Bidhaa feki zipigwe vita nguvu zote

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,315
33,111
Inakadiriwa kuwa wateja wapato milioni tatu wa mitando ya simu za mkononi nchini wanatumia simu ambazo ama ni feki au hazina viwango na kwamba ni hatari kwa usalama wao. Katika kulinda ubora wa huduma ya mawasiliano nchini, Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) itaziondoa simu hizo katika matumizi kwa kuzizima kama ambavyo mataifa mengine ya Afrika Mashariki yamekwisha kufanya.

Tangu simu za mkononi kuanza kutumika nchini yapata miaka 18 sasa, mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kijamii yameharakishwa mno kwa matumizi ya zana hizo ambazo zimevunja kuta za zamani za mawasiliano ya mfumo wa simu za nyanya.

Kutokana na manufaa ya simu za mkononi hasa katika siku za hivi karibuni yakiongezewa nguvu na matumizi ya benki za kwenye simu, kila raia mwenye uwezo wa kumiliki chombo hicho cha mawasiliano amejikongoja kukimiliki ili kurahisisha maisha yake kwa njia mbalimbali.

Katika uchangamkiaji wa fursa na tekinolojia kama ilivyo sasa, wapo watu wachache wanaotumia mwanya huo kuingiza nchini bidhaa hizi, yaani simu, ambazo hazina viwango au feki kwa nia moja tu ya kuwaibia wananchi ili wao wapate utajiri wa haraka haraka katika biashara ambayo kwa hakika haizingatii haki ya mlaji wa bidhaa husika.

Ni katika mazingira kama hayo mamlaka za udhibiti wa huduma na ubora zinapashwa kuwa macho kuwalinda walaji wake ili wasizidi kujeruhiwa kwa ulafi wa wanaotaka kuchuma bila hata kuwa na chembe ya maadili katika biashara huru ya ushindani.

Tunajua TCRA wamesema wazi kwamba kabla ya kuzima simu hizo feki au zisizo na kiwango watatoa elimu ya kutosha kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kuwapa muda wa kutosha kutafuta simu mbadala zenye viwango ili wasikose huduma za mawasiliano na nyingine zinazoambatana na umiliki wa nyezo hizo za mawasiliano.

Tunafikiri ni jambo jema kabisa Tanzania kuwa sawa na majirani zake katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kuweka viwango vya ubora wa bidhaa na huduma ili tusigeuzwe kuwa taifa la kukimbiziwa bidhaa duni ambazo zimekosa soko kwa majirani zetu.

Pamoja na kuunga mkono suala la simu za viwango, pia tungependa kuona wigo wa ubora wa bidhaa na huduma kwa ujumla ukipanuliwa ili kila kinachotumiwa na wananchi wetu kiwe kimeingizwa nchini kutoka nje au hata kama kimetengenezwa humu nchini, kwa kiwango kikubwa ubora wake upewe umuhimu wa kipekee kwa ajili siyo tu kulinda thamani ya fedha zinazotumika kupata huduma husika bali pia afya ya walaji kwa ujumla wake.

Kila uchao vifaa vya kieletroniki vinaingizwa nchini vikiwa na thamani ya mabilioni ya Shilingi, wananchi wananunua kwa kasi wakifurahia fursa ya soko huria na upatikanaji wake, lakini kwa ujumla ubora wake unakuwa siyo wa kiwango cha kuridhisha kabisa. Hizi ni kama redio, kompyuta, televisheni, vifaa mbalimbali muziki na vinginevyo. Tunafikiri hata katika eneo hili udhibiti wa dhati unatakiwa ili kuwalinda walaji wapate thamani halisi ya fedha yao wanunuapo bidhaa hizi.

Hali ni iyo hiyo kwenye vifaa tiba na dawa, nguo, vifaa vya magari na ujenzi; ubora umewekwa sana reheni kwa malengo ya faida na utajiri wa haraka. Wanaoumia kwa hakika ni wananchi, walaji. Kila tukipiga picha pana tunaona kwamba mamlaka za udhibiti wa ubora kama TBS, TDFA, TFCC na nyinginezo zina kila sababu ya kujipanga na kuwa makini zaidi katika kutimiza wajibu wake ili kuiepusha Tanzania kuwa jalala la bidhaa feki na ambazo hazina ubora.

Gharama ya bidhaa feki na ambazo hazina viwango ni kubwa mno, kubwa zaidi ni kuzidisha makali ya umasikini kwa wananchi wetu; juhudi za mwananchi mmoja mmoja kujinasua kwenye lindi la umasikini haziwezi kufua dafu kama kile apatacho kitaishia tu kununua bidhaa feki na ambazo hazina viwango, hazidumu na zinazidi kumdidimiza mwaka baada ya mwaka.

Tunaunga mkono kwamba wakati sasa umefika wa kuondoa simu feki na zisizo na viwango katika matumizi ya mawasiliano nchini.




CHANZO: NIPASHE

 
Back
Top Bottom