BASATA laagiza wasanii wote kusajiliwa, laonya mapromota watakaotumia wasanii wasiosajiliwa

RUCCI

JF-Expert Member
Oct 6, 2011
1,701
1,714
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) linawataka wasanii wote nchini kuhakikisha wamesajiliwa na kuwa na vibali vya Baraza kwani kufanya vinginevyo ni kuvunja sheria ya Bunge namba 23 ya mwaka 1984 iliyolianzisha BASATA ambayo inamtaka mtu yeyote anayejihusisha na shughuli za Sanaa kuwa amesajiliwa na kupewa kibali na BASATA.

Aidha, BASATA linawaagiza Wakuzaji Sanaa wote (Mapromota) wanaoendesha matukio ya Sanaa kama vile matamasha, mashindano, maonyesho na utoaji tuzo nchini kuhakikisha wanafanya kazi na Wasanii waliosajiliwa na wenye vibali vya BASATA na si vinginevyo.

Sambamba na hili, BASATA linawaagiza wamiliki wote wa studio (Production Houses) zinazozalisha kazi za Sanaa kuzisajili mara moja na kuhakikisha zinakuwa na vibali halali vya Baraza la Sanaa la Taifa.

Ieleweke kwamba kwa mujibu wa sheria hii ya BASATA, Baraza limepewa mamlaka ya kutoa vibali na kuratibu matukio yote ya Sanaa nchini hivyo kuanzia sasa Baraza litaanza udhibiti wa matukio haya ya Sanaa hasa katika kuongeza sharti la kuwataka waandaaji wote wa matukio ya Sanaa kuwataka wasanii watakaoshiriki matukio yao kuwa wamesajiliwa na kupewa vibali na BASATA.

BASATA halitavumilia kwa namna yoyote kuona Mkuzaji Sanaa (Promota) akitumia wasanii wasiosajiliwa na kuwa na vibali kutoka BASATA kwani kufanya hivyo ni kuvunja sheria za nchi hasa sheria hiyo namba 23 ya mwaka 1984 inayoelekeza usajili na utoaji vibali kwa wadau wote wa Sanaa.

Itakumbukwa kwamba mnamo Mwaka 2013 Serikali kupitia Sheria ya Ushuru wa Forodha ilitangaza rasmi kuzirasmisha sekta za muziki na filamu. Sheria hii pia inawataka wasanii wote nchini kusajiliwa na kupewa vibali na BASATA na kinyume chake ni uvunjaji wa sheria.

Hata hivyo, toka kuanza kwa mchakato huu wa urasmishaji sekta ya Sanaa ni wasanii wa muziki wa injili pekee ndiyo wamekuwa wakisajiliwa kwa wingi huku wale wa muziki wa kizazi kipya na filamu wakisuasua bila kuwepo kwa sababu za msingi.

BASATA limekuwa likichukua hatua kadhaa kurahisisha mfumo wa usajili wa wasanii ambapo kwa sasa msanii anaweza kupata fomu ya usajili kupitia mtandaoni www.basata.go.tz au kwa maafisa Utamaduni wa Wilaya na baadaye kujaza fomu na kutakiwa kuziwasilisha BASATA zikiwa zimeambatanishwa na wasifu binafsi (CV) wa Msanii husika.

Aidha, gharama za usajili ni kiasi cha Tsh. 75,000/- pekee ambapo fomu hupatikana kwa Tsh. 5, 000/-, Usajili 30,000/- na kibali cha kila mwaka 40,000/-

Kwa upande wa studio na wakuzaji Sanaa (Mapromota) gharama ni sawa na za msanii isipokuwa tofauti huwa kwenye kibali abapo wao hulipa kiasi cha Tsh. 200.000/- kwa mwaka.
SANAA NI KAZI TUIKUZE, TUILINDE NA KUITHAMINI.

Godfrey L. Mngereza

KATIBU MTENDAJI, BASATA
 
Back
Top Bottom