Bei juu, saruji, nondo, bati, mchanga n.K.

mbongowakweli

JF-Expert Member
Aug 24, 2011
844
673
Kupanda ghafla kwa bei ya vifaa vya ujenzi kwazua mjadala.

Kwa ufupi Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi pamoja na wananchi waliohojiwa umeonyesha kupanda kwa bei ya saruji na vifaa vingine vya ujenzi kama mabati na nondo, hali inayoongeza gharama za ujenzi.

“Haya ni matokeo ya sera mbaya za uchumi zinazotokana na Serikali kubana matumizi na viwanda kukosa mikopo (working capital) kutoka kwenye mabenki.” Huku akitoa mifano, Zitto anaandika kuwa mwaka 2017, mkulima wa Mikese Morogoro alipata mifuko 10 ya saruji kwa kuuza gunia moja tu la mahindi (gunia lilikuwa Sh120,000 na mfuko wa saruji kilo 50 ulikuwa Sh12,000). “Mwaka 2018 mkulima huyo anapata mifuko ya saruji 3.5 tu (gunia moja la mahindi gunia ni Sh50,000 na saruji sasa ni Sh14,000),” alisema. Alitoa mfano mwingine akisema mkulima wa maharage wa Msambara Kasulu aliuza kilo 7.5 na kupata mfuko mmoja wa saruji (kilo ya maharage Sh2,000 na mfuko wa saruji ulikuwa Sh15,000). “Mwaka 2018, mkulima huyo atapaswa kuuza kilo 14.6 za maharagwe kupata mfuko mmoja wa saruji (sasa anauza kilo moja ya maharage kwa Sh1,300 na saruji mfuko mmoja ni Sh19,000),” alisema. Baadhi ya wachangiaji katika ukurasa huo waliotoa maoni yao kati ya Machi 12 saa 3:26 na Machi 13 saa 5:17 asubuhi na kuendelea, wameeleza hali ilivyo katika maeneo yao. Mmoja wao aliyejitambulisha kwa jina moja la Augustine amesema: “Mwezi wa nne mwaka jana nondo ya milimita 12 ilikuwa inanunuliwa Sh13,000, sasa ni Sh17,000, mfuko wa saruji Sh10,500, sasa Sh13,000. Hizo ni bidhaa ambazo hutumiwa na wananchi wa kawaida.” January Kalubandike alisema, “Ni kweli kabisa Desemba nilinunua nondo ya milimita 12 kwa Sh17,000 wiki iliyopita nimeinunua Sh23,000. Nondo ya milimita 16 mwaka jana Desemba nilinunua kwa Sh26,000, wiki iliyopita nimenunua kwa Sh36,000, hizi ni nondo zinazozalishwa hapahapa Tanzania. “Saruji ya Twiga Plus mwaka jana mwezi Desemba nilinunua kwa Sh13,000 jana nimenunua kwa Sh14,000 na ni hapahapa Dar es Salaam, kisha nikafikiria labda huku kwangu ni kijijini. Eneo langu lipo kilomita tisa kufika Kiwanda cha Saruji cha Twiga.” Maximilian Kweka aliyeko Wilaya ya Hai, Mkoa wa Kilimanjaro alisema nondo ambazo zilikuwa zinauzwa kwa Sh12,000 Januari, sasa ni Sh13,000, bati la mita tatu liliwa Sh17, 000, sasa ni Sh20,000.

Mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Kilaya Chande alisema katika Wilaya ya Liwale mkoani Lindi, saruji ya Dangote imefikia Sh20,000 kutoka Sh13,500, huku nondo za milimita 12 zikifikia Sh19,500 kutoka Sh17,000. Fraterm Thomas kutoka Arusha alisema nondo za milimita 12 zimefika Sh21,000 kutoka Sh16,000 na za milimita 10 zimefikia Sh15,000 kutoka Sh12000 wakati misumari ya kawaida imefika Sh4,000 kutoka Sh3,000 na misumari ya bati imefika Sh6,000 kutoka Sh3,500 kwa kilo. Alisema bati la mita tatu limefikia Sh20,000 kutoka Sh17,000. Brighton Salvatory kutoka mji wa Rulenge wilayani Ngara, Mkoa wa Kagera alisema nondo milimita 12 imefika Sh19,000 na saruji ni kati ya Sh18,000 na Sh20,000.

Juma Msemele wa Mwanza alisema nondo za milimita 12 zimepanda kutoka Sh16,000 hadi Sh18,000, saruji kutoka Sh13,000 hadi Sh17,000 na bati la geji 30 kutoka 250,000 hadi Sh320,000 (kwa bei ya jumla). Ethos Ntiganizwa wa Kigoma Mjini alisema saruji inauzwa Sh19000 kutoka Sh16,500, nondo milimita 12 ni Sh20,000 kutoka Sh15, 500. Bei ya bati ni Sh300,000 toka Sh245,000 (kwa bei ya jumla). Kwa mara ya mwisho uchunguzi wa bei kwa mujibu wa Mwananchi ulifanyika Ijumaa iliyopita. Maoni ya wadau Akizungumzia kupaa huko kwa bidhaa za ujenzi, Profesa wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Humphrey Moshi alisema huo unaitwa mfumuko wa bei wa uingizwaji wa bidhaa ambao alisema hautadumu kwa muda mrefu. “Siyo kwamba mfumuko wa bei umepanda sana, huo unaitwa ‘imported inflation’. Unatokana na kuporomoka kwa shilingi kwa sababu ya kuagiza bidhaa nyingi kutoka nje ya nchi kutokana na kushuka kwa uzalishaji,” alisema Profesa Moshi. “Hata hivyo, hali hii ni ya muda tu, kwa sababu mvua zikinyesha kwa wingi chakula kitazalishwa kwa wingi hivyo hata dola zitaiongezeka. Lakini tukitaka kuimarisha uchumi wa viwanda ni lazima tuzalishe kwa wingi na tuuze bidhaa nje na kutosheleza matumizi ya ndani.” Alisema sababu nyingine ni uzalishaji hafifu wa kilimo ambao umechangia kushuka kwa shilingi kwa sababu kilimo chenyewe sio cha kisasa.

Mhadhiri wa Uchumi wa UDSM, Dk Haji Semboja alitaja sababu tatu za kupanda huko bei, huku kwa upande mwingine akisema ni kuimarika kwa uchumi. “Inawezekana ni kutokana na utekelezaji wa kodi mpya zilizoanzishwa hivi karibuni, pili ni kutokana na bidhaa nyingi kuagizwa kutoka nje, inawezekana zimepanda bei na tatu ni mabadiliko ya fedha za nje (foreign exchange),” alisema Dk Semboja. “Hali hiyo inaonyesha uchumi utapanda kwa sababu kuna ongezeko la ujenzi kuliko ilivyokuwa awali. Maeneo yanayoonekana kuimarika kwa ujenzi ni Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza na maeneo yanayopakana na reli ya kati. Haiwezekani wafanyabiashara wapandishe bei wakati hakuna wajenzi.” Bright Naimani, ambaye ni mkandarasi wa ujenzi alisema japo kuna ongezeko la ujenzi kidogo, lakini ongezeko hilo haliakisi kukua kwa uchumi. “Kuna ongezeko la ujenzi, lakini ni kidogo. Vifaa vingi vya ujenzi vinaingia kutoka nje ya nchi na kwa sasa waagizaji wengi wamesitisha uagizaji kwa sababu hakuna uhakika wa biashara. “Zamani ukiagiza kontena unajua kabisa faida yako, lakini siku hizi TRA wanakagua mizigo kiasi kwamba huwezi kuambulia kitu. Kwa hiyo vifaa vilivyomo ndani ni lazima vipande bei.” Alitaja pia kusuasua kwa kiwanda cha saruji cha Dangote akisema kumechangia kupanda kwa bidhaa hiyo. “Kabla ya kuja kiwanda cha Dangote kilo 50 za saruji ziliuzwa Sh15,000, baada ya hapo ikashuka hadi Sh9,000, sasa inapanda tena. Kuna kiwanda cha Wachina kinajengwa Tanga, huenda kitasaidia kushusha bei tena,”alisema na kuongeza: Akieleza sababu ya viwanda kuongeza bei ya saruji, mkurugenzi wa biashara wa kiwanda cha Twiga cha Dar es salaam, Yves Mataigne alisema ni kutokana na kupanda kwa gharama za uzalishaji. “Kwanza kuna mfumuko wa bei nchi nzima, halafu gharama za nishati kama gesi, umeme na mafuta zimepanda na tunatakiwa kulipa mishahara na posho. Yote hayo, lazima bei ipande,” alisema Mataigne. Mkurugezi wa Takwimu za Jamii na Sensa ya Watu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Ephraim Kwesigabo alisema hawezi kuthibitisha mfumuko huo kwa sababu ni sehemu ndogo ya tathmini zao.

“Inawezekana kweli kuna mfumuko wa bei au usiwepo, lakini hatuwezi kujua kwa kuwa hatufanyii kazi bidhaa moja moja. Huwa tunaangalia kwa umoja wake,” alisema Kwesigabo na kuongeza: “Tuna vitu 278 huwa tunaangalia tunapofanya utafiti wa bei na vifaa vya ujenzi vimo ndani yake na tunatoa taarifa kila mwezi.”

CHANZO :-
Kupanda ghafla kwa bei ya vifaa vya ujenzi kwazua mjadala Kupanda ghafla kwa bei ya vifaa vya ujenzi kwazua mjadala via @MwananchiNews
 
Cjui kwanini viwanda vyetu vya ndani vinauza bei yajuu hivi... Naona viko kimaslahi Zaid
 
Acheni kupiga kelele fanyeni kazi.Hii ni tanzania ya viwanda tumenunua ndege,standad geji hii yote itawafanya wanyonge wafurahie maisha katika awamu hii
 
Hapo wanaccm utawasikia. "'wanaolia ni wapiga dili na wamezoea mteremko''
Ngoja tuone. Uchumi umekuwa kwahiyo wananchi wataweza kununua
 
Cjui kwanini viwanda vyetu vya ndani vinauza bei yajuu hivi... Naona viko kimaslahi Zaid
Fanyeni kazi. Hapa kazi tu. Km unachapa kazi huwezi kusema vyuma vimekaza in jpm's voice.
Ngoja nikae pembeni nione. Naona kila mmoja anafikiwa japo kuna watu wanajitahidi kujificha lkn wanafikiwa tu.
 
Back
Top Bottom