Bilal Rehani Waikela na historia ya TANU Western Province 1955

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,857
30,205
BILAL REHANI WAIKELA NA HISTORIA YA TANU WESTERN PROVINCE 1955

‘’Juhudi za kuihuisha TANU zilikuja mwaka 1955 mwaka mmoja baadae kupitia Young New Strong Football Club - kilabu ya kandanda iliyoanzishwa miaka mingi nyuma ambayo ilikuwa maarufu pale mjini.

Wanachama wa kilabu hiyo baadhi yao ndiyo walikuwa waasisi wa African Association, mashuhuri miongoni mwao walikuwa Fundi Mhindi na Maulidi Kivuruga.

Mwenyekiti wa kilabu hiyo alikuwa Juma Mrisho, mcheza kandanda mashuhuri kwa siku zile.

Shaaban Mohamed Silabu na Bilali Rehani Waikela walikuwa Katibu na Naibu Katibu.

Uongozi huu wa klabu hiyo ya kandanda ulikutana katika nyumba ya Abeid Kazimoto aliyekuwa akifanya kazi Medical Department, kujadili jinsi ya kuifufua TANU.

Uongozi wa kilabu uliamua kumualika Julius Nyerere na Bibi Titi Mohammed kuja Tabora. Mwaka 1955 Bibi Titi Mohamed na Julius Nyerere waliitika mwaliko na kuja Tabora.

Mkutano ulifanyika katika Young New Strong Football Club.

Waliohudhuria mkutano ule walikuwa Germano Pacha, Juma Mrisho, Shaaban Mohamed Silabu, Bilali Rehani Waikela, Mohamed Mataka wakati ule akiwa muadhin wa Masjid Nur - msikiti wa Wamanyema pale Tabora, Hassan Mohamed Ikunji, Ramadhani Mussa Wajaku, Swedi Mambosasa, Said Ali Kiruwi na Hamis Khalfan.

Uongozi wa club ulimwambia Nyerere na Bibi Titi kuwa club hiyo ya kandanda ilikuwa ikitaka udugu na TANU ili ifanye kampeni ya kuipatia TANU wanachama wengi.

Uongozi huo wa TANU kutoka Makao Makuu, New Street, Dar es Salaam uliambiwa kuwa maadam club hii ya mpira ilikuwa ikipendwa na kuungwa mkono na watu wa Tabora na ilikuwa maarufu sana, sifa hizo zingeweza kutumiwa kwa manufaa ya TANU.

Vilevile Nyerere alifahamishwa kuwa club hiyo ingependa kuvijumuisha vyama vitatu vya lelemama na vikundi vya taarabu, Nujum ul Azhar, Waridatil Hubb na Egyptian Club.

Nyerere na Titi waliyakubali mapendekezo haya na usiku ule akifuatana na uongozi wa club Nyerere alizungumza na kikundi cha watu waliyokusanyika nje ya nyumba ya Young New Strong Footbal Club juu ya hali ya Tanganyika katika siku zijazo.’’

Kutoka kitabu cha Maisha ya Abdul Sykes (1998)

Picha ya kwanza Julius Nyerere akihutubia wananchi na wanaBhama wa Young New Strong Footbal Club mwaka wa 1955.

Picha ya pili Bilal Rehani Waikela mmoja wa viongozi wa Young New Strong Footbal Club na muasisi wa TANU.


 

Similar Discussions

Back
Top Bottom