Bila fedha za Stiegler’s Gorge, bajeti ya nishati isipite!

Mdondoaji

JF-Expert Member
Mar 17, 2009
5,108
1,136
Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 27 July 2011

Gumzo la Wiki


TANGU taifa hili lijitumbukize katika kutafuta tiba ya ugonjwa wa kukosekana umeme wa uhakika, serikali imetumia mabilioni ya shilingi za umma bila mafanikio.

Ni kwa sababu, Watanzania wako tayari kutumia mamilioni ya shilingi kufanya kitu kidogo kuliko kutumia fedha kidogo kufanya kitu kikubwa.

Kwa hakika, fedha ambazo taifa hili limetumia kati ya mwaka 1997 hadi Januari 2011 kwa ajili ya kujiondoa katika sakata la "umeme wa dharura" ni nyingi mno; endapo zingetumika mara moja zingetosha kujenga bwawa la kuzalishia umeme kwenye
Genge la Stilger, kwenye Mto Rufiji kwa karibu mara tatu.

Kimsingi tangu serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ilipoamua kushughulikia tatizo hili la upungufu wa nishati ya umeme nchini hasa kwa kutumia "njia za dharura" tumeingia gharama nyingi. Gharama za mikataba yenyewe zenye kujumuisha ununuzi wa mitambo, uzalishaji, uwekaji wa mitambo, mafuta hadi umeme wenyewe.

Tokea wakati huo hadi sasa, serikali imekuja na "mipango" kadhaa ya umeme" na kwamba mipango hiyo imehusisha mikataba mbalimbali ambayo kwa kiasi kikubwa imeingiza taifa kwenye mkenge.

Kwa miaka hii 14 tu, serikali imeingiza nchini vijitambo vidogo vya kuzalisha umeme. Gharama za mitambo hiyo midogo iliyojengwa hadi sasa na ambazo zinaifanya serikali kujipa ujiko, zingetosha kujenga bwawa hilo linatokana na jina la raia mmoja wa Uswisi aliyeuawa maeneo hayo na tembo miaka zaidi ya 100 iliyopita.

Eneo hilo lenye upenyo mwembamba, huteremsha maji ya mto Rufiji katika mteremko wa kama mita 50 kwenda chini na kwa muda mrefu ni miongoni mwa maeneo mazuri zaidi ya kutengeneza bwawa la kuzalisha umeme nchini.

Likiwa na upana wa mita 100 na kina cha mita 100 sehemu ya genge hilo huenda kwa karibu kilomita nane. Kingo mbili za mto huo zimepambwa na miamba mikubwa ambayo mgongoni kwake vilima vilivyopambwa kwa miti ipendezao ya kijani vinasimama kama walinzi wa kudumu wa raslimali zetu wakitungojea wenye nacho tuje.

Natamani, wabunge wetu wangechukua siku moja kwenda kuangalia siri hii iliyo wazi, tunu hii aliyotupa Mwenyezi Mungu na zawadi ambayo twaweza kuwaachia watoto na watoto wa watoto wetu kwa fahari.

Kujenga bwawa la umeme hapo kungegharimu katika miaka ya themanini karibu dola 1.2 bilioni (karibu Sh. 3.29 bilioni) – yaani fedha za mwaka huo zinaweza kuwa kiasi gani katika mwaka huu kununua kitu kile kile.

Uwezo wa umeme unaoweza kuzalishwa hapo kama tukitumia teknolojia ya kisasa na yenye ufanisi zaidi unakadiriwa kuwa kati ya MW2100 na MW6000 – japo mara nyingi tunataja kiwango hicho cha chini.

Hadi hivi sasa, miradi yote ambayo watawala wameingiza taifa mkenge - IPTL, ubinafsishaji ulioshindwa wa TANESCO na mkataba wake Net Group, Alstron Power Rentals, Songas, Richmond, na hata ungizaji wa majenereta ya mafuta kuzalisha megawati zisizozidi 200.

Kama ulipata nafasi ya kumsikiliza Rais Jakaya Kikwete katika mahojiano yake na BBC wiki iliyopita akiwa Afrika Kusini utakumbuka kuwa alisema tangu uhuru nchi imeweza kuzalisha megawati 600 za umeme pekee, na kwamba kuanzia 2009 hadi mwisho mwa mwaka huu serikali yake itakuwa imeongeza megawati 310.

Kwa maneno mengine katika miaka 50 ya uhuru wa taifa hili, tutakuwa tunazalisha megawati 900 (kuzidi kidogo tu mahitaji ya uchumi wetu unaokua kwa kasi). Sasa jumla ya fedha walizolipia kukamilisha miradi hii na kuitumia kwa miaka 14 iliyopita inakaribia – kwa kiwango cha chini tu – dola 8 bilioni (Sh. 12 trioni)!

Yaani, tumetumia doza za Marekani 8 bilioni kwa miaka 14 kuzalisha megawati 600 za vitabuni? Kwani kinachozalishwa sasa hivi kutoka kwenye vyanzo hivyo vyote ni megawati 421 tu - rejea hotuba ya mbunge wa Ubungo (CHADEMA) John Mnyika aliyeitoa bungeni na ambayo serikali haijaweza kuikana.

Kiukweli basi ni kuwa tumetumia karibu dola 8 bilioni kuzalisha megawati 421! Sisi Watanzania ni watu wa ajabu sana. Tuko tayari kutumia fedha nyingi kufanya kitu kidogo kuliko kutumia fedha kidogo kufanya kitu kikubwa; na kwa hakika hatuko tayari kutumia fedha nyingi kufanya kitu kikubwa zaidi.

Kwamba, kama tungeamua kutumia dola bilioni 3.5 hivi sasa tungeweza kuzalisha MW2100 - kwa kiwango cha chini tu - kama tungeamua kujenga bwawa kwenye Genge la Stielger. Labda mfano huu hauoneshi vizuri.

Miaka kama miwilil hivi serikali ya CCM (na wengi wa wabunge hawa hawa) walikubali serikali itenge Sh. 1.7 bilioni (sawa na dola bilioni 1.2) kwa ajili ya "kuwafidia wakulima" walioathirika na kuporomoka kwa uchumi wa dunia.

Kiasi hicho walichotenga ni sawa na asilimia 51.6 ya fedha ambazo leo hii zingeweza kutumika kujenga bwawa la Stielger. Labda mniruhusu niliweke kwa namna nyingi - kinadharia tu. Kama tukitumia dola 3.29 bilioni kujenga bwawa zima basi tunaweza kuzalisha kwa kiwango cha chini kabisa cha MW 2100.

Kama tungeamua hizo fedha zao "stimulus package" kujengea mwanzo tu wa GS, tungeweza kuzalisha kiasi cha MW766. Hicho ni kiasi kikubwa cha umeme kuliko ambacho tunazalisha sasa.

Hapa lazima ujiulize, ni kitu gani hasa kingeanza kati ya nishati ya umeme na kuwafidia wakulima bei ya mazao yao? Miye kama mshamba mmoja naweza kusema tungewekeza fedha hizo kwenye nishati, labda leo tungeanza kuzungumzia mambo mengine.

Watawala wetu wanajua kabisa kuwa wakitatua tatizo la nishati, sehemu kubwa ya kisima cha ufisadi kitakuwa kimezibwa na hivyo wanaendelea kujivuta miguu hadi wananchi tukasirike kweli.

Ni kwa sababu hiyo, Watanzania wasikubali bajeti yoyote ambayo haitatenga kuanzia mwaka huu - kama walivyoweza kutenga mwaka ule - shilingi zisizopungua trilioni 1.5 kuanza ujenzi wa Stielger. Hujanisoma vibaya.

Tusikubali watenge bilioni 2, tusikubali watenge bilioni 50, tusikubali watenge bilioni 200. Kama kweli tunataka kuondokana na hili tatizo la nishati mara moja na daima, mwaka huu lazima zitengwe si chini ya trilioni hizo ili ujenzi uanze- hakuna haja ya athari za mazingira kwani zimeshaandikwa nyingi, anahitajika mtu mmoja tu kuzisoma na kuziweka pembeni.

Kuziweka pembeni si kwa sababu ya kupuuzia, bali kwa sababu mahitaji yetu na maisha yetu yanahusiana na raslimali zetu na kuna wakati jamii inaitwa kulipa gharama ya maisha yake na katika hili ni lazima Bwawa la Stielger lijengwe.

Kuna mtu kasema "hatuna fedha hizo zote", really? labda niwakumbushe wasahaulifu wa Tanzania; kwenye bajeti hii posho peke yake zimetengewa karibu Sh. 987 bilioni! Karibu hivi na theluthi moja tu ya kujenga bwawa la Stielger! Tukijumlisha posho zote za miaka mitano ya urais wa Rais Kikwete, utakuta kwamba, kwa fedha za posho peke yake tungeweza kujenga Stielger!

Bajeti hii isipopitishwa - kama wakikataa kutenga hizi fedha - Bunge litavunjwa, na wote kuanzia Kikwete na wabunge wote warudi kwa wananchi, ili iingia madarakani serikali yenye uwezo na nia ya kututoa kwenye utumwa wa nishati pungufu! Hatutakuwa taifa la kwanza kuitisha uchaguzi mapema!

Swali linabakia, kwanini watu wenye akili timamu, ambao wengine wana dalili za usomi (wana vyeti, majina yao yanafuatiwa na herufi mbili au tatu - na wengine majina yao yanatanguliwa na "dokta") wanaweza kukaa na kujiita viongozi wakikubali kutumia fedha nyingi kufanya mambo madogo ambayo wanataka watu wajivunie?

Naomba niwe mtabiri, wabunge wa CCM watapitisha bajeti ijayo ya Nishati na Madini BILA kutenga fedha za kuanza kujenga Stielger, watatenga fedha kwa madudu mengine yote - kama tulivyozoea - lakini kutenga fedha za kutuondoa kwenye laana hii ya umeme waliyotupa hawatofanya, unajua kwanini?

Naomba nijirudie:Sisi Watanzania ni watu wa ajabu sana. Tuko tayari kutumia fedha nyingi kufanya kitu kidogo kuliko kutumia fedha kidogo kufanya kitu kikubwa; na kwa hakika hatuko tayari kutumia fedha nyingi kufanya kitu kikubwa zaidi. Sisi ni watu wa wastani.

Msemo huu wa Kiswahili unasema vizuri; sisi ni watu tunaopenda vya kunyonga, vya kuchinja hatuviwezi. Na ukifika muda wa kuchinja, kila mtu anatafuta kisingizio kwanini asipewe kisu! Ila wakati wa kunyonga, hawakosekani wanyongaji!na kunyonga wananyonga kweli!

mwanakijiji@jamiiform.com

Source: Mwanahalisi.

My take: Hongera Mzee Mwenzangu. Sina cha kuongeza ila kuna tetesi kuwa wabunge wa CCM wanapanga kuipitisha Budget ijayo ya wizara ya Nishati na Madini baada ya kuwekwa sawa wasiipinge tena. Solution ya tatizo la umeme la kudumu ni hili, ni busara wananchi tukawa kitu kimoja kupambana na mafisadi wa nchi hii!!!!
 
Back
Top Bottom