Budget Mbadala 2008/09

George Kahangwa

JF-Expert Member
Oct 18, 2007
547
147
HOTUBA YA KIONGOZI WA UPINZANI NA MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI
MHESHIMIWA HAMAD RASHID MOHAMED (MB) WIZARA YA FEDHA KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA WA FEDHA 2008/2009.
______________________

I. UTANGULIZI

1. Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Kambi ya Upinzani naomba upokee shukrani zetu za dhati kwa kunipa nafasi hii ili nitoe maoni ya Kambi ya Upinzani kuhusu hotuba ya bajeti ya mwaka wa fedha 2008/2009 kwa mujibu wa Kanuni za Bunge Kifungu cha 99(7) toleo la Mwaka 2007.

2. Mhe. Spika, Awali ya yote naomba kutoa shukurani zangu za dhati kwa wabunge wote wa Kambi ya Upinzani kwa ushirikiano wao mkubwa, wakiongozwa na Dr.Wilbrod Slaa (Mb) waliofanikisha hadi kuniwezesha kusimama mbele yenu kuwasilisha hotuba ya maoni ya Kambi ya Upinzani, kutokana na hoja iliyowasilishwa na Waziri wa fedha na Uchumi tarehe 12.06.08. Mhe. Spika, Wabunge wa Upinzani na wabunge wote kwa ujumla wao, kwa pamoja tuna wajibu wa kushirikiana katika kuwatumikia Watanzania kwa lengo kuu la kuwaondolea umasikini uliokithiri, maradhi na ujinga pamoja na kujenga UTAIFA wetu wa dhati. Mwenyezi Mungu aziweke pamoja nia zetu na kuzibariki katika kutekeleza azma hiyo.

3. Mheshimiwa Spika, Bajeti ya Serikali ni zaidi ya urari wa mapato na matumizi ya Serikali. Bajeti ni tamko la kisera lenye lengo mahususi katika kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi, kuongeza ajira na kupunguza umasikini miongoni mwa wananchi.

4. Mheshimiwa Spika, Kambi ya upinzani Bungeni chini ya uongozi wangu na msaidizi wangu Mhe. Dr. Wilbrod Slaa,(Mb) Mbunge wa Karatu, inaundwa na vyama vya CUF, CHADEMA, na UDP. Naomba kumpongeza Dr. Slaa kwa kuishinda tena CCM katika kesi ya uchaguzi. Pia napenda kutumia fursa hii kuvishukuru vyama vyetu kwa kuanza kujenga maelewano ambayo sio tu kusaidia juhudi za kambi yetu kutoa maoni ya pamoja juu ya hutuba ya Mipango na bajeti ya Waziri wa Fedha bali kuisaidia Serikali katika muono wa pili wa shilingi. Aidha Mhe. Spika naomba niwashukuru wapiga kura wa Jimbo langu la Wawi kwa kuendelea kuniunga mkono katika kazi walizonikabidhi katika kipindi cha 2005-2010. Nawaahidi, kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu nitaendelea kuwatumikia kwa uadilifu mkubwa.

5. Mhe. Spika, mnamo tarehe 14.06.2006 Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete alifanya mazungumzo na wabunge wa CCM na hatimaye wabunge wa Kambi ya Upinzani. Katika kikao hicho pamoja na mambo mengine mengi, Rais aliendelea kutoa ahadi yake ya kuumaliza mpasuko wa kisiasa ulioko Zanzibar na kusema “Tumeisha anza, siyo rahisi sana lakini tutaumaliza.”

6. Mhe. Spika, Kambi ya Upinzani itaendelea kuunga mkono juhudi za Mhe. Rais katika kuutafutia ufumbuzi mpasuko wa kisiasa wa Zanzibar pamoja na kero za Muungano (ambazo Rais Mstaafu Mkapa aliahidi kuzimaliza katika kipindi cha miezi sita wakati alipoingia madarakani), ila Kambi ya Upinzani ingelipenda kuweka bayana kwamba imani ya Watanzania inaendelea kupungua siku hadi siku kutokana na kuchelewa kufikiwa kwa MUAFAKA BAINA YA CCM NA CUF. Ni imani yetu kuwa, ahadi aliyotoa hivi karibuni alipokuwa Uingereza, Rais atatumia busara zake kukamilisha mazungumzo ili nchi yetu iepukane na aibu inayoitwa ya ngariba wa Kilwa.”Anatahiri watu lakini mwenyewe hakutahiriwa”.

7. Mheshimiwa Spika,naomba kwa niaba ya Kambi ya Upinzani, kukushukuru wewe, naibu Spika, wenyeviti wa Bunge na watendaji wa Ofisi yako,wakiongozwa na Kaimu Katibu wa Bunge, kwa kutupatia fursa mbali mbali sisi wabunge kujifunza shughuli za mabunge ya wenzetu. Moja tulilojifunza katika mabunge mengi, kambi ya upinzani huwa inapata fursa ya kutoa bajeti mbadala, yote hayo hufanywa kwa nia tu ya kuisaidia Serikali ili ione upande wa pili wa shilingi. Nia yetu sote ni kumsaidia Mtanzania aondokane na umasikini wa kila aina.

8. Mhe. Spika, naomba kumpongeza Waziri wa Fedha Mhe. Mustafa Mkullo (Mb), Manaibu Waziri, Katibu Mkuu na Manaibu wake, pamoja na wakuu wa vitengo na asasi zilizo chini yao kwa kazi nzito ya maandalizi ya Bajeti hii. Kambi ya Upinzani inafanya uchambuzi wake ikiamini kuwa Waziri atakuja kutoa ufafanuzi zaidi katika baadhi ya maeneo kwa kadiri tutakavyoainisha . Uchambuzi wetu nitauelezea baadae kwa kifupi na kwa kirefu utaelezewa na Mawaziri Vivuli wa Wizara mbali mbali.

9. Mhe. Spika, naomba nitumie fursa hii fupi kuwakumbusha tena Watanzania kupitia Bunge lako Tukufu, kuwa tokea Nchi yetu ipate Uhuru (Tanganyika) 1961 kukawa na “Republic of Tanganyika” na baada ya Mapinduzi (Zanzibar) 1964, kukawa na “People’s Republic of Zanzibar” na hatimaye Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Nchi yetu imeongozwa na TANU na ASP na Hatimaye CCM. Hivyo ni dhahiri kuwa mafanikio na mapungufu yote ya maendeleo ya Nchi yetu yametokana na Uongozi na Sera za CCM.

10. Mhe. Spika ni wajibu wetu sote kujiuliza, katika kipindi hichi chote cha uongozi wa Chama kimoja. Je sera zilizokuwepo, Mtanzania wa kawaida maisha yake yameboreka? Kwamba sasa anaweza akapata angalau milo miwili bila ya wasi wasi? Mwananchi wa kawaida anaweza akasomesha watoto wake na watoto hao wakasoma vizuri na hatimaye wakapata ajira? Au anaweza kujiajiri kwa kupata mikopo kwa urahisi yenye riba nafuu? Au Anaweza kupata huduma ya kijamii bila ya kulipia kwa gharama kubwa na kama anaweza kupata bei muafaka ya mazao yake kwa kuuza anakotaka kama ilivyokuwa kabla ya Uhuru na Mapinduzi? Je hata anayefanya kazi amepata mshahara unaokidhi mahitaji yake?

11. Mheshimiwa Spika, tunapo kumbushana haya hatusemi kwamba Tanzania hakuna maendeleo au mabadiliko, lakini je maendeleo hayo ni endelevu kiasi cha kumhakikishia Mtanzania kwamba baada ya “Sera ya Kilimo ni Uhai” ya Mwaka 1976, je tunajitosheleza kwa chakula cha kutosha na hata ukame ukitokea tuna chakula cha akiba,au chakula kinapokuwa bidhaa adimu duniani tunaweza kuuza na kubakiwa na akiba? Au bado tunaendelea kuhemea chakula? Kwamba tuliwahi kuwa na hekta 450,000 za umwagiliaji sasa zipo 298,888 tu, hayo ni maendeleo endelevu? Kwamba Mwalimu alituambia “ kupanga ni kuchagua” Je, kununua ndege kwa pesa taslim Tsh 42 billion, inayoweza kutua katika viwanja visivyozidi vitano katika nchi nzima na hata kushindwa kutua Dodoma ambayo ni Makao Makuu ya nchi na ya Bunge; ndege inayotumia wastani wa Tsh.6 million kwa saa ya kuruka,na kuwa na ndege nyingine mbili ambazo hata bajeti ya mwaka huu zimeshindwa kutengewa fedha za matengenezo,na kuacha kuwatengenezea barabara wanachi wa Mikoa ya Kusini ambao ni wazalishaji wakubwa wa Korosho, Muhogo, Ufuta na raslimali za Misitu na au kuacha kujenga zahanati, shule zenye kuwanufaisha wananchi walio wengi bila ya wao kujitolea. Kwamba unaweza kutumia raslimali nyingi za nchi kusafiri kutafuta wawekezaji bila ya kuwa na mipango ya kuwarasimisha wananchi, hivyo kuwafanya wawe omba omba, Au ndio ule msemo wa kiswahili kwamba “Punda afe lakini mzigo wa bwana ufike”. Kwamba huku unataka kumuondolea umasikini, upande wa pili unamuongezea kodi kwa mlango wa nyuma, bei za mafuta ya taa kwenye soko la dunia ni kubwa ukilinganisha na bei za mafuta ya petrol na dizeli, bei za mafuta ya taa ni 1,182.22 kwa lita huku petrol ikiwa 934.97 na dizeli 1,027.40 ,na hali ya bei hizo kwa hapa nyumbani ni tofauti haswa ukizingatia ya kuwa kodi na tozo mbalimbali kwa kila lita yaani shilingi 59.10 mafuta ya taa, 545.1 petrol na 520.80 dizeli .
12. Mhe, Spika kambi ya Upinzani inaona kwamba katika kuonyesha umakini wa kuinua uchumi wetu hizo kodi za ndani zinazotozwa kwenye mafuta tunatoa punguzo la shilingi 250.00 kwa kila lita moja ili kukabiliana na bei ya soko la dunia, hii ndio njia pekee ya kuufanya uchumi wetu ukue.
13. Mheshimiwa Spika, Bajeti ya Taifa ni chombo muhimu pekee cha kutafsiri na kutekeleza sera za Chama Tawala na Serikali kwa vitendo. Katika bajeti Serikali inapata fursa ya kupanga matumizi ya fedha kidogo zilizopo katika maeneo na sekta zinazohitaji kupewa kipaumbele ili malengo makuu ya Serikali yatekelezwe. Aidha, Rais Mpaka katika hotuba zake za kila mwezi alisema “Bajeti ni kipimajoto cha uhai wa mtu, na afya ya uchumi wa Taifa…………” “Daktari mzuri wa uchumi ataitumia bajeti kutoa tiba ya kupambana na umasikini na kuongeza kasi ya kukua kwa uchumi.” …..mwisho wa kunukuu.
14. Katika nchi masikini kama Tanzania malengo ya Sera za Serikali yanapaswa kuwa ya kujenga mazingira mazuri ya kukuza uchumi na kuongeza ajira ili kupunguza na kuutokomeza umaskin. Katika kuendeleza uchumi matumizi ya Serikali yanapaswa kuwa na malengo matatu makubwa:-

(a) Matumizi ya Serikali yalingane na uwezo wa mapato ya Serikali matumizi ya Serikali yawe endelevu, pasiwe na nakisi kubwa ya bajeti inayojazwa kwa kuchapisha fedha, kukopa ndani au kukopa nje. Bajeti ya Serikali lazima ilenge katika kupunguza kutegemea misaada na mikopo.

(b) Bajeti ya Serikali igawanywe katika sekta mbali mbali kwa lengo la kuongeza ufanisi na kutoa kipaumbele katika maeneo yanayokuwa chachu katika kukuza uchumi, kuongeza ajira na kupunguza umasikini.

(c) Matumizi ya fedha za Serikali katika sekta zilizopewa fedha hizo yaendeshwe kwa ufanisi na kwa kuongeza tija. Darasa linalogharimu shilingi milioni moja lisijengwe kwa gharama kubwa zaidi.

15. Mheshimiwa Spika, kwa kutekeleza Ilani ya uchaguzi ya CCM, Mipango na Ubinafsishaji ilipanga mkakati wa kutekeleza Sera za Uchumi kama ifuatavyo:-
(a) Kuona kuwa uchumi unakua kwa viwango na kasi kubwa ukilinganisha na mwaka uliopita.
(b) Mikakati ya kupunguza umasikini hasa usio wa kipato.
(c) Kuratibu mipango kitaifa, uwekezaji na ubinafsishaji.

16. Mheshimiwa Spika, je misingi hii imeheshimiwa na Serikali? Mhe. Spika sote ni mashahidi wa wafanyakazi wetu waliotumikia Taifa hili kwa maagizo na miongozo ya Serikali yao wanavyo sumbuka na kutaabishwa katika kudai haki zao zilizotokana na ahadi za Serikali.
17. Mhe. Spika, Pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya CCM kudai kuwa “Katika kuendeleza kuufufua na kuujenga uchumi wa Taifa Serikali ya CCM itaongozwa na siasa ya Ujamaa na Kujitegemea inayolingana na wakati tulionao. Shabaha ya Ujamaa katika kipindi hiki ni kuwafanya wananchi wenyewe kuwa ndio wamilikaji wakuu wa uchumi wa dola kuwa zaidi mhimili wa uchumi wa Taifa. Je? Ubinafsishaji umewafanya wananchi wa Tanzania kuwa wamilikaji wakuu wa uchumi?
18. Mheshimiwa Spika, Bajeti ya mwaka 2008/2009 ni Bajeti ya tatu ya Serikali ya awamu ya Nne. Lengo letu kama Kambi ya Upinzani ni kupitia utekelezaji wa Bajeti ya mwaka unaokwisha kwa shabaha ya kuonesha mafanikio na mapungufu na kisha kupendekeza njia muwafaka ya kuwa na Bajeti bora itakayoleta unafuu wa maisha kwa wananchi wetu.

TAKWIMU MPYA ZA PATO LA TAIFA.

19. Mheshimiwa Spika, ili kutathmini maendeleo ya uchumi tunahitaji tuwe na takwimu sahihi. Ni jambo la kawaida kufanya marekebisho katika takwimu za pato la taifa kwa madhumuni ya kuziboresha. Kwa kawaida marekebisho hayo huwa hayabadilishi muundo halisi wa uchumi.
20. Mheshimiwa Spika, vigezo vingi vya kupima mafanikio ya uchumi kama ukuaji wa uchumi, ukusanyaji wa mapato ya serikali, ubora wa mfumo wa fedha (financial deepening), pato la wastani la mwananchi n.k. vinatumia takwimu za pato la Taifa. Takwimu mpya za pato la taifa limeongeza ukubwa wa pato hilo katika miaka ya 1998 - 2006 kwa wastani wa asilimia 21.3. Ghafla, Watanzania wanaelezwa kwamba pato la taifa halisi lilikua kwa wastani wa asilimia 7.2 kati ya mwaka 2002 – 2006 na siyo asilimia 6.3 kama takwimu za zamani zilivyoonyesha.
21. Mheshimiwa Spika, takwimu mpya zinaonyesha kwamba ukame na ukosefu wa umeme wa mwaka 2006 uliotuletea kadhia ya ufisadi wa Richmond, eti hakuathiri uchumi wa Tanzania kwani uchumi uliendelea kukua kwa asilimia 6.7.
22. Mheshimiwa Spika, marekebisho yaliyofanywa hivi karibuni yanatia mashaka makubwa kwani yamebadilisha kabisa muundo wa uchumi. Takwimu za zamani zinaonyesha kuwa katika mwaka 2005 sekta ya kilimo ilichangia pato la Taifa kwa asilimia 46.1. Takwimu mpya zinaonyesha katika mwaka huo huo 2005, sekta ya kilimo imechangia asilimia 29 tu. Mchango wa Kilimo umepungua kwa asilimia 17.1! Ikiwa takwimu mpya za pato la taifa ni sahihi, basi mipango yote ya serikali ya kukuza uchumi kwa ujumla na kisekta, haina maana kwani imejikita katika takwimu ambazo hazielezi hali halisi ya uchumi wetu.
23. Mheshimiwa Spika, Waziri ameeleza kuwa takwimu za pato la taifa za sasa zimezingatia taarifa mpya kama zile zilizotolewa na utafiti wa bajeti ya kaya (Household Budget Survey) ya mwaka 2000/01. Tathmini hii ya mapato na matumizi ya kaya inaonyesha kuwa asilimia 84.2 ya nguvu kazi ya Tanzania inaajiriwa katika sekta ya kilimo. Kwa takwimu za zamani, nguvu kazi hii ilichangia asilimia 44.7 ya pato la taifa. Kwa takwimu mpya kilimo na uvuvi vimechangia asilimia 30.7 tu mwaka 2001. Ikiwa mchango wa sekta ya kilimo ni mdogo kiasi hicho wakati asilimia 84.2 ya nguvu kazi ya Tanzania iliajiriwa katika kilimo mwaka 2001.Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali ikiri kuwa umaskini vijijini ni wa kutisha zaidi kuliko ilivyokadiriwa mwaka 2001.
24. Mheshimiwa Spika, Mtanzania wa kawaida haamini kuwa uchumi unakua kwa sababu haoni matunda ya kukua uchumi. Waheshimiwa Wabunge ambao ndio wawakilishi wa wananchi na wako karibu nao, wanapata shida kupata picha halisi ya ukuaji huu kwa sababu maisha ya Mtanzania wa kawaida yameendelea kuwa duni siku hadi siku.
25. Mheshimiwa Spika, Ripoti ya Umaskini na Maendeleo ya Watu ya 2007 imebaini kuwa Watanzania wengi wanaona kuwa maisha yao yanazidi kuporomoka siku hadi siku. Wananchi wengi hawaamini kuwa uchumi unakua na maisha ya mwananchi wa kawaida yanaboreka. Wananchi wengi wanaamini kuwa misaada ya nje inawanufaisha wakubwa wa Serikali huku wafanyakazi na wakulima wakiwa wanaambulia patupu.
26. Mheshimiwa Spika, Wananchi vijijni wanalalamika kuhusu hali mbaya ya barabara, ukosefu wa maji safi na salama na gharama kubwa za huduma za afya. Ahadi ya Serikali kuwa watoto na wazee wa miaka 60 na zaidi watapata huduma za afya bure katika zahanati na hospitali za Serikali haitekelezwi na wala haitekelezeki kutokana na ukosefu wa mipango madhubuti.
27. Mheshimiwa Spika, kuna udhaifu mkubwa katika ukusanyaji wa takwimu za pato la taifa. Katika Jumuia ya kimataifa Tanzania ni maarufu kwa kutokuwa na takwimu za uhakika. Wafanyakazi na wataalam katika Taasisi ya Taifa ya Takwimu wana motisha zaidi wa kukusanya takwimu za miradi maalum inayofadhiliwa toka nje kama vile tathmini ya bajeti za kaya kwa sababu ina posho na marupurupu mengi.(Hizi ni takwimu za World Development indicators 2007).
28. Mheshimiwa Spika, Shughuli za kila siku kama vile kuandaa Takwimu za pato la taifa hazipewi kipaumbele kwani hazina posho na magari ya mradi. Mipango yetu ya kukuza uchumi ni dhaifu kwa kutokuwa na takwimu sahihi.
29. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inapendekeza kuundwa Jopo la Wataalam wa ndani na nje kutathmini usahihi wa takwimu mpya za pato la taifa na kupendekeza taratibu za kuboresha ukusanyaji wa takwimu hizo.

UTEKELEZAJI WA BAJETI YA 2007/2008.

30. Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha mbele ya Bunge lako Tukufu tathmini ya Kambi ya Upinzani kwa ufupi juu ya utekelezaji wa Bajeti ya Serikali ya mwaka 2007/2008, na baadaye nieleze misingi na shabaha ambayo kama Serikali ingalizingatia Mapato na Matumizi ya Serikali ya mwaka 2008/2009 yangaliboreka zaidi.

31. Mheshimiwa Spika, Waziri wa Fedha na Uchumi amelieleza Bunge lako tukufu kuwa na ninanukuu “kwa ujumla, bajeti ya mwaka 2007/08 imetekelezwa kwa msingi wa sera mbalimbali zilizotangazwa wakati wa kuwasilisha bajeti hiyo Bungeni mwezi Juni 2007. Mapato ya kodi yanakusanywa kama yalivyolengwa, na matarajio ni kwamba tutafikia malengo ya makusanyo ya mwaka mzima wa 2007/08 bila wasiwasi. Mheshimiwa Spika, Matumizi ya Serikali yanaendelea kulingana na bajeti na inatarajiwa kwamba bajeti ya 2007/08 itakuwa imetekelezwa kama ilivyoidhinishwa na Bunge.” Mwisho wa kunukuu
32. Mheshimiwa Spika, Waziri pia aliwasilisha taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa katika mwaka 2007. Nawaomba Wabunge watazame Jedwali namba 26 katika ukurasa wa 75 na 76 linaloonyesha mgawanyo wa matumizi yote ya serikali katika huduma na sekta mbalimbali. Jedwali hili ndiyo taarifa pekee inayotolewa na serikali kuhusu magawanyo wa matumizi halisi.
33. Mheshimiwa Spika, Waziri ameeleza kuwa maeneo makuu ya kipaumbele katika matumizi ya serikali ni Elimu, Afya, Kilimo, Miundombinu , maji na Nishati. Sekta zote hizo zimetengewa fedha nyingi zaidi katika mwaka 2008/09 ukilinganisha na mwaka 2007/08, isipokuwa sekta ya maji.
34. Mheshimiwa Spika,hata hivyo ongezeko la bajeti ya sekta hizi ni ya maneno tu kwani matumizi haya hayatekelezwi kwa vitendo. Katika mwaka 2007/08, Sekta ya Elimu ilitengewa Shilingi trilioni 1.086.0, Miundombinu ilitengewa shilingi bilioni 777.2, Sekta ya afya ilitengewa shilingi bilioni 589.9, Sekta ya Kilimo ilitengewa shilingi bilioni 379.0, Sekta ya Maji ilitengewa shilingi bilioni 354.0.
35. Mheshimiwa Spika, matumizi halisi ya sekta hizi katika mwaka 2007/08 kama yalivyochambuliwa katika Hali ya Uchumi wa Taifa Jedwali na. 26, Elimu imetumia Shilingi bilioni 552.7 sawa na asilimia 51 tu ya fedha zilizotengwa. Sekta ya Ujenzi imetumia Shillingi bilioni 596.3 ikilinganishwa na shilingi bilioni 777.2 zilizotengwa kwa sekta ya Miundombinu ya barabara peke yake sawa na asilimia 76.7. Sekta ya Afya imetumia shilingi bilioni 373.9 ikilinganishwa na shilingi bilioni 589.9 zilizotengwa sawa na asilimia 63.4. Sekta ya Kilimo imetumia shilingi bilioni 151.4 ikilinganishwa na shilingi bilioni 379 zilizotengwa sawa na asilimia 39.9. Sekta ya Maji imetumia shilingi bilioni 208.3 ikilinganishwa na shilingi bilioni 309.1 zilizotengwa sawa na asilimia 67.4.
36. Mheshimiwa Spika, kwa takwimu za Hali ya Uchumi wa Taifa mwaka 2007, Sekta zimekadiriwa kutumia kama ifuatavyo, elimu asilimia 9.1 badala ya asilimia 18 zilizotengwa katika bajeti, sekta ya afya imetumia asilimia 6.2 badala ya asilimia 9.7 na sekta ya kilimo asilimia 2.5 badala ya asilimia 6.2 ya bajeti yote ya mwaka 2007/08.
37. Kwa utaratibu huu Mheshimiwa Spika, pamoja na bunge lako tukufu kuonekana linasimamia kidete matumizi ya Seriakali lakini bado serikali inatumia fedha za wananchi maskini wa Tanzania bila umakini. Serikali imeandaa makadirio ya bajeti na Bunge likayapitisha kama yalivyoletwa lakini haiheshimu bajeti yake yenyewe. Sekta zilizopewa kipaumbele zinatumia nusu mpaka theluthi mbili tu ya fedha zilizotengwa katika bajeti.
38. Mheshimiwa Spika, utaratibu wa Serikali wa kutumia kulingana na mapato yaliyoko (cash budget) unafanya zoezi la kutayarisha bajeti kuwa la mzaha kwani haiongozi matumizi ya serikali, matokeo yake shule za sekondari za serikali za bweni (boarding ) zinafungwa kwa kukosa chakula, zahanati na hospitali hazina dawa na wakulima hawapati mbolea na huduma za ugani.
39. Mheshimiwa Spika, tunawadanganya Watanzania kuwaeleza kuwa tumeongeza bajeti ya Elimu, Afya, Kilimo na Miundombinu ya barabara ikiwa bajeti haiongozi matumizi ya serikali.
40. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inataka ili kuliwezesha Bunge lako liweze kuisimamia serikali katika utekelezaji wa bajeti, Waziri wa Fedha na Mipango atupe taarifa kamili ya makadirio yaliyoidhinishwa na matumizi halisi ya kifungu kwa kifungu ya mwaka wa fedha 2005/06, 2006/07 na 2007/08 ili tuweze kuhakiki kwa kiasi gani matumizi yanayopitishwa na Bunge lako ndiyo yanayoiongoza serikali katika utendaji wake wa kazi. Kupata taarifa ya matumizi kwa kifungu ni kazi rahisi kwa kuwa matumizi na mapato ya serikali yanatumia teknolojia ya habari na mawasiliano.
41. Mheshimiwa Spika, Katika Bajeti ya mwaka 2007/2008 Serikali ilipanga kutumia jumla ya Tshs. 6.066 trillion na 2008/2009 Tshs.7.216 trilion. Ongezeko la Tshs. 1.150trilion. Aidha Serikali mwaka huu imepanga kupunguza utegemezi kutoka aslimia 42% ya mwaka jana na kuwa asilimia 34% punguzo la asilimia 8%. Kambi ya Upinzani mwaka jana ilipendekeza punguzo la kutoka asilimia 42% hadi 31.8% .Tunasisitiza malengo ya kufikia 31.8% bado yafikiwe kwa uhai wa Taifa letu.
42. Mheshimiwa Spika, Ili tupunguze umaskini vijijini kilimo kinastahiki kikue kwa wastani wa asilimia 6 – 8 kwa mwaka katika kipindi cha mpito. Kilimo chetu bado kinatumia zana duni na kutegemea mvua. Wakulima wadogo ndio tegemeo la kilimo cha Tanzania lakini hawajasaidiwa kuboresha kilimo chao. Wakulima wadogo wa China na Vietnam wenye wastani wa mashamba chini ya hekta moja ndio wanaotegemewa katika sekta ya kilimo kwa kuwa wakulima hawa wamejengewa mazingira mazuri na serikali ya kupata mbolea, mbegu bora, utaalam, miundo mbinu ya umwagiliaji maji na barabara bora za vijiji zinasaidia kufikia masoko.
43. Mheshimiwa Spika, Pamoja na MKUKUTA kuweka lengo la kukuza sekta ya Kilimo hadi kufikia asilimia 10 kwa mwaka na Ilani ya Uchaguzi ya CCM kueleza kuwa kilimo kitakuwa kwa asilimia 20, ukuaji wa kilimo kati ya mwaka 2000 – 2006 ulikuwa wastani wa asilimia 4.5. Malengo yaliyomo ndani ya ILANI ya Uchaguzi ya CCM yalikuwa ni ya kisiasa tuu.
44. Mheshimiwa Spika, hakuna nchi ambayo imefanikiwa kukuza kilimo kwa asilimia 20. Kwa kawaida kilimo ndicho kinachokuwa kwa kasi ndogo kuliko sekta nyingine kama vile Viwanda, mawasiliano na huduma za biashara. Ikiwa sekta ya kilimo itakua kwa asilimia 20, pato la taifa litakua kwa zaidi ya asilimia 20. Baadhi ya malengo ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ni ya kusadikika, hayawezi kufikiwa na kwa hiyo hayawezi kuongoza uandaaji wa mipango ya uchumi na bajeti ya nchi nitatoa kasoro kadhaa ya kasoro hii.
45. Mheshimiwa Spika serikali ya awamu ya nne iliahidi kutoa kipaumbele katika suala la kilimo cha umwagiliaji maji kwa kuchimba mabwawa ya umwagiliaji maji 160, wastani wa mabwawa 32 kila mwaka. Hali ya uchumi wa taifa haielezi mabwawa yeyote yaliyochimbwa kwa sababu hakuna lililofanyika.
46. Mheshimiwa Spika serikali ya awamu ya nne iliahidi kuwa itaongeza uzalishaji wa korosho toka tani 90,000 kufikia tani 180,000 mwaka 2010. Uzalishaji wa korosho umepungua toka tani 122,287 msimu wa mwaka 2000/01 na kufikia tani 90741 mwaka 2005/06. Kufuatana na Ilani ya CCM uzalishaji wa kahawa unategemewa kuongezeka kufikia tani 120,000 mwaka 2010. Uzalishaji wa kahawa umepungua toka tani 76,428 msimu wa mwaka 2002/03 na kufikia tani 54838 mwaka 2006/07. Ni wazi malengo ya serikali ya awamu ya nne hayatafikiwa kwa sababu hakuna sera sahihi za kilimo na wala hayakuwekewa mpango mkakati wa utekelezaji.

MFUMO WA BAJETI.
47. Mheshimiwa Spika, mfumo wetu wa bajeti bado hauko wazi kiasi cha Wabunge kushindwa kufuatilia kwa undani vifungu vya mapato na matumizi. Wakati Waziri akiwasilisha mtazamo wa bajeti kwenye Kamati ya Fedha na Uchumi, tatizo hili lilijitokeza.Hatuwezi kufuatilia na kujua fungu linaloitwa (Other Charges) ‘O/C’ na ‘Employment Allowance’ lina vifungu vingapi vidogo vidogo. Aidha baadhi ya Wizara kama Elimu, Kilimo na Afya, Fedha zao zinatoka katika mikondo zaidi ya minne, hivyo wahasibu,hasa wa Halmashauri wanashindwa kufuatilia kwa undani fedha zinazoingizwa katika Halmashauri zao hasa kutokana na Halmashauri moja kuwa na Akaunti za Benki zaidi ya mia tano (500 Bank Accounts) huku tukielewa uwezo wa kiutendaji wa Halmashauri zetu. Ni dhahiri kuwa mapato mengi ya Serikali yanazinufaisha zaidi Benki za Biashara kwa kuzifanyia biashara ya kununulia hati fungani (T.Bills) na amana zafedha za Serikali huku Halmashauri zikishindwa kutimiza majukumu yake. Haya tuliyasema mwaka jana, Kamati zimeyasema, Kambi ya Upinzani inaitaka serikali kurekebisha kasoro hizi mara moja.
48. Mhe Spika, utaratibu huu unasababisha kujirudia (double accounting) kwa mapato na matumizi. Kambi ya upinzani inaona haya ni mapungufu makubwa. Mhe. Spika, Hapa kwetu mafungu ya Bajeti yanachukuliwa kwa ujumla jumla tu, hivyo kuwafanya Wabunge kutokufahamu kwa kina matumizi ya mafungu hayo. Hii ni tofauti na nchi nyingine nyingi kama Zambia, Mauritius, Uganda na India kutaja chache tu, zinazofuata mfumo kama wa kwetu wa CPA ambapo hata Mshahara wa Rais unaonyeshwa, Ziara za Rais, kwa mwaka zinajulikana. Aidha ziara zote za Mawaziri, Wabunge na Watumishi wote zinaorodheshwa na hivyo kuifanya kazi ya Wabunge ya kuisimamia Serikali kuwa rahisi lakini pia kuondoa mianya yote ya matumizi hewa. Kambi ya upinzani inaona haya ni mapungufu makubwa yanayohitaji kurekebishwa mara moja, kwani uwezekano wa kuwa na matumizi mabaya na au ubadhirifu na wizi wa mapato ni mkubwa.
49. Mhe.Spika, bado Serikali inakusudia kutumia zaidi katika matumizi ya kawaida (shs.4.726 trillion) kuliko matumizi ya maendeleo (shs.2.489 trillion.) zaidi ya hapo katika miaka 12 ya bajeti za nyuma, matumizi halisi ya maendeleo yamekuwa madogo kuliko yalivyoidhinishwa katika bajeti. Hii ni kama tulivyo wahi kusema kuwa ukubwa wa Serikali utasababisha matumizi makubwa ya kawaida. Kambi ya Upinzani inaona kuna kasoro kubwa ya kiuwiano kati ya matumizi ya kawaida na yale ya maendeleo, hivyo kuchelewesha ukuaji wa uchumi na kupunguza umasikini. Fedha nyingi zinatumika katika uendeshaji wa Serikali kuliko katika maendeleo na huduma za jamii na hivyo kupanda kwa pato la Taifa kutokuwa na manufaa ya moja kwa moja kwa mwananchi wa kawaida.
50. Mhe. Spika, Kutokana na taarifa ya Makaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG) katika Wizara na Idara za Serikali tulizochambua mathalani tumebaini kuna upungufu wa makusanyo ya mapato, mrahaba usiokusanywsa kutoka kampuni ya almasi ya Williamson diamond Ltd ni shilingi 841,137,251. ,Tansort, Tsh.206,662,556. Aidha, misamaha ya Kodi nayo imekuwa ya kutisha, kwani hadi kufikia mwezi huu wa Juni2008,kiasi cha Tshs.819.9 billion zilikuwa zimesamehewa kama kodi huku misamaha hii mingi ukiondoa ya mashirika ya dini ikiwa haijamnufaisha mwananchi masikini. Hiki ni kiasi kikubwa kwa nchi inayoomba misaada kila kukicha. Kambi ya Upinzani inaona huu ni upungufu mkubwa wa mapato ya wanyonge wa Watanzania kwa kuyatupa bila utaratibu wa wazi na unaoeleweka.
51. Mheshimiwa Spika, tunaomba kumalizia tathmini yetu kwa kukumbusha kwamba Kambi ya Upinzani mwaka jana ilikataliwa ombi lake la kuunda Kamati ya Bunge kuchunguza EPA, Twin tower, Mwananchi Gold Mine na Meremeta.
Kambi ya Upinzani, inamtaka waziri tena kutoa ufafanuzi, kuhusu mambo yafuatayo:-
(i) Waziri alieleze Bunge lako Tukufu thamani halisi ya gharama za ujenzi wa majengo ya Benki Kuu (Twin Tower) ambayo kwa taarifa ya Benki Kuu gharama imeshazidi USD500 million au wastani wa Tshs. 600 billion. na mjenzi bado hajakabidhi rasmi majengo pamoja na kwamba lilifunguliwa na Rais Mstaafu Mkapa mwaka 2005 kabla ya kustaafu. Aidha kuna wasiwasi kuwa matumizi haya pia yalisabababisha mfumuko wa bei. Tunataka maelezo. Pia tunamtaka atupatie taarifa ya uchunguzi iliofanywa na Benki Kuu yenyewe ili tuweza kulinganisha na taarifa tulizo nazo.
(ii) Bunge lililopita tuliomba Bunge lako Tukufu lipewe maelezo juu ya uwekezaji wa BOT katika Mwananchi Gold Mine wa Dola za Marekani 5,512,398.55 hadi tarehe 30 June, 2006, kwamba je BOT iliendelea kuwekeza katika kampuni hiyo binafsi na kiasi gani cha mapato yaliopatikana hadi sasa? Tunataka Serikali itupatie maelezo ya kina ambayo tuna tumaini yatakuwa tofauti na ya mwaka jana, yatakuwa si majibu ya kisiasa.
(iii) Katika kikao cha bajeti cha 2006/07 Bunge lilielezwa kuwa ule Mradi ulioasisiwa na Marehemu Baba wa Taifa wa kuwapatia wanajeshi wetu fedha kwa ajili ya kuendeshea mradi wa Nyumbu, Meremeta Gold Co. ambayo ilikuwa chini ya uongozi wa Time Mining ya South Africa, na kudhaminiwa na BOT kwa USD100million, iko katika hatari ya kufilisika, lakini tukaambiwa kuwa BOT ilikuwa ikifanya tathmini.. Kambi ya Upinzani inataka kupata taarifa ya kina kuhusu tathmini iliofanywa na BOT juu ya mradi huo .Aidha tunataka kupatiwa taarifa rasmi juu ya umiliki wa mgodi huu sasa.

(iv) Kuhusu EPA, tumeambiwa kuwa Serikali itatoa taarifa rasmi Bungeni. Mheshimiwa Spika tunasubiri kwa hamu taarifa ya Serikali katika mkutano huu wa Bunge.
(v) (a) Katika Kamati tuliomba kupewa taarifa juu ya JFC, Waziri katika majibu yake (mwaka jana 2007/2008) kwa kamati(uk2.) alijibu “wakati uamuzi kuhusu mapendekezo ya Tume unasubiriwa,bajeti ya 2007/08 imetenga mgao wa Zanzibar kwa utaratibu wa asilimia 4.5 ya misaada ya kibajeti” . Mwaka huu Waziri katika hotuba yake Uk. wa 20 amesema .....”Tume ya Pamoja ya Fedha inachambua maeneo ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi ya ziada ili kuziwezesha Serikali hizo mbili kufikia maamuzi kuhusu mapendekezo ya Tume” mwisho wa kunukuu..

(b) Mheshimiwa Spika. Wakati Bunge lako likipitisha msaada wa Sheria ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu, Mh.Nimrod Mkono (Mb) aliomba ufafanuzi juu ya mipaka ya kutumika kwa sheria hii na kusema kuwa Zanzibar inapata Fedha kutoka Serikali ya Jamhuri, lakini CAG hawezi kuzikagua. Waziri katika majibu yake alikubaliana na hoja ya mapungufu ya sheria na Katiba.

(c) Mhe.Spika kwanza Serikali ikubali kuwa yenyewe ndio iliosababisha matataizo haya kutokana na Kuvunjwa kwa Katiba pale miaka yote ilipochelewa kuanzisha Tume ya Pamoja ya Fedha na baada ya kuanzishwa kushindwa kwa Tume hiyo hadi Mwenyekiti wake amemaliza muda wake bila kutekeleza mapendekezo ya Tume. Pili sio kweli kwamba Zanzibar inafadhiliwa na SMT, bali inapewa kidogo kuliko haki stahili ambayo ingepata kama ingelikusanya kodi zake yenyewe, kuomba misaada na kukopa bila ya kupitia Serikali ya Jamhuri na hatimae kuchangia katika mfuko wa Pamoja wa Muungano kama Katiba mbili zinavyoelekeza katika Katiba Ibara ya 135(1) na 136(1). Ushahidi wa hayo Mhe.Spika, ni pale SMZ ilipotoa bila ya malipo MIG 7 za kivita, mizinga ya masafa marefu na mifupi kadhaa, magari ya TATA, fedha Taslim USD 15 million ambazo hazikulipwa hadi leo n.k. Hatuna haja ya kusema mengi, tatizo ni kutokutekelezwa Katiba juu ya tafsiri sahihi ya mchango wa Mfuko wa Pamoja wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano.Wachangiaji ni nani kwenye mfuko huo?

(d) Kambi ya Upinzani mara hii inataka kupata tarehe ya kuanza mfuko huu, hatuko tayari kuendelea kushiriki kuvunja Katiba ya Nchi.

52. Mhe. Spika, wakati tukiwasilisha maoni ya Kambi ya Upinzani katika Bajeti ya 2004/2005/2006/2007 na 2007/2008 tuliulizia juu ya kukiukwa kwa utaratibu wa kumpata mzabuni wa kuchunguza mauzo ya dhahabu unaofanywa na kampuni ya Alex Stuart Asseyers, Mwaka huu tulitegemea Serikali ingelisema ni kiasi gani cha mapato kimepatikana kutokana na taarifa ya Alex Stuwart Asseyers baada ya Serikali kuilipa kampuni hiyo si chini ya USD 65,000,000/- sawa na Tshs. Billion 85 inayotokana na mapato ya mrahaba wa 1.9% kati ya 3% inayopata Serikali kiasi ambacho kingeweza kukopesha wanafunzi 20,000 wa Vyuo Vikuu ambao leo tunawataka walipe kwa viwango mbalimbali na kutokana na umasikini uliokithiri hivi sasa vijana wetu wengi wanashindwa kulipa wakati raslimali zao zinatolewa “sadaka.”
53. Mhe. Spika, Kambi ya Upinzani na Watanzania kwa ujumla tunaona haya ni mapungufu makubwa katika matumizi ya rasilimali na zaidi pale Serikali inaposhindwa kueleza Bunge lako Tukufu mapato yaliyopatikana kutokana na kazi ya Alex Stuwart Asseyers. Badala yake Serikali imeunda Kamati ya Bomani ambayo ni ya sita katika miaka mitano (5yrs) kuhusu jambo hilo hilo moja. Je? huu ni usanii au nini , Mheshimiwa Spika ?

54. Mhe. Spika, Katika Hotuba ya Bajeti ya mwaka jana 2007/08 (uk.59) Serikali ilikusudia “kuanzisha utaratibu wa kupitisha moja kwa moja (fast tracking) bila ukaguzi bidhaa zote zinazoagizwa…” Mhe.Spika, utaratibu huu ni mzuri kama upo uadilifu wa kutosha wa walipa kodi na wakusanyaji wa kodi. Mhe.Spika, Serikali ilipoona kuna udhaifu katika utekendaji Bandarini, iliamua kukodisha shughuli za bandari kwa makampuni mbali mbali. Kambi ya Upinzani ilitegemea Serikali kuja na tathmini ya utekelezaji wa makampuni hayo ili iwe rahisi kwa Bunge lako tukufu kuamua, juu ya utaratibu uliopendekezwa na Serikali kama usimamiwe na TRA au kampuni binafsi, kwani kuna mashaka kwamba makampuni yaliyoko bandarini yameshindwa kufanya kazi zao kama ilivyotakiwa.
55. Mhe. Spika utaratibu wa fast tracking unaweza kutumiwa kuficha udhaifu wa makampuni yaliyopewa kutekeleza shughuli za bandari. Aidha, utaratibu huu unaweza kuwa njia moja ya kuipunguzia mapato Serikali. Kambi ya Upinzani, inamtaka Waziri atupe tathmini ya mpango huu kwa kungalia makusanyo ya kodi kwa walipa kodi hao hao wakati walipokuwa wakikaguliwa na sasa ambapo hawakaguliwi Bandarini.
56. Mheshimiwa Spika, Inaeleweka kuwa sehemu kubwa ya mapato ya bidhaa zinazoagiziwa kutoka nje zinatokana na bidhaa za Petroli na Mafuta. Serikali imeweka viwango vya kodi katika mafuta vya juu hivyo kufanya gharama za usafiri wa abiria na bidhaa kuwa kubwa na kumuongezea mzigo Mtanzania anayeishi kijijini na kuyafanya maisha yake kuwa magumu zaidi. Kwa mfano kodi zote kwa jumla katika Petroli ni Tshs 545.10 kwa lita na kwa dizeli Tshs. 520.80 kwa lita. (Bei za mafuta ya dizeli kwa makao makuu ya mikao kwa tarehe 16-31 Mei 2008 ilikuwa kama ifuatavyo kwenye baadhi ya mikoa, Dar es salaam 1,654.09 petrol na 1,884.89 kwa dizeli kwa lita huku mafuta ya taa yakiwa 1,488.24 kwa lita, Kagera 1,748.93 petrol na 1,979.73 kwa dizeli kwa lita huku mafuta ya taa yakiwa 1,583.08 kwa lita, Kigoma 1,930 petrol na 2,080 dizeli kwa lita huku mafuta ya taa 1,550 kwa lita na hali katika mkoa wa Mbeya 1,850 petrol na 2,000 dizeli kwa lita huku mafuta ya taa 1,500 kwa lita) . kati ya wastani wa bei ya 1800/- kwa lita. Hizi ni bei za mijiji, vijijini ambako kuna umasikini uliokithiri na mahitaji ya nishati kwa ajili ya usafiri,kilimo n.k. wastani wa bei ni Tshs.2,200 kwa lita.
57. Hivyo hivyo kwa bei za bidhaa nyengine kama cement,mabati n.k.jee umasikini utapungua wakati sehemu kubwa ya jamii inaishi vijijini. Mhe.Spika,Nchi kama India bei za vijijini na mijini nitafauti na ndio maana wamemudu kuzalisha chakula cha kutosha.Ili kuendana na dhana nzima ya kukua kwa uchumi na kupunguza umasikini,na kutekeleza programu nzima ya Mkukuta na uzalishaji kuna haja ya kufidia bei za bidhaa maalum vijijini.. Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali iondoe misamaha ya kodi kwa mafuta wanayotumia wazalishaji wa makampuni ya maadini katika migodi mikubwa na ya kati , na mapato yatakayopatikana yaanzishiwe mfuko maalum wa kutoa ruzuku kwa ajili ya nishati ya mafuta ili bei iwe sawa kwenye Mikoa yote (Price Stabilization).

BAJETI YA SERIKALI YA 2008/09.

58. Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza wakati ninachambua matumizi ya serikali ya mwaka wa bajeti 2007/08, matumizi halisi yaliyoainishwa katika hali ya Uchumi wa Taifa na bajeti iliyopitishwa na Bunge ni vitu viwili tofauti. Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Uchumi hakufanya uchambuzi wa matumizi halisi kisekta au kwa kila fungu. Mheshimiwa Spika, hatuna sababu ya kuamini kwamba katika bajeti hii matumizi yatafuata makadirio yatakayopitishwa na Bunge hasa ukizingatia kuwa serikali bado inasisitiza kuendelea na utaratibu wa cash budget wa “kutumia tulichonacho.”
59. Mheshimiwa Spika, tukizingatia umaskini wa Tanzania, umuhimu wa elimu na afya katika maendeleo na ujenzi wa nguvu kazi iliyo na tija, nafasi ya mapinduzi ya kilimo katika kuchochea kukua kwa uchumi, kuondokana na baa la njaa na kuutokomeza umaskini, na ulazima wa miundombinu hasa barabara na nishati katika kuiwezesha sekta binafsi kuwekeza na kuzalisha bidhaa na huduma, mfumo wa bajeti utakaokidhi mahitaji ya maendeleo ni kuitengea Elimu asilimia 22, Afya asilimia 11, Kilimo asilimia 12, Miundombinu asilimia 20, Maji 10, Nishati asilimia 8, na mambo mengine asilimia 17 ya bajeti ya serikali.
60. Mheshimiwa Spika, kwa wastani bajeti ya serikali itumie asilimia 25 ya pato la taifa. Asilimia 20 ya pato la taifa likusanywe kama kodi na mapato mengine ya ndani ya serikali, na asilimia 5 ya pato la taifa itokane na misaada. Kwa kuanzia ikiwa misaada toka nje itakuwa mikubwa bajeti ya miundombinu iongezwe ili kuongeza kasi ya kukua kwa uchumi. Uchumi unavyokua mapato ya serikali yataongezeka na kutegemea misaada ya nje kutapungua. Matumizi ya serikali hayafuati mwongozo huu.
61. Mheshimiwa Spika, Waziri wa Fedha na Uchumi kaeleza kuwa “mapato ya ndani yamelengwa kufikia shilingi bilioni 4, 728.595 (trilioni 4.728) sawa na asilimia 18.5 ya Pato la Taifa (kwa takwimu za sasa). Hili ni ongezeko la asilimia 31 kutoka mapato yaliyotegemewa kukusanywa mwaka 2007/08.” Mapato ya kodi yanakadiriwa kuongezeka kwa asilimia 39 ukilinganisha na makadirio ya mwaka jana. Mheshimiwa Spika, Waziri hakufafanua maeneo yatakayoongeza mapato hayo. Ni vyema angalau Waziri akatueleza vianzio vya mapato haidhuru kwa mafungu makubwa kama vile kodi ya ongezeko la thamani (VAT), kodi ya ushuru wa forodha, kodi ya mauzo na excise duty, kodi na tozo ya mafuta, kodi ya mapato na kadhalika.
Mheshimiwa Spika ,Kambi ya Upinzani inamtaka Waziri atoe maelezo kwani hata kwenye “Finance Bill” nayo haifafanui vyanzo hivyo vya mapato ni vipi na hili linatutia wasiwasi kuwa Bunge halitaweza kujua vyanzo vya mapato kwa ajili ya Bajeti hii kama ilivyo kwenye Finance Bill 2008 vifungu vya 20,21,23,24,26 na vinginevyo,ambavyo havionyeshi kuwa vyanzo vya mapato hayo ni kitu gani .Badala yake vifungu hivyo vinampa Waziri mamlaka ya kuamua aina na tozo za Kodi kwenye mamlaka mbalimbali za Serikali bila hata kulitaarifu Bunge lako tukufu.
62. Mheshimiwa Spika, Ni vyema serikali ifanye utafiti wa kina kuhusu vianzio vya kodi na kutoza kodi ambazo hazitabadilika badilika kila mwaka. Kwa mfano mwaka jana serikali iliongeza kodi ya mafuta mazito ya mitambo (HFO) kutoka shilingi 109 kwa lita hadi shilingi 117 kwa lita. Mwaka huu imepunguza “kiwango cha Ushuru wa Bidhaa kwenye mafuta mazito ya HFO kutoka Shilingi 117 kwa lita hadi Shilingi 97 ili kupunguza gharama ya uzalishaji viwandani, na kuongeza uwezo wa ushindani wa bidhaa zetu katika soko.” Jee mwaka jana ilikuwa haijulikani umuhimu wa mafuta haya katika uzalishaji viwandani?
63. Mheshimiwa Spika, viwango vya ada za leseni za magari viliongezwa mwaka jana toka shilingi 20,000/- na kuwa na viwango vinavyoanzia shilingi 80,000/- hadi 230,000/- kwa mwaka. Hata hivyo Waziri alieleza kuwa “Kwa magari yenye ujazo wa injini unaozidi 5,000cc kiwango cha ada kitakuwa shilingi 100,000 kwa mwaka. Haya ni magari ya mizigo na mabasi ya abiria.” Mwaka huu Waziri anaeleza kuwa magari yenye ujazo wa injini unaozidi cc5000 yamepunguziwa kiwango cha ada kutoka shilingi 175,000 hadi shilingi 150,000. Ikiwa mwaka jana Waziri alilieleza Bunge kiwango cha ada kiwe shilingi 100000/-, mwaka huu anapendekeza kiwe shilingi 150,000/-. Je hili ni ongezeko au punguzo.?


MTAZAMO WA KAMBI YA UPINZANI JUU YA VIPAUMBELE VYA BAJETI;

Kupunguza Bajeti Tegemezi kutoka 34%-31.8%:

64.Mheshimiwa Spika, katika jambo hili kambi ya upinzani haina budi kuikumbusha serikali kile ambacho tulikisema kwenye bajeti ya mwaka 2007/2008 kuwa tuliweza kupunguza utegemezi wa bajeti hadi kufikia asilimia 31.8%, tunashukuru serikali kwa kufanyia kazi mapendekezo yetu japo haikuweza kufikia lengo tulilokuwa tumeliweka mwaka jana kwani serikali imeweza kupunguza utegemezi hadi kufikia asilimia 34 tuu kwa makadirio ya bajeti ya mwaka huu.
65. Mheshimiwa Spika, Katika mkutano uliopita wa Bajeti tulisema sana juu ya jambo hili la kutegemea wafadhili katika maendeleo yetu. Kambi ya Upinzani inaipongeza TRA kwa kukusanya mapato kwa kiwango marudufu kulingana na miaka iliyopita. Lakini pia tulisema kuwa uwezo wa Serikali kukusanya mapato ni mkubwa zaidi, ila kuna uzembe mkubwa na kutojali (laxity), ubadhirifu,na ufisadi kama inavyodhihirishwa na Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali mwaka hadi mwaka. Madhara ya Bajeti ya namna hii ni kwamba tunapopata matatizo inabidi kupita pita (realocation) na kupunguza matumizi kadhaa ili tu kuweka hali sawa ya madhara yaliotokea. Hii ni hatari kwa Maendeleo ya Watanzania kwa kiasi kikubwa kwani hata bajeti ya mwaka huu baadhi ya Wizara zilipunguziwa fedha bila mpangilio.

Vyanzo Vipya vya Mapato.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani katika kuinua uchumi wa nchi na mwananchi imeibua vyanzo vipya vya mapato na vile ambavyo mwakajana tulivisema na baadhi kufanyiwa kazi na serikali kwenye bajeti yake ya 2008/2009 na vingine imeshindwa kuvifanyia kazi.

a) Uvuvi katika Bahari Kuu;
66. Mheshimiwa Spika, Uvuvi katika Bahari Kuu ni moja ya maeneo ambayo kama Serikali ingelikuwa makini na kuchukua maamuzi tunayopendekeza,mapato ya Serikali yangeliongezeka marudufu bila kugusa mafuta. Meneo yenyewe ni kama yafuatayo:-

i. Kuongeza ada ya leseni kwa meli za nje zinazovua katika bahari kuu hadi kufikia USD 50, 000 kutoka, inayotozwa sasa ambayo ni USD18, 000 kwa mwaka. Kulingana na takwimu zilizopo ni kuwa kuna meli 140 (japo Kumbukumbu za Bunge-Kikao Cha tatu 5th.Feb.2004 Serikali ilisema kuwa imetoa leseni 193 za Meli za Uvuvi) za nje zilizopatiwa leseni za uvuvi katika bahari kuu ya Tanzania. Kwa maoni haya mapato ya yatakuwa Tshs 9.5bn. Ambayo sasa hayakusanywi.
ii. Kuongeza tozo la mrahaba wa mauzo la asilimia 10 katika bidhaa za Samaki zinazovuliwa katika Bahari Kuu. Kila meli kwa mwezi inavua wastani wa tani 2000 za samaki, kwa makisio ya chini sana, japo kwa kawaida wanavua Tani 1,500 kwa siku. Bei ya soko kwa kilo ya samaki ni USD2.5 . Kwa wanaojua biashara ya sekta hii, kiwango cha uvuvi ni kikubwa zaidi. Kwa maoni haya Mapato yatakuwa shs. 370 bn. ambayo sasa hayakusanywi na Serikali.
iii. Katika kuhakikisha kuwa sekta hii ya uvuvi inaleta mabadiliko ya kiuchumi kwa nchi na wananchi kwa ujumla Bandari ya Mtwara, Dar es Salaam,Tanga na Zanzibar inashauriwa zitenge maeneo ya bandari za samaki (Fish Ports and Fish Processing plants) ili meli zote za uvuvi wa bahari kuu zilazimike kununua mahitaji yao yote ya mafuta ,maji,chumvi na vyakula wanapo kuja kukaguliwa kwa ajili ya kukusanya mapato. (Vyombo vyetu vya ulinzi,vikishirikiana na TRA na Mamlaka ya Uvuvi kudhibiti mapato haya) Kwa uamuzi huu mapato yatakuwa Tshs.3bn. ambayo nayo sasa hayakusanywi na Serikali;
iv. Uvuvi katika maziwa ya Lake Victoria na Tanganyika, haujadhibitiwa vizuri. Hivi sasa kuna uvunaji haramu wa wastani wa Tani 36,000 kwa mwaka,kama uvunaji huu haramu ukidhibitiwa Serikali inaweza kujipatia kiasi cha shilingi 45 bn kwa mwaka .Pia uvunaji huu haramu katika maziwa hayo matokeo yake viwanda vyetu vinakosa mali ghafi.Tunataka hatua ya dharura kuikabili hali hii kwa kutumia vyombo vya ulinzi na TRA ili kuongeza mapato na ajira. Zoezi hili litaongeza wingi wa samaki hivyo viwanda vya samaki vitaongeza uzalishaji na kodi itaongezeka. . Serikali imeshindwa kushughulikia jambo hili hadi leo.

67. Mhe. Spika, Maoni haya Kambi ya Upinzani sio tu yamepanua wigo wa kodi, lakini pia kwa hatua hizo tutakuwa tumedhibiti uvunaji wa raslimali zetu ambapo sasa hazivunwi kikamilifu.

b) Mapato yanayotokana na Misitu;

68. Mheshimiwa Spika, Chanzo kingine kikubwa ambacho vile vile mapato yake hayakusanywi sasa na Serikali katika sekta ya maliasili na hasa bidhaa za magogo na mbao. Kutokana na ripoti za kiutafiti kutoka kwa kundi la wahisani na pia asasi kadhaa zisizo za kiserikali, (Kama TRAFFIC) (2005/2006) Serikali ilikusanya asilimia 4 tu ya mapato kwa mwaka 2004 yaliyopaswa kukusanywa kutoka katika bidhaa za magogo na mbao. Wanunuzi wakubwa ni China, India na Japan. Katika utafiti huo, katika kipindi cha 2001/2005 China peke yake ilinunua Cu.mita 18,316 x $150 kwa rekodi za Maliasili Tanzania kwa bei ya wastani wa USD2.7m. sawa na Tshs. 3.5bl. na CU.mita 108,605 kwa rekodi za Forodha za China, kwa maana hiyo ama kwa ufisadi au vyenginevyo Serikali imekosa mapato ya Cu.mita 90,289 x $450 = $40.6m. sawa na Tshs.52.8bn. utafiti huu ulihusu Magogo na mbao zinazotoka Mikoa ya Kusini tu. Taarifa hii inathibitisha Taifa lilikoseshwa fedha kwa kuuza kwa Dola 150 tu wakati bei halisi China ilikuwa Dola 450. Pia kiwango kilichouzwa kimefichwa. Huu ni Ufisadi.
Mheshimiwa Spika ,Kambi ya Upinzani inataka majibu ya timu ya aliyekuwa Waziri wa utalii na maliasili aliyosema kuwa ataituma China kwenda kuchunguza jambo hili ndani ya wiki mbili ila hadi leo hatuna majibu ya timu hiyo. Pia bajeti ya Waziri haionyeshi kama kuna mapato yeyote yatakayopatikana kutokana na chanzo hiki.
69. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inashauri hatua zifuatazo zichukuliwe:-

i. Halmashauri za Wilaya zilizo katika maeneo ambayo bidhaa hizi zinapatikana ziwe mawakala wa kukusanya mapato kutokana na bidhaa za maliasili. Uamuzi huu utapunguza kwa kiasi kikubwa ufisadi uliopo sasa katika Wizara ya Maliasili. Kila Halmashauri inayokusanya kodi ipatiwe gawio kutoka sehemu ya makusanyo;
ii. Mapato yote yakusanywe na TRA kwa kutumia stakabadhi za TRA kupitia Halmashauri za Wilaya kama ilivyo elezwa hapo juu;
iii. Mtu yeyote atakayekamatwa kwa kutorosha maliasili afilisiwa kwa mujibu wa sheria kama haipo itungwe;
iv. TRA mbali na kukusanya mapato ishirikiane na Bodi ya Mauzo ya Nje kuhakiki bei za Bidhaa zetu zinazouzwa nje ili kupata mapato halali ya Rasilimali zetu.
70. Mhe. Spika, Kwa hatua hizi mapato ya maliasili misitu yataongezeka kwa asilimia 90 ya mapato ya sasa, makusanyo halisi yatakuwa Tshs 100bn ambazo hazikusanywi sasa.

C) Mapato yatokanayo na Utalii:
71. Mhe. Spika, Serikali inaona kuwa inakusanya mapato kwa wingi hadi kufikia asilimia 16.8% ya pato la Taifa katika Sekta hii. Hata hivyo, Serikali imeshindwa kufikia malengo ya watalii milioni moja kwa mwaka kama ilivyokuwa imepanga. Idadi ya watalii wanaokuja nchini ni wastani wa laki saba (719,031). Isitoshe, Serikali imekuwa ikipoteza mapato kutokana na watalii kulipia gharama za safari zao na baadhi ya huduma kwa Tour Operator huko huko kwao kwa wastani wa USD200-300 kwa mtu mmoja kwa siku. Mtalii anapo fika Tanzania ,huwa analipa wastani wa USD80-150 tu. Hivyo kuzipunguzia mapato hoteli zetu na kwa maana hiyo na Serikali.Kama watalii hawa wangelikua wanakuja katika “Packege Tour” na kuwa tunakusanya wastani wa USD100 kwa siku kwa kila mmoja kwa muda wa siku 7, ukiacha mapato yasio ya moja kwa moja,katika eneo hili Serikali ingelikusanya kama kodi ya mapato 30% sawa ma Tshs 67.5bn ambazo hazikusanywi hivi sasa.


d) Mapato yatokanayo na Uwindaji:

72. Mhe.Spika, Kwa mujibu wa takwimu za Maliasili, kuna vitalu 152. Kwa wakati huu Serikali inakodisha kwa wastani wa USD7500=kwa mwaka (mara nyingi wamiliki nao hukodisha kwa wenye fedha kwa wastani wa USD100,000.kwa mwaka) Ili kuongeza mapato ya Serikali, Kambi ya Upinzani inataka hatua zifuatazo zichukuliwe ili kuongeza mapato kama ifuatavyo :-
• Kuwajasirimisha Watanzania vitalu vyote vya uwindaji;
• Ili kupata thamani halisi washauriwe kuingiza Vitalu hivyo katika soko la mitaji kwa kutumia”eletronic commerce.”;
• Kupandisha viwango vya kodi ya Uwindaji;
• Kutoza asilimia 30% ya mapato yatokanayo na Mtanzania atakayekodisha kwa mtu mwingine.
Mheshimiwa Spika , Kambi ya Upinzani inaamini kuwa hatua hizi zinawezekana kwani Tanzania ni Nchi ambayo imejaliwa wanyama wengi zaidi kuliko Nchi nyingine za Bara la Afrika, wanyama wanene zaidi na ambao wanaishi kwenye mazingira halisia,na hivyo kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kipekee na hivyo kuwavutia wawindaji kutoka sehemu mbalimbali za Ulimwengu kutaka kuja na kuwekeza kwenye sekta ya uwindaji.
73. Kwa hatua hii Watanzania watakuwa wamewezeshwa kumiliki rasilimali zao wenyewe na pia kwa kuongeza viwango vya kodi ya uwindaji makusanyo yanakisiwa kuwa Tshs. 85bn ambayo hayakusanywi hivi sasa.

e). MAPATO KATIKA SEKTA YA MADINI;

74. Mheshimiwa Spika, Katika sekta ya madini, kwa kulingana na ukaguzi uliofanywa na Kampuni ya Alex Stuart, kwa kipindi cha miaka mitatu Serikali imepoteza shillingi 1.3 trillion. Na hii imetokana na Serikali kutokuwa makini katika kufuatilia nyaraka halali zinazotumiwa na makampuni ya kuchimba madini. Ili kuifanya sekta hii ya madini kuwa na manufaa kwa Taifa na Watanzania wote hatua zifuatazo zikichukuliwa sekta hii itachangia zaidi:-

i. Kufanya mapitio ya sheria ya madini na kupandisha asilimia ya mrahaba toka 3% hadi 5% kwa kuanzia;.
ii. TRA kuimarishwa kiutendaji na kukusanya kodi zote katika sekta ya madini;
iii. Katika mpango wa maendeleo wa kampuni husika, maendeleo ya jamii zinazozunguka migodi yaonekane wazi wazi na kuingizwa katika mpango wa mwekezaji;.
iv. Kati ya asilimia 5% za mrahaba utakaotozwa asilimia 2% ibaki katika Halmashauri ya Wilaya/Mji ambamo mgodi upo.
v. Katika masharti ya kuwekeza kwa wageni,ni lazima waingie ubia na Mtanzania au Halmshauri angalau kwa asilimia 10% ikiwa ni pamoja na thamani ya ardhi.
vi. Kuweka sharti ndani ya Mikataba na kubadilisha sheria kwamba atake kiuka mkataba au kusafirisha mali itokanayo na raslimali za nchi kampuni husika itafilisiwa;
vii. Kuhakiki madeni waliyokopa wawekezaji ili kupata kiasi halisi walichokopa, ikiwa ni pamoja na Tax Holiday kwa lengo la kufuatilia muda wa Kusamehewa Kodi.

75. Mheshimiwa Spika, Rais Kikwete aliunda Kamati ya kupitia Miktaba ya madini mwezi Novemba mwaka 2007 kufuatia Hoja Binafsi ya Buzwagi. Kamati imetoa mapendekezo swali la kujiuliza ni je?mapendekezo ya kamati yamezingatiwa vipi kwenye bajeti hii ya mwaka 2008/2009?
Kambi ya Upinzani inaitaka serikali kuiwasilisha ripoti hiyo ndani ya Bunge mapema iwezekanavyo .
76. Mheshimiwa Spika, kuna taarifa kuwa serikali imepoteza zaidi ya shilingi 883 bilioni katika kipindi cha miaka 10,kutokana na sheria mbaya ya kodi ya Mapato katika sekta ya madini iliyotungwa na Bunge mwaka 1997. Kupitia Financial Laws (misc. Ammendments) Act, 1997, nafuu ya ziada ya uwekezaji Asilimia 15 iliwekwa na kuleta upotevu huo wa mabilioni ya fedha za kodi. Sheria hii bado ipo katika sheria za nchi kwa kampuni zote zenye Mikataba (MDA) kabla ya mwaka 2001. Kambi ya upinzani Bungeni ilitarajia kuwa serikali ingefuta sheria hii na kuangalia uwezekano wa makampuni ya Madini kulipa fedha hizi kwani nafuu haikuwa na ulazima wowote na haimo katika kanuni za kodi.Kambi ya Upinzani inategemea kukusanya mapato haya kwa kiasi cha shilingi 88.3bn
77. Mheshimiwa Spika, Kambi ya upinzani inapendekeza kuwa msamaha wa Ushuru wa Bidhaa kwenye mafuta kwa Kampuni za madini ufutwe. Mwaka 2007/2008 Serikali kupitia msamaha huu haikukusanya sh 59bn kutoka kampuni sita za madini. Waziri wa fedha hajagusia kabisa msamaha huu ambao unalitafuna taifa, kulikosesha mapato na hivyo kupunguza faida ya ukuaji wa sekta ya madini katika uchumi. Kambi ya upinzani inataka kuwa msamaha wa kodi ya Ushuru wa Mafuta kwa kampuni za madini ufutwe mara moja. Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali iondoe misamaha ya kodi kwa mafuta wanayotumia wazalishaji wa makampuni ya madini katika migodi mikubwa na ya kati na kuanzisha mfuko maalumu wa kufidia punguzo la mafuta yanayopelekwa vijijini.
Aidha, Kambi ya Upinzani inaitaka serikali ilieleze Bunge lako tukufu pamoja na wananchi kwa ujumla juu ya hali ya uchimbaji wa madini mbalimbali katika machimbo ya KABANGA NIKEL yaliyoko Mkoani Kagera Wilaya ya Ngara na uhalali wa wachimbaji walioko kwenye eneo hilo.
78. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani Bungeni inaona kuwa serikali inafanya mzaha na umuhimu wa sekta ya madini katika mapato ya serikali na kwamba kitendo cha Waziri kutokuzungumzia chochote juu ya Mapendekezo ya kamati ya Rais na utekelezaji wake ni dalili tosha kuwa serikali inatilia maanani zaidi maslahi ya wawekezaji kuliko ya Watanzania. Serikali ituambie kwanini wawekezaji wa madini wanaogopwa?.


f).Mapato kutoka madini ya Vito.
79. Mheshimiwa Spika, Taarifa mbalimbali za kitafiti zinaonesha kuwa Tanzania inapoteza mapato mengi sana katika madini ya vito kwa sababu ya uzembe na ufisadi. Kwa mfano, Katika soko la dunia mauzo ya Tanzanite mwaka 2005 yalikuwa na thamani ya Dola za kimarekani 400m. Hata hivyo rekodi ya Tanzania ni Dola 16m tu.Tuna taarifa kuwa Kenya ilipata tuzo kwa kusafirisha Tanzanite nyingi duniani wakati hawana Tanzanite.
Kwa kutumia vito vyetu vya aina mablimbali kama vile Tanzanite,Alexadrite,Safaya,Ruby za aina zote n.k serikali ingeliweka usimamizi madhubuti tungeweza kulipatia taifa fedha kwa ajili ya kuendesha uchumi na kuwanufaisha wananchi wengi zaidi kuliko hali ilivyo hivi sasa kuwa wananufaika zaidi wawekezaji wakubwa tuu huku wananchi wa maeneo yenye vito hivyo wakibakia kwenye lindi la umaskini mkubwa.

80. Mheshimiwa Spika, kama Serikali ingekubaliana na ushari wa Kambi ya Upinzani, Serikali ingepitia upya kabisa mwenendo mzima wa biashara ya madini haya ili kuwa na chanzo kimoja tu cha mauzo. Udhibiti huu ungipatia Serikali mapato ya jumla ya Tshs. 200bn. ambayo hayakusanywi hivi sasa.
g).MAPATO KATIKA KODI NYENGINEZO:

i).Misamaha ya Kodi;
81. Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo tumekuwa tukipoteza fedha nyingi sana ni eneo la misamaha ya kodi. Kama ilivyo katika taarifa ya kamati ya fedha na uchumi ya Bunge, inakadiriwa kuwa takribani shilingi 819.9 billion zilitolewa kama misamaha ya kodi katika mwaka wa fedha unaomalizika. Aidha hali ya misamaha ya kodi kwa upande wa Zanzibar ilikuwa ni ya kutisha kwani mwaka 2006/2007 TRA ilikusanya kiasi cha shilingi 20.4 bilioni huku misamaha ya kodi mbalimbali ikifikia shilingi 19.6 bilioni hili ni jambo la ajabu sana,Kwani misamaha hii ukiondoa ile inayolenga mashirika na madhehebu ya kidini haiwanufaishi wananchi masikini wa taifa hili. Ili kuongeza mapato yetu ya ndani Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali ipunguze misamaha ya kodi kwa asilimia 50%. Uamuzi huu utaweza kuongeza mapato na kuwa Tsh. 409.95billion ambazo hazikusanywi hivi sasa.
ii) Kodi katika Posho ‘ALLOWANCES’
82. Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa sheria ya kodi ya mapato, sheria na.11 ya mwaka 2004 kifungu cha 7(1) na (2) , kila atakachokitoa mwajiri itabidi kikatwe kodi isipokuwa kama mfanyakazi atatumia fedha zake na mwajiri akamrudishia. Kwa mujibu wa sheria hii posho zote za warsha, semina, makongamano, mikutano na vikao zinapaswa kukatwa kodi ya mapato. Hii pia inajumuisha posho wanazopata Waheshimiwa Wabunge kutokana na vikao hapa Dodoma na Dar es Salaam.Ikirekebishwa sheria ya kodi ili kutoza kodi mapato haya kwa kiwango cha VAT yaani 20%. Hatua hizi pia ingelenga kupata manufaa yafuatayo:-
(a) Mifuko ya Pensheni itapata wanachama zaidi.
(b) Kodi ya Serikali ambayo ni ya uhakika (P.A.Y.E. itapanda maradufu kwani employment allowance haitozwi).

83. Mhe. Spika, uamuzi huu Serikali ingepata mapato ya Tshs.8bn ambazo hazikusanywi hivi sasa.

h).Mauzo ya hisa za Serikali.

84. Mheshimiwa Spika, eneo lingine linaloinyima Serikali mapato yake ni uuzwaji wa hisa zake kwa bei isiyokuwa ya soko.Kwa mfano hisa 25% za Serikali za Wiilliamson Diamond ziliuzwa kwa USD 183,000 tu Na pia kuna taarifa kuwa asilimia 25% za serikali zilizokuwa zimebakia zimetolewa bure kwa mwekezaji tunataka maelezo kutoka serikalini juu ya taarifa hizi. NIC, ilitaka kubinafsishwa kwa thamani ya shs3bn tu, hadi Kamati ya Fedha na Uchumi ilipodai tathmini mpya, kulingana na tathmini mpya iliyofanywa na Chuo Kikuu kishiriki cha Ardhi. thamani imepanda hadi shs.6bn.
85. Mheshimiwa Spika, Hisa za NMB zinatarajiwa kuuzwa kwa Tshs. 58bn. Kiwango hiki ni cha chini kulingana na ukweli kuwa NMB ni benki inayopata faida sana na imeweza kutoa gawio kwa wanahisa wake.Kambi ya Upinzani tunaitaka Serikali kuuza hisa zake za NMB kwa bei ya soko.
Mhesimiwa Spika, Serikali imekubali maoni ya Kambi ya Upinzania kuhusiana na thamani ya hisa za Benki ya NMB. Mwaka 2007/2008 serikali ilikadiria kupata 15bn kwa kuuza hisa za benki ya NMB. Kambi ya upinzani tukasema thamani ya hisa ilishushwa makusudi. Sasa serikali imekadiria kupata shs 58bn. Hii inaonesha jinsi kambi ya upinzani inavyojali maslahi ya wananchi na tunaitaka serikali itekeleze maoni yetu yote kwa manufaa ya wananchi na sio hilo moja tu. Hivyo basi, Kambi ya Upinzani inaamini kuwa dhamani halisi ya hisa za Serikali za NMB ni shilingi 120 billion badala ya shilingi 58billion za Serikali.

86. Mheshimiwa Spika, Bado kuna makampuni ambayo serikali ina hisa ambayo sasa ingefaa hisa hizo kuuzwa kwa wananchi lakini serikali ipo kimya katika hili. Kwa mfano, ni kwa nini serikali haiuzi hisa zake katika benki ya CRDB na kampuni la simu la CELTEL katika soko la hisa? Kwa nini haiuzi hisa zake ili serikali kupata mapato ya kuendesha uchumi? Iwapo serikali ingeuza hisa zake ingeweza kupata fedha kulipia punguzo la kodi ya mafuta kwa wananchi na wazalishaji katika mwaka wa fedha 2008/2009. Kenya wameuza hisa zao za Safaricom na zimekuwa over subscribed. Soko la Hisa la Dar es Salaama lapaswa kuboreshwa kwa kuingiza kampuni nyingi zaidi ili kumilikisha wananchi hisa za makapuni na kufanya biashara ya hisa kuwa nzuri na yenye kuweza kutabirika.

i).Mapato kutokana na Bandari ya Mtwara na Tanga;

87. Mheshimiwa Spika, Eneo lingine ambalo bado halijatumiwa vizuri ni la kuuza mauzo nje ya nchi na hasa nchi jirani (Bonded Goods). Kama bandari ya Mtwara ingejengewa maghala ya kuhifadhia mazao na bidhaa kwa kufanya mauzo ya bidhaa zetu za viwandani kama vile cement na mifugo,mchele na bidhaa nyingine katika nchi ya Comoro, ambayo matumizi yao ni saruji tani 70,000, Mchele tani 40,000 kwa mwaka, na ng’ombe ni 4000 kwa wiki. Comoro inaitegemea sana Tanzania katika vyakula na vifaa vya ujenzi. Aidha tutasukuma uuzaji wa bidhaa zetu nje kama Muhogo, korosho,ufuta na samaki. Uimarishaji huu utaweza kutuingizia kiasi cha shilingi 4 billioni kutokana na kodi peke yake ambayo sasa haikusanywi.

j).Kodi itakayo tokana na Leseni za Madereva;

88. Mheshimiwa Spika,Kambi ya Upinzani inashauri kuwa mfumo wa leseni za madereva uboreshwe kwa kutoa leseni mpya kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya komputa. Leseni hizi zitakuwa na uwezo wa kuhifadhi taarifa zote muhimu za madereva. Hii itasaidia kupunguza uhalifu na hasa ajali za barabarani na pia itakuwa ni sehemu ya kitambulisho. Mradi huu uendeshwe kwa utaratibu wa PPP. Kwa makisio ya chini, madereva laki mbili na nusu mwaka huu wa fedha na ada ya leseni kuwa shs. 50,000, tutakusanya jumla ya shilingi 6.25bn ambazo sasa hazikusanywi.

k).Mapato kutokana na kuuza ndege ya Rais;
89. Mheshimiwa Spika, kutokana na dhamira yetu toka mwaka 2003 kwamba ununuzi wa ndege ya Rais ni anasa na gharama zisizo na msingi kwa sasa Serikali inatumia Shs 6 Millioni kwa saa ya kuruka ndege hii.Kambi ya Upinzani bado inaendelea na ushauri wake kwamba ndege hii kama alivyofanya Rais wa Ghana Bw. John Kufouri iuzwe kwa mnada. Kwa uamuzi huu Serikali itapata mapato Tshs 30 billion. Pia hatua hii itaiwezesha Serikali kupata fedha za kutengenezea ndege zake.
90. Mheshimiwa Spika, ushauri huu uliotolewa na Kambi ya Upinzani,kama Serikali ingekubali kuufanyia kazi kuhusu sera ya mapato, yangeipatia Serikali jumla ya mapato ya ziada ya Tsh. 2,234.348. bn. Ushauri wa Mapato haya yote ni kutokana na kuboresha Vianzio vilivyopo na Kubuni vipya ambayo Serikali haikuviona.

91. Kuwarahisishia Watanzania kwa kuifanya mamlaka ya manunuzi nchini ijitegemee kwa kutumia utaratibu wa manunuzi wa mtandao (e-Procurement) kwa ajili ya kusajili makampuni katika ngazi za wilaya, Mkoa hadi Taifa na nje zinazotoa huduma kwa Serikali. Kuiboresha mamlaka hii ili isaidie kupunguza rushwa katika manunuzi na kuipunguzia Serikali bei ya manunuzi kwa wastani wa si chini ya 15% ya manunuzi yake yote.Njia hii itatuingizia mapato kiasi cha shilingi 250 bn .

Mhe.Spika, muhtasari, wa ushauri wetu juu ya vyanzo vipya vya MAPATO ya Serikali ni kama ifuatavyo:-
Na. MAPATO KIASI(Tshs.)
1. Ada za leseni za meli zinazovua bahari kuu 9.5bn
2. Mrahaba kutokana na Uvuvi katika Bahari kuu 370bn
3. Mapato kutokana na mafuta kwa meli za uvuvi 3bn
4. Mapato kutokana na bidhaa za misitu 100bn
5. Mapato kutokana na biashara na Comoro kupitia Bandari ya Mtwara
4bn
6. Mapato kutokana na punguzo la 50% ya Misamaha ya kodi .
409.9billion
7. Kodi ya 20% kutokana na posho za semina nk. 8bn
8. Mauzo ya hisa za Serikali i.e NMB 120 bn
9. Ukusanyaji wa kodi isiyokusanywa kwenye madini. 88.3 bn
10. Ushuru wa mauzo kutokana na madini ya Vito ie Tanzanite 100bn
11.
Mapato kutokana na Vitalu vya uwindaji wa Kitalii. 85bn
12. Mrahaba wa asilimia 5% katika madini 41.8bn

13. Mauzo ya Ndege ya Rais 30bn
14. Mapato kutokana na leseni za madereva 12.5bn
15. Mapato kutokana na utalii 67.5bn
16 Kodi isiyokusanywa Williamson Diamond Ltd 841 mil.
17 Mapato toka Tansort 206.6 mil.
18 E -procument 250 bn
19 Ushuru wa mafuta kampuni sita za madini 59 bn
20 Mauzo ya hisa za celtel 20% 243bn.

21 Fedha (Commitment) za EPA 131.8 bn
JUMLA 2,234.348bn

NOTE.Fedha za EPA zimewekwa kama chanzo cha mapato na Kambi ya Upinzani kwani zimetambuliwa na Mdhibiti na mkaguzi mkuu wa Serikali kama mapato halali (Ripoti ya mkaguzi na mdhibiti mkuu wa hesabu za Serikali kwa mwaka wa Fedha unaoishia Juni 30 2007,“kama taarifa ya mihadi ambayo haijatekelezwa’).

92.Mheshimiwa Spika, Kwa ushauri wetu wa mapendekezo yetu ya mapato tungeweza kukusanya jumla ya shs. 5,736,930 bn kama mapato ya ndani. Makusanyo haya yangekuwa ni ziada ya makusanyo ambayo Serikali imepanga kuyakusanya kwa kiasi cha shs. 4,786,595 bn Tofauti ya zaidi ya Trillion 1.030.336 na bila kumuumiza mwananchi wa kawaida
93. Mheshimiwa Spika, Tukizingatia kuwa nchi yetu itapata misaada na mikopo kutoka nje kama jinsi ambavyo imeainishwa katika Makadirio ya Bajeti ya Serikali ya mwaka 2008/2009, Makadirio ya Mapato ya Bajeti hii yangefikia jumla ya Tshs. 8.166Trilion.

MAONI YA KAMBI YA UPINZANI KUHUSU KODI MBALIMBALI.
94.Mheshimiwa Spika, baada ya Kambi ya Upinzani kuainisha vyanzo vipya mbalimbali vya kodi ambavyo havimuumiza mwananchi wa kawaida na pia baada ya mapato ya Serikali kuongezeka kutokana na vyanzo hivyo, hivyo basi tunaitaka Serikali ichukue hatua zifuatazo ili kuweza kuinua uchumi na kukuza ukuaji wa pato la taifa kama ifuatavyo;

Mishahara kwa watumishi wa Serikali;

94.Mheshimiwa Spika, Kutokana na kuongezeka kwa mapato ya ndani,Kambi ya Upinzani inashauri kiwango cha chini cha Mshahara Wa wafanyikazi wa Umma kiwe Tshs 250,000/ kwa mwezi, kwa ngazi nyingine mshahara ungepanda kwa asilimia ambayo italeta uiwiano baina ya kipato cha chini na cha juu. Ufafanuzi wa kina wa utatolewa na Waziri Kivuli wa Utumishi wa Umma.Kiwango hiki hakitatozwa kodi ili kuweza kumfanya mtumishi wa ngazi ya chini aweze kumudu gharama za maisha ,japo hatua hii itapunguza mapato ya Serikali kwa kiasi fulani.

95.Mheshimiwa Spika, Elimu ni kipaumbele chetu kikuu katika matumizi ya Serikali.Kwa maoni ya Kambi ya Upinzani nikuwa Serikali imejikita zaidi katika hatua ya awali kuwa na shule nyingi,idadi kubwa ya wanafunzi,jambo ambalo limefanikiwa kwa kiasi kikubwa.Kutokana na kazi kubwa iliofanywa na Kambi ya Upinzani ya kutafuta mapato zaidi,muono wetu ni kuimarisha hatua iliofikiwa kwa kuelekeza matumizi yetu katika kuboresha viwango vya elimu ili kuwa na ELIMU BORA Hivyo, tunashauri,kuwa tuhakikishe mkazo mkubwa unawekwa katika kuwaelimisha walimu,katika ule mtindo wa zamani.Pia Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kuaondoa kodi kwenye vifaa vyote vya elimu kama vitabu, madaftari,kalamu n.k. Hatua hii itawawezesha wananchi kuweza kumudu gharama za kusomesha watoto wao na kuliendeleza taifa .

96.Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani inaitaka serikali kupunguza kodi kwenye mafuta ya Petrol na Dizeli kwa kiasi cha shilingi 250 kwa kila lita moja ya mafuta hayo ,hii itamwezesha mwananchi masikini kuweza kumudu gharama za maisha na hata kuweza kukuza uchumi wa wananchi masikini.

97.Mheshimiwa Spika , Kambi ya Upinzani inaitaka serikali kuondoa ushuru mpya uliopendekezwa kwenye vinywaji na haswa Bia ambazo malighafi yanayotumika kuzitengeneza yanapatikana hapa nchini na hii inalenga kuwanufaisha wakulima ambao wanazalisha malighafi hizo.Pia vinywaji baridi kama Soda ushuru unaopendekezwa na Serikali hakuna budi uondolewe.

98.Mheshimiwa Spika ,Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kuondoa kodi zote za vifaa vya Kilimo kama vile majembe ya Trekta, vipuri n.k. Hatua hii itamwezesha mwananchi masikini kuweza kumudu kutumia zana za kisasa katika uzalishaji na kukuza tija ya kilimo hapa nchini.

99.Mheshimiwa Spika ,Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kuondoa kodi kwenye malighafi ya kutengenezea Majiko ya Moto poa ,hii ni hatua muhimu ili kuhakikisha kuwa wananchi wanaweza kumudu gharama za kununulia majiko hayo , Serikali isiondoe Kodi kwenye mafuta tuu kwani wananchi watashindwa kumudu kuwa na uwezo wa kupata mashine hizo.

100.Mheshimiwa Spika ,Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kuondoa ushuru uliopendekezwa kwenye magari yote yenye cc zaidi ya 5000 ,kwani magari haya ni malori na mabasi kwa ajili ya abiria .Hatua hii itawawezesha wananchi kuweza kumudu gharama za nauli na pia kuweza kusafirisha vyakula kwa kutumia malori hayo hadi kwenye masoko na hili litapunguza bei kubwa ya kununua vyakula .
USHAURI WA KAMBI YA UPINZANI JUU YA UTARATIBU WA MGAO WA KUTUMIA FEDHA;
101.Mheshimiwa Spika, kama tulivyoshauri katika hatua mbali mbali za maoni yetu, katika kutekeleza mipango ya Serikali, na kuwafanya watekelezaji wa mipango hiyo waweze kutekeleza vyema,, utaratibu wa “cash budget” haufai. Utaratibu uliokuwa unatumika zamani wa ”Warrant system”urudiwe. Aidha Fedha badala ya kutolewa kwa mtindo wa kila mwezi, utaratibu wa kutoa fedha kwa kipindi cha miezi minne minne utumike.
102.Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa vipaumbele tulivyo shauri, tumegawa mapato kama ya bajeti hii mbadala kama ifuatavyo:-

1. Elimu, asilimia 22% sawa na shilingi 1,796.5564bn
2. Miundombinu, asilimia 20% sawa na shilingi 1,633.2332bn.
3. Kilimo,asilimia 12% sawa nashilingi 979.9398bn.
4. Afya, asilimia 11% sawa na shilingi 897.2782bn.
5. Nishati asilimia 8% sawa na shilingi 653.2932bn.
6. Maji, asilimia 10% sawa na shilingi 816.61656bn.
7. Matumizi mengine 17% ni shillingi 1388.2481bn.


USHAURI WA KAMBI YA UPINZANI JUU YA SURA YA BAJETI

Mapato: shilingi bilioni
A. Mapato ya Ndani 5,736.9306

B. Mikopo na Misaada ya Nje Ikijumuisha 2,429.535bn.
HIPC/MDRI


JUMLA YA MAPATO YOTE 8,166.1656bn.

Matumizi

C. Matumizi ya Kawaida 3,940.213
1) Deni la Taifa 648.284bn.
2) Wizara,Mikoa na Halmashauri 2,907.929bn.

3). Matumizi mengine 384.0bn.

D. Matumizi ya Maendeleo 4,225.952bn .
(i) Fedha za Ndani 2674.852
(ii) Fedha za Nje 1,551.100bn

JUMLA YA MATUMIZI YOTE 8,166.1656bn.

103. Mheshimiwa Spika, kutokana na mchanganuo huo, tofauti za kimsingi za hoja ya Waziri wa Fedha na Ushauri wa Kambi ya Upinzani ni kama ifuatavyo:-
1. Ushauri wa Kambi ya Upinzani kupitia bajeti hii kivuli utaiwezesha Serikali kutumia fedha za ndani kwa miradi ya maendeleo hata kama wafadhili wataondoa fedha zao. Tutaweza kutekeleza miradi yote ya sasa. Fedha ya wafadhili itakuwa ni ziada tu. Hivi sasa bajeti ya maendeleo inategemea wafadhili kwa asilimia 63.
2. Ushauri wa Kambi ya Upinzani kupitia bajeti hii kivuli utaiwezesha Serikali kutumia kiasi kisichopungua asilimia 51% ya bajeti yote kwa ajili ya maendeleo, badala ya asilimia 34% tu iliyo wasilishwa na Serikali .
3. Ushauri wa Kambi ya Upinzani kupitia bajeti hii kivuli utaiwezesha serikali kupunguza Bajeti tegemezi.Mikopo na misaada toka kwa wahisani ni asilimia 30% ya bajeti nzima kivuli badala ya utegemezi wa asilimia 34% uliowasilishwa katika bajeti ya Serikali.
104 . Mhe. Spika, mlinganisho wa kati ya Ushauri wa Kambi ya Upinzani kupitia bajeti yake kivuli na Sura ya Bajeti ya Serikali ni kama inavyoonekana kwenye Kiambatanisho 1.

MWISHO
105. Mheshimiwa Spika, Lengo kuu la Ushauri wa Kambi ya Upinzani kupitia bajeti hii kivuli niliyowasilisha ni kuchochea ukuaji wa uchumi, kuondokana na bajeti tegemezi kama Taifa na kuwa na Taifa lililoelimika lenye Utawala unaoheshimika. Katika hotuba yetu nimeonyesha wazi wazi kuwa tunazo fursa kubwa za kupata mapato ya ndani. Tatizo ni mtazamo wa kifikra “MIND SET”. Changamoto kubwa tuliyonayo kama Taifa ni kwa viongozi kuwa tayari kujifunza kutoka kwa wengine bila kujali itikadi za kisiasa, ili kwa pamoja tuwaondolee umasikini Watanzania waliokalia rasilimali zinazozidi mahitaji yao.Lazima sote tujiulize kwa nini wageni na wajanja wanatajirika,lakini wakulima na wafanyakazi wetu ni masikini? Taifa hili ni letu. Tusemezane, tujadiliane hatimae tusonge mbele.

106. Tuliyosema yanawezekena, yanahitaji viongozi na watumishi kuweka maslahi ya Taifa mbele. Raslimali tulizonazo zinatosheleza kama zitasimamiwa na kutumika kwa maslahi ya watu wetu.

107. Mheshimiwa Spika, naomba tena kukushukuru na kuwashukuru waheshimiwa Wabunge na Wananchi kwa kunisikiliza..Mungu Ibariki Tanzania.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.


. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .
HAMAD RASHID MOHAMED (MB)
KIONGOZI WA UPINZANI BUNGENI NA MSEMAJI MKUU WIZARA YA FEDHA.
16 JUNI, 2008.

TOFAUTI YA SURA YA BAJETI YA SERIKALI NA BAJETI MBADALA:
BAJETI YA SERIKALI (Bn. TShs) BAJETI MBADALA (Shs)
Mapato

A. Mapato ya Ndani na Mauzo ya Hisa
4,786.070
5,736.9306bn.
B. Mikopo na Misaada ya Nje ikijumuisha HIPC/MDRI 2,429.535bn. 2,429.535bn

JUMLA YA MAPATO YOTE 7,216.130bn. 8,166.1656bn.

Matumizi
D.Matumizi ya Kawaida 4,726.650bn. 3,940.213bn

I. Deni la Taifa.
II. Wizara,Mikoa na Halmashauri
III. Matumizi Mengine
648.284bn.
3466.598bn605.768bn. 648.284bn.
2907.929bn.384.0bn.
E.Matumizi ya Maendeleo. 2,489.480bn. 4,225.952bn.
i. Fedha za Ndani
ii. Fedha za Nje 938.380bn.
1,551.100bn. 2,674.852bn
1551.100 bn
Jumla ya Matumizi yote 7,216.130bn. 8,166.165 bn
 
upinzani hasa CHADEMA wamekuwa wakijitahidi sana kuandaa budget mmbadala nyingi ambazo huwa zinatoa mwanga na njia ya nini kinachoweza kufanyika.Nawapa big up sana lakini je 2kiwachagua hamtataka maslahi?
 
Back
Top Bottom