Bashe: Serikali kuunga mkono sekta binafsi katika uzalishaji wa mbolea nchini

JUMA JUMA

JF-Expert Member
Jan 5, 2013
664
829
BASHE: SERIKALI KUUNGA MKONO SEKTA BINAFSI KATIKA UZALISHAJI WA MBOLEA NCHINI

Dodoma,

Naibu Waziri wa Kilimo *Mhe. Hussein Bashe mapema leo ametembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa kiwanda cha mbolea cha INTRACOM kinachojengwa mkoani Dodoma.

Katika ziara hiyo, Bashe amebainisha ya kuwa “Serikali itashirikiana na sekta binafsi kuhakikisha sekta Ndogo ya viwanda vya mbolea kwenye kilimo inaimarika ili kuwa na uwezo mkubwa wa uzalishaji na wenye kuleta ushindani ambao utapelekea kushuka Kwa gharama za mbolea nchini”

Aidha, Mheshimiwa Bashe aliambatana na taasisi mbalimbali zilizo chini ya Wizara ya Kilimo Kwa lengo la kuhakikisha kunakuwa na ushirikiano imara baina ya taaisi hizo na sekta binafsi hasa katika kuboresha na kuimarisha Upatikanaji wa masoko ya kutosha kwa makampuni na wazalishaji wa ndani.

Kwa mujibu wa taarifa ya hali ya uchumi kutoka Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) iliyotolewa Juni 2021, uzalishaji wa mazao ya chakula nchini Tanzania uliongezeka kwa asilimia 11.7 kutoka tani 16,293,637 mwaka 2019 mpaka tani 18,196,733 mwaka 2020.

Aidha, mojawapo ya sababu inayotajwa kupelekea ongezeko hilo ni pamoja na matumizi ya teknolojia na pembejeo bora hususani matumizi ya mbolea za viwandani. Hii ina maana kwamba kama bei za mbolea zitabaki kuwa juu inaweza kupelekea kupungua kwa uzalishaji wa mazao ya kilimo hususani chakula.

Kwa mujibu wa taarifa za Wizara ya Kilimo, kwa msimu wa mwaka 2020/21 hadi kufika April 2021 uzalishaji wa mbolea kutokana na viwanda vya ndani ulifikia tani 32,239 huku tani 426,572 zikiagizwa toka nje ukilinganisha na mahitaji kwa msimu wa mwaka 2020/21 yakiyofikia tani 718,051.

Hii ina maana kwamba hadi kufika April 2021 viwanda vya ndani vilizalisha takribani asilimia 5 ya mahitaji ya mbolea, hali inayoonesha kwamba Tanzania inatumia fedha za kigeni zaidi ya dola milioni 200, sawa na shilingi billioni 463.8, kwa mwaka kuagiza mbolea za viwandani kutoka nchi za nje.

Hivyo uwekezaji unaofanywa na sekta binafsi kwenye sekta Ndogo ya mbolea utaongeza tija kwenye kilimo, uzalishaji na kupunguza uhaba wa mbolea ambao umekuwa tatizo Kwa nchi nyingi barani Afrika na mataifa mbalimbali hasa kutokana na kupungua Kwa uzalishaji wa mbolea kutokana na janga la Korona (UVIKO-19) ambalo limeathiri biashara nyingi duniani. Hivyo ongezeko la uwekezaji wa sekta binafsi katika viwanda vya mbolea ni moja kati ya maeneo muhimu ya kimkakati katika kujenga uchumi wa nchi Kwani sehemu kubwa ya nguvu kazi imeajirwa katika sekta hii ya kilimo ambayo pia huchangia karibia ya asilimia 29 ya pato la Taifa

Imeandaliwa na,

Felician Andrew
21 Disemba 2021

IMG-20211221-WA0017.jpg

IMG-20211221-WA0019.jpg

IMG-20211221-WA0018.jpg

IMG-20211221-WA0020.jpg
 
  • Thanks
Reactions: Lee
Back
Top Bottom