Brazil: Meya wa Mji wa Sao Paulo asema hospitali zinaweza kuzidiwa ndani ya wiki mbili zijazo

beth

JF-Expert Member
Aug 19, 2012
3,877
6,326
Meya wa jiji kubwa zaidi nchini Brazili, Sao Paulo amesema kuwa mfumo wa afya unaweza kuporomoka huku kukiwa na ongezeko la mahitaji ya vitanda vya dharura ili kuwahudumia wagonjwa wa corona.

Bruno Covas amesema hospitali za umma za jiji hilo zinaweza kujaa katika kipindi cha wiki mbili zijazo.

Sao Paulo ni moja kati ya miji iliyoathirika zaidi nchini Brazil kukiwa na watu 3,000 waliopoteza maisha mpaka sasa kutokana na corona.

Siku ya Jumamosi, Brazil ilizidi nchi ya Uhispania na Italia na kuwa taifa la nne lenye idadi kubwa ya watu walioambukizwa virusi vya corona.

Wizara ya afya imeripoti maambukizi mapya 7,938 katika kipindi cha saa 24, jumla ya watu walioambukizwa ikifikia 241,000.

Marekani, Urusi na Uingereza ndizo zilizo na idadi kubwa zaidi ya watu waliopatwa na maambukizi.

Idadi ya waliopoteza maisha katika nchi hiyo ya Amerika ya Kusini katika kipindi cha saa 24 ni watu 485, ikiwa na jumla ya vifo 16,118, takwimu zinazolifanya taifa hilo kushika nafasi ya tano kati ya nchi zenye idadi kubwa ya vifo.

Wataalamu wa afya nchini Brazil wameonya kuwa idadi kamili ya walioambukizwa nchini humo inaweza kuwa kubwa zaidi kuliko takwimu zilizotolewa na serikali, kutokana na upungufu wa vipimo.

Rais wa Brazil Jair Bolsonaro amekosolewa vikali ndani na nje ya nchi kwa namna anavyoshughulikia janga la corona linaloendelea kushika kasi.

Alipuuza ushauri wa wataalamu wa afya duniani kuhusu kutochangamana siku ya Jumapili alipopiga picha na watu wanaomuunga mkono na watoto katika mji wa Brasilia.

Meya wa Sao Paulo alisema nini?
Bwana Covas alisema kuwa sasa yuko kwenye mazungumzo kuhusu hali hii na Gavana wa jimbo kwa ajili ya kuweka marufuku ya kutotoka nje ili kujaribu kupunguza maambukizi kabla hospitali hazijazidiwa.

Gavana wa jimbo la Sao Paulo ana mamlaka kwa polisi, na msaada wake utakuwa muhimu ikiwa amri ya kutotoka nje itakuwa ya mafanikio.

Sao Paulo ina jumla ya watu karibu milioni 12, na takwimu zinaonesha kuwa wengi wa wakazi wa mji huo wamekuwa wakikiuka sharia ya kutochangamana.

Jimbo la Sao Paulo lilianzisha utaratibu wa karantini karibu miezi miwili iliyopita -Biashara, hospitali na maeneo ya Umma yalifungwa na watu walitakiwa kukaa nyumbani.

Lakini hakuna adhabu yoyote kwa mtu atakayevunja sharia hizo. Wakazi wengi wa Sao Paulo wamekuwa wakiendesha magari mpaka kwenye fukwe za bahari wakati wa mwisho wa juma.

Kutokana na hali hiyo paliwekwa sheria ya kuvaa barakoa ambayo nayo inapuuzwa mara kwa mara-watu walionekana wakiwa matembezini wakiwa hawana barakoa wengine wakiwa wamezivalia shingoni barakoa zao. Inaonekana kabisa kuwa ugonjwa huu hautiliwi maanani.

Wakati huohuo, watu wanashuhudia Ulaya ikifungua shughuli zake na kuna mashaka kitakachotokea nchini Brazil. Lakini kama Meya alivyozungumza mwishoni mwa juma, mji unapaswa kusimamisha shughuli zake kabla haujafunguliwa tena. Watu wengi wanatarajia kukabiliwa na masharti makali ya kutotoka nje katika majuma yajayo.

Rais Bolsonaro anashughulikia vipi janga hili?
Rais wa mrengo wa kulia ni maarufu mjini São Paulo, na amekuwa akisema amri ya kutochangamana itauharibu uchumi.

Bwana Bolsonaro ameendelea kupinga hatua ya kusalia nyumbani akisema kuwa ''huo ni ugonjwa mdogo wa mafua'' na kusema kuwa kuwa kusambaa kwa Covid-19 hakuwezi kuepukika.

Mwezi Aprili, Bolsonaro aliwaunga mkono waandamanaji waliokuwa wakitaka kuondolewa kwa marufuku ya kutotoka nje. Anasema kuwa masharti hayo yanaharibu uchumi wa nchi, kusababisha ukosefu wa ajira na njaa.

Wiki iliyopita, Waziri wa afya nchini Brazil Nelson Teich alijiuzulu baada ya kuwa katika nafasi hiyo kwa kipindi cha chini ya mwezi mmoja.

Bwana Teich alijiuzulu baada ya kumkosoa waziwazi bwana Bolsonaro aliyeruhusu maeneo ya kufanyia mazoezi na maeneo ya saluni kufunguliwa.

Mtangulizi wa Teich alifutwa kazi baada ya kutokubaliana na msimamo wa Rais Bolsonaro.

Wataalamu wa afya wanasema nini?
Wataalamu wa afya nchini Brazil wametoa angalizo kuwa idadi ya watu walioambukizwa inaweza kuwa kubwa zaidi kuliko takwimu zilizotolewa na serikali, kutokana na upungufu wa vipimo.

''Brazil inawapima watu wanaokuwa hospitalini,'' anasema Domingo Alves kutoka Chuo Kikuu cha tiba cha Sao Paulo, Shirika la habari la AFP lilielezwa juma lililopita.

''Ni vigumu kujua hasa kinachofanyika kuhusu takwimu zinazopatikana. Hatuna sera ya kukabiliana na mlipuko,'' alisema.

Bwana Alves ni mmoja kati ya watafiti ambao walikisia kuwa idadi inaweza kuwa mara 15 zaidi ya takwimu zilizotolewa na serikali.

Hali ikoje katika eneo la Amerika Kusini?
Brazil, nchi kubwa zaini eneo la kusini mwa Amerika, kwa majuma kadhaa imekuwa ikiathirika kwa kiasi kikubwa na mlipuko wa virusi vya corona.

Amerika ya Kusini na Caribbean zimerekodi maambukizi ya watu zaidi ya 500,000, huku Brazil ikiwa na maambukizi ya asilimia karibu 50.

Mexico hivi karibuni imeshuhudia ongezeko la maambukizi, huku Ecuador ikishuhudia kuzorota kwa mfumo wake wa afya mwezi Aprili.

Ongezeko kubwa la maambukizi katika eneo la Amerika Kusini limesababisha Shirika la Afya duniani, (WHO) kusema kuwa eneo hilo liko kwenye kitovu cha janga hilo.

Mwezi Machi, WHO ilitangaza Ulaya kuwa ''kitovu cha janga la corona'' lakini eneo hilo limeanza kupunguza makali ya masharti yaliyokuwa yamewekwa ili kupunguza kasi ya maambukizi ya virusi.

BBC Swahili
 
Asante kwa taarifa nzuri, muhimu ni kuendelea kumomba Mungu kwa kumaanisha ili ateupushie hili janga,vinginevyo uchumi wa Dunia nzima utayumba sana...
 
Duh Asante kwa taarifa bidada... Mungu atusaidie
=========
Ila nina swali nje ya mada,hivi kati ya Sao Paulo na Rio de Jeneiro upi ni mji mkubwa zaidi Brazil?
 
Vipi Brazil Mungu ni kwenye mpira tu, ni kwa nini wasimuombe na kwenye hili suala linalotishia maisha yao!?
 
Back
Top Bottom