Binti Kamba: Mwasisi wa TANU aliyepo kwenye nembo ya Uhuru na Umoja

Kurzweil

JF-Expert Member
May 25, 2011
6,622
8,397
bibi.jpg


SAFARI ya kumsaka Khadija binti Kamba, haikuwa nyepesi. Ilianza kwa kudadisi, kupiga simu na kuzunguka hapa na pale hadi kufika katika ofisi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ilala.

Safari haikuishia hapo, iliendelea hadi nyumbani kwake, eneo la Ilala, Bungoni jijini Dar es Salaam .

Binti Kamba mwenye umri wa miaka 90 sasa, ni miongoni mwa waasisi wa chama cha TANU, ambaye kwa sasa maisha yake ni kitandani kwa kuwa hajiwezi kiafya.

Pamoja na maradhi mbalimbali yanayomsumbua, maumivu yake

hayakuwa kikwazo kikubwa kwa mazungumzo yetu. Hakusita kueleza historia ya chama cha TANU na harakati za uhuru zilivyoanza.

Anaanza kwa kusema: “Nilijiunga na siasa nikiwa na umri wa miaka 18 tu, nilikuwa bado kigori,’ Anasema harakati za siasa wakati huo zilianza kushika kasi huku zikiendeshwa na wanaume pekee. Baadaye kukatokea haja ya kuwashirikisha wanawake.

Kwa sababu hiyo anasema alifuatwa ili ajiunge katika ulingo wa siasa, lakini haikuwa kazi rahisi kujiunga baada ya kukatazwa na walezi wake.

Alipokataa anasema akafuatwa mwanamke mwingine aliyeitwa Tatu Mzee, ambaye alipopelekwa kwa waasisi wa siasa, hakuweza kuzungumza kwani alijawa na aibu.

Kura nyingine iliangukia kwa marehemu Bibi Titi Mohamed ambaye wakati huo alikuwa mwimbaji mahiri katika harusi na sherehe za jando na unyago.

“Bibi Titi alipopelekwa mbele ya waasisi wa TANU, alizungumza kwa umahiri na alipata kura zote,” anasema

Bibi Titi alikuwa ni mwanamke wa kwanza kuingia katika siasa hata kabla chama cha TANU hakijazaliwa.

Mkutano wa kwanza wa watu weusi

Mkutano wa kwanza wa chama ulifanyika mwaka 1952. Maelfu ya Watanganyika walifurika, akiwemo Binti Kamba ili kusikia walichotaka kukisema Watanganyika wenzao.

Anasema maajabu ya kwanza ya Mwalimu Nyerere yalijionyesha siku hiyo mara baada ya wingu la mvua kubwa na la ajabu kutanda angani dakika chache kabla mkutano haujaanza.

“Mwalimu alikuwa na kitu cha kipekee pengine ndio maana wengine walimwita mchawi. Mkutano wake wa kwanza ulikuwa na miujiza,” anasema

Anasimulia zaidi na kusema kuwa, wahudhuriaji waliokuwa wamebeba miamvuli kwa ajili ya kujilinda na jua, walianza kuitumia kujilinda kwa ajili ya mvua iliyoanza kudondosha manyunyu.

Anasema: “Mara baada ya Nyerere kupanda jukwaani, aliwaambia Watanganyika washushe miamvuli na wala wasijifunike kwani mvua hiyo haitanyesha,” anasema na kuongeza:

“Watu walishusha miamvuli, wingu lilipotea na mkutano ukapamba moto. Basi tangu siku ile watu walianza kumfananisha Nyerere na nabii.”

Binti Kamba baada ya kusikia sera za Nyerere kwa mara ya kwanza na kuuona ushupavu aliokuwa nao, hakusita kujiunga na siasa mara moja, akiwa ni mwanamke wa pili kuingia katika chama.

“Nilikata kadi yangu ya uanachama siku ile ile kwa shilingi mbili tu nikiwa mwanamke wa kwanza katika chama cha vijana(TYL) kilichoongozwa na Joseph Nyerere na mwanamke wa pili katika TANU” anasema

Anasema, wakati ule kila mmoja alikuwa na mapenzi na chama, wote walikuwa na nia moja na walipumua pumzi moja tu, nayo ni uhuru.

Ampiga kofi mzungu

Mwasisi huyu mkakamavu licha ya kuwa umri umeshamtupa mkono, anasema miongoni mwa mambo yaliyompatia sifa ni pale alipompiga askari wa Kiingereza kofi.

Anasimulia mwanzo wa tukio hilo na kusema kuwa baada ya kufukuzwa katika ofisi yao ya awali ya chama iliyokuwa mtaa wa Livingstone Kariakoo, walipata eneo ulipo Uwanja wa Taifa sasa.

“Eneo hilo lilikuwa ni pori lenye miba na miti mirefu migumu. Tukiwa vijana wa chama wenye ari na nguvu, tulisafisha kwa mikono yetu na kuanza kujenga ofisi,”anasema

Anasema baada ya ofisi kujengwa na eneo la kufanyia mikutano kujengwa pia, njama za wakoloni za kutaka kuwapoteza zilionekana waziwazi.

“Tuligundua siri nzito iliyofanywa na Serikali ya Kiingereza. Walitegesha baruti na mafuta petroli karibu na jukwaa ili watulipue. Lakini sisi kama mabinti warembo enzi zile, tulitumia uanamke wetu na tuliijua siri ile,” anasema Binti Kamba akicheka kwa fahari

Anasema walipokwenda kumweleza Nyerere siri ile, alipanga mikakati mizito ya ulinzi ikiwamo kuwatahadharisha wanachama na wananchi wengine kutovuta sigara au kutupa kitu chochote chenye moto katika eneo lile.

“Mimi, Simkoko na Lumumba tulikuwa kwenye jeshi la ulinzi, tuliwekwa katika milango minne ya jengo lile ili kulinda usalama, wakati mkutano ukiendelea,” anasema

Anasema akiwa amesimama mlango wa mbele wa ofisi hiyo, alimuona Mwingereza akija kwa kunyata katika ofisi ile, kisha akawasha sigara na kuanza kuvuta.

“Kwa hofu nilimrukia na kumzaba kofi kali kwani nilijua kabisa kuwa akitupa sigara ile katika eneo lenye baruti au petroli, basi tutaungua wote,” anasema

Anasema kwa kuwa alikuwa hafahamu lugha ya Kiingereza, alimwambia Mwingereza huyo “no speaker hapa” akiwa na maana ya “no smoking here”yaani usivute sigara hapa.

Kitendo chake cha kuthubutu kumwadhibu mkoloni aliyeogopewa kwa ajili ya taifa lake anasema kilimpa heshima kwa wanachama wengine.

Anasema baada ya hapo mkutano uliendelea na harakati za kudai uhuru zilishika kasi siku hadi siku.

Tambiko na chanzo cha nembo ya uhuru na umoja

Anaeleza kuwa yeye Binti Kamba na marehemu Juma(mwasisi wa TANU) ndiyo walioko katika picha ya nembo ya Uhuru na Umoja.

Chanzo cha picha ile kilikuwa ni tambiko maalum kwa ajili ya Nyerere mara baada ya wakoloni kumpa cheo cha Uwaziri Mkuu.

Mwasisi huyu wa TANU anasema baada tu ya wazee wa wakati ule kusikia kuwa Waingereza wamempa Nyerere cheo hicho, Chifu Fundikira alitoka Tabora na kuja Dar es Salaam kumsihi Nyerere afanye tambiko kabla ya kuanza kazi.

“Ilikuwa ni lazima tumfanyie tambiko kwa sababu tulijua kuwa wakoloni wana yao na walitaka kumrubuni Nyerere kwa cheo, ili asahau harakati za kupigania uhuru,” anasema

Tambiko hilo lilikuwa ni pamoja na unga maalum uliokuwa ndani ya kibuyu, ngao na pembe za ndovu. Kibuyu hicho nje kilikuwa na picha ya sura ya mtu

“Wazee kadhaa akiwemo Chifu Fundikira walikuwa wakichukua unga kutoka katika kibuyu hicho na kummwagia mwalimu pamoja na mke wake usoni,” anasema

Anasema hawakutakiwa kuingia ndani ya nyumba yao mpya au ofisi bila kufanyiwa tambiko hilo.

“Wakati wa kufanywa kwa tambiko lile, mwalimu na mke wake walitakiwa wakae nyuma ya ngao na pembe za ndovu zikae kulia na kushoto kwao,” anasema

Anasema kwa kuwa yeye na Juma walikuwa ndiyo vijana wenye nguvu ilibidi wateuliwe kuzishika pembe hizo, huku Mwalimu

Nyerere pamoja na mke wake wakiwa nyuma ya ngao hiyo, ngao na pembe vyote vilisimamishwa kama vinavyoonekana katika nembo.

Hata hivyo, Binti Kamba ambaye hakuwahi kuwa na mtoto katika maisha yake anaongeza kuwa ngao na pembe zile zilikuwa na siri nzito ambayo katu hawezi kuisema.

“Mwanachama wa TANU anatakiwa kutunza siri na si mropokaji, nimekula kiapo sitofanya hivyo” anasema

Anasema picha ya nembo ya uhuru na umoja haikuwahi kupigwa kwa kutumia kamera bali ilichorwa kutokana na tukio hilo la tambiko na kuongezewa mchoro wa mlima Kilimanjaro na maneno yanayosomeka ‘Uhuru na Umoja’

Maisha ya sasa

Hivi sasa mwasisi huyo yupo taabani kitandani. Maradhi hasa ya miguu yamemwandama, huku akilia kukosa uwezo wa fedha kukidhi mahitaji yake mbalimbali.

Anadai kuwa wanachama wa CCM wa sasa wamemsahau na wala hawajui umuhimu wake kwa Taifa hili.Anasema wamemtelekeza na kumtupa mithili ya ganda lisilo na thamani tena kwa mlaji.


- Mwananchi(ILIANDIKWA 2013)
 
Nahitaji kuonana na huyu bibi angu aise.
Naombe unielekeze ilala bungoni maeneo gani aise
 
Mimi nimeona sentensi ya mwisho ya habari kabla ya neno Mwananchi
 
Kimsingi nawaza namna ya kutunza historia pana ya kuzaliwa kwa taifa hili (Tz) pamoja na mapambano ya uhuru kwa kuzitafuta, kuzitunza taarifa muhimu za waasisi wa hili taifa letu.
Maana hofu yangu kubwa ni hatari ya kupotea kwa taarifa hizi kwa vizazi vijavyo!
 
nilivyokuwa nikiichora hii primary ni balaa hasa, ni takribani miaka saba tangu iandikwe na mwanainchi. vipi hali yake kwa sasa?
 
Hivi huyu bibi yupo
Dah, historia yake watu, wanafunzi hawaijui kbsa
Sahv Watoto wa nawajua wakina zuchu, nandy, ggy money shilole tu
What a shame

Ova
 
Back
Top Bottom