H1N1
JF-Expert Member
- May 29, 2009
- 4,217
- 1,579
Benki Halisi ya Kitanzania
TAARIFA KWA WAFANYAKAZI
TAARIFA KWA WAFANYAKAZI
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya Posta Tanzania anapenda kuwafahamisha Wafanyakazi wote wa Benki ya Posta kwamba Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amemteua Bw. Sabasaba Kitewita Moshingi (40) kuwa Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Benki ya Posta Tanzania.
Bw. Moshingi anachukua uongozi wa Menejimenti ya Benki ya Posta Tanzania kutoka kwa Bw. Alphonse Kihwele ambaye amekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Posta Tanzania kwa kipindi cha miaka kumi na mitatu (13) iliyopita. Bw. Kihwele ameitumikia Benki ya Posta Tanzania kwa uadilifu mkubwa akiwa mtumishi wa Umma na akishika nafasi mbalimbali katika Benki kwa kipindi cha miaka arobaini na miwili (42) iliyopita toka alipoajiriwa kwa mara ya Kwanza na iliyokuwa Benki ya Akiba ya Posta.
Bw. Moshingi (pichani) anajiunga na Benki ya Posta Tanzania akitokea Benki ya Standard Chartered, Kanda ya Mashariki ya Kati (Middle East Region) alipokuwa akifanya kazi kama "Regional Head of Consumer Banking Operational Risk and Sales Governance".
Kwa ujumla Kanda ya Mashariki ya Kati, ambayo Bw. Moshingi alikuwa akisimamia shughuli za kibenki za Benki ya Standard Chartered, inajumuisha nchi tano za Bahrain, Lebanon, Jordan, Qatar na Oman, makao yake makuu yakiwa Falme za Bahrain (the Kingdom of Bahrain) ambako ndiko Ofisi ya Bwana Moshingi ilipokuwa.
Kabla ya kuhamishiwa Mashariki ya Kati, Bw. Moshingi alikuwa Mkuu wa Idara ya TEKNOHAMA na Uendeshaji (Head of Technology and Operations) wa Benki ya Standard Chartered Tanzania.
Bw. Moshingi ni mtaalamu wa shughuli za kibenki anayetambulika (Chartered Banker) na ni mwanachama wa taasisi za wataalamu wa shughuli za kibenki za Tanzania na Uingereza (Tanzania Institute of Bankers and the Institute of Bankers UK).
Bw. Moshingi ana shahada ya Uzamili ya Usimamizi wa Biashara na Uongozi (MBA-Finance) aliyotunukiwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Ana mke na watoto watatu (3).
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya Posta Tanzania, Prof. Lettice Kinunda-Rutashobya, amesema "Bw. Sabasaba Moshingi ni mtaalamu na anao uzoefu wa kusimamizi shughuli za kibenki alioupata ndani na nje ya nchi yetu, hivyo atasaidia sana katika kuimarisha usimamizi wa shughuli za Benki ya Posta Tanzania ili kuifanya Benki ya Posta Tanzania kuwa moja ya Benki imara kabisa hapa nchini.
Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya Posta Tanzania inajivunia ujio wake na inamkaribisha Bw. Moshingi na familia yake hapa nchini na ndani ya familia ya Benki ya Posta Tanzania".