Boriti ya Lowassa, Kibanzi cha Sitta | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Boriti ya Lowassa, Kibanzi cha Sitta

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Frankie_ngoka, Nov 11, 2009.

 1. F

  Frankie_ngoka Member

  #1
  Nov 11, 2009
  Joined: Nov 9, 2009
  Messages: 15
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Na Absalom Kibanda


  KAMATI maalum ya kutafuta chanzo cha uhasama miongoni mwa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) inayoongozwa na rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, ilimaliza kazi mjini Dodoma mwishoni mwa wiki, baada ya kufanikiwa kupora kwa kiwango kikubwa muda wa vikao vya Bunge la Jamhuri ya Muungano.
  Katika vikao vyake vilivyofanyika kwa takriban siku tatu mfululizo, kamati hiyo ya Mwinyi ilikusanya maoni kutoka kwa wabunge mbalimbali ambao wengi wao walikuwa wakizungumza kwa hisia kali kueleza kile ambacho kila mmoja alikuwa akiamini kuwa ndicho kiini hasa cha matatizo yanayowakabili.
  Siku kadhaa tangu kumalizika kwa vikao hivyo ambavyo pasi na shaka vilikuwa vikilenga kukijengea chama hicho mustakabali mwema baada ya uhasama kati ya makundi mawili kuonekana kukua kila kukicha kwa kiwango cha kumtikisa Rais Jakaya Kikwete, serikali na kwa kiwango kikubwa CCM yenyewe, maneno mengi yameibuka.
  Yaliyotokea ndani ya vikao hivyo ambayo baadhi wameyapa majina na sifa tofauti na zinazokinzana kama, matendo ya aibu, fedheha, ugomvi, kupakana matope, kusafishana na mengine mengi, sasa yamebakia historia na kwa hakika mbali ya kuacha vidonda, yanaweza yakawa tiba ya kudumu kwa baadhi ya watu.
  Ni wazi kwamba, baada ya kuibuka kwa misukosuko mikubwa ya kisiasa ndani ya vikao hivyo, uamuzi wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM kuamua kuunda kamati hiyo ya Mwinyi, haupaswi kubezwa na pengine kuonekana usio na msingi kwani kwa mara nyingine tena, chama hicho tawala kimetuwezesha kujua mengi ambayo kama si mikutano hiyo tusingeweza kuyasikia.
  Leo hii baada ya mikiki mikiki ya mikutano hiyo hatimaye Watanzania kwa mara ya kwanza wameweza kujua kwa uhakika kwamba, yule mfanyabiashara maarufu, Reginald Mengi ambaye katika miaka ya hivi karibuni ameingia katika kitovu cha siasa za ushindani ndani ya CCM, kuwa ni mwanachama wa siku nyingi wa chama hicho.
  Baadhi yetu ambao kwa siku nyingi tumekuwa tukijiuliza maswali yasiyo na majibu kuhusu kiini hasa cha Mengi kuonekana akiwa mstari wa mbele kusaidia harakati za kundi moja la wabunge wa CCM wanaojipambanua kuwa wapambanaji wa ufisadi, leo hii tumepata jibu la uhakika na la wazi kwamba, mzee huyo ni miongoni mwa makada wa kimya kimya wa chama hicho tawala ambaye hatimaye ameamua kujitokeza hadharani.
  Hata hivyo, wakati tukitafakari hatua hii ya Mengi ambayo sina shaka kwamba imewashtua baadhi ya marafiki na maadui zake wa ndani ya CCM na nje ya chama hicho tawala, tuna kila sababu ya kutambua kuwa, kama si maneno makali yaliyopewa kila aina ya tafsiri, yaliyosemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Sophia Simba, basi huenda leo hii tungeendelea kubakia gizani kuyajua mengi.
  Wachambuzi wa mambo wasiopendelea upande wowote juu ya kile kilichoripotiwa katika vyombo vya habari kuhusu maneno makali yenye mwelekeo wa piga nikupige, kusutana na kunyosheana vidole yaliyotamkwa na Waziri Simba ndani ya vikao hivyo, ndiyo ambayo leo hii yametoa mwongozo usio rasmi na rasmi wa mustakabali wa mambo mengi ndani na nje ya chama hicho.
  Ni kutokana na maneno hayo ya Waziri Simba ambayo sina shaka kwamba, Kamati ya Mwinyi haitayapuuza kwa wema au kwa ubaya, tumeweza kuwasikia wanasiasa na wasio wanasiasa wa kariba ya Mzee John Malecela, mkewe Anne Kilango Malecela, Mengi na Katibu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Kirumbe Ng’enda kila mmoja akitoa matamshi dhidi ya mama huyo.
  Kama hiyo haitoshi, nyuma ya maneno hayo ya Waziri Simba na yale yaliyotolewa pia na wabunge wengine ndani ya vikao hivyo, mara nyingine tena tumeweza angalau kuona na kutambua malezi ya kijamii, kisiasa na kiserikali waliyonayo viongozi wetu na kimsingi aina ya watu wanaoliongoza taifa hili katika safari ya kutafuta maendeleo ya kweli.
  Lakini pengine kubwa kuliko yote katika vikao hivyo, tumeweza kushuhudia namna chama tulichokipa dhamana ya kutuongoza, kilivyofikia hatua ya kupoteza dira kwa kiwango cha wawakilishi wa wananchi wanaotokana nacho na viongozi wengine wakongwe na wenye nyadhifa kubwa, wanavyoshindwa kutambua kiini hasa cha matatizo ambayo yamewafikisha hapo walipo leo.
  Hakuna siri kwamba, kwa watu wanaofikiri sawasawa wanaweza wakakubaliana nami kuwa, moja ya fedheha ya wazi ya kile kilichojionyesha na kujitokeza ndani ya vikao hivyo, ni hulka iliyoota mizizi ya viongozi wetu kushindwa kujadili kiini cha matatizo ya msingi yanayolikabili taifa kwa kudhani chanzo cha yote hayo ni watu fulani fulani.
  Ni kwa sababu hiyo basi, ndiyo maana habari za uhakika ambazo zilikuwa zikivuja kutoka ndani ya vikao hivyo ziligawanyika katika makundi mawili, moja likiongozwa na majemedari wa vita ya ufisadi, likirusha makombora yake dhidi ya akina Edward Lowassa, Rostam Aziz, Andrew Chenge, Nazir Kamaragi, Sophia Simba, Peter Serukamba, Makongoro Mahanga na wengine wanaounda kundi jingine.
  Katika hilo, hoja za wanaharakati wa kundi hilo la majemedari wa vita ya ufisadi, ambalo ndani ya Bunge linaongozwa na Spika wa Bunge, Samuel Sitta na serikalini likiaminika kufanya kazi chini ya uratibu wa karibu na uzoefu wa kikachero wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, liliendeleza hoja zile zile za ‘kuwa-brand’ akina Lowassa, Rostam na wenzao kuwa ni mafisadi na watu ambao hakuna shaka wanapaswa kuwajibishwa kisiasa na kisheria ili kuinusuru nchi.
  Huku wakitumia staili ile ile ya kusema na kuyarudia maneno yale yale na tuhuma zile zile mara nyingi na kwa namna ya kupindisha mambo, lengo kuu la msingi likiwa ni kumlinda Rais Kikwete na/au serikali dhidi ya tuhuma zote nzito ili uchafu wote ubebwe na watu wachache, majemedari hao wakafanya kile ambacho hakuna shaka walipanga kukiwakilisha ndani ya kamati hiyo ya Mwinyi.
  Huku wakijua kwamba walikuwa wakienda Dodoma kukata mzizi wa fitina, majemedari hao katika mazingira ambayo kwa hakika hawakuyatarajia, wakashangazwa na namna kundi la wana CCM ambalo kwa siku nyingi limekuwa likionekana kuwa la majeruhi, lilivyojipanga kukwepa kila kombora lililoelekezwa kwao.
  Huku wakitumia hoja za kale na mpya za kujibu mashambulizi, ‘majeruhi hao wa ufisadi’ wakizungumza kwa utaratibu maalum waliokuwa wamejiwekea, wakarusha makombora hewa na halisi dhidi ya makamanda wa ufisadi kwa kiwango cha kusababisha mtikisiko mkubwa ambao hakuna aliyeutarajia.
  Aliposimama Chenge na kueleza namna sakata la Richmond lilivyopindishwa kwa lengo la kumng’oa Lowassa na mawaziri wengine wawili na kisha akazungumza Rostam akiweka bayana kusudio la kuwa tayari kuwajibika iwapo utafanyika uchunguzi huru kuhusu sakata la Richmond lililomgusa, kidogo kidogo hali ya hewa ilionekana kubadilika na kuchukua mwelekeo tofauti.
  Wakati majemedari hao wa vita dhidi ya ufisadi wakikusanya hadidu rejea nyingine za kukabiliana na wapinzani wao, wakasimama Mahanga, Waziri Simba, Serukamba na kisha Kingunge akafunga pazia kuvurumisha makombora ya tuhuma za kila aina kuanzia za ukiukwaji wa maadili ya uongozi hadi za ufisadi dhidi ya Malecela, Sitta, Kilango, Sendeka, Mwakyembe na wengine wengi.
  Katika yote hayo, aliyeonekana kuwa na hoja mpya alikuwa ni Waziri Simba ambaye alikwenda mbele akaamua kupimana ubavu na Mzee Malecela, Kilango, Membe na mwishoe akafikia hatua ya kujaribu kutoka nje ya kikao hicho, akimshika sharubu jemedari wa makamanda hao wa ufisadi Mzee Mengi, ambaye hakuna shaka amekuwa kinga muhimu kwa kundi hilo.
  Tuhuma nzito za kweli na za kutiliwa shaka alizozivurumisha dhidi ya vigogo hao takriban wote, zikasababisha kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hii, watu waliotuhumiwa katika kikao ambacho kilikuwa ni cha siri, watafute namna ya kujibu mashambulizi nje ya chumba cha mikutano iliyokuwa ikiongozwa na Mzee Mwinyi.
  Wa kwanza kufanya hivyo alikuwa Mengi ambaye pamoja na kumwita Waziri Simba mjinga na kusema asingependa kulumbana naye, akakata mzizi wa fitina kwa kufichua siri ‘aliyoificha moyoni’ kwa miaka mingi kuwa, yeye ni kada wa CCM aliyejiunga na chama hicho mwaka 1977, tena ikiwa ni miezi miwili tu tangu kilipozaliwa.
  Wakati Mengi akitoa majibu hayo na kuelekeza mashambulizi dhidi ya Waziri Simba na makada wengine wa CCM, ambao katika miezi ya hivi karibuni wamekuwa wakimsakama na kuhoji uanachama wake, Kilango akaibuka Dodoma na kuzungumza na waandishi wa habari akieleza kusikitishwa na tuhuma zilizokuwa zikielekezwa kwake.
  Siku moja baadaye, Mzee Malecela naye akanukuliwa akirusha kombora la kisasi kwa Waziri Simba, ambaye mbali ya kumtuhumu kuwa si mtu safi kama alivyofanya Mengi, akaenda mbele zaidi na kudai kwamba waziri huyo alikuwa mgonjwa wa akili aliyekuwa akipaswa kwenda kutibiwa.
  Niliposikia tuhuma hizo zikijibiwa kwa tuhuma, mara moja nikakumbuka hadithi ya boriti na kibanzi katika kitabu kitakatifu cha Biblia (Mathayo 7: 3-5) na kuwashangaa wana CCM hao, ambao siku zote hoja zao zimekuwa zikijengwa kwa mtindo wa kushambulia wengine na kuwarushia kila aina ya shutuma na wakati huo huo tuhuma za namna ile ile za ukweli na za uzushi zinapoelekezwa kwao huwa wakali kama pilipili.
  Wakati majibu hayo ya akina Malecela yakitoka nje ya kikao chao cha usuluhishi, majemedari wengine wa vita dhidi ya ufisadi, wakanukuliwa wakizungumza ndani ya mkutano wa kamati ya Mwinyi wakieleza kusikitishwa na kile ambacho kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa kimepewa sifa mbaya ya ‘kuwasafisha mafisadi’ kunakokwenda sambamba na sifa ya upande wa pili ya ‘kuwachafua majemedari wa vita hiyo’.
  Mwakyembe na Lucas Selelii wakanukuliwa wakiwaonya wana CCM wenzao wanaofanya jitihada za ‘kumsafisha’ Lowassa kwa kiwango cha kujaribu kuiponda ripoti ya Kamati Teule ye Bunge iliyochunguza kashfa ya Richmond kuwa, gharama za kufanya hivyo zinaweza zikawa mbaya zaidi kwao kuliko wanavyotarajia.
  Sifa hii ya ‘kusafisha’ na ‘kuchafua’ ambayo sasa imeanza kutumiwa na makundi yote mawili yanayokinzana, yakihalalisha harakati zao hizo kupitia katika mtandao mpana wa vyombo vya habari, ikatumiwa na akina Selelii na kimsingi kabla hawajafanya hivyo katika kikao hicho, Chenge na Mahanga walikuwa nao wametumia propaganda hiyo hiyo.
  Ni jambo la bahati mbaya sana kwamba, propaganda hii inayoongozwa na majemedari wa ufisadi wa CCM, walioipora vita takatifu ya ufisadi kutoka katika mikono safi ya viongozi wa kiimani na wale wa kambi ya upinzani ndani na nje ya Bunge na kuifanya turufu ya kumalizana na kupakana matope, imekifanya chama hicho tawala na serikali yake kujijengea uhalali ambao kimsingi hakipaswi kuwa nao.
  Uhalali huu wa CCM kuendelea kustawi katika mioyo ya wengi kwa sababu ya upotoshaji unaofanywa na wabunge wake kwa uratibu wa makachero waliolelewa na kukulia katika mfumo wa chama kimoja, ndiyo ambao umefikia hatua ya boriti zilizo katika macho ya akina Lowassa, Rostam, Mahanga, Serukamba na wengine kuonekana kuwa ni jambo linalopaswa kuangaliwa na kufanyiwa kazi kubwa na ngumu kuliko vibanzi vilivyo kwenye macho ya akina Sitta, Sendeka, Selelii, Malecela, Kilango na wenzao wengine wengi.
  Vita hii ya kupambana na boriti na kuviacha vibanzi, ndiyo injili mpya ambayo akina Mengi, Sitta na majemedari wenzao wa kupambana na ufisadi wanaihubiri kwa nguvu kubwa leo hii kwa gharama ya kufifisha na pengine kufisha kabisa juhudi za makusudi za kujenga ustawi mpya wa maridhiano ya kitaifa. Tusubiri tuone nini kitatokea huko tuendako. SOURCE:http://www.freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=10278
   
Loading...