nngu007
JF-Expert Member
- Aug 2, 2010
- 15,860
- 5,799
Na Jabir Idrissa - Imechapwa 14 September 2011
AYOUB Hashim Jaku, mbunge wa Bunge la Muungano (CCM), ni mmoja wa wanaotajwa kumiliki meli ya mv Spice Islander 1 iliyozama na kuangamiza maisha ya watu zaidi ya 250 visiwani Zanzibar.
Jaku ameingia bungeni kupitia nafasi tano za wabunge wanaotokana na baraza la wawakilishi Zanzibar. Ni mwakilishi wa jimbo la Muyuni, mkoa wa Kusini Unguja.
Taarifa kutoka ndani ya serikali ya Muungano, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na Chama Cha Mapinduzi (CCM), zinasema Jaku anamiliki meli hiyo, pamoja na wafanyabiashara wengine wanne.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, wamiliki wengine wa meli hiyo, ni familia ya mfanyabiashara maarufu visiwani, Salum Battash, pamoja na mfanyabiashara mwingine aliyefahamika kwa jina moja la Thinei anayeishi Dubai.
Meli ya mv Spice Islander 1 ilizama usiku wa manane Ijumaa iliyopita, katika mkondo mkuu wa Nungwi, kaskazini mwa kisiwa cha Unguja.
Katika ajali hiyo mbaya ya kwanza kutokea katika historia ya Zanzibar, watu 610 wameripotiwa kuokolewa wakiwa hai.
Hata hivyo, takwimu hizo bado zina utata kutokana na watu mbalimbali kuripoti kutowaona ndugu zao.
MwanaHALISILI lilipowasiliana na Jaku kutaka kufahamu umiliki wake katika meli hiyo, alikana kuhusika na lolote katika meli hiyo.
Alisema, "Mimi sihusiki katika hao wanaotajwa kumiliki meli hii. Sina hisa na wala siwafahamu wamiliki wake."
Alipoambiwa gazeti hili limeelezwa kuwa jina lake linatajwa ndani ya viongozi wa serikali na jeshi la polisi kuwa mmoja wa wamiliki wa meli ya mv Spice Islander 1, Jaku alisema, "Hao wananitaja tu. Mimi simo."
Hata hivyo, MwanaHALISI limedokezwa na vyanzo vyake vya ndani kwamba Jaku ni mmoja wa wamiliki wa meli hiyo; mara kadhaa amekuwa akionekana bandarini kufuatilia kazi za meli yake.
"Sikiliza kijana, hii meli ni Jaku na wenzake. Sisi ndani ya serikali tunafahamu hivyo; nyaraka tulizonazo zinaonyesha hivyo pia," ameeleza kiongozi mmoja mwandamizi ndani ya serikali ya Zanzibar.
Habari zinasema jina la Jaku na Battash limetajwa hata ndani ya kikao cha viongozi wakuu wa visiwani kilichoshirikisha Kamati ya Kudumu ya Bunge, ulinzi na usalama kilichofanyika Zanzibar, juzi Jumatatu.
Meli hiyo iliyotengenezwa nchini Ugiriki mwaka 1967 (miaka 44 iliyopita) na kupewa jina la Mariana ilibeba zaidi ya abiria 1000.
Mwaka 1988 mmiliki wa meli hiyo aliuza na kupewa jina la Apostolos na mwaka 2007 iliuzwa tena kwa kampuni ya Honduras, ya nchini Marekani Kusini, na kupewa jina la sasa la mv Spice Islander.
Hadi sasa, hakuna taarifa yoyote kutoka serikalini inayoeleza sababu ya kuzama kwa meli hiyo.
Hata hivyo, duru huru za kiuchungizi zinasema meli ya mv Spice Islander 1 imezama kutokana na kuzidiwa na uzito wa mizigo na abiria.
Serikali ya Zanzibar imesita kutaja mmiliki wa meli hiyo, jambo ambalo linatiliwa shaka na baadhi ya wachambuzi kwamba linalenga kuendeleza utamaduni wa kulindana.
"Ndugu yangu, hapa Zanzibar hakuna asiyefahamu kuwa Jaku ndiye mmiliki wa meli hii. Lakini inaoenekana wakubwa wanataka kuficha ukweli. Sisi tunajua kwamba, kila meli ikitia nanga Zanzibar, Jaku anafuatilia utendaji wake," anaeleza Farahani Saidi, mmoja wa wabeba mizigo bandarini Unguja