singidadodoma
JF-Expert Member
- Nov 11, 2013
- 4,394
- 1,536
SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS), limeteketeza bidhaa zenye ubora hafifu na zilizokwisha muda wake zenye thamani ya shilingi milioni 20 kutoka nchini Marekani na China.
Akizungumza wakati wa uteketezaji wa bidhaa hizo Dar es Salaam jana, Ofisa habari wa TBS, Roida Andusamile alizitaja bidhaa hizo kuwa ni dawa za meno, nepi (diapers), sabuni za kuogea na wipes.
Alisema miongoni mwa bidhaa hizo zilikuwa ni kwa ajili ya kutoa msaada katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime mkoani Mara huku nyingine zikiingizwa kwaajili ya biashara.
"Kazi ya kuteketeza bidhaa zenye ubora hafifu ni endelevu lengo letu ni kuhakikisha tunaepusha madhara kwa watumiaji ambao wanashindwa kutambua bidhaa hafifu," alisema.
Alisema bidhaa zote zinazoingia nchini ziwe za biashara au misaada ni lazima zipimwe kwa lengo la kuondoa changamoto ya kuwauzia au kugawa zikiwa ni hafifu au kuisha muda wake.
Kwa upande wake, Ofisa Mdhibiti Ubora wa TBS, Salome Emmanuel alitoa mwito kwa wafanyabiashara kuhakikisha wanaingiza bidhaa zenye ubora na kuongeza kuwa wafanyabiashara ndiyo walinzi tosha wa kuhakikisha bidhaa hafifu haziingizwi nchini, hivyo ni vyema wakafuata sheria kukwepa matatizo.
Katapila likizikanyagakanyaga kwa lengo la kuziharibu bidhaa mbalimbali zikiwemo pampasi na dawa za meno zilizopitwa na wakati na zingine zisizo na ubora katika Dampo la Pugu Kinyamwezi, Dar es Salaam. Bidhaa hizo zenye thamani ya sh. mil. 20, kutoka Marekani na China zilikamatwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), katika Bandari ya Dar es Salaam hivi karibuni.