Barua ya wazi kwa ndugu Muhingo Rweyemamu

Mzalendo_Mkweli

JF-Expert Member
Jan 30, 2012
1,638
2,000
Kwako ndugu yangu, Muhingo Rweyemamu.

Salaam sana, natumaini kwa neema za Mungu unaendelea vyema, japo kupitia kwa wenzangu kwenye mtandao wa wahariri Tanzania yaani TEF nimefahamishwa kuwa unaumwa na muda mwingi upo nyumbani unapumzika.

Nakuandikia waraka huu nikiwa Moshi mkoani Kilimanjaro ambapo nipo kikazi.

Naamini kuwa kwa uwezo wa Mungu afya yako itaimarika mapema, ili urejee katika ujenzi wa taifa ambao umeufanya kama mwalimu, mwandishi wa habari, mkuu wa wilaya, na kwa sasa ukijishughulisha na mambo binafsi yakiwemo yale ya kilimo na ufugaji.

Baada ya kusikia unaumwa, akili yangu ilirudi nyuma mwaka 1993, ambapo ndio uliacha kazi ya ualimu ukaja kujiunga nasi pale gazeti la Mwananchi, wakati huo likimilikiwa na Rihaz Gulamani, na likitoka mara mbili kwa wiki.

Ulipokuja uliwakuta wahariri wetu ambao ni mzee Barnabas Maro, Hamis Mzee na Ernest Zulu, huku waandishi tukiwa ni pamoja na mimi, Jamillah Mwanjisi, John Ngahyoma, Amabilis Batamula, Obed Mwangasa, Moses Kitundu na wengineo.

Pamoja na kuwa ulitokea kwenye ualimu, ulianza kuandika stori nzuri na za kuvutia kuliko sisi wengine ambao tulikuwa ndio tumetoka vyuoni, na kwa sababu ya umakini wako ulipata lead stori mara nyingi kutushinda.

Baada ya mimi kwenda masomoni nje ya nchi mwishoni mwa mwaka 1994 hatukuwasiliana tena hadi miaka tisa baadaye, niliporejea nchini na kuajiriwa na vyombo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Habari Corporation, The Guardian Limited, na Daily News ambako nilifanya kazi kwa miaka kumi mfululizo.

Ukiwa Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Muhingo ulivutia wengi, na hasa azma yako ya kuhakikisha mtoto wa kike anakwenda shule, na ni bahati mbaya hadi leo watetezi wa haki za mtoto hawajatambua mengi uliyoyafanya Handeni, na hasa ile kampeni yako ya ‘Niache nisome’.

Kwenye mtandao wa Facebook uliendelea kuwasiliana nasi waandishi wenzako ukitushukuru kwa jinsi tunavyotiana nguvu katika shughuli zetu mbalimbali.

Mwezi Mei mwaka 2012 uliteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa Mkuu wa Wilaya ya Handeni na ulipofika kule ukakuta watoto wanazuiwa kupata haki yao ya kuitwa watoto.

Ulikuta wasichana wadogo walioko shuleni wakipewa mimba hovyo na watoto wa miaka hata 12 wakiozwa, na kila mara ukatuambia kuwa hata ukibaki peke yako kwenye juhudi zile ungeendelea kupambana hadi mwisho.

Muhingo uliwatoa watoto wengi kwenye ndoa za utotoni na nakumbuka mmoja ulimfuata Bagamoyo ambapo mume wake alikuwa anapara samaki ferry na kumwajibisha, huku ukimrudisha yule binti shuleni.

Ulianza kazi Handeni ukakuta kuwa watoto wenye ujauzito wakiwa asilimia 11 kwa wanafunzi wa sekondari, na ulitoka wilayani humo mwaka 2015, na mimba zikawa zimeshuka na kuwa asilimia 0. 03. Hongera sana kwa juhudi zako za kumwendeleza mtoto wa kike.

Uliwahi kutuambia kuwa ulipofika Handeni serikali ilikuwa inapeleka chakula cha msaada wilayani humo kila mwaka lakini kwa juhudi zako, ulihimiza umuhimu wa kilimo na ulihama Handeni wilaya hiyo ikiwa ni moja ya maghala ya taifa ya chakula, kwani ghala la NFRA lipo pale tarafa ya Tengwe.

Muhingo uliingia Handeni ambapo misitu wilayani kule ikiwa kama shamba la bibi ambapo watu waliingia na kujikatia miti wapendavyo, lakini ukienda pale ofisi ya TAFORI Handeni, jina la Muhingo limeandikwa ofisini kwao kwa juhudi zake za kurejesha miti ya asili.

Ndugu yangu Muhingo ulipofika Handeni mauzo ghafi ya mifugo katika minada yakizalisha milioni 400 kwa mwezi, lakini ulipotoka mauzo ghafi ya mifugo ilikadiriwa kufikia shilingi bilioni mbili kwa mwezi.

Kwa miaka mitatu Muhingo ulipokuwa Handeni ulijifunza mengi, na shukrani zako za dhati uliwapa wana Handeni popote walikokuwa, na shukrani za pekee ukazielekeza kwa waandishi wa habari wenzako katika tasnia ya habari, ambao ulikiri walikutia moyo sana katika kazi zako.

Kile ulichoagizwa kufanya ulikitenda kwa mujibu wa maelekezo ya kanuni, sheria, na taratibu za kiutendaji, na tunajua ulifarijika sana kuona unaelekea Makete huku ukiacha watoto wa kike wakisoma kwa bidii na kesi za ujauzito mashuleni ikiwa imepungua kwa asilimia kubwa.

Hukuacha daima kumshukuru mke wako Dk. Fatma na marafiki zake wa kundi la Divine Friends for Life (DFFL) ambao walisoma wote Chuo Kikuu cha Dar es Salaam waliokushauri kufanya utafiti kabla ya kuanza kuchukua hatua, na hapo ndipo ulipoanza ile kampeni maarufu ya ‘NIACHE NISOME’.

Shukrani zako ulizielekeza kwa wote mliokuwa pamoja katika kampeni ya kulinda misitu na Handeni ikaanza kurudi katika u-kijani wake.

Uliwashukuru sana vijana wa Segera ambao waliokubali kutekeleza wazo lako la kupanda miti ya mbao, bila kuwasahau Kambi Mbwana na wanamtandao wote wa ‘Handeni Kwetu’.

Nakumbuka wale vijana wa vijiji vya Kwamsisi, Pozo, Kweidikabu na Kwasunga ambao mliongozana kwenda Msata kuangalia jinsi vijana wenzao wa huo wanavyofaidi na kilimo cha mananasi.

Wakulima wa mbogamboga wa kijiji cha Masatu mlioongozana kwenda Hai mkoani Kilimanjaro kuangalia wakulima wa huko wanavyopata faida kutoka kwenye mbogamboga.

Wafugaji wa Handeni uliongozana nao kwenda Kongwa kwenye ranchi ya taifa kuona ufugaji wa kisasa na mliporudi wakakuomba uwatafutie madume bora nawe ukafanya hivyo.

Kwa pamoja wafugani walipata madume 64 waliyokabidhiwa na mheshimiwa rais Kikwete na kwa hakika ufugaji wao ukaanza kubadilika.

Ukweli ni kwamba hata ulipohamishwa kwenda Makete mwaka ule wa 2015 hukuondoka kinyonge, bali ulisindikizwa na umati wa watu waliotambua mchango wako wa maendeleo katika wilaya ile.

Nakumbuka kule Makete ulikaa miezi mitano tu labda kwa sababu za kiafya, lakini ukiwa huko ukafanya kazi moja ya kuhakikisha madume bora ya ng'ombe wa Kitulo yanasambaa vijijini na wengi tunajua ulifanikiwa sana kwa jambo lile.

Morogoro napo umekaa kwa muda mfupi tu, hata hivyo wananchi kule watakukumbuka kwa maamuzi ya haki, na kwa uchache tunaweza kuyasema hayo.

Kwa niaba yako wahariri wengi wanamshukuru sana Kikwete aliyekuteua na kukufanya uongeze ujuzi, busara na hekima katika maamuzi, na pia Rais John Magufuli aliyepokea ombi lako la kustaafu na kwenda kuwa mjasiriamali.

Muhingo nakumbuka darasa ambalo umekuwa ukitoa kuhusu darasa la tea bag, yaani kile kifuko kibebacho majani ya chai ambacho huwa unasema hata mfuko wenyewe unajua kwamba cha muhimu zaidi ni kile kilichopo ndani ya kimfuko hicho.

Umekuwa ukitualika tugundue kuwa yale majani ya chai ndani ya vile vimfuko yanatengenezwa kwa urembo mwingi na ukatuambia kama zilivyo zile tea bags, basi na sisi wanadamu tupo hivyo hivyo.

Katika andiko lako moja kwetu sisi marafiki zako wa facebook ulisema kuwa pesa tuliyonayo, majumba yetu, vyeti vyetu, na hata magari tunayoendesha, hakuna cha maana kama huduma kwa wananchi tunaopaswa kuwahudumia ni ya hovyo.

Kwa mfano huo huo wa majani ya chai ndani ya kifungashio ni kwamba ladha yake inapatikana tu wakati majani hayo yakichanganywa na maji moto, hivyo ukasema kuwa kwa binadamu kukumbana na misukosuko, tabia yake inajulikana kama maji ya moto yanavyotumika kupima ubora wa majani, misukosuko inampima binadamu kujua tabia ya kiongozi fulani.

Ulituambia kuwa tea bag ni lazima iwe na matundu ya kuingiza maji ndani, na sisi katika maisha yetu hatuwezi kuishi kama visiwa.

Kiongozi ni lazima awe mwangalifu ili asijenge ukuta utakaowazuia wananchi kumfikia, na hakuna uongozi kama wananchi wanamwogopa yule anayewaongoza.

Muhingo kuna kipindi ulimwandikia Waziri Ummy Mwalimu, ukimpongeza sana kwa juhudi zinazofanywa za kuwalinda watoto wa kike, na ukasema ilikuwa imani yako kwamba serikali haitaisahau kampeni uliyoanzisha na kuendesha Handeni ya NIACHE NISOME.

Kilichowasaidia ni kwamba hamkuwaacha nyuma waathirika ambao ni wasichana, kwani jamii ilisaidia kuwapata wahusika wa ujauzito kwa wasichana wadogo.

Kuna kipindi Muhingo ulikiri ulikuwa “ume-miss” sana kuandika, na ukakumbuka wakati fulani uliwahi kuandika safu ukaiita ‘Acha niandike kama mwendawazimu’ lakini uandishi wako tunaokujua huwa unalenga kumgusa kila mtu.

Ni katika mema haya nathubutu kutamka kuwa Muhingo Rweyemamu uliiwakilisha vyema tasnia ya habari katika wajibu wako kama mkuu wa wilaya.

Katika mateso ya ugonjwa wako kwa sasa unapaswa kujiona fahari kwa kile ulichokifanya kwa nchi hii, na wengi tunaamini kuwa mwenyezi Mungu atakupa ahueni na urejee katika shughuli zako za kawaida.

Hakuna gumu limshindalo Mungu, na naamini Mungu atatenda, ili uanze kuchonga penseli yako tena, na kuandika habari na makala ya kuvutia kama ilivyo kawaida yako.

Muhingo nimekuandikia barua hii ya wazi, ili ndugu, marafiki na wote walioguswa na kazi ulizowahi kufanya wajitokeze na kuchangia matibabu yako ambayo kwa sasa yanahitaji mchango mkubwa wa fedha.

Niwashukuru baadhi ya wahariri ambao tayari wamechanga kitu kidogo na kukutumia, na bado ninaamini kuna Watanzania wengi watajitokeza na kukusaidia kwa kadiri ya uwezo wao, ili upone haraka na kurudi katika shughuli zako za kawaida mapema iwezekanavyo.

Get well soon my dear brother.

Source : Barua ya wazi kwa ndugu Muhingo Rweyemamu – Raia Mwema
 

UMASIKINI BWANA

JF-Expert Member
Oct 17, 2013
936
1,000
Kweli Pia Aliwasaidia Vijana Wa Mkata Mawazo Ya Biashara Na Kilimo Na Baadhi Yao Wakaacha Kate Kamtindo Kakufanya Miguu Minne Ipige Tikitaka
 

FRANCIS DA DON

JF-Expert Member
Sep 4, 2013
22,592
2,000
Aisee R.I.P Muhingo, tujifunze kuwaenzi watu kwa mema waliyofanya wakiwa hai kabla hawajaaga dunia, big up mtoa mada!
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom