BoT: Uchunguzi mwingine wa ufisadi BoT waanza

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,825
287,847
Uchunguzi mwingine wa ufisadi BoT waanza
Waandishi Wetu
Daily News; Friday,March 28, 2008 @00:02

*Wahusu bilioni 420/- za ghorofa pacha

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT), imeamua kuanzisha uchunguzi juu ya gharama halisi za ujenzi wa ghorofa zake pacha mjini Dar es Salaam na ofisi mpya ya tawi lake la Zanzibar, ambazo ni za utatanishi na zimegubikwa na tuhuma za ufisadi wa mabilioni ya walipa kodi.

Benki hiyo imesema katika taarifa jana kwamba ina lengo la kutambua gharama halisi zilizotumika katika ujenzi huo ambazo hazikuwahi kuwekwa bayana hata wakati jengo la Dar es Salaam lilipozinduliwa na Rais mstaafu Benjamin Mkapa mwaka 2005.

Taarifa zisizo rasmi na madai mbalimbali ambayo yamekuwa yakitolewa, yamekuwa yakilenga katika kueleza kwamba hadi ilipofika Julai mwaka jana, ujenzi wa ghorofa pacha za BoT uligharimu takribani dola za Marekani milioni 340 (Sh bilioni 420), ingawa taarifa za awali zilionyesha kwamba ujenzi huo ulikadiriwa kugharimu dola milioni 89.

Kwa mujibu wa madai hayo, gharama hizo zilimaanisha kwamba ujenzi wa mita moja ya mraba ya majengo hayo uligharimu dola kama 8,600 (Sh milioni 10.3), kiasi ambacho kinaelezwa ni takribani mara nne ya gharama za ujenzi katika miji yenye gharama za juu kama New York, Marekani, Tokyo, Japan au London, Uingereza.

BoT imesema katika taarifa yake ya jana kwamba ujenzi wa miradi yote miwili “unakaribia kumalizika” na mkandarasi tayari amekabidhi baadhi ya sehemu za majengo hayo. Ujenzi wa jengo la Zanzibar katika eneo la Gulioni ulikadiriwa kugharimu dola milioni 25 (Sh bilioni 30), lakini unaelezwa kuchelewa kumalizika kwa wakati kutokana na kuongezeka kwa gharama.

“Benki ina lengo la kufanya uchunguzi na ukaguzi huru wa ufundi na wa thamani halisi ya fedha ili kufahamu kwa hakika nini hasa kilihusika katika mradi huo, gharama halisi zilizotumika katika kuutekeleza na kama fedha zilizotumika ndiyo thamani halisi inayostahili kwa ujenzi wa mradi huo,” taarifa ya BoT imesema.

Kutokana na hali hiyo, BoT imesema ina lengo la kutumia kampuni ya ushauri yenye uzoefu na ujuzi wa kutosha kufanya kazi hiyo ya utathmini.

Bila kusema iwapo kampuni hiyo inapaswa kuwa ya Tanzania au kama kampuni za kigeni zinakaribishwa, BoT imesema inakaribisha maombi kutoka kwa kampuni zinazoona zina uwezo wa kufanya kazi hiyo na baada ya kuzipitia itazikaribisha kampuni zenye sifa kutuma maombi ya zabuni.

Utata na tetesi za kutia shaka kuhusu gharama halisi za ujenzi wa ghorofa pacha, ambao ulibuniwa tangu enzi za utawala wa Mwalimu Nyerere, lakini baadaye ukasimamishwa baada ya kuonekana kuwa ni wa gharama kubwa, ulianza baada ya BoT kukataa kubainisha kiasi kamili kilichotumika wakati lilipozinduliwa na Rais mstaafu Mkapa bila kukamilika, miaka mitatu na nusu iliyopita.

Baadaye, Aprili mwaka juzi, aliyekuwa Waziri wa Fedha, Zakia Meghji aliliambia Bunge kwamba hadi kukamilika kwa ghorofa pacha ujenzi huo ungegharimu Sh bilioni 200.

Hata hivyo, Septemba mwaka jana BoT ilisema katika taarifa yake kwamba gharama hizo zimefika Sh bilioni 418, huku kukiwa na taarifa kwamba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ilikuwa ikifanya uchunguzi kuhusu suala hilo.

Muda mfupi kabla ya hapo, katika kikao cha bajeti, kulikuwa na shinikizo bungeni kutoka kwa wabunge wakitaka serikali ibainishe kuhusu gharama halisi za ujenzi wa majengo hayo pacha.

Wakati kukiwa na vuta nikuvute hiyo, yalitolewa madai kwamba wakaguzi wa kampuni ya nje waliokuwa wakifuatilia hesabu za BoT mwaka juzi walinyimwa katakata nyaraka muhimu kuhusu gharama za ujenzi huo walipoziomba kutoka menejimenti ya BoT, suala ambalo linadaiwa kusababisha baadaye kuibuliwa kwa hoja kadhaa za matumizi yasiyostahili ya benki hiyo.

Akizungumza na HabariLeo jana kuhusu uamuzi wa BoT wa kufanya uchunguzi wa gharama halisi za ujenzi wa majengo yake, Mbunge wa Karatu, Dk. Wilbrod Slaa ambaye alilivalia njuga suala hilo, alisema kama ukaguzi huo ni wa taratibu za kawaida hawezi kusema lolote, lakini kama ni kwa ajili ya kufichua ufisadi, anaamini itakuwa sawa na “kesi ya nyani kumpelekea ngedere.”

Dk. Slaa alisema ni vyema washauri watakaopewa zabuni hiyo wawe ni kampuni ya kigeni ambayo anaamini itakuwa na uhuru wa kugundua thamani halisi ya miradi hiyo.
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom