Bomani: Serikali isione aibu kuondoa Muswada wa Katiba | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Bomani: Serikali isione aibu kuondoa Muswada wa Katiba

Discussion in 'KATIBA Mpya' started by BAK, Apr 14, 2011.

 1. BAK

  BAK JF-Expert Member

  #1
  Apr 14, 2011
  Joined: Feb 11, 2007
  Messages: 70,420
  Likes Received: 81,471
  Trophy Points: 280
  Bomani: Serikali isione aibu kuondoa Muswada wa Katiba
  Wednesday, 13 April 2011 21:05


  [​IMG]
  Mwanasheria Mkuu Mstaafu wa Serikali Jaji Mark Bomani

  Ramadhan Semtawa na Exuper Kachenje
  MWANASHERIA Mkuu Mstaafu wa Serikali Jaji Mark Bomani, ameitaka Serikali, kutoona aibu kuuondoa Muswada wa Marejeo ya Katiba bungeni akionya kwamba kinyume chake, utaivuruga nchi.Jaji Bomani alitoa wito huo hivi karibuni alipokuwa akizungumza na gazeti hili katika mahojiano maalumu ofisini kwake, Dar es Salaam.

  "Serikali isione aibu kuondoa muswada huo, isije ikafikiri labda kuuondoa itakuwa ni aibu la... Itakuwa imeonyesha usikivu na umakini wa kusikiliza hoja za wananchi walio wengi. Katiba si kitu cha kuchezea hata kidogo," alisema.Jaji Bomani alifafanua kwamba si vizuri kwa muswada juu ya jambo zito kama la Katiba, ukatolewa kwa hati ya dharura na kuhoji: "Hiyo pupa ya nini?Kutokana na uharaka huo ndiyo maana hata muswada wenyewe umejaa makosa na dosari.''

  "Kwa hiyo kwa ushauri wangu, muswada uliokwisha chapishwa uondolewe (withdrawn), kwa maelezo kwamba umekwenda nje ya mstari na kwamba utaletwa mwingine utakaokuwa umezingatia maoni mbalimbali yaliyokwishatolewa.''Kwa mujibu wa Jaji Bomani, muswada huo tayari umekiuka taratibu za awali na kusisitiza: "Kama Serikali ikiendelea kushinikiza uendelee, wapo watu wanaoweza kupinga kwa njia hasi na chanya. Kwa maoni yangu, kila kitu lazima kiangaliwe upya."

  Mwanasheria huyo alisema muswada huo umetenga mambo nyeti yasijadiliwe, kitu ambacho alisema ni kosa, kwani Katiba mpya inapaswa kugusa kila eneo... "Kwa maneno mengine, masuala kama aina ya Muungano, muundo wa Serikali, kazi na muundo wa Bunge, aina ya madaraka ya Serikali za Mitaa, aina ya Mahakama na kazi zake n.k."
  Alisema mambo hayo yote ni lazima yafikiriwe na kufanyiwa mabadiliko au marekebisho itakavyolazimu na kusisitiza: "Kwa mtazamo huu, kila kitu kinastahili kujadiliwa."

  Njia za kuanza mchakato
  Jaji Bomani alisema kuna njia nyingi za kujadili suala hilo na mambo mawili lazima yazingatiwe; "Kwanza wananchi lazima washirikishwe vya kutosha ili Katiba itakayotokana na mjadala huo waione kuwa ni yao maana walishiriki katika kuijadili."

  Pili, alisema ni lazima mchakato wenyewe uendeshwe kwa makini ili kufika mahali ambako itapatikana Katiba mpya yenye tija: "Maana yangu ni kwamba pamoja na kuwashirikisha wananchi, lazima wahusishwe pia wataalamu na watu wenye uzoefu kwani hatuanzii (zero) sifuri."

  Alisema haiwezekani kuacha umma wa watu zaidi ya 40 milioni kujadili na kupitisha Katiba.'' Lazima uwepo utaratibu ambao utawezesha kufikia lengo la katiba kihalali,''alisema.
  Kwa mujibu wa Jaji Bomani njia ya Tume maalumu kukusanya maoni ya wananchi wa makundi mbalimbali na baadaye kutoa mapendekezo, ni njia mojawapo inayoweza kufanikisha lengo la kupata katiba mpya.

  Muundo wa Tume
  Akizungumzia muundo wa Tume, Jaji Bomani alisema lazima iwe kubwa ya kutosha ili ijumuishe makundi na rika mbalimbali."Lakini isiwe kubwa mno kiasi cha kuifanya ishindwe kufanya kazi zake kwa tija na kupata muafaka," alisema. Kuhusu muda wa tume hiyo kukamilisha kazi yake, Jaji Bomani alisema: "Nchi yetu ni kubwa. Ili angalau sehemu nyingi zifikiwe muda wa kutosha unahitajika, labda kati ya mwaka mmoja na miwili. Ni lazima pia izingatiwe kwamba wajumbe wa tume hiyo wana shughuli zao, haiwezekani ukapata watu makini ambao watakuwapo wakati wote."

  Uandaaji hadidu za rejea
  Akizungumzia suala la hadidu za rejea kwa tume hiyo, Jaji Bomani alisema: "Ni mapema mno kwa Serikali kuandaa hadidu za rejea (terms of reference) na kwamba kilichotakiwa kufanyika ilikuwa ni kwa Rais kuchagua kamati ambayo ndiyo ingeandaa hadidu za rejea baada ya kushauriana na vikundi mbalimbali."
  Alisema kamati hiyo ndiyo ambayo ingemshauri Rais juu ya hadidu za rejea na mambo mengine husika na huo ndiyo ungekuwa msingi wa kuandaa muswada wa kupeleka bungeni: "Kamati ya namna hii yenye wajumbe takriban 30 ingeweza ikapewa, tuseme, miezi mitatu kukamilisha kazi hiyo ya kuandaa hadidu za rejea."

  Ushauri wa Dk Salim, Butiku kuhusu muswada
  Katika hatua nyingine waasisi wawili wa CCM wamesema kuwa yanayotokea sasa hayaepukiki na kushauri mjadala huo uendelee kwani ni wakati muafaka kuwapo.Waasisi hao, aliyekuwa Katibu Mkuu wa uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), Dk Salim Ahmed Salim na Mwenyekiti wa Mfuko wa Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku walitoa maoni hayo jana kwa nyakati tofauti nje ya ukumbi wa Nkurumah, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam walipohudhuria kongamano la tatu la Kitaaluma la Kigoda cha Mwalimu Julius Nyerere.

  "Yanayotokea sasa hayaepukiki, unajua nchi yetu kwa miaka mingi ilikuwa katika mfumo wa chama kimoja cha siasa, lakini sasa tupo katika mfumo wa vyama vingi na haujawa wa miaka mingi, hivyo tunayoyaona yanatokea ni kutokana na mfumo huo na hayaepukiki," alisema Dk Salim.

  Hata hivyo, Dk Salim alionya kuwa itakuwa hatari kwa Watanzania kutumia hali hiyo na kuhatarisha amani ya taifa na kuwagawa watu kwa misingi ya dini, rangi, itikadi za kisiasa au kabila na kuwataka wasiwe wepesi kulaumu mataifa ya kigeni, badala yake wajizuie kufanya makosa yanayoweza kutumiwa na nchi hizo kujinufaisha.
  Alisema badala yake, katika kujadili hoja au jambo lolote, ni muhimu kila mmoja kufanya hivyo akiweka mbele maslahi ya taifa kwa kuwa Tanzania ni ya Watanzania wote.

  Alisema wakati wa uhai wake, Mwalimu Nyerere aliweka misingi bora ya utaifa kwa maslahi ya Watanzania wote, hivyo ni muhimu misingi hiyo ikadumishwa na ndiyo sababu ya uwepo wa tamasha la Kigoda cha Taaluma cha Mwalimu Nyerere.

  Kwa upande wake, Butiku alisema: "Napenda, nashauri, tuzungumze kuhusu Katiba, maana iliandikwa muda mrefu na watu wengi wapya. Labda misingi imepitwa na wakati au haieleweki kwao."
  Alishauri kuwa mazungumzo hayo kuhusu Katiba yafanyike kwa uhuru na kwamba mawazo yatakayotolewa yaonyeshe kama inahitajika mpya au la na kusiwapo kulazimishana.

  "Mazungumzo yafanyike kwa uhuru, mawazo yaonyeshe kweli tunahitaji Katiba au la, yatuonyeshe kwa uwazi waliyoamua Watanzania na tusilazimishane," alisema Butiku.Alisema kuwa zipo kauli alizoziita za hapa na pale ambazo si zake, zinazoeleza kuwa huenda mambo hayaendi vizuri kwa sababu ya Katiba iliyopo, huku wengine wakieleza kuwa ingekuwa vizuri kuwapo kwa maelewano kuhusu sheria mama, yaani Katiba, lakini akasema haoni kama Katiba yote ina matatizo, bali maeneo machache.

  Hata hivyo, alisema ni jukumu la Watanzania wenyewe kuamua iwapo wanataka mabadiliko ya Katiba au vinginevyo."Katiba kama itatuzuia kufikiri, kutenda au kuamua, hapo nafikiri ni sahihi kuangaliwa upya, lakini kama si hivyo, hiyo ni Katiba tu, inaweza kuwa karatasi tu, tatizo likawa utekelezaji wa yaliyoandikwa.
   
 2. Nyani Ngabu

  Nyani Ngabu Platinum Member

  #2
  Apr 14, 2011
  Joined: May 15, 2006
  Messages: 73,651
  Likes Received: 35,408
  Trophy Points: 280
  Wala nchi yetu si kubwa kihivyo bana....
   
 3. Aza

  Aza JF-Expert Member

  #3
  Apr 19, 2011
  Joined: Feb 23, 2010
  Messages: 1,672
  Likes Received: 34
  Trophy Points: 145
  litakuwa jambo jema sana wakitoa huo "uharaka" wao
  nautilia mashaka sana kwanini wanalazimisha?
   
Loading...