Bashe aipasha CCM

Kizimkazimkuu

JF-Expert Member
Nov 8, 2007
337
234
Frederick Katulanda, Geita na Daniel Mjema, Igunga

MJUMBE wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Hussein Bashe, ameonya kuwa iwapo CCM hakitajadili matatizo ya wananchi sasa, kitarajie kupoteza dola mwaka 2015, kama ilivyotokea kwa chama tawala Zambia.

Akizungumza katika Kata ya Kasamwa wilayani Geita katika maadhimisho ya miaka 33 ya kuanzishwa kwa UVCCM, Bashe alisema kuwa uchaguzi wa Zambia umemalizika na chama kilichoongoza kwa zaidi ya miaka 20 kimeondolewa madarakani, tukio linalopaswa kuwa funzo kwa CCM.

Alisema katika mazingira ya sasa ambayo wapiga kura wengi ni vijana, CCM kinapaswa kuwasikiliza, kujadili matatizo yao na kuyapatia ufumbuzi, vinginevyo kitang'oka madarakani muda mfupi ujao.

“CCM kianze kujiandaa leo kwa kutoa majibu ya matatizo ya vijana kinaowaongoza ikiwa ni pamoja na viongozi wake kuepuka kukaa ofisini na umangimeza kwani bila hivyo, mwaka 2015 wataanza kutafuta mchawi,” alisema Bashe na kuendelea:

“Kiache kutafuta mchawi mmoja mmoja, kiache kujadili watu kijadili matatizo ya watu tujadili watu wanapata wapi maji, watu wanapata wapi ajira, wanapata wapi zahanati na fedha zinazotengwa katika halmashauri ya wilaya kwenda kwa wananchi zinawafikia... haya ndiyo mambo ya msingi kabisa kama yakifanyiwa kazi CCM kitaendelea kushika dola.”

Alisema wakati UVCCM leo ukisherehekea miaka 33 tangu kuanzishwa kwake, viongozi wanatakiwa kujiuliza ni kwa nini watu wengi hawajaichagua CCM na ni vipi vijana wengi ndiyo wanaoonekana hawataki kuiunga mkono CCM. Alisema hii ndiyo changamoto kubwa inayokikabili chama hicho tawala kwa sasa.

Bashe alisema vijana wa Tanzania leo watapenda CCM kama tu kitawahakikisha elimu bora, afya bora, fursa ya kufanya kazi na kujiajiri na uchumi ulio imara.

“Taifa linakwenda kwenye uchaguzi mwaka 2015, kipindi hicho kitakuwa na wapiga kura wapya zaidi ya milioni sita ambao wengi watakuwa ni wale wenye umri wa miaka 30. Vijana hawajui habari za uhuru na amani wala nini, wanataka kusikia wamepata zahanati, elimu bora na wamepata fursa za kufanya kazi basi, hapo ndipo chama kitakuwa kimejibu matatizo yao.”

Alisema CCM ya leo siyo ile ya miaka 10 iliyopita na kwamba ndani yake kumejaa migawanyiko mingi aliyoieleza kuwa haina maslahi kwa watu wanaowaongoza huku, akisema kumejaa mizengwe mingi na matokeo yake watu wamekuwa wakikimbilia upinzani.

“Lazima tujiulize maswali kulikoni hali hii? Lakini majibu tunayo ni kwa sababu UVCCM imeshindwa kufikia mahitaji ya vijana wengi na sasa wanakichukia chama hiki.”

Alisema vijana wengi wamezaliwa na kukua na kuukuta uhuru ambao leo, unasherehekewa na taifa kutimiza miaka 50. Wakati huo vijana wa CCM nao wakisherehekea miaka 33 ya kuzaliwa umoja wao, uhuru huo umetokana jitihada binafsi za wazee na vijana wa wakati ule, vijana wa sasa hawana habari na uhuru.

“Nimeambiwa CCM tulishindwa uchaguzi katika Kata ya Kasamwa tuliyopo ambayo tunaadhimisha miaka 33 ya umoja wetu. Kata ipo chini ya Chadema na nimeambiwa hapa kumewahi kutokea vurugu. Labda niseme jambo moja kuwaambia Kasamwa uamuzi mlioyafanya wa kuchagua kutoka Chadema ni wenu na ndiyo demokrasia. Mmempa udiwani mbaye hatokani na CCM, lakini niwaombe tofauti za kisiasa zisiwagawe kufikia hatua ya kushambuliana.”

“Nilipata taarifa kwamba mlifikia hatua ya kuchomeana nyumba hapa Kasamwa. Niwaombe vijana wenzangu haya maslahi ya kisiasa yasitugawe vijana wenzangu, tutofautiane kwa sera na itikadi, lakini tusivurugane, haisaidii mtu yeyote ikitokea vurugu hapa na vijana ndiyo watakuwa wa kwanza kuathirika.”

Alisema viongozi wa UVCCM wanapaswa kuepuka ‘Ndiyo mzee’ bali kuhakikisha wanazibana halmashauri za wilaya zifanye kazi ambayo itasaidia kuleta maendeleo kwa wananchi na vijana kwa ujumla na alionya kuwa CCM kinapaswa kuhakikisha kuwa maeneo yaliyochukuliwa na upinzani hayaachwi kwa kuhakikisha kinafikisha maendeleo.
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom