Bodi ya Mikopo (HESLB) imetoa Tshs 459/- bilioni kama mikopo ya Wanafunzi

figganigga

JF-Expert Member
Oct 17, 2010
25,658
55,484
10584081_835477716563204_8051305505711873150_n.jpg

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetoa jumla ya Tshs 459/- bilioni kama mikopo ya elimu ya juu kwa wanafunzi 122,486 wanasoma katika vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi katika mwaka wa masomo 2015/2016.

Hii ni idadi kubwa zaidi ya wanufaika na fedha kuwahi kutolewa tangu kuanzishwa kwa Bodi mwezi Julai, 2005 na kwa ujumla, katika historia ya utoaji wa mikopo nchini. Fedha hizi zimetolewa kati ya mwezi Novemba, 2015 na Januari 10, 2016.

Katika mwaka uliopita wa masomo, 2014/2015, Serikali kupitia Bodi ilitoa jumla ya Tshs 341/- bilioni zilizowanufaisha wanafunzi 99,069.

Kati ya fedha zilizotolewa, jumla ya Tshs 199.7 bilioni zinakwenda kwa wanafunzi 53,537 waliojiunga na masomo kwa mwaka wa kwanza mwezi Novemba, 2015 katika vyuo mbalimbali na Tshs Tshs 259.1 bilioni zinalipwa kwa wanafunzi 68,916 wanaoendelea na masomo, yaani mwaka wa pili, wa tatu na kuendelea katika vyuo vya umma na binafsi.

Kwa mujibu wa taarifa ya Bodi kwa vyombo vya habari iliyotolewa Dar es Salaam leo (Jumatano, Januari 13, 2016), kundi kubwa katika ya wanafunzi waliopata mikopo ni wale wanaosoma programu za kipaumbele ambazo zimetajwa katika mwongozo (Guidelines) uliotolewa na Bodi mwezi Mei mwaka jana, 2015.

Programu hizo ni Udaktari wa Binadamu, Udaktari wa Meno, Udaktari wa Wanyama, Ufamasia na Uuguzi na Ualimu wa Masomo ya Sayansi na Hesabu na Uhandisi wa Umwagiliaji. Wanufaika wengine ni yatima na walemavu.

Katika hatua nyingine, Bodi ya Mikopo inatoa wito kwa waajiri katika taasisi za umma na binafsi nchini kuhakikisha wanazingatia matakwa ya sheria iliyoanzisha Bodi inayowataka kuwatambua waajiriwa wao ambao ni wanufaika wa mikopo inayotolewa na Bodi; kukata sehemu ya mishahara yao na kuwasilisha kwa bodi kama marejesho.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Bodi, Kifungu cha 20 (1) (c) cha sheria ya iliyoanzisha Bodi (Higher Education Students’ Loans Board Act (as amended)), kinawataka waajiri kuwatambua waajiriwa, kuijulisha Bodi kwa maandishi ndani siku 28 tangu wapate ajira. Aidha, Kifungu cha 20 (2) cha sheria hiyo, kinawataka waajiri, baada ya Bodi kuthibitisha kuwa muajiriwa ni mnufaika wa mikopo ya Bodi, (mwajiri) kuitaarifu kuitaarifu Bodi, ndani ya siku 30 za ajira yake na kukata makato kutoka katika mshahara wa mwajiriwa na kuyawasilisha Bodi ndani ya siku 15 baada ya kila mwisho wa mwezi.

Taarifa hiyo imesisitiza kuwa waajiri wote wanapaswa kutimiza matakwa hayo ya kisheria na kuwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ameanza kukagua taaasisi za umma kama zinazingatia matakwa haya ya kisheria.

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) ni Taasisi ya Serikali iliyoanzishwa kwa mujibu wa Sheria Na. 9 ya mwaka 2004 na kuanza kazi rasmi mwezi Julai, 2005. Bodi ina majukumu kadhaa, lakini mawili makubwa ni kutoa mikopo kwa wanafunzi watanzania wahitaji; na kusimamia urejeshaji wa mikopo kutoka kwa wanufaika wa mikopo.
 
Kama CAG anafuatilia taasisi za serikali ambazo haziwakati marejesho wanafaika,nani anafuatilia sekta binafsi ambayo ndio imewaficha wengi ambao hawalipi?
Kila mtu akupe,sio wengine walipe na wengine wapete tu.Huo ni wizi wa kuaminiwa.
Serikali ikusanye kila hela iliyohalali yake,toeni double standards
 
Kama CAG anafuatilia taasisi za serikali ambazo haziwakati marejesho wanafaika,nani anafuatilia sekta binafsi ambayo ndio imewaficha wengi ambao hawalipi?
Kila mtu akupe,sio wengine walipe na wengine wapete tu.Huo ni wizi wa kuaminiwa.
Serikali ikusanye kila hela iliyohalali yake,toeni double standards
Ninakubaliana na wewe!

Serikali lazima itafute njia mbadala za kufuatilia hata waajiriwa wa sekta binafsi.

Hati ya kujiandikisha kama mlipa kodi TRA (TIN) ni muhimu sana katika kutambua sekta binafsi.
 
Back
Top Bottom