Bora mikono mitupu kuliko mikono michafu inayosambaza kipindupindu | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Bora mikono mitupu kuliko mikono michafu inayosambaza kipindupindu

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Mbonea, Oct 2, 2009.

 1. Mbonea

  Mbonea JF-Expert Member

  #1
  Oct 2, 2009
  Joined: Jul 14, 2009
  Messages: 640
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 33
  [​IMG]
  Hidaya ​
  [​IMG]

  Kwa Waziri wa Mikiki na Makeke,
  Uzitoni Street,
  Bongo.​
  Mpenzi Frank,
  Vipi mpenzi wangu wa moyo? Ni matumaini yangu waendelea na uchoyo wa mapenzi kwa wote isipokuwa mimi. Upande wangu nalalamikiwa ubahili kabisa eti siwezi kumgawia mwingine. Nawaambia hii ni hifadhi ya kitaifa. Ila hifadhi hii haiingiliwi na mbogo wala mwekezaji kutoka nje. Kwa hiyo, nisije nikakuta orodha ya wapenzi hewa katika simu yako mpenzi, nitakuloliondo!
  Nakutania mpenzi maana kwa bahati nzuri, mapenzi yetu hayafanani na ahadi za wanasiasa, tungekuwa tumeshaachana zamani.
  Na sasa nashangaa kusikia watu wanavyojaza wafanyakazi hewa katika mawizara na hata idara ndogo kama hospitali. Kisha wanauita uzembe tu. Uzembe!!
  Kweli katika hospitali moja waweza kujaza wafanyakazi hewa zaidi ya mia tatu kwa uzembe. Haiwezekani.
  Kwa mfano, hapa katika idara yangu, mama bosi akimkuta mende mmoja hapa jikoni atanifokea kwa uzembe na kunitisha kunifukuza kazi kama kawaida yake.
  ‘We Hidaya, kama umechoka kazi si useme tu. Wako wengi wanaotaka kazi hii …’
  Lo, wangeambiwa mawaziri hivi si wangeondoka kila siku. Sisi wadogo tunawajibishwa na walewale wakubwa wasiowajibika hata kidogo. Watu wanaambiwa makazi yao salama kisha wengine wanalipuliwa, nani amewajibika?
  Na hili ni bomu, si mende tu. Mikataba feki inazidi kutula lakini wahusika haoooo wanaendelea na midhifa ya kitaifa tu. Haya na sasa watumishi hewa kibao; tuone kama mhusika mkuu atawajibika kweli.
  Sasa hebu fikiria mpenzi, mende mmoja tu akimendea, limdomo la MB halitulii saa nzima. Mara nyingine naona kwamba chakula chote ni kichungu kwake kama hapati nafasi ya kumaliza sumu ya usiku kwangu mimi au kwa mwingine. Je akute mende mia! Si itakuwa mwisho wa dunia?
  Nataka kusema nini? Mambo yakiwa makubwa namna hii, haiwezekani kuwa uzembe! Mtu amefanya makusudi na aliyeacha hayo aendelee naye amefanya makusudi. Upande wangu siwezi kufaidi mimi zaidi ya kucheka nikiona sura ya MB. Lakini hawa wanaojaza watumishi hewa, wanajaza matumbo yao pia.
  Nadhani ndiyo maana ingawa tunasikia hali ya uchumi duniani ni mbaya sana, na sisi tusio na kitu tunasikia kweli hali ya uchumi ni mbaya, lakini kuna kundi la watu hata hawasikii lolote maana hawatumii pesa zao. Juzi nilishangaa wakati nikimsindikiza MB kwenye mizunguko yake. Nilishangaa kuona huko barabara ya Ali Hassan Mwinyi kila nyumba ya pili imekuwa ghala ya magari ya kuuzwa. Magari yote hayo yananunuliwa na nani wakati hali inapaswa kuwa mbaya? Nani mwenye uwezo huo kama si hao wanaojaza watumishi feki katika idara zao.

  Na wao wanajifunza kutoka kwa serikali yao. Hivi wamepata wapi ghafla pesa zote hizi za kulipa walimu? Wamedai ukata hadi walimu wamekatika sasa mwezi mmoja kabla ya uchafuzi wa mitaa pesa zinadondoka kama mvua za masika! Jamani ee!
  Unakumbuka huko kwetu jinsi walimu walivyokuwa wakilalamika kwamba wajanja wanakwapua mishahara yao na kuyajazilia katika akaunti ya benki kwa muda maalumu ili wale riba. Kama ni hivyo, waliokwapua pesa za walimu wamekula faida kiasi gani? Na sasa pesa zinaonekana. Huu kweli ni uzembe? Ni makusudi kabisa.
  Nadhani nakubaliana kweli na fyatu wako, Makengeza. Bora tungekuwa na uchaguzi kila miaka mitatu. Hata walimu wetu wangelipwa ipasavyo badala ya kuwasotesha hivyo na sisi tungesoma vizuri zaidi.
  Kwa hiyo, kama unavyoona mpenzi, wiki hii nimejaa mabifu kibao. Na mara nyingine sijui hata nifanye nini na mabifu hayo maana ni kama vipele vya joto vilivyosambaa mwili mzima. Hujui uanze kukuna wapi, uache wapi.
  Kwa mawazo yangu tumezoea uovu kiasi kwamba hatuoni. Ni kama alivyosema mwalimu wetu, katika nchi ya vipofu, mwenye chongo ni mfalme. Lakini hapana. Sisi si vipofu. Hatutaki kufumbua macho tu.
  Nakumbuka siku moja, mgeni alikuja hapa. Baada ya kushika wiski zao sawasawa, yule mgeni alianza. Naona ni rafiki yake bosi siku nyingi maana bosi alikuwa anacheka tu.
  ‘Unajua mheshimiwa mnafanya kosa moja kubwa.’
  ‘Kosa gani tena?’
  ‘Mnadhani kila ishu inatatuliwa kwa warsha tu. Kama wanaua watu hospitali kutokana na ujuzi mdogo, peleka warsha ili wajifunze kutoua.’
  ‘We Bwana mbona chumvi hizo?’
  ‘Sivyo. Wahasibu wakivuruga hesabu na kujaza wafanyakazi hewa, wapelekwe kozi ya kujifunza kutojaza watu hewa. Kweli walikuwa hawajui? Nangoja mwite semina elekezi siku yoyote kwa ajili ya mafisadi (maana fisadi hawezi kwenda kitu kidogo kama warsha tu) ili wafundishwe ubaya wa kufisadi.’
  ‘Wazo zuri hili. Naweza kupeleka kwa mkuu.’
  ‘Unaona sasa? Badala ya kutambua kwamba hawa wana roho ya kutu na watatuambukiza pepopunda na kutu zao zote, hivyo wakwanguliwe ili kutu zote zitoke, unataka kuwalipa tena ili kuwaambia yale wanayojua tayari lakini hawataki kusikia maana wameshakuwa kama Wamaasai na ng’ombe. Mali yote ya taifa ni mali yao ndiyo maana hawawezi kuiba. Wanaweka mali yao tu mfukoni.’
  ‘Sasa wewe unataka kufanya nini?’
  ‘Katika kampuni yangu, mtu akifanya makosa kama hayo, nje!! Akitaka kunishtaki poa kabisa. Angalao kwa wakati anaoshtaki anasota na yeye na sisi tunapata muda wa kufanya mambo ya maana ndani ya kampuni yetu. Na wengine wanaogopa kuiba kwa sababu vitisho havimbadilishi mtu hadi aone mwenzie kweli amepatikana.’
  ‘Kwa staili hii utajaza mahakama bure.’
  ‘Si bure. Wewe unawajaza mahakama maana watu wamekatishwa tamaa na wizi wote huo hadi hawana njia ya kujikimu zaidi ya kuiba. Nakuhakikishia mkifunga wezi wakubwa (yaani mafisadi) kumi tu, mtakuwa mmepunguza wezi wadogo elfu moja.
  Na watu pia watajifunza kwamba hawa si wa kuheshimiwa na kushangiliwa kwa sababu wanadondosha mabaki ya ulaji wao ili waweze kula tena.’
  ‘Hapa unasema ukweli kidogo. Na wao wataacha ufisadi wao pia.’
  ‘Unafikiri wamejifunza kutoka kwa akina nani?’
  Bosi akachangamka ghafla.
  ‘Tena hawa wananichosha kabisa. Mimi si Waziri wa Mikiki! Basi inabidi nishughulikie madai kibao ya fidia. Nakuambia mara nyingi wa kwanza kutokea ni wale wasiostahili kabisa. Na wa kwanza kwenda kwenye vyombo vya habari na kupiga kelele wamedhulumiwa ni walewale wasiostahili fidia kabisa bali wanataka kukwapua ya wenzao.’
  ‘Wamejifunza kutoka kwa akina nani? Hata kwangu. Wa kwanza kuleta maproposal ya kazi za kufanya ni walewale ambao hawafanyi kitu. Wale wanaofanya kitu hawana muda wa kuandika miproposal.’
  ‘Sasa kwa nini vyombo vya habari havitaki kuchambua hivi? Wanatuchambua sisi tu.’
  ‘Ni kweli mheshimiwa lakini mnajitakia wenyewe mnavyotetea yasiyoteteka. Kwa hiyo mmejaza imani kwa wananchi kwamba hata kama unasema ukweli kwamba wengine hawastahili, ni nyinyi mnaosema uongo. Watu wamezoea uongo wenu kiasi kwamba wanaona kila kitu ni uongo.’
  ‘Na wewe nawe umezidi!’
  ‘Kawaulize wananchi! Si ajabu watawachagua tena maana hawajaona mwingine. Lakini haina maana wanawaamini hata kidogo. Wanakubali yaishe tu!’
  ‘Sasa rafiki yangu umekuja nyumbani kunitukana au …’
  ‘Basi yaishe! Waonaje mpira wa Arsenal mwaka huu?’
  Waliendelea na mpira lakini nadhani hoja zilimwingia bosi; maana baada ya yule jamaa kuondoka, bosi kakaa kimya muda mrefu. Mwisho akasema kwa sauti ndogo.
  ‘Hivi kweli mwanasiasa anaweza kuishi kwa kusema ukweli? Mikono mitupu italambwa kweli?’
  Lakini kwa mawazo yangu mpenzi, kwa nini isilambwe? Bora mikono mitupu kuliko mikono michafu inayosambaza kipindupindu.
  Akupendaye na moyo madhubuti usio na hewa hata kidogo
  Hidaya.
   
Loading...