Miss Zomboko
JF-Expert Member
- May 18, 2014
- 4,500
- 9,279
WATU wawili wamenusurika kifo baada ya kushambuliwa na wanyama aina ya fisi wasiojulikana idadi yao baada ya kuvamia kwenye mji uliokuwa na msiba Kijiji cha Kasahunga wilayani Bunda mkoani Mara.
Kwa mujibu wa Daktari wa Hospitali ya Misheni Kibara, Dk Samwel Paul, ambako majeruhi David Robert amelazwa, alithibitisha kupokea majeruhi huyo aliyejeruhiwa sehemu mbalimbali ikiwamo mikono yake.
Naye Muuguzi wa Kituo cha Afya Kasahunga aliyefahamika kwa jina moja la Happy ambako majeruhi mmoja amelazwa, alimtaja majeruhi huyo kuwa ni Elizabeth Mgeta (60), na amejeruhiwa mkono mmoja.
Mashuhuda wa tukio hilo lililotokea saa sita usiku wa kuamkia jana, walidai fisi hao walivamia msibani hapo na kuanza kushambulia waombolezaji waliokuwa wamekaa nje wakisubiri kulala baada ya ibada kuisha.
Katika hatua nyingine, wavuvi wanne wamekufa maji kutokana na mtumbi wao waliokuwa wanavulia samaki kutoboka na kuzama katika ziwa Victoria, eneo la mwalo wa Kibara katika Wilaya ya Bunda mkoani Mara.
Taarifa ya Polisi Mkoa wa Mara ilieleza kuwa mvuvi Doto Mfungo (18) ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Kenkombyo wilayani Bunda alinusurika kifo baada ya kushikilia mtumbwi huo na kupiga kelele za kuomba msaada, ambako wananchi walifika katika eneo hilo na kumuokoa.
Wavuvi waliokufa maji ni Kabenjulilo Magere (17), Godluck Yohana (15), Kaitila Julius (19) na Philipo James (17) ambaye alikuwa mwanafunzi wa Shule ya Msingi Kenkombyo aliyefaulu mtihani wa darasa la saba mwaka huu, ambao wote ni wakazi wa Kijiji cha Kenkombyo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Juma Ndaki alithibitisha kutokea kwa tukio hilo usiku wa kuamkia jana saa 7:30. Dakitari wa Hospitali ya Misheni ya Kibara wilayani Bunda, Dk Samwel Paul na muuguzi mmoja wa hospitali hiyo Nurie Mabele, wamethibitisha wavuvi hao kufa maji.