Barua ya wazi kwa Rais Samia Suluhu juu ya Katibu Mkuu wa TAMISEMI

Ndumbusya

New Member
Sep 25, 2014
2
4
BARUA YANGU YA WAZI KWA MHESHIMIWA RAIS SAMIA SULUHU HASSAN KUHUSU KATIBU MKUU WA TAMISEMI INJINIA JOSEPH NYAMHANGA.


Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa mama Samia Suluhu Hassani, naomba kwa heshima na unyenyekevu mkubwa nitoe ombi langu kwako juu ya Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) mheshimiwa Injinia Joseph Nyamhanga.

Mheshimiwa Rais, mimi ni mwalimu katika shule mojawapo ya sekondari katika mkoa wa Morogoro Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero na mke wangu ni mwalimu yuko katika Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo mkoa wa Dar es Salaam.


Mheshimiwa Rais, mimi na walimu wenzangu tumekuwa tukihangaikia sana suala la uhamisho kama watumishi wa umma tangu mwaka 2018 na walimu wengine tangu mwaka 2017 bila mafanikio.


Mheshimiwa Rais, matakwa yote ya uhamisho ikiwepo kupitishiwa barua mbalimbali za Waajiri (wakurugenzi) zimekuwa zikipitishwa na kupelekwa kwa Makatibu Tawala wa Mikoa lakini zinapofika TAMISEMI Dodoma hazifanyiwi kazi kabisa na Katibu Mkuu. Hali hiyo imewafanya walimu kufika Dodoma kufuatilia suala hilo lakini majibu yamekuwa ya kukatisha tamaa.


Mathalani, Mwezi Januari 2019 nilifika ofisi ya TAMISEMI jijini Dodoma na kuuliza iwapo barua ya mke wangu kutoka Ubungo kuhamia Morogoro imeshaandikwa. Nilijibiwa kwamba nisubiri kwa kuwa sisi walimu ni waongo sana. Tunataka uhamisho kwa sababu zisizokuwa na maana. Aidha, nilimsikia Naibu Waziri wa wakati huo Mwita Waitara akisisitiza hilo Bungeni kwamba walimu wa Tanzania ni waongo sana. Wanataka kuhama maeneo mbalimbali kwa sababu za uongo hivyo akalieleza Bunge kwamba uhamisho umesitishwa.

Mheshimiwa Rais, mwezi Juni mwaka 2020 nilifika ofisi ya TAMISEMI Dodoma kujua nini ni kikwazo cha kumzuia mwalimu ambaye ni mke wangu kuhamia Morogoro au mimi kuhamia Dar Es Salaam kutoka Morogoro??. Majibu yalikuwa ni kwamba barua zipo ila Katibu Mkuu hayupo. Majibu hayo yalitutia mashaka walimu wengi tuliokuwepo kwa kuwa baadhi ya walimu walituambia walimuona Katibu Mkuu akiingia ofisini.

Baada ya walimu kutaka kupatiwa majawabu ya hatima ya uhamisho wetu, aliingia Katibu Mkuu na kutambulishwa na wasaidizi wake kwamba sisi walimu tumekuja kuleta fujo jambo ambalo halikuwa la kweli. Katibu Mkuu alivua miwani yake na kutuangalia bila kusema chochote. Aliingia ofisini na baadaye tuliambiwa tuandike majina yetu na Halmashauri tunazotokea. Mmoja wa wasaidizi alitutaarifu kwamba ikiwa tutakubali kuandika majina basi wakurugenzi wetu watapigiwa simu na kutaarifiwa kwamba tunaleta vurugu TAMISEMI ili tuchukuliwe hatua.


Mheshimiwa Rais, walimu tangu zamani tuna makundi ya facebook na Whatsaap ambayo tunayaita walimu kubadilishana vituo vya kazi. Tumekuwa tukipata watu wa kubadilishana. Mathalani, mwalimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Dodoma anaomba kubadilishana kituo na Mwalimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro. Lakini uhamisho huo wa kubadilishana nao Katibu Mkuu wa TAMISEMI Joseph Nyamhanga ameuzuia. Inasikitisha.


Walimu tunajiuliza, tumeikosea nini serikali yetu ya Tanzania?. Tuna kosa gani mbele za Mungu?. Mbona sekta zingine kama Mambo ya Ndani ya Nchi kama Magereza,Polisi,Uhamiaji uhamisho ni jambo la kawaida tena uhamisho wa malipo wakati sisi walimu tunanyimwa hata wa kujihamisha bila malipo?. Inakuwaje sekta za Maendeleo ya Jamii, Afya, Sheria, Mahakama, Maafisa Utumishi nk wanahama kila uchao lakini walimu tumezuiwa??. Sisi walimu tunaadhibiwa kwa makosa gani haya yasiyosameheka??. Tumeikosea nini serikali ya Tanzania chini ya CCM??

Mheshimiwa Rais, kutokana na baadhi ya wasaidizi wa Katibu Mkuu kutoridhishwa na ubabe wa Joseph Nyamhanga na namna anavyopuuza watu, inaonekana kuna baadhi walivujisha majina 8000 ya watumishi wa umma waliopaswa kuhama Oktoba 2020 na kuyatuma majina hayo katika mitandao ya Kijamii.


TAMISEMI iliyakataa majina hayo kwamba siyo sahihi lakini kimsingi yalikuwa ni majina ya walimu mbalimbali walioomba uhamisho tangu mwaka 2017 na watumishi wengine na hata hivyo wengine walipata barua zao kwenda vituo vipya.Hakukuwa na watu ambao hawakuomba uhamisho walioonekana katika orodha ile. Wale ambao walikuwa wameomba na wengine tayari walikuwa wameshahama na kuripoti katika vituo vipya.

Mheshimiwa Rais, nisikuchoshe sana, naomba nimalizie kwa kusema kwamba, tunaomba uhamisho wa walimu uwe ni haki na tupate haki hiyo. Hatumuombei mabaya Katibu Mkuu ya kumuondoa au kumtumbua, bali tunaomba kama mamlaka yake ya uteuzi umuelekeze atende haki kwa walimu na watanzania kama ambavyo haki iko kwa wengine.

Tunakuomba mheshimiwa Rais, walimu kama binadamu wengine tunazo changamoto zinazotukabili na tunatakiwa kuhama maeneo fulani kwenda mengine ili kuboresha utendaji. Tunaomba TAMISEMI ya Katibu Mkuu Injinia Joseph Nyamhanga ibadilike na kutenda haki.Tuna imani kubwa sana na uongozi wako mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassani kwamba ni uongozi uliojaa Hofu ya Mungu na wenye kufuata sheria , Katiba ya Tanzania na utu wenye hekima na busara kubwa.


Wako katika ujenzi wa Taifa.

Mwalimu
Mvomero Morogoro.
 
Nyamhanga keahaliwa kichwa, subiria hotuba ya maza siku ya uapisho au mei mosi utasikia ya tamisemi na uhamisho.
 
TAMISEMI ipo ofisi ya rais hivo kila walifanyalo wanapata maelekezo toka kwa rais,tusimwonee eng.Nyamhanga au Jaffo.
 
Dah kazi kweli kweli. Yaani akavua miwani akawaangalia akanyamaza akaingia ofisini
 
Back
Top Bottom