Binti wa Kingindo alinitoa jasho, lakini subira, uvimilivu na ubunifu vikalipa | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Binti wa Kingindo alinitoa jasho, lakini subira, uvimilivu na ubunifu vikalipa

Discussion in 'Mahusiano, mapenzi, urafiki' started by vukani, Jul 30, 2012.

 1. vukani

  vukani JF-Expert Member

  #1
  Jul 30, 2012
  Joined: Dec 30, 2009
  Messages: 245
  Likes Received: 9
  Trophy Points: 35

  Ilikuwa ni mwaka 1999 baada ya kuwa nimetumikia shirika la umma kwa takribani miaka 20 nilijikuta nikiwa miongoni mwa wafanyakazi 70 wa shirika hilo tuliotupwa nje ya ajira kwa kile kilichoitwa ridandansi, ili kulinusuru shirika hilo ambalo lilianza kuyumba kutokana na ushindani wa kibiashara baada ya serikali kufungua milango kwa wawekezaji kutoka nje.

  Baada ya kupata mafao ambayo hata hivyo hayakulingana na muda niliotumikia shirika hilo, nilikaa chini na kuanza kutafakari mustakabali wa maisha yangu ya baadae na familia yangu. Nilikuwa bado naishi nyumba ya kupanga nikiwa na mke na watoto wawili, wa kwanza wa kike aliyekuwa na miaka 5 na wa pili wa kiume aliyekuwa na miaka 2. Nilikuwa na jukumu zito la kuhakikisha watoto wangu wanapata elimu bora, Je hilo litawezekana baada ya kupoteza ajira? Nilijiuliza.

  Katika kipindi cha miaka hiyo ishirini niliyofanya kazi katika shirika hilo, sikubahatika kujenga, ingawa nilifanikiwa kununua kiwanja maeneo ya Tabata Segerea, ambapo palikuwa ni kama porini wakati huo, tena kiwanja chenyewe kilikuwa ni cha mkopo ambao niliumaliza mwezi mmoja kabla sijapewa ridandansi. Ukweli ni kwamba sikubahatika kujenga kutokana na maslahi kuwa madogo, kwani tulikuwa tukilipwa mshahara mdogo na kulikuwa hakuna marupurupu ya kutosha na hivyo nikajikuta nikiwa na maisha magumu. Hata hivyo ilibidi nianzishe mradi mdogo wa kupiga picha mitaani na hata kazini ili kujiongezea kipato, ingawa sikuwa napata hela za kutosha lakini si haba, fedha nilizokuwa napata zilikuwa zikinisaidia kupunguza ukali wa maisha.

  Kwa upande wa mke wangu, naomba nikiri kuwa hakuwa na msaada sana kwangu. Alikuwa ni mama wa nyumbani, lakini hakupenda kujishughulisha kama wanawake wengine. Alikuwa ni mtu wa kushinda nyumbani kutwa akijiremba na kushindana na wanawake wenzie kwa mavazi, ilikuwa kila Khanga au Vitenge vipya vikiingia hakutaka vimpite na hata mtindo mpya wa mavazi ukiingia pia hakutaka umpite, nilikuwa na wakati mgumu kumridhisha kutokana na tamaa aliyokuwa nayo.

  Tofauti na wenzangu niliokuwa nikifanya nao kazi, wake zao walikuwa ni wachapa kazi, hawakubweteka, na baadhi yao walifanikiwa hata kujenga nyumba zao baada ya kuunganisha nguvu kati yao na wake zao. Waliosema, nyuma ya mafanikio ya mume kuna mke na nyuma ya anguko la mume kuna mke hawakukosea. Hii ina maana gani? Ina maana kuwa kufanikiwa kwa mwanaume au kutofanikiwa, kunategemea na aina ya mke aliyeoa.

  Nakumbauka nilishauriwa sana na baba yangu nikaoe kijijini kwetu lakini nilikataa kwa madai kwamba siwezi kuoa kijijini, kwa kuwa wanawake wa kule ni washamba, kwa hiyo nikaamua kuoa hapa hapa jijini Dar es salaam, binti wa kingindo aliyezaliwa na kukulia mjini. Tulikuwa tukiishi Magomeni wakati huo, eneo lililojaa uswahili, ushindani na na ushabiki wa kishagingi.

  Hata kwao na mke wangu kulikuwa na uswahili mtupu, dada zake wote watatu walikuwa wameolewa na kuachika na wote wako nyumbani kwa wazazi wao, sijui ni kwa nini sikuliona hilo. Katika kipindi ambacho nilikuwa nyumbani baada ya ridandansi nilikiona kigumu hasa, kwani baada ya mke wangu kujua kuwa nimepata mafao ya kuachishwa kazi alianza kutamba kuwa wanawake pale mtaani watamkoma, alikuwa na mahesabu ya kuvaa vito vya thamani na mavazi ya gharama ili wajue kuwa na yeye anazo.

  Akili yake ilikuwa ni tofauti kabisa na ya kwangu, mimi nilikuwa na mipango tofauti kabisa. Nilikuwa na mpango wa kupandisha vyumba viwili haraka haraka kule katika kiwanja chetu kisha tuhame ili kuepuka gharama za kulipa kodi ya pango, halafu nianzishe biashara ili niweze kumudu kupambana na ugumu wa maisha. Siku moja nikiwa nimetulia chumbani usiku nilimuita mke wangu ambaye alikuwa nje akipiga soga na wanawake wenzie, alipofika nilianza kumueleza juu ya mipango yangu, lengo likiwa ni kumshirikisha katika mipango yangu niliyokuwa nimeiratibu tangu nilipopewa ridandansi.

  Mke wangu alipinga kwa nguvu zote mipango yangu niliyopanga na hakutaka kunisikiliza, kwa maoni yake alitaka eti tugawane yale mafao ili kila mtu afe na chake kwani hakuwa tayari kwenda kuishi huko porini Segerea. baada ya kumweleza kuwa nilikuwa nimedhamiria kufanya kile nilichokisema na nilikuwa sitanii, alianza kuzungumza kwa sauti kubwa na kutukana. Nilihisi hasira zikinipanda nikaamua kuondoka na kwenda kuzurura kidogo ili kupoteza mawazo, Nilirudi majira ya saa tano usiku, nilipofika nyumbani nilipokelewa na matusi na kashfa kutoka kwa mke wangu, kwani alinituhumu kuwa nilikwenda kwa wanawake wengine kwa kuwa sasa nina fedha.

  Nilijikuta nikimpiga kwa hasira na kama si wapangaji kuamka kutokana na kelele za mke wangu na watoto labda ningeua, kwani nilipandwa na hasira kupita kiasi, na tangu nimuoe mke wangu siwahi hata kumfinya, hatua ya mimi kumpiga ilimshangaza hata yeye. Ndio tulikuwa tunatofautiana lakini haijawahi kufikia hatua ya kupigana. Wapangaji wenzangu walipofika pale waliamua ugomvi wetu halafu wakinitoa nje ili nisije nikaendelea kumpiga mke wangu kwani alikuwa akiendelea kunitukana na kunikashifu hadharani bila ya aibu.

  Aliondoka usiku ule ule na taxi kwenda kwao akiwa na watoto wetu maeneo ya mwananyamala ambapo ndipo wazazi wake walipokuwa wakiishi. Baba wa mke wangu alikuwa ni mfanyakazi Bandarini na alifanikiwa kujenga nyumba nne hapa jijini Dar es salaam mbili zikiwa Mwananyamala na nyingine mbili zikiwa Kinondoni, na hiyo ndiyo iliyokuwa ikimpa mke wangu kiburi. Niliingia ndani na kujifungia na kujitupa kitandani, na kuanza kutafakari juu ya lile tukio. Sikupata usingizi kabisa kutokana na mawazo niliyokuwa nayo, na nilijilaumu sana kwa kile kitendo nichokifanya cha kumpiga mke wangu. Nilijiona mjinga kwa kitendo kile.

  Siku iliyofuata nilikwenda ukweni kwangu asubuhi na mapema ili kusuluhishwa. Nilipofika nilipokelewa na baba mkwe wangu na baada kusalimiana waliitwa wazee kadhaa wa pale jirani ili kuweza kusuluhishwa. Katika kikao hicho mke wangu alidai talaka na alitaka fedha za mafao nilizopata baada ya kupewa ridandansi kazini tugawane na pia kile kiwanja chetu kilichokuwa segerea kiuzwe na fedha tugawane vile vile ili kila mtu afe na chake, nilipinga wazo lile kwa nguvu zote kwani sikuwa tayari kutoa talaka, nilikuwa nawahurumia wanangu kukosa malezi ya wazazi wote wawili.

  Baba yangu mkwe alikuwa ni mtu mwenye busara sana hakuafiki wazo la mwanae na aljitahidi sana kumuelewesha mwanae kuwa kile ninachotaka kukifanya sio kwa ajili yangu peke yangu bali ni kwa ajili yake na watoto, kwani si vyema kukaa katika nyumba za kupanga, na watoto wanakua. Lakini mke wangu kwa kushirikiana na mama yake pamoja na dada zake walishupalia talaka itolewe na mali igawanywe .

  Wale wazee waliokuwepo katika kile kikao walijitahidi kutoa hekima zao ili kuinusuru ndoa yangu lakini haikusaidia. Mwishowe ikaamuliwa shauri lile lipelekwe BAKWATA, baraza la kiislamu ili tuweze kusuluhishwa. Nilirudi nyumbani nikiwa nimechanganyikiwa kabisa, sikulala usiku kucha nilikuwa nikiwaza juu ya mustakabali wa watoto wangu. Je maisha yao yatakuwaje baada ya sisi wazazi kutengana? Je watapata elimu kama nilivyokusudia? Nilijiuliza maswali mengi bila ya kupata majibu.

  Ingawa nilikuwa na kipato kidogo lakini nilikuwa na ndoto za kutaka watoto wangu wapate elimu bora tofauti na mimi baba yao.
  Nilikuwa ninaamini tu kuwa nitaweza na sikuwa na wasiwasi na hilo. Mara nyingi nilikuwa nikiwaambia wanangu kuwa lazima wasome mpaka chuo kikuu, lakini mke wangu alikuwa akiguna kila nikisema hivyo, alikuwa akinidharau wazi wazi na wakati mwingine alikuwa akinisema kwa mafunbo akidhani kuwa simuelewi.

  Kusema ukweli kama ni kipaji mke wangu alikuwa nacho, alikuwa ni hodari wa kusema kwa mafumbo, kubeza na kushushua mpaka mtu akajisikia vibaya. Unaweza ukasema jambo mbele ya mgeni akakushushua hivi hivi bila kujali kama kuna mgeni. Baada ya kutafakari sana niliamua nikubali yaishe, nimpe talaka halafu tugawane kile alichoita mali. Ulikuwa ni uamuzi mgumu lakini nilikuwa sina jinsi, niliona kuwa ile itakuwa ni njia sahihi ya kuepuka kero na kupoteza muda na pesa pasipo sababu.

  Siku iliyofuata, asubuhi na mapema nilikwenda ukweni na talaka yangu ambayo niliiandika usiku ule ule. Nilipofika na kumueleza baba mkwe juu ya uamuzi wangu wa kuridhia kutoa talaka, baba mkwe alistuka, kwani hakutegemea uamuzi wangu ule. Baada ya majadiliano tulikubaliana kiwanja kiuzwe na hela itakayopatikana pamoja na ile hela ya mafao ya kupunguzwa kazi tugawane sawa kwa sawa na hata vitu vya ndani pia vigawanywe kila mtu akaanze maisha kivyake. Iliniuma sana lakini sikuwa na jinsi. Ndani ya wiki moja tuliuza kiwanja na tukagawane fedha pamoja na vitu vya ndani, nikawa nimeutuwa mzigo. Nikaanza maisha mapya nikiwa peke yangu. Niliamua kusafiri na kwenda nyumbani kuwaona wazazi na kupumzisha akili.

  Nilirudi Dare s salaam baada ya wiki moja, hiyo ni baada ya kukaa na wazazi wangu kwa muda wa wiki moja nikipata ushauri kutoka kwa wazazi wangu namna nitakavyoweza kupambana na maisha baada ya kutengana na mke wangu. Nilipofika tu nilitafuta kiwanja maeneo ya kule kule Segerea na nilibahatika kupata eneo la eka moja na haraka haraka nilisimamisha kibanda changu chenye chumba na sebule. iliamua kujikita zaidi kwenye kazi ya kupiga picha na niliamua kununua kamera mpya ya kisasa, kama masihara nilianza kuzururra mitaani maeneo ya Tabata kutwa nikipiga picha kwenye mabaa na mitaani na ghafla nikawa maarufu.

  Nilianza kupata tenda za kupiga picha kwenye sherehe mbali mbali, misibani na kwenye matukio mbali mbali mitaani, na kijipatia fedha za kutosha. Baadae nilipata wazo la kununua video kamera, hiyo ni baada ya kuwa naulizwa sana na wateja wangu. Ili niweze kuitumia vizuri nikajiunga na chuo kimoja hapa mjini ili kusomea mambo ya Video Production ili niweze kufanya kazi zangu kwa ufanisi.

  Ilinichukuwa miaka miwili kupata cheti changu cha diploma. Nilikuwa napata kazi mbali mbali mpaka za mikoani na mpaka kufikia mwaka 2005 nilikuwa nimejenga nyumba yangu ya kubwa na kufungua studio yangu pale pale nyumbani ambapo nilikuwa nikifanya shughuli zangu mwenyewe. Mke wangu tuliyeachana alikuwa akiendelea kujirusha na wanaume kwenye kumbi za starehe, niliamua kuwachukuwa wanangu na kuwapeleka nchini Uganda wakasomee huko. waka 2006 aliyekuwa mke wangu alifariki kwa kile wazazi wake walichoita TB, lakini niliambiwa na watu wake wa karibu kwamba dalili zote zilikuwa ni za kuugua ukimwi. Sikusikitika sana kwani hayo yalikuwa ndio majaaliwa yake, alikuwa amevuna kile alichopanda.

  Mnamo mwaka 2007 nilifunga ndoa na mchumba wangu baada ya kuwa wachumba kwa takribani miaka miwili. Mchumba wangu huyu ambaye ni mwenyeji wa Mkoani Kilimanjaro ni mtumishi katika kampuni moja binafsi. Ni mwanamke makini ambaye anajiheshimu na kuwathamini watoto wangu na amekuwa ni mshauri wangu katika mambo mengi na hata wazo la kuwapeleka watoto wangu Uganda kwa ajili ya kusoma ni yeye aliyelitoa. Mpaka sasa tumejaaliwa kupata watoto wawili wote wa kiume ambapo wa kwanza ana umri wa miaka minne na huyu wa pili ana umri wa miaka miwili.
  Ili kuimarisha kazi yangu hii nimenunua mitambo yangu ya kusafishia picha na vyombo vya kupigishia muziki Katika sherehe mbalimbali. Kutokana na kazi yangu kuwa nzuri na yenye ufanisi nimekuwa nikipata kazi mbalimbali za mikoani. Nimeweza kujenga nyumba zangu nyingine mbili, moja ikiwa Tabata Kimanga na nyingine ikiwa maeneo ya Kimara na zote nimezipangisha.

  Matarajio yangu ni kumsomesha mke wangu mambo ya upambaji ili tufungue kampuni kubwa itakayojishughulisha na upambaji katika sherehe mbalimbali. Maisha ninayoishi sasa ni ndoto nilizokuwa nazo miaka 20 iliyopita kwani baada ya subira, pamoja na misukosuko mingi hatimaye nimeweza.
  Subira, Uvumilivu na ubunifu vikalipa, hata wewe ukiamua unaweza.

  Hiki kisa ni cha kweli na nilikipata kutoka kwa kaka wa rafiki yangu niliyewahi kusoma nae. Sikutaja jina la mhusika na pia majina ya baadhi ya maeneo nimebadili ili kuficha utambulisho wa mhusika ili kuepuka usumbufu.
   
 2. Ruttashobolwa

  Ruttashobolwa JF-Expert Member

  #2
  Jul 30, 2012
  Joined: Feb 22, 2012
  Messages: 43,747
  Likes Received: 12,841
  Trophy Points: 280
  Kuna funzo
   
 3. platozoom

  platozoom JF-Expert Member

  #3
  Jul 30, 2012
  Joined: Jan 24, 2012
  Messages: 7,325
  Likes Received: 2,320
  Trophy Points: 280
  Asante kwa story nzuri
   
 4. s

  sithole JF-Expert Member

  #4
  Jul 30, 2012
  Joined: Mar 13, 2012
  Messages: 304
  Likes Received: 27
  Trophy Points: 45
  Dah!safi sana!maisha ni safar ndefu aisee!
   
 5. Asabaya

  Asabaya JF-Expert Member

  #5
  Jul 30, 2012
  Joined: Feb 12, 2012
  Messages: 1,317
  Likes Received: 35
  Trophy Points: 145
  Maisha kweli safairi ndefu na unakutana na kila aina ya misukosuko.....
   
 6. Bourgeoisie

  Bourgeoisie JF-Expert Member

  #6
  Jul 30, 2012
  Joined: Mar 26, 2009
  Messages: 611
  Likes Received: 36
  Trophy Points: 45
  Kisa kizuri hiki,kina mafunzo mazuri.Jamani tuyatumie mafunzo haya hata kama si kwetu moja kwa moja basi kuwatia moyo wenzetu. Kisitafsiriwe kuwa ni ngano tu na kuacha mafunzo haya yakipita hivi hivi.
   
 7. Kaunga

  Kaunga JF-Expert Member

  #7
  Jul 30, 2012
  Joined: Nov 28, 2010
  Messages: 12,591
  Likes Received: 801
  Trophy Points: 280
  Duh kweli maisha ni mwalimu!
   
 8. jamiif

  jamiif JF-Expert Member

  #8
  Jul 30, 2012
  Joined: Apr 30, 2012
  Messages: 2,417
  Likes Received: 26
  Trophy Points: 135
  ...ni ndefu ila ngoja niendelee kusoma!!!
   
 9. Elli

  Elli JF-Expert Member

  #9
  Jul 30, 2012
  Joined: Mar 17, 2008
  Messages: 26,828
  Likes Received: 10,140
  Trophy Points: 280
  Mbona siku hizi hii bidhaa inapatikana kil amahali kabisa Mpwa, huna haja ya kuumia na kusubiria kiasi hicho, yaani suiku hizi kama vile unanua vocha vile, unakwangua papo hapo na kuingiza papo hapo!!!
   
 10. cacico

  cacico JF-Expert Member

  #10
  Jul 30, 2012
  Joined: Mar 27, 2012
  Messages: 8,392
  Likes Received: 130
  Trophy Points: 160
  Kha! Wanawake tunatofautiana wallah! Inafundisha, thanx!
   
 11. FirstLady1

  FirstLady1 JF-Expert Member

  #11
  Jul 30, 2012
  Joined: Jul 29, 2009
  Messages: 16,575
  Likes Received: 543
  Trophy Points: 280
  thanx very nice one...
   
 12. jamiif

  jamiif JF-Expert Member

  #12
  Jul 30, 2012
  Joined: Apr 30, 2012
  Messages: 2,417
  Likes Received: 26
  Trophy Points: 135
  ni kweli mkuu! maisha ni kutokata tamaa na kuwa na malengo na kumbshirikisha Mungutu. Pole sana kwa huyo bwana.
   
 13. MadameX

  MadameX JF-Expert Member

  #13
  Jul 30, 2012
  Joined: Dec 27, 2009
  Messages: 7,847
  Likes Received: 64
  Trophy Points: 145
  Duuh kisa kizuri na mafunzo yamefika. Mwanamke ni nguzo msibabane baa tu angalia kama ana akili ya maendeleo.
   
 14. kbosho

  kbosho JF-Expert Member

  #14
  Jul 30, 2012
  Joined: Jun 4, 2012
  Messages: 12,505
  Likes Received: 3,314
  Trophy Points: 280
  maisha yana changamoto nyng' ujasiri waitajka
   
 15. Smile

  Smile JF-Expert Member

  #15
  Jul 30, 2012
  Joined: Jul 18, 2011
  Messages: 15,427
  Likes Received: 194
  Trophy Points: 160
  sisi wachaga noma...usisubiri kuhadithiwa
   
 16. SnowBall

  SnowBall JF-Expert Member

  #16
  Jul 30, 2012
  Joined: Sep 13, 2011
  Messages: 3,067
  Likes Received: 27
  Trophy Points: 145
  Very interesting..kama kawaida 'malipo ni hapa hapa'
   
 17. Spinster

  Spinster JF-Expert Member

  #17
  Jul 30, 2012
  Joined: Mar 19, 2012
  Messages: 393
  Likes Received: 51
  Trophy Points: 45
  mungu hamtupi mja wake
   
 18. Asulo

  Asulo JF-Expert Member

  #18
  Jul 30, 2012
  Joined: Jun 25, 2012
  Messages: 733
  Likes Received: 2
  Trophy Points: 35
  Maisha ni safari ndefu tunajua tulipotoka hatujui tunapokwenda.
  Ila kila linalotokea ktk maisha yetu ni vyema kumshukuru Mungu.
  Nimeipenda inafundisha sana.
   
 19. ram

  ram JF-Expert Member

  #19
  Jul 30, 2012
  Joined: Oct 5, 2007
  Messages: 6,224
  Likes Received: 918
  Trophy Points: 280
  Asiyefunzwa na wazazi......
  Mvumilivu .........

  Ni kisa che mafunzo sana hasa kwa dunia ya leo
   
 20. SHIEKA

  SHIEKA JF-Expert Member

  #20
  Jul 30, 2012
  Joined: Dec 20, 2011
  Messages: 8,136
  Likes Received: 945
  Trophy Points: 280
  Stori tamu sana imejaa mafundisho. Imekaa kama vile imeandikwa na Mtambuzi.
   
  Last edited by a moderator: Jan 4, 2016
Loading...