Bunge kuingiza viraka ‘bandia’ - Mabadiliko sheria ya Katiba

nngu007

JF-Expert Member
Aug 2, 2010
15,862
5,797
Mabadiliko sheria ya Katiba

Mwandishi Wetu - Raia Mwema

Dodoma

katiba225.jpg



Freeman Mbowe na Rais Kikwete wakijadili Katiba mpya

Mabavu ya Rais yalindwa upya kwa mlango wa nyuma

CHADEMA, NCCR, CUF, NGOs waambulia ‘kiduchu'


WAKATI mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011, yakiwasilishwa bungeni wiki hii, imebainika ya kuwa bado sheria hiyo itakuwa na ‘matundu' mengi yanayompa madaraka makubwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuendesha mchakato huo kinyume cha matarajio ya wengi.

Mapendekezo hayo ya mabadiliko yatakayowasilishwa wakati wowote sasa bungeni na Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani, ni matokeo ya majadiliano ya mapendekezo yaliyofanywa kwa kushirikisha baadhi ya vyama vya upinzani na asasi za kiraia, chini ya uenyekiti wa Rais Jakaya Kikwete.

Baadhi ya makundi hayo mahsusi ya kijamii, vikiwamo baadhi ya vyama vya siasa na asasi za kiraia, mara kwa mara, kabla na baada ya muswada wa sheria ya mabadiliko ya Katiba kuridhiwa na Bunge, Novemba mwaka jana, yalikuwa yakilalamika Rais kupewa madaraka makubwa, hali hiyo ikamshinikiza Rais Kikwete kukutana na wadau hao na kuwasilikiza.


Taarifa zilizovuja za sehemu ya mapendekezo hayo yanaendelea kumpa nguvu kubwa Rais kuendesha mchakato huo kwa kuzingatia uundwaji wa tume ya kukusanya maoni pamoja na namna ya kuchukua hatua ya kumwondoa mjumbe wa tume atakayekwenda kinyume cha taratibu zilizowekwa.


Raia Mwema
imebaini kuwa, ingawa Rais hataweza moja kwa moja kumwondoa mjumbe wa tume aliyekwenda kinyume cha taratibu wakati wa mchakato wa utekelezaji wa majukumu ya tume ambayo ni pamoja na kukusanya maoni, kazi hiyo itafanywa na kamati maalumu atakayoiteua. Kikubwa kinachoendelea kumpa madaraka makubwa Rais katika ‘kuchomoa' wajumbe ni namna ya kuteua wajumbe wa kamati hiyo na maeneo wanakotoka.


Rais anapewa wigo mpana wa kuunda kamati ya kuwachunguza wajumbe wa tume kwa kutakiwa kuteua wanakamati kutoka maeneo maalumu ambayo hata hivyo, ndani ya idara hizo ndimo wamo wateule wake wengi.


Kwa mujibu wa taarifa, marekebisho yanapendekeza pamoja na mambo mengine, kuwa kama suala la kumuondoa mjumbe kwa kukiuka kanuni za maadili litajitokeza, Rais atateua kamati itakayoundwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani; Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala bora; Kamishna wa Sekretariati ya Maadili ya viongozi wa umma; wakili wa Mahakama Kuu Zanzibar atakayependekezwa na Chama cha Wanasheria Zanzibar na Wakili wa Mahakama Kuu atakayependekezwa na Chama cha Wanasheria Tanganyika.


Inaelezwa na baadhi ya wachambuzi kuwa, katika eneo hilo kamati itaundwa na watu watano lakini utaratibu wa kikanuni wa kuwasilisha majina kwa Rais hautakuwa wa kumlazimisha kuridhia majina anayoletewa kwa mfano na Chama cha Wanasheria Tanganyika au Zanzibar lakini wakati huo huo, wajumbe wengine kama makamishna kutoka tume ya haki za binadamu au sekretariati ya maadili ni watu ambao amekuwa akiwateua yeye katika nafasi hiyo, achilia mbali hii ya sasa ya kuwateua tena kuwa wajumbe wa kamati ya ‘kufukuza' au ‘kutofukuza' wajumbe wa Tume ya Katiba ya kukusanya maoni.


Lakini pia kamati hiyo ya kukuza au kutofukuza wajumbe wa Tume ya Katiba imepewa jukumu la kisheria kujitengenezea utaratibu wa kufanya uchunguzi na vile vile inapewa ‘rungu' la kuwa ndiyo mamlaka ya nidhamu kwa wajumbe wa sekretariati ya Tume ya Katiba.


Mapendekezo mengine kwa mujibu wa taarifa hizo ni ya kuwaondoa wakuu wa wilaya katika mchakato wa shughuli za Tume ya Katiba na badala yake, kuwaweka wakurugenzi wa manispaa au katibu wa baraza.


Hoja hiyo ya kuwaondoa wakuu wa wilaya na kuwaweka wakurugenzi inatajwa kutumiwa kisiasa na chama kimoja cha siasa cha upinzani kuwa ni yenye manufaa kwao kwa kuzingatia kile kinachofananishwa na hisia kuwa, wakurugenzi wengi ni mashabiki wa chama hicho lakini gazeti hili limebaini kuwa, wakurugenzi hao bado wako chini ya himaya ya uteuzi wa Rais na wakati wowote wa mchakato wa Katiba mpya, kwa kadiri itakavyokuwa ikimpendeza Rais, wanaweza kuhamishwa vituo vya kazi au kuteuliwa wapya.


Lakini mbali na hayo, imebainika kuwa si tu CHADEMA, NCCR-Mageuzi, CUF na asasi zisizo za kiserikali ndizo zimewasilisha mapendekezo yao kwa Rais, bali hata CCM kama taasisi achilia mbali wabunge wake kufanya kazi hiyo bungeni, nacho pia kiliwasilisha mapendekezo yao ya ziada kimya kimya kwa Rais.


Miongoni mwa mapendekezo hayo ambayo hata hivyo, yamekuwa pia yakielezwa kuwa yanatokana na CHADEMA ni Rais kuweza kuwateua wanasiasa kuwa wajumbe wa Tume ya Katiba, na hapo wakilengwa wanasiasa wenye uzoefu mkubwa au hata wale ambao walishika nyadhifa kubwa serikalini lakini wana uwezo mkubwa licha ya kuanza kwao kuishi maisha ya kustaafu.


"Kwa mfano, mtu amewahi kushika nafasi kubwa kitaifa kama Waziri Mkuu lakini amewahi pia kuwa ni mjumbe pengine wa Halmashauri Kuu ya CCM, lakini ni mtu mwenye kuheshimika katika jamii nchini na hata kimataifa, ni kwa nini mtu wa namna hii asichukuliwe kusaidia kazi hii muhimu kwa taifa, sasa kama hoja ni kuchukuliwa tayari huyu anayo sura ya mwanasiasa lakini hilo si muhimu, bali muhimu ni uwezo wake na mchango wake unaoatarajiwa," anaeleza mmoja wa viongozi waandamizi serikalini, aliyezungumza na mwandishi wa gazeti hili mjini Dodoma.


Kwa upande mwingine, marekebisho hayo ya sheria ya mabadiliko ya Katiba yataweka muda maalumu wa uhai wa Bunge la Katiba, ambalo tofauti na sheria hiyo kabla ya mabadiliko sasa ukomo wa Bunge hilo ni miezi minne lakini kuna fursa ya kuliongezea uhai wa mwezi mmoja kama kutakuwa na haja ya kufanya hivyo.


Suala jingine ni kigezo cha jinsia katika kuwapa wajumbe wa tume hiyo ya katiba lakini jingine kubwa zaidi ni kuwawekea mamlaka ya kisheria, wajumbe wa Tume ya Katiba kuweza kuingia katika Bunge la Katiba kutoa ufafanuzi kila inapohitajika, mapendekezo ambayo ni tofauti na ilivyokuwa awali kukiwa na masharti kuwa, wajumbe hao wataweza kuingia kwenye Bunge la Katiba kwa kibali maalumu (bila nguvu za kisheria).


Gazeti hili pia limeelezwa kuwa kundi la asasi za kiraia, sehemu ya mapendekezo yao yamekubaliwa kuingizwa kwenye mabadiliko haya na moja ya mapendekezo yao yaliyokubaliwa ni kuwasilisha majina kwa Rais kutoka asasi husika ili aweze kuteua miongoni mwao kuwa wajumbe.


"Rais hatateua moja kwa moja majina kutoka NGOs au taasisi nyingine za kijamii bali taasisi hizo ndizo zitakazowasilisha majina na yeye atateua kutoka humo," anaeleza mmoja wa viongozi wa asasi ya kiraia nchini.


Kwa mujibu wa taarifa tulizokuwa nazo hadi tunakwenda mitamboni, marekebisho hayo yamepangwa kuwasilishwa bungeni wakati wowote kuanzia leo baada ya Rais Kikwete kukutana na wabunge wa CCM katika makundi maalumu. Taarifa za awali zilionyesha kwamba jambo hilo lilikuwa limesababisha mvutano.








 
Back
Top Bottom