imebainika Bunge ndilo liliiandikia Mahakama barua.

Kwa mujibu wa vyanzo vyetu, barua hiyo ya Bunge iliandikwa na Katibu, Dk. Thomas Kashilila Novemba 14 mwaka huu, ingawa alipohojiwa na Tanzania Daima hakukiri wala kukanusha kuhusiana na suala hilo.

Katika barua hiyo ya Bunge, Dk. Kashilila anaiomba Mahakama iwaorodheshee idadi ya kesi zote zinazohusiana na IPTL zilizopo ndani na nje ya nchi.

Kwa maana hiyo, Mahakama iliandika barua kwa Bunge kujibu maombi ya Dk. Kashilila, hivyo kuibua hisia kwamba inafanya njama za kuzuia mjadala huo bungeni.

Kwa mujibu wa taarifa ya mahakama kwenda Bunge, kesi za IPTL zilizopo ndani ya nchi ni zaidi ya 10 huku kukiwa na jitihada za kupata idadi kamili ya zilizopo nje ya nchi.

Alipotafutwa na Tanzania Daima juzi, kuzungumzia barua hiyo, ambayo kwa kiasi fulani imeibua mvutano mkali kwa wabunge na mahakama, Dk. Kashilila alihoji ni wapi taarifa hizo zilipopatikana.

Alisema hawezi kulizungumzia suala hilo kwa kuwa hajui taarifa hizo zilipotoka huku akimtaka mwandishi afike ofisini kwake mjini Dodoma.

Alipoelezwa kuwa mwandishi aliyepiga simu yupo Dar es Salaam, Dk. Kashilila bado alishikilia uamuzi wa kutumiwa mwakilishi ofisini kwake.

"Sijui hiyo ‘information' (taarifa), umepata wapi lakini hilo pia si limeshaongelewa na Bunge… sasa unataka mimi niongee nini wakati ufafanuzi umeshatolewa," alihoji Dk. Kashilila.

Alipoelezwa kuwa taarifa ya Bunge ilikanusha mahakama kuandika barua kwa Bunge kuzuia ripoti ya CAG kuhusu Escrow isijadiliwe, Dk. Kashilila alisisitiza afuatwe ofisini kwake muda huo saa 10 jioni ya Novemba 22.

"Wewe njoo ofisini muda huu mimi ninakusubiri au tuma mwakilishi wenu wa huku, si mna watu wenu huku Dodoma," aliuliza.

Hata hivyo, mwakilishi wetu alipofika ofisini kwake, aliambiwa kuwa Dk. Kashilila alikuwa ameondoka hapo zaidi ya saa 1:30 zilizopita na hakuacha maagizo yoyote.

Gazeti hili liliendelea kuwasiliana na Dk. Kashilila na kumueleza kutokuwepo kwake ofisini, ambapo alijibu kuwa atawasiliana na mwandishi wa Dodoma baada ya kupewa namba yake ya simu.

Katika majibu yake kwa mwandishi wetu aliyeko Dodoma, Dk. Kashilila alisema hana jambo jipya zaidi ya majibu yaliyotolewa bungeni kuhusiana na barua.

Jumatano iliyopita, wabunge wanaounda kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), walizungumza na waandishi wa habari na kueleza kuwa kuna mkakati wa mahakama kuzuia suala Escrow lisijadiliwe bungeni.

Baada ya taarifa hiyo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alilieleza Bunge liangalie namna watakavyojiepusha na kuingilia mhimili wa mahakama katika kujadili suala hilo, hali iliyozua mtafaruku bungeni kwa baadhi ya wabunge kupingana naye.

Katika kuonyesha kuwa hawakubaliani na ushauri huo, baadhi ya wabunge hao akiwemo James Lembeli (CCM), walieleza kuwa ni vema ripoti hiyo ikawekwa hadharani huku Tundu Lisu (CHADEMA), akisema kama kuna barua kutoka mahakamani, jina la Jaji aliyeiandika lifikishwe mbele ya Bunge kwa ajili ya kujadiliwa kwa kuingilia mamlaka yao.

Utata huo ulipoozwa Ijumaa baada ya Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu kuliambia Bunge kuwa hakuna barua yoyote ya mahakama iliyopokelewa kwa ajili ya kuzuia ripoti ya Escrow isijadiliwe.

Chanzo:Tanzania daima
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom