Beijing yapamba maadhimisho ya Siku ya Kiswahili kwa shamrashamra mbalimbali

ldleo

JF-Expert Member
Jan 9, 2010
1,008
1,031
VCG41N94261979.jpg


Mwaka jana mnamo mwezi Novemba, Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) liliipa heshima lugha ya Kiswahili kwa kutangaza rasmi kwamba kila ifikapo tarehe 7 Julai ya kila mwaka itakuwa ni siku ya Kiswahili duniani.

Heshima hii ya kipekee ikafanya Kiswahili kuwa lugha ya kwanza ya Afrika kutambuliwa na Umoja wa Mataifa na kuwa na siku yake maalum ya kuadhimishwa. Kuanzia hapo mataifa mbalimbali yanayozungumza lugha ya Kiswahili na hata yale yasiyozungumza lugha hii, lakini yana balozi za nchi zinazozungumza Kiswahili, au vyuo vinavyofundisha Kiswahili, na makampuni yanayofanya shughuli zao kwa kutumia lugha ya Kiswahili, yote yanaungana kwenye siku hii kuadhimisha siku ya Kiswahili.

Huu ni mwaka wa kwanza kabisa tangu maadhimisho hayo yatambuliwe rasmi, ambapo China ikiwa na wadau wengi wa Kiswahili wakiwemo wanafunzi na wafanyakazi, waswahili na wachina, pia inaadhimisha siku hii kwa kuipamba na matukio mbalimbali ambayo yanaratibiwa na ubalozi wa Tanzania nchini China.

Kwa mujibu wa afisa mwandamizi wa ubalozi wa Tanzania nchini China Ussi Miraji Ukuti, hafla ya maadhimisho haya itaambatana na mambo mbalimbali yakiwemo kuandaa semina ambayo itafanyika tarehe 7 na kushirikisha wadau wa Kiswahili waliopo China na hata wale walipo nje ya China.

“Mdahalo wetu utakuwa umechanganyika na vitu mbalimbali, yakiwemo maonesho mbalimbali ya wanafunzi Wachina wa vyuo vinavyofundisha lugha ya Kiswahili, ambao wataonesha umahiri wao kwa kucheza na maneno ya Kiswahili na lugha yenyewe ya Kiswahili. Pia kuna taasisi za habari zinazotangaza kwa kutumia lugha ya Kiswahili, ambazo zitapata nafasi ya kueleza changamoto wanazokabiliana nazo katika kufanya shughuli zao. Mbali na hapo kutakuwa na mjadala ambao mada zake zitakazotolewa na wataalamu wa Kiswahili, na kujadiliwa kwa upana wake.” alisema Dkt Ussi

Shughuli zote hizi zinalenga pia kuangalia ni namna gani lugha hii itazidi kuenea katika mataifa mbalimbali, pamoja na changamoto zake katika kutimiza lengo hili. Jambo lolote lile linapofanyika kwa mara ya kwanza huwa na changamoto mbalimbali. Ndio maana waswahili wana msemo kwamba “mwanzo ni mgumu”, kwa kutambua hilo, katika hekaheka za kuandaa siku hii ya Kiswahili, hapa China pia kumekuwa na changamoto kadha wa kadha ambazo zimetokana na hali ya janga la virusi vya Corona. Tunatambua kuwa hadi leo China inaendelea kuchukua hatua za kuhakikisha wananchi wote wanakuwa salama kwa wakati wote.

Hata hivyo kwa mujibu wa Dkt Ussi, ambaye pia ni mwambata wa masuala ya uchumi katika ubalozi wa Tanzania nchini China, “hakuna tatizo lisilokuwa na ufumbuzi wake” Kwa kuzingatia hilo, shamrashamra hizi zitafanyika kwenye mtandao wa internet.

“Changamoto bado ni ileile kwamba kuifanya shughuli yetu iendane na matakwa ya kimamlaka. Kwasababu vyuo sasa vimefungwa, na wanafunzi ambao ni washiriki wakubwa wapo katika mapumziko. Lakini pia mikusanyiko mikubwa bado imezuiliwa, kwa hiyo ni changamoto kubwa kwasababu tulitegemea kwamba, kama hakuna vizuizi vya namna hiyo tuwe na shughuli kubwa ambayo inawaweka watu pamoja na kupata kubadilishana mawazo kujua tamaduni, lahaja na hata vyakula mbalimbali vya Kiswahili” alifafanua Dkt Ussi

Katika shughuli hii ya maadhimisho ya siku ya Kiswahili duniani ambayo kwa mwaka huu ni ya kipekee kabisa, mgeni rasmi atakuwa balozi wa Tanzania nchini China, Mheshimiwa Mbelwa Kairuki, lakini mbali na yeye, pia maadhimisho haya yatahudhuriwa na mabalozi wengine wa nchi mbalimbali hapa nchini China ambao wanazungumza Kiswahili, kama vile wa Kenya na nchi nyingine za Afrika Mashariki. Naye balozi wa Oman pia atashiriki kwenye shughuli hiyo na kubeba jukumu la kufunga maadhimisho hayo.

Mwanafunzi mmoja wa Chuo Kikuu cha Lugha za Kigeni cha Beijing, ambaye ni Mchina anayeitwa Tang Xukang, anasoma mwaka wa pili katika chuo hicho, na anasema amefurahi sana kupata fursa ya kushiriki kwenye maadhimisho hayo, yeye pamoja na wenzake. Kwa upande wao wameandaa shairi safi kabisa la kukisifu Kiswahili ambalo watalighani yeye na wenzake.

“Nimefurahi sana kupata fursa hii adhimu ya kuonesha uwezo wetu wa kuzungumza lugha ya Kiswahili, ingawa nipo mwaka wa pili lakini nashukuru kwani naweza kuwasiliana vizuri tu na wenyeji wa lugha ya Kiswahili. Shairi letu tutalighani kwa kupokezana na wenzangu huku tukionesha umahiri wetu wa kughani, kukisifu, pamoja na kukienzi Kiswahili.” alisema Daudi

Kiswahili hadi sasa tayari kimekuwa kinatambulika kama miongoni mwa lugha rasmi kwenye Umoja wa Afrika, na kinatumika kama lugha rasmi kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki na bunge la Afrika, na ni moja ya lugha za Afrika zinazozungumzwa na watu wengi duniani.
 
Back
Top Bottom