Breaking News:Watoto wamchinja baba yao hadi kufa kwa kumtuhumu kamloga mama yao

Gumzo

JF-Expert Member
Jan 2, 2012
211
7
Watu wawili, Nelson Mkini (37) na Cuthbert Mhegama Mkini (28), wamemuua kwa kumchinja kwa panga baba yao mzazi Ejid Mkini (65), kwa tuhuma kwamba amemloga mama yao mzazi anayeendelea kusumbuliwa na ugonjwa wa mapafu na kuvimba miguu.

Wakati Nelson ni mkazi wa kijiji hicho, Cuthbert ni mwanafuni wa Chuo cha Ualimu Agafilo, kilichopo wilayani Njombe, mkoani Njombe.

Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Gerald Guninita alitembelea kijijini hapo na kutoa msimamo wa serikali kuhusiana na mambo ya kishirikina kabla hajatoa pole kwa familia ya marehemu.

Akiwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo, Guninita alikiagiza kijiji hicho kuendesha kura ya siri ili kuwabaini waganga wa kienyeji wanaopiga ramli. Guninita alisema upigaji ramli ni vitendo vinavyohatarisha amani na wakati mwingine
matokeo yake hugubikwa na chuki binafsi, "Poleni sana na msiba wa mzee huyu, taarifa kutoka kwenu wenyewe zinadai kwamba ameuawa kwasababu ya imani za kishirikina, na kwa vyovyote vile watoto wake wanaohusika na tukio hilo watakuwa walipata taarifa hizo kutoka kwa waganga wa kienyeji," alisema.

Wakati akiagiza kijiji hicho kiendesha kura ya siri dhidi ya waganga wa kienyeji, Guninita aliliagiza jeshi la Polisi kuwasaka watuhumiwa wa mauaji hayo popote walipo na kuwatia nguvuni, "Dola ina mkono mrefu, wito wangu kwa wananchi wa kijiji hiki, tuoeni ushirikiano kwa jeshi la Polisi na viongozi wa kijiji chenu, ili kazi ya kuwakamata watuhumiwa hao iwe rahisi," alisema.

Wakati huo huo, ndugu wa watuhumiwa hao wamesikitishwa na kitendo kilichofanywa na watuhumiwa hao wa tumbo moja.

Nicko Mkini (35) alisema taarifa za baba yao kuhusishwa na imani za kishirikina amezisikia baada ya kufika msibani akitokea kijiji cha Itona alikoweka makazi yake, "Huu ni uzushi mkubwa, sio kweli kwamba marehemu baba yetu alikuwa mchawi na hakuna mganga yoyote wa kienyeji aliyethibitisha hilo," Nicko alisema.

Naye Mke wa Nelson, Roida Kivamba alisema jitihada zake za kumzuia mume wake na shemeji yake wasimchinje baba yao hazikuzaa matunda na alichoambulia ilikuwa kipigo kikali kutoka kwao kilichomchanganya na kumfanya akimbie kutoka katika nyumba hiyo.

Tukio hilo la kusikitisha lilitokea majira ya saa 3.40 usiku nyumbani kwa marehemu huyo, katika kijiji cha Pomerini (Ng'uruhe), wilayani Kilolo, mkoani Iringa.

Akizungumzia jinsi tukio hilo lilivyotokea, Roida alisema katika mazingira ya kutatanisha mumewe huyo na shemeji yake, walifika nyumbani kwa baba yao kwa madai kwamba wamekuja kumjulia hali mama yao mzazi anayeendelea kuugua ndani ya nyumba yao. Baada ya kumjulia hali mama yao, walisema watalala katika sebule ya nyumba hiyo yenye vyumba viwili vya kulala. Hatua hiyo ilipingwa na baba yao aliyekuwa amepumzika katika moja ya vyumba vya kulala katika nyumba yake hiyo kwa madai kwamba uamuzi wao huo ungemletea bugudha mama yao na wanaomuugaza pindi wanapotaka kutoka nje ya chumba kingine cha kulala, kwa ajili ya kujisaidia. Zogo hilo lilihitimishwa kwa watuhumiwa hao, kumpa kipigo kikali baba yao kabla ya kuchukua panga na kuanza kumchinja kama kuku.

Wakati wakifanya hivyo, Roida aliyekuwa akisaidia kumuuguza mama mkwe wake, alijaribu kumnusuru baba mkwe wake bila mafanikio yoyote na badala yake aliambulia kipigo kilichomfanya ageuke kama mwendawazimu kwa kukimbia na kupiga kelele.

CHANZO: GUMZO LA JIJI
 
Back
Top Bottom