BAWACHA: nafasi za uongozi wanawake ziongezwe

MASEBUNA

JF-Expert Member
Oct 9, 2011
243
54
Baraza la Wanawake wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Bawacha),
limesema fursa za wanawake ngazi
mbalimbali za uongozi bado ni chache licha ya
maazimio kadhaa yaliyopitishwa kitaifa na
kimataifa kuhakikisha kuna kuwa na usawa baina ya wanawake na wanaume. Mwandishi Wetu amezungumza na Katibu
Mkuu wa Bawacha ambaye pia ni mbunge wa
viti maalum mkoa wa Mbeya, Naomi Kaihura,
wakati akizungumzia siku ya wanawake
duniani ambayo huadhimishwa Machi 8 kila
mwaka. Naomi anasema dhana hiyo bado ni vigumu
kufikiwa kwa sababu wanawake na wasichana
wengi hawajajitokeza kwa wingi kupigania
nafasi za uongozi licha ya ukweli kwamba
wengi wanazimudu. Anasema mpaka sasa ni asilimia 30 tu ambayo
imefikiwa, na kwamba asilimia 20 iliyobakia
sio kazi rahisi kuifikia endapo hakutakuwepo
na jitihada za dhati za kupambana na
vipingamizi vinavyosababisha wanawake
wasijitokeze katika nafasi hizo. Kaihula anasema elimu, mila na desturi ni
moja ya sababu kubwa zinazochangia lengo
hilo lisifikiwe kwani baadhi ya watu bado
wanafikra potofu kuwa uongozi ni kwa ajili ya
wanaume. Anaeleza kwamba mpaka sasa baadhi ya
makabila hapa nchini, bado yanatawaliwa na
mfumo dume kutokana na misingi mibovu
iliyojengeka tangu awali, ya kuthamini na
kumpa kipaumbele mtoto wa kiume kuliko
mtoto wa kike. Anafafanua kuwa, kuanzia katika ngazi za
shule za msingi hadi elimu ya juu, watoto wa
kike wanashindwa kupambana na watoto wa
kiume katika masomo kutokana na mazingira
mabovu waliyomo ingawa wakati mwingine
hujidharau au kukatishwa tamaa na wenzao au mila na desturi walizojengewa nazo tangu
awali. Anasema kutokana na mila na desturi
walizolelewa tangu awali, baadhi ya watoto
wa kike hushindwa kujiamini wakiwa bado
shuleni, kwamba baadhi ya masomo ni ya
wavulana wao hawayawezi, na hivyo
kusababisha kushindwa hata kama walikuwa na uwezo wa kufanya vyema kwenye
masomo hayo. Anasisitiza kwamba uwezo wa mtu unatokana
na namna anavyojiamini na kwamba hilo ni
moja wapo ya kikwazo kinachowafanya
wanawake washindwe kupambana na
wanaume hata wanapokuwa wakubwa. Akizungumzia upande wa siasa, anasema
baadhi ya vyama vya siasa bado vinambagua
mwanamke kushiriki katika nafasi za juu,
vikiamnini kwamba labda hawezi kufanya
vizuri. Anatolea mfano katika nafasi ya urais,
kwamba karibu vyama vilivyo vingi havitowi
nafasi hiyo kwa mwanamke kugombea, jambo
linaloonyesha dhahiri kwamba bado
mwanamke hajapewa kipaumbele. Kadhalika anasema baadhi ya wanawake
wanashindwa kupata nafasi kutokana na
ubinafsi ambao upo kwa wanaume walio
katika ngazi za juu. Anasema wanaume wengine hasa wale walio
katika ngazi ya utoaji wa ajira, mara nyingi
hawatoi ajira kwa wanawake na wakati
mwingine huwataka wawatumie kimapenzi
ndiyo wawajiri. “Wanawake wanapata shida sana, kwa sababu
wakati mwingine wanapotafuta ajira
hawapewi, hasa pale waajiri wanapokuwa
wanaume, baadhi yao wanataka mpaka
wawatumie katika mapenzi eti ndiyo
wawaajiri, kwa taswira hii ni vigumu kufikia 50 kwa 50”, anasema. Anasema mpaka sasa idadi ya wawakilishi wa
wanawake katika nyanja mbalimbali za
uongozi ni chache sana, na kwamba ndio
sababu kubwa inakwamisha wasipate haki zao
za msingi. Anaongeza kwamba endapo wataondoa hofu
na kuanza kupigania ipasavyo nafasi hizo,
wataunganisha nguvu na kufikisha ipasavyo
changamoto mbalimbali zinazowakabili. “Bado tunapigania wanawake wengi
wajitokeze katika nyanja mbalimbali za
uongozi, ili tuunganishe nguvu ya pamoja
kupigania haki zetu”. “Hivi unafikiri ni jambo rahisi mtu kupigia
kelele matatizo yako, kama wewe
mwenyewe haujayapigia?, hivi ndivyo ilivyo
kwa wanawake, matatizo yao hayawezi
kutatuliwa endapo wao wenyewe
hawatajipigania, na itakuwa rahisi sana kufikisha kero zao sehemu husika endapo wao
wenyewe watashika nafasi”, anasema. Akizungumzia suala la nafasi ya viti maalum
anasema, licha ya nafasi hiyo kuwasaidia
wanawake kuonyesha uwezo wao katika
nyanja ya uongozi, lakini baadhi ya wananchi
wameanza kubeza nafasi hiyo na kutaka
iondolewe. Anasema inasikitisha kuona baadhi ya
wananchi wanabeza nafasi hizo, huku
wakisahau kwamba ndiyo nafasi ambayo
imesaidia kuonyesha uwezo wa mwanamke,
na hata kuchangia wanawake wengi kuanza
kujitokeza katika nafasi mbalimbali za uongozi na kutetea haki zao. “ Viti maalum ni nafasi pekee ambayo
imetusaidia wanawake kufikia hapa tulipo,
kwa kupigania na kuyapigia kelele matatizo
yaliyokuwa yanatukabili, mbali na hilo pia
tunafanya kazi nyingi sana huko mikoani. Anaongeza kwamba, kuweka wabunge wa viti
maalumu ilikuwa ni chachu ya kuwapa nafasi
ya kuonyesha uwezo wao, hasa baada ya
kuonekana wamekandamizwa sana na mila na
desturi za mfumo dume, na kwamba nafasi
hiyo ndiyo imesaidia katika kumkomboa mwanamke na kuonekana anaweza. Anawata wananchi kuacha kubeza nafasi ya
viti maalum kwani ndiyo, imechangia
kuonyesha uwezo wa mwanamke na
kusisitizia kwamba sio kweli kwamba
wabunge wa viti maalum hawafanyi kazi. Pia anaiomba serikali, taasisi za kiserikali na
zisizo za kiserikali kuendelea kupigia kelele
mifumo kandamizi kwa wanawake ili
ibomolewe kabisa. Kwa upande wake, Victor Kimesera, ambaye
ni Katibu Mtndaji wa Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (Chadema), anasema
mwanamke ni msingi mkubwa wa maendeleo,
hivyo anatakiwa kuthaminiwa. Anasema kati ya viongozi ambao ni waaminifu
wanaposhika uongozi ni wanawake, na ndio
maana baadhi ya vyama vinapohitaji
mafanikio katika vyama vyao hutumia sera ya
kutatua matatizo ya wanawake. Haki ya wanawake ya kushiriki katika maisha
ya kisiasa pia imesisitizwa katika mikataba
kadhaa ya kimataifa, lakini kuibadirisha haki
hiyo kutoka katika maandiko hadi kwenye
vitendo kunahitaji jitihada zaidi miongoni mwa
wahusika. Kulingana na ripoti mpya ya utafiti
iliyochapishwa kwa ushirikiano wa Shirika la
Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa –
UNDP na Taasisi ya Taifa ya Demokrasia kwa
Masuala ya Kimataifa, ni kwamba ijapokuwa
asilimia 40 hadi 50 ya wanachama wa vyama vya kisiasa kote ulimwenguni ni wanawake,
asilimia 10 pekee ndio inashikilia nyadhifa za
uongozi. Msimamizi wa UNDP Helen Clark, anasema
kuwa huku kukiwa na chini ya asilimia 20 ya
viti vya bunge ulimwenguni vinavyokaliwa na
wanawake, ni wazi kwamba vyama vya
kisiasa vinahitaji kupiga hatua zaidi na
vinahitaji kusaidiwa katika juhudi hizo, za kuwasaidia wanawake katika kujiimarisha
kisiasa. Mkurugenzi wa Kikundi cha Jinsia cha Shirika
la UNDP Winnie Byanyima, anasema ikiwa
tunataka kueneza demokrasia na kuwapa
uwezo wanawake kisiasa, ni sharti tushirikiane
na vyama vya kisiasa na ikiwa wanawake
hawapewi uongozi wa vyama vya kisiasa, basi hawawezi kuziongoza serikali. Utafiti wa kimataifa unasema, idadi ya
mawaziri wanawake serikalini ni asilimia 16
tu, huku idadi ya viongozi wanawake wa nchi
na serikali bado iko chini, na kwamba idadi
hiyo imepungua katika miaka ya hivi karibuni
hadi kufikia asilimia 5 mwaka 2011. Utafiti huo unasema idadi hiyo ya chini
imeendelea kushuhudiwa katika miongo
mitatu iliyopita ya uhamasisho na juhudi za
jamii ya kimataifa kuangamiza ubaguzi na
kuwapa uwezo wanawake. Aidha, Umoja wa Mataifa ulitambua umuhimu
wa wanawake katika maendeleo na kuamua
kuwapa uwezo kama mojawapo ya malengo
manane ya Maendeleo ya Milenia wa mwaka
2000. Hata hivyo, kwa mujibu wa utafiti huo,
hakuna eneo lolote ulimwenguni ambalo liko
katika harakati za kufikia asilimia 30 ya
wanawake katika nafasi za kufanya maamuzi,
japokuwa kuna maeneo yanayojaribu
kujidhatiti na kutimiza lengo hilo. Kutokana na takwimu za hivi karibuni za
Chama cha Kimataifa cha Wabunge IPU na
Wanawake wa Umoja wa Mataifa, idadi ya
wanawake viongozi wa nchi na serikali ni 18
tu, kutoka katika nchi 193. Utafiti huo wa UNDP na NDI unataja baadhi ya
mikakati inayoweza kutumiwa wakati wa
uchaguzi, kama vile kuwapa mafunzo na
kuwahimiza wagombea wa kike kwa
kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi katika
kampeni. Shirika la NDI linasema linajitahidi kufanya
kazi na zaidi ya vyama 720 vya kisiasa,
mashirika na nchi zaidi ya 80, ili kuweka
mazingira bora na ya wazi ambapo wanaume
na wanawake wanaweza kushiriki kikamilifu
katika mchakato wa demokrasia. Shirika hilo linasema, kabla ya uchaguzi, usajili
na uteuzi wa wagombea ni muhimu
kuhakikisha kuwa wanawake wanashirikishwa
ipasavyo katika siasa.
 
Back
Top Bottom