Bongo hapo zamani:Lipumba niliyekutana nae akiwa na chupa ya maji mkononi.

Konzo Ikweta

JF-Expert Member
Oct 3, 2013
735
1,464
Ndugu zangu,

Nimepata kuandika hili, kuwa kwangu mimi, Profesa Ibrahim Rehani Lipumba ni mmoja wa wanasiasa makini na wenye misimamo, tunapozungumzia siasa za upinzani hapa nchini.

Profesa Lipumba alipata kung’olewa na chama chake cha CUF. Hata hivyo, Afrika miti mingine huachwa izeeke na kuanguka yenyewe. Ni kama mibuyu, kuing'oa kwake lazima iache kishindo na ardhi kutikisika.

Kwa mimi niliyebahatika kufuatilia kwa karibu siasa za nchi hii sikuliona lile la Profesa kung'olewa CUF kuwa ni jambo jepesi. Niliandika, kuwa wenye kumbeza Profesa Lipumba ikiwamo humu mitandaoni hawajisumbui kuyasoma ya jana yenye kutusaidia kuyatafsiri ya leo na kutusaidia kuyabashiri yatakayotokea kesho.

Kwa kuyaangalia ya jana, na kwa kumwangalia Profesa, tunaona, kuwa kwenye siasa za nchi hii, Profesa Lipumba si kama mti wa mpapai wa kuweza kukatwa kwa kiwembe. Profesa ni mbuyu mkongwe uliota mizizi ikasambaa. Kuung'oa kwakwe kunahitaji si shoka, bali mashoka. Na lazima mengine yakatike.

Naam, kung'olewa kwa Profesa ilikuwa ni lazima kuache majeraha makubwa na yatakayochukua muda mrefu kupona, si tu kwa CUF, bali kwa siasa za upinzani hapa nchini.

Maana, niliandika, kuwa simwoni Profesa atakayehamia CCM, bali atakayebaki mpinzani wa CCM nje ya wapinzani wa CCM.

Ni nani basi Profesa Ibrahim Lipumba?

Ni ukweli, kuwa Profesa Lipumba kwa wakati tulio nao, ni mwanasiasa pekee kwenye upinzani na pengine kwa nchi nzima mbobezi kwenye masuala ya kiuchumi na anayetambulika kimataifa.

Kwenye siasa zetu, uchumi ni moja ya ajenda zinazopaswa kuwa sehemu ya mijadala muhimu katika kupima uwezo wa wagombea. Ni katika kutafuta majibu ya ni kwa namna gani wagombea wamejipanga kimikakati katika kutuambia sio tu watafanya nini , bali ni kwa namna gani, kwenye kututoa hapa tulipo na kwenda kwenye hali bora zaidi kiuchumi, kama taifa.

Nakumbuka, kwenye Uchaguzi wa mwaka 2005, Vyombo vya Habari vilikazana kuandika habari za JK na Freeman Mbowe. Ikawa ni habari za CCM na CHADEMA kila kukicha. Vikasahau, kuwa kulikuwa na mgombea wa urais aliye kwenye mbio na mwenye umuhimu pia, maana, kuna wengi walimkubali. Yawezekana jambo hilo lilifanywa na media yetu kwa bahati mbaya au kwa makusudi. Kumsahau Profesa Ibrahim Haruna Lipumba aliyekuwa wa Chama Cha Wananchi ( CUF).

Kwangu mimi, mwaka ule wa 2005, katika wote walioshiriki mbio za Urais, Prof. Lipumba ndiye alikuwa mwenye uzoefu zaidi wa njia ya urais ambayo wenzake na yeye walikuwa wanaikimbilia.

Ikumbukwe, Profesa Lipumba ana uzoefu wa kinyang'anyiro cha urais tangu mwaka 1995. Ilikuwa ni kwenye Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi.
Ikumbukwe pia , Profesa Lipumba anaingia kwenye historia ya kushiriki mdahalo wa kwanza wa wagombea urais akiwa mpinzani. Wenzake wawili; Augustino Mrema na Gideon Cheyo ( Bwana Mapesa) waliingia kwenye mdahalo ule wakipambana na Ben Mkapa, lakini, hatuwezi leo, kwa yakini, kusema hapa kuwa walibaki na wamebaki kwenye upinzani na chama tawala.

Kwenye mdahalo ule wa wagombea urais wa mwaka wa 1995, Profesa Lipumba aliiibuka wa pili kwenye mdahalo kwa kupewa alama za juu kutokana na maoni ya wananchi yaliyokusanwa na mashirika ya habari ya kigeni mara baada ya kumalizika kwa mdahalo.

Ni mdahalo huo wa 1995 uliomwacha Ben Mkapa akiongoza na Mrema akiambulia nafasi ya tatu, huku John Cheyo akikamata mkia.

Bila kuchezesha kalamu, kiukweli Profesa Lipumba alikuwa na anabaki kuwa ni mpiganaji mahiri kwenye harakati za kisiasa. Mwaka 1995 aliingia kwenye mbio za Urais kama ‘ Profesa’. Hilo lilikuwa kosa, akalirudia tena mwaka 2000. Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, Profesa Ibrahim Lipumba alionekana zaidi kama ‘ Ibrahim Lipumba’. Profesa aliamua kushuka chini, kuwa na watu na kuongea lugha yao.

Nakumbuka kukutana na Profesa Lipumba ana kwa ana kwa mara ya kwanza mwezi Oktoba 2005, wiki kadhaa kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu. Ni pale Isimila Hotel, Iringa. Ni Hotel ya kawaida kabisa. Ndugu yangu Saed Kubenea alikuwa kwenye msafara wa kampeni wa Profesa Lipumba, na ni Saed Kubenea aliyefanya maandalizi ya mimi kukutana na Profesa Lipumba.

Ilikuwa siku ya Alhamisi, nilifika pale Isimila Hotel kunako saa tatu asubuhi. Ni siku ya kutoka jarida ls Rai ( Ya wakati huo na mimi nilikuwa mmoja wa waandishi wa makala).

Aliponiona, Profesa Lipumba alinijia akiwa mwingi wa tabasamu;
“ Kumbe, ndiye wewe Maggid!” Alitamka huku akionyesha furaha. Mkono wa kushoto alikamata jarida la Rai na chupa ya ‘Maji Afrika’. Saed Kubenea alisimama kando, mbali kabisa na sisi ili kupisha mazungumzo ya Profesa na mimi.

Kwenye mazungumzo yetu nilimwona Profesa Lipumba kuwa ni mtu wa kawaida sana. Tukiwa tumesimama, kuna wakati kwenye mazungumzo yetu, Lipumba alikuwa akipukuta vumbi kwenye suruali yake kwa kutumia gazeti la Rai.

Kwa kawaida, mwanasiasa huyu Lipumba anaongea kwa mpangilio na kwa kutulia. Kushiriki kwake katika uchaguzi wa 1995, 2000 na 2005 kumempa uzoefu zaidi katika vinyang’anyiro vya urais. Lipumba ana uwezo na kipaji cha kufafanua mambo magumu na yakaeleweka kwa mtu wa kawaida.

Mwaka ule wa 2005, kuna wakati nilimsikia Lipumba akitoa mfano wa ajira elfu moja zenye uhakika kwa vijana zinavyoweza kuathiri maisha ya mama mwuza vitumbua. Profesa Lipumba alitamka;

“ Ndugu zangu, bila ya vijana hawa kuwa na ajira na kipato , mama huyu atashinda na vitumbua vyake vikimtazama !.”

Hakika, Lipumba ana uwezo pia wa kutengeneza sentesi fupi na zenye kishindo; Mwaka ule 2005 nilimsikia akitamka;

”Wananchi nikopesheni kura zenu, nitawalipa maendeleo!” Hizi ni baadhi tu ya nguvu za Profesa Ibrahim Lipumba katika rethorik, sanaa ya kuzungumza.

Tuliofuatilia kampeni za Profesa za urais, tumeona kuwa huwa na sura za mikakati ya kijeshi. Mwaka 2005 tulimwona Lipumba akianza kampeni kwa kuanzia na kule ambapo aliamini kuna matumaini ya kupata ushindi, matumaini ya kuvuna kura.

Itakumbukwa, 2005 Lipumba alianza kampeni zake kwenye ‘ngome’ ya CUF kwa wakati huo. Ni mikoa ya Kusini; Lindi na Mtwara. Huko Profesa ‘alipiga kambi’ ya zaidi ya juma moja akifanya kampeni.

Baada ya kule kusini, tulimwona Profesa akichagua maeneo ya kwenda. Na kila alikokwenda kulikuwa ni kule ambako, CUF ilionekana kuungwa mkono.

Mwaka 2005, staili ya kampeni ya Profesa Lipumba ilibadilika pia. Profesa Lipumba alionekana kuwavutia zaidi wasikilizaji na watazamaji kwenye hotuba zake.

Lipumba baada ya kuongea majukwaani alishuka chini na kuongea na wapiga kura akiwa karibu nao sana. Kila mahali alipofika, aliunganisha masuala makubwa na yale ya mahali hapo. Aliachana na staili ya kutumia muda mwingi kukishutumu Chama Cha Mapinduzi bila kuwafafanulia wapiga kura yeye akiingia madarakani atafanya nini na kwa namna gani. Hivyo, kwa mwaka ule wa 2005, Profesa Lipumba alisisitiza zaidi nini angekifanya, yeye na chama chake, na kwa namna gani. Kile ambacho CCM wameshindwa kukifanya.

Kabla ya mikutano ya hadhara, Profesa alifanya jitihada za kuikaribia jamii ya mahali hapo. Mathalan, Profesa Lipumba alikwenda sokoni . Huko aliongea na wananchi, aliuliza bei za vyakula. Kule Musoma tukamwona Profesa akipima nguo kwa fundi cherehani, alitaka fundi huyo amshonee suti yake. Pale Bunda Lipumba akamtembelea nyumbani kwake Mzee Raphael, mwanachama wa CUF wa miaka mingi. Kule Geita tulimwona Lipumba akizungumza na wachimbaji madini wadogowadogo akiwa kwenye machimbo yao.

Ndio, tulimwona Lipumba akibeba mawe kuweka chini ya tairi na hata kusukuma gari lake kule Kondoa . Ni wakati msafara wake ulipokwama njiani. Tulimwona Lipumba akishiriki shughuli ya mazishi kule Mafia na Kagera. Kwamba kila alipokwenda kukampeni, Profesa Lipumba alitafuta habari kuhusiana na mahali hapo, ikiwamo pia habari mbaya kama misiba. Kwenye misiba kuna wapiga kura.

Hii nayo ni staili ya kampeni aliyoionyesha Lipumba katika uchaguzi mwaka 2005. Kushuka chini kwa watu. Mgombea usijikite tu kwenye kukusanya watu, unapaswa pia kuonekana iliko mikusanyiko ya watu, kuongea nao katika hali za kawaida, na si za maonyesho kwa vyombo vya habari.

Na bila shaka, nguvu za Profesa Lipumba za mwaka 2005 na mavuno makubwa ya kisiasa aliyovuna yeye na chama chake, hayakutokana na Profesa peke yake.

Nilipokutana naye mwaka ule wa 2005 pale Isimila, Profesa hakusita kuniambia, kuwa alijivunia nguvu za chama chake, CUF. Kwamba kimejitahidi sana kuweka mizizi chini waliko watu.

CUF ilitoka wapi?

Chama cha CUF kiliundwa Mei 28, 1992. Ni chimbuko la kuunganishwa kwa Chama cha kutetea haki za Wananchi (Civic Movement) kwa upande wa bara na chama cha KAMAHURU cha Zanzibar.

CUF imetokana na vuguvugu la mageuzi nchini. Ingawa NCCR-mageuzi kilikuwa ni chama cha kwanza cha upinzani, CUF kilikuwa chama cha pili kusajiliwa katika mfumo wa vyama vingi baada ya CCM.

Hii ilitokana na sura yake ya muungano kuonekana dhahiri. Hii ni moja ya nguvu kubwa za CUF. Hakuna anayejisumbua kuweka hadharani, ukweli kuwa, kwa sasa, CUF ni chama pekee cha upinzani, chenye uhakika wa kuwa na wawakilishi bungeni kutoka Unguja, Pemba na Bara. Na kwa upande wa Bara, Profesa Lipumba, kutokana na kuaminika kwake, amekuwa mhimili muhimu wa kuhakikishia CUF viti upande wa Bara.

Chadema, na NCCR, pamoja na umaarufu wao Bara, vyama hivi viwili, havijapata kuwa na hakika ya kuvuna viti vya Ubunge Unguja na Pemba. Na siku ikitokea, hiyo itakuwa ni habari kubwa.

Naam, miaka zaidi ya 18 imepita tangu nikutane na kuongea na Profesa Lipumba. Mengi yametokea, ikiwamo ya yeye mwenyewe Profesa kuachia ngazi ndani ya CUF kwa kujiuzuru uongozi na kubaki mwanachama, kisha baada ya kuombwa, kama anavyosema, ameamua kurudi kugombea nafasi yake na kuibua sintofahamu ya ndani ya CUF. Hii ni moja ya changamoto ya demokrasia ya ndani ya vyama- Intra party democracy.

Nitapenda siku moja nikutane tena ana kwa ana na Profesa, nizungumze nae, ni katika kuendelea kujifunza, hata kwangu.

Maggid,

IMG-20190804-WA0029.jpeg
 
Ujinga uliochanganyika na udwanz...MTU alikimbia chama akakimbilia Rwanda badae akarudi bila aibu wenzake wamepigania ubunge yeye anajirudishwa tena kwakusukumizwa na watu Fulani!! Amewahi kusimamia chama kikapata ushindi gani?? Usiandike upoyoyo kwa mahaba binafsi simamia ukweli kama ww wakiume kama wakike basi itakuwa unaongozwa na mahisia yako ambayo nivizuri umweleze mwusika direct sio huku jukwaa lenye wasomi
 
Ujinga uliochanganyika na udwanz...MTU alikimbia chama akakimbilia Rwanda badae akarudi bila aibu wenzake wamepigania ubunge yeye anajirudishwa tena kwakusukumizwa na watu Fulani!! Amewahi kusimamia chama kikapata ushindi gani?? Usiandike upoyoyo kwa mahaba binafsi simamia ukweli kama ww wakiume kama wakike basi itakuwa unaongozwa na mahisia yako ambayo nivizuri umweleze mwusika direct sio huku jukwaa lenye wasomi
Jenga hoja
 
Kuvuruga upinzani ,kushirikiana na adui ,kuwa mamluki ,kuendesha siasa za uchumi tumbo nakushiriki kuhujumu timu yako ndio ukongwe wa siasa ? .
 
Lipumba,Mbowe, Zitto, Seif na JK wote ni watoto wa Mjini ndio sababu Awamu ya Nne ilikuwa Ujanja Mwingi


Mbowe pamoja na Mikwala yote alipewa Msamaha wa kodi kwny baishara zake ikiwemo Bilicanus na Hotel zake zilipata semina nyingi za Serikal na hata Tanzania Daima ilikula Tenda nyingi za matangazo za Serikal

Lipumba pamoja na Mikwala yote alikula sana u Facilitator wa Semina za WB na IMF kwa connection za Don wa wakati huo

Maalim na Mikwala yote alikula Umakamu wa Kwanza wa Rais SMZ

Zitto na Mikwala yote kila Kamati zenye minofu za Bunge alikuwa hakosi na Trip za Nje za Bwana Mkubwa alikuwepo

James Mbatia akaponzwa njaa kwa kuchapwa Ubunge wa Ikulu wa Nafasi Maalum

Mzee Warioba na Butiku vumbi la uraiani lilipozidi wakapigwa Tume maalum ya Katiba ya kula laki 5 kwa siku pamoja na Pole pole wakajikuta hawana muda was kuandika Waraka kama kina Mzee Makamba
 
Kama mwandishi wa bandiko hili alilenga kumjenga Profesa Lipumba basi nadhani atakuwa ameghafilika, maana sio tu anazidi kumshusha Lipumba bali hata yeye mwenyewe (Mwandishi) kwa kuandika porojo hizi pia anajishusha. Katika watu ambao wameshusha hadhi ya 'uprofesa' hapa nchini yeye ni mmoja wao. Kwa aliyoyafanya Profesa wetu huyu nchini, mwandishi na wengine wote walio karibu naye wanapaswa kutahayari badala ya kuona fahari.
 
Ujinga ni nini? Ujinga ni kuiwa mwandishi mzuri kama wewe anayeandika upuuzi mtupu kama huu..
Hivi hujaelewa tu kuwa huyo Lipumbavu lako lilijitowa lenyewe CUF na kurudishwa kwa usimamizi wa nguvu za dola?
 
Back
Top Bottom