Mzee Mwanakijiji
Platinum Member
- Mar 10, 2006
- 33,771
- 41,036
Na. M. M. Mwanakijiji
Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
YAH: Iongoze Afrika kupinga utawala wa kidhalimu wa Robert Mugabe
Naomba husika na kichwa hicho cha habari;
Hivi hadi nini kitokee ndipo viongozi wetu wataona kuwa kinachoendelea Zimbabwe ni aibu ya bara letu, na udhalilishaji wa utu, hadhi, na tunu ya mwafrika? Ni mpaka nini kifanyike ndipo tutaweza kuchukua msimamo wa kupinga uvunjaji mkubwa wa haki za binadamu, na kuchukua msimamo ulio dhahiri dhidi ya Robert Mugabe? Kwanini Tanzania nchi ambayo inadai katika Katiba yake kuwa "kila mtu anastahili haki ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake" ifumbie macho utu wa wana wa Zimbabwe ambao wanateswa katika mikono ya utawala wa kidhalimu wa Robert Mugabe?
Inakuwaje wanasiasa wetu na wabunge wetu wanashindwa kutoa msimamo wa kulaani kauli za kidikteta ambazo zimekuwa zikitolewa na utawala wa Robert Mugabe? Hivi kweli tunahitaji wazungu kutuonesha kuwa kinachotokea Zimbabwe hakina mfano wa haki za binadamu? HIvi kweli tunataka hadi Amnesty International na Human Rights Watch waje na kutuambia kuwa ya Mugabe ni uovu uliokithiri?
Je tumekuwa watii na wenye kuheshimu sura za watu kiasi hiki hadi tunaogopa kumwambia kuwa "tunashukuru kwa mchango wako lakini kwa hili tunakukana"? Je hakuna watu waliofanya mambo mazuri huko nyuma na katika maisha yao ya baadaye wakaharibu na historia zao zikatajwa na nyota pembeni?
Wale wanaolalamikia ukiukwaji wa haki za binadamu kule Palestine, Iraq na Afghanistani, walioandamana ujio wa Bush na ambao wakitetea haki za watu wa huko wako wapi leo hii wakati ndugu zetu wanaishi maisha ya wasiwasi na hofu kubwa chini ya mkono wenye kucha ndefu zichomazo wa Robert Mugabe?
Wakati umefika kwa viongozi wetu kuacha mazingaombwe ya diplomasia ya ukimya ambayo kimsingi ni ukimya wa kidiplomasia. Ni ukimya ambao unaendelea kutoa kibali kwa Utawala haramu wa Robert Mugabe kuendelea kutesa wananchi wa nchi hiyo. Je sisi Tanzania ambao tuliwahi kukiri katika imani zetu kuwa "binadamu wote ni sawa, na Afrika ni moja" leo hii tuko wapi?
Mch. Martin Luther King alipoandika barua yake kutoka Jela ya Alabama alisema wazi kuwa "udhalimu mahali fulani, ni udhalimu mahali pote" Je tunaweza vipi kukaa katika "kisiwa cha amani" wakati ndugu zetu wanateseka na kufanywa wakimbizi katika nchi yao wenyewe. Kwanini kina Morgan na wenzao waonekane si wananchi wa Zimbabwe kweli kwa sababu tu wanataka kuiokoa nchi yao?
Nini ambacho utawala wako unaogopa kusema na kufanya mbele ya Robert Mugabe? Hivi tukimtolea uvivu na kumuita kwa jina lake kuwa ni dikteta na kusema kuwa yanayofanyika Zimbabwe hayana nafasi katika bara la Afrika Mugabe atasema nini? Atatufanya nini? Hii heshima ya wazee ni heshima kweli wakati mzee anasimamia ubakaji na utesaji wa watu wake?
Naomba kutoa wito wa wazi, wa moja kwa moja na usio na utata kwako uwa Mhe. Kikwete kama Rais wa Tanzania, nchi ambayo imetoa na kulipa kwa damu ili nchi hizi za kusini mwa Afrika ziwe huru, asimame sasa na kusema "kama kutosha inatosha". Rais Kikwete ukiwakilisha mawazo ya kizazi kipya uungane na Botswana kwa kumwita Balozi wa Zimbabwe nchini na kuonesha kutokufurahishwa na yanayoendelea Zimbabwe.
Zaidi ya yote, Rais Kikwete akiwa ni Mwenyekiti wa AU aitishe mkutano wa haraka kati ya Morgan na Mugabe Jijini Dar (na si mtu mwingine nje yao) ili kujadiliana na kukubaliana jinsi uchaguzi wa marudio utakavyokuwa na kupata uhakika kuwa kila mmoja wao ataheshimu matokeo ya uchaguzi huo. Kikwete anaweza kufanya hivyo kwa kutumia kivuli cha NEPAD ambamo ndani yake kuna "African Peer Review Mechanism". Huu ni wakati wa kuonesha uongozi.
Na endapo Mugabe hatokuwa tayari kusikiliza ushauri wa rafiki, basi wakati umefika wa kuvunja uhusiano wetu wa kidiplomasia na Zimbabwe. Itauma, lakini inabidi.
Nikukumbushe maneno ya Rais Nyerere kwenye mkutano wa Jumuiya ya Madola mwanzoni mwa miaka ya sitini ambapo hoja ya kukubali kuiingiza Afrika ya Kusini katika jumuiya hiyo. Nyerere alisema wazi kuwa kwa kadiri ya kwamba siasa za kibaguzi zilikuwepo Afrika ya Kusini basi Afrika ya Kusini haiwezi kuwa mwanachama. Na akatamka yale maneno mashuhuri ya msimamo wa kiongozi mbele ya Malkia "Mkiwapigia kura kuwaingiza Afrika ya Kusini, mtakuwa mmepika kura kututoa sisi". Na hoja ya Mwalimu ikashinda.
Na ni Mwalimu huyo huyo ambaye alizungumzia suala la "uraia" baada ya Idi Amin kuanza kuhoji uraia wa waasia wa Uganda na kuanza sera zake za kibaguzi kule. Mwalimu alizungumza siku ile August 21, 1972 pale Chuo cha Ualimu Chang'ombe, Mwalimu alisema hivi "Afrika lazima ikatae kudhalilishwa, kunyonywa, na kusukumwa sukumwa. Na kwa moyo huo huo ni lazima tukatae kuwadhalilisha, kuwanyonya, na kuwasukuma sukuma wengine. Ni lazima tutende siyo maneno tu".
Mhe. Rais, Afrika inadhalilishwa na vitendo vya Mugabe na mashabiki wake. Afrika inafanywa duni kwa viongozi kama yeye. Ni kweli tuna matatizo yetu Tanzania, nafahamu tuna kashfa zetu za mambo ya fedha nchini na uongozi wa kishkaji; nafahamu wazi kabisa ndani ya CCM na serikali kuna kubebana na kulindana. Lakini ukweli ni wazi kuwa hatujafikia walipofikia Zimbabwe, hatujafikia mahali pa kufanyana vibaya kiasi cha Zimbabwe. Ni kweli tuna matatizo yetu lakini tukiyaweka ya Zimbabwe upande wa pili, ya kwetu yanaonekana ni kheri tupu!
Sisemi upuuzie matatizo yetu, sitoi ushauri kuwa ya kwetu kwa vile ni madogo basi usiyafuatilie. La hasha, ninachosema ni kuwa chukua msimamo kama kiongozi na kwa niaba ya wale waliotangulia mbele ya haki, kwa niaba ya wale waliomwaga damu yao kukomboa bara letu, usimame na kumwambia Mugabe inatosha na saa na wakati wake umepita aamue kujiuzulu na kustaafu kwani yeye kama wanadamu wengine, atakufa tu, na Zimbabwe itatawaliwa na mwingine. Mugabe hana ubavu wa kuzuia hatima ya nchi hiyo, na siku moja wengine watasimama mahali pake.
Akiamua kuachia ngazi sasa na kufanya mapatano ya kisiasa na wale walioumia chini yake, labda historia itamuonea huruma. Lakini Zimbabwe haiwezi kuendelea jinsi ilivyo, huku sisi rafiki zao na ndugu zao tukikaa nje kuangalia. Mhe. Rais, onesha msimamo sasa, na uliongoze Taifa letu kuchukua msimamo dhidi ya Mugabe ili tuwape nafasi ya ndugu zetu wa Zimbabwe ya kuishi katika nchi ya amani, utulivu, na mshikamano.
Sijaomba vingi, lakini hilo nakuomba kwa machozi.
Nimalizie kwa kukumbusha maneno haya ya baba wa Taifa tena alipozungumza mwaka 1959 kwenye mkutano ule uliofanyika Uingereza Juni 26 (karibu miaka 50 kamili iliyopita). Katika mkutano huo uliokuwa unazungumzia Afrika ya Kusini na utawala wa Makaburu Mwalimu alisema maneno haya "Serikali ya Afrika ya Kusini inapigana na historia, ni wao watakaoshindwa. Tunafahamu harakati za ukombozi zitafanikiwa katika Afrika ya Kusini. Kama tunajiamini tutashinda".
Mheshimiwa, Mugabe anashindana na historia na kwa hakika atashindwa; harakati za mabadiliko ya kisiasa yanayoendelea yatafanikiwa, na kama sisi sote tunajiamini kwamba tuko sahihi basi tutashinda. Tuongoze katika hili kwani bwana mdogo kutoka Botswana ameshaonesha njia.
Wasalaam katika Kuliinua Bara letu
M. M. M.