Barua ya Wazi kwa Mhe. Waziri Mkuu, Mizengo Peter Kayanza Pinda, a.k.a. Mtoto wa Mkulima

MwanaHaki

R I P
Oct 17, 2006
2,401
1,225
Miaka hamsini ya kujenga na kuuimarisha umaskini nchini Tanzania


NILISIKILIZA kwa makini hotuba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda, maarufu kwa jina la “Mtoto wa Mkulima”, aliyoitoa hivi karibuni kwenye Bunge la Jamhuri, alipokuwa akiwasilisha hoja kuhusu bajeti ya mwaka 2010-11 ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mojawapo ya “vilio” alivyovitoa Waziri Mkuu ni shutuma kali alizozilenga kwa upande wa wale wote ambao wamedai, kwa namna moja au nyingine, kwamba Serikali ya Chama Tawala, CCM, “haijafanya kitu chochote”.

Mhe. Waziri Mkuu alidai kwamba wale ambao wameibeza Serikali ya CCM – ambayo imetawala kwa zaidi ya miaka thelathini na tatu (33) sasa – ambayo ilirithi utawala wa nchi kutoka kwa chama cha TANU baada ya Muungano wa vyama viwili vikuu vilivyokuwa vikitawala kwenye Jamhuri, Tanganyika African National Union (TANU) na Afro Shirazi Party (ASP), kuungana na kuwa Chama Cha Mapindu i (CCM), tarehe 7 Julai 1977, kwamba watu hao wamepotoka, kwani ukweli wa kazi kubwa iliyofanywa na CCM inaonekana dhahiri.

Binafsi nina hakika kwamba Mhe. Waziri Mkuu hakuwaelewa, wala hakuwasoma vizuri watu hao ambao wana kila haki ya kuilalamikia Serikali ya CCM. Mhe. Waziri Mkuu hakuchanganua vyema hoja nzito ambazo zimeelekezwa kwa Serikali ya CCM, ambayo inadai “kuwakomboa” wananchi kupitia sera zake “nzuri” kwa maendeleo ya taifa. Hakika, Mhe. Waziri Mkuu hakutafakari ni mambo gani yalikuwa yanajadiliwa kwenye hoja hizo, kwani, iwapo angefanya tafakuri hiyo, angegundua ni mambo gani ambayo Watanzania walio wengi, mpaka leo wanalalama kuhusu nchi yao.

Alipokuwa akiwahutubia wadau wa sekta ya mazao ya bustani mapema mwezi Juni 2010 mjini Arusha, alihoji ni nani “aliyewaroga” Watanzania mpaka wakashindwa kwenye sekta hiyo muhimu na wadau wa nchi jirani ya Kenya. Napenda kukufahamisha Mhe. Waziri Mkuu kwamba, hakuna aliyewaroga Watanzania; unayoyaona ni “matunda” ya sera mbovu – zisizo na mapana wala marefu – za chama chako, CCM, ambazo zimepitwa na wakati, zimeandaliwa na watu ambao wamepoteza sifa ya kutambua maana halisi ya dhana ya “maendeleo ya taifa”.

Mhe. Waziri Mkuu, ashakum si matusi, ukichukua mkojo na kuuweka kwenye mvinyo, hautakuwa mvinyo tena. Ashakum si matusi, sera za CCM ni sawa na mkojo uliowekwa kwenye chupa ya mvinyo, kisha kuwekwa nembo nzuri na kuinadi kwamba ni ‘safi’.

Baada ya kusoma makala yangu haya, Mhe. Waziri Mkuu utanielewa. Hebu keti vizuri kwenye sofa, nyoosha miguu yako mbele, rekebisha mawani yako, tulia, usome makala haya – ushauri wa bure – kisha utaelewa ni nini wanachokitaka Watanzania kutoka kwa “serikali yao”!

UTAWALA BORA: Ingawa dhana hii imeonekana kuwa “nyepesi”
kwa ujumla wake, kiasi kwamba imebaki kuwa kaulimbiu ya “kusadikika”, utawala bora ni nguzo muhimu isiyokwepeka ambayo inaweka msingi wa kupata maendeleo endelevu kwa wananchi. Bila utawala bora, hakuna chochote kitakachofanikiwa, hata kama Masihi, Yesu Kristo, atarudi leo nchini na kuamrisha maendeleo kuletwa!

Mhe. Waziri Mkuu, wananchi wamekosa imani na Serikali yao; wamekosa imani na vyombo vyote vya dola ambavyo ni sehemu ya utawala bora, kuanzia Bunge, Serikali Kuu na Mahakama. Mhe. Waziri Mkuu, wananchi wamesalimu amri kwamba “mwenye nguvu ya pesa” ndiye “mwenye haki” wakati wa kuisaka haki huko Mahakamani. Wamenyoosha mikono juu na kukiri kushindwa vita dhidi ya mafisadi, ambao kila wakati wa Uchaguzi Mkuu wanakuwa mstari wa mbele “kugawa misaada” na zawadi lukuki, ili wachaguliwe kwa kura nyingi. Na baada ya kuchaguliwa hawaonekani tena majimboni hadi wakati mwingine wa Uchaguzi Mkuu, ambao mimi naupa jina la “Uchafuzi Mkuu”!

Mhe. Waziri Mkuu, wananchi wamebaini kwamba, “wenye nguvu ya pesa” ndio watakaotawala daima, kwani, wananchi – viongozi watarajiwa – wenye uchungu na uzalendo kwa nchi yao hawana “nguvu ya pesa” kuweza “kununua haki” ya kuchaguliwa kutawala, si kuiongoza nchi hii. Mhe. Waziri Mkuu, chama chako, Chama Cha Mapinduzi, kimewazoesha wananchi kwamba, kila ufikapo wakati wa kuwachagua, samahani, “kuwachakachua” wawakilishi wao – wabunge, madiwani, n.k. – basi, wakati huo ni wa “mavuno” kwao, kwani, kila atakayekinga bakuli apewe “vijisenti”, atamwagiwa humo lukuki mpaka bakuli lifurike, ilhali awe na uhakika wa kwenda kumpigia kura, samahani, “kumpa kula”, aliyemjazia bakuli lake hilo, Mtanzania huyo ambaye hana hili wala lile, hana mbele wala nyuma, kulia kwake hakuna tofauti na kushoto kwake, kaskazini kwake hakuna pia tofauti na kusini kwake. Tunasema, mitaani, “yupo yupo tu”!

Mhe. Waziri Mkuu, wananchi wamebaini kwamba yeyote yule atakayediriki kukwapua na kupeleka anakotambua yeye, fedha za umma, kwenye halmashauri, mashirika ya umma, na sehemu nyingine, hatapata tabu ya “kusulubiwa kwa Pilato” kama inavyokuwa kwa “walalahoi” wenzao, ambao wengi wao hupata “hukumu ya kifo ya papo kwa hapo” na “wananchi wenye hasira”, kwa tuhuma – si ushahidi – za wizi wa kuku, simu za mkononi, mikoba ya wanawake, na kadhalika. “Mahakama” hizi za mtaani zimesheheni zaidi sehemu ambapo idadi ya maskini ni kubwa, ambako kuna nyumba nyingi za udongo – wenyewe huita “mbavu za mbwa” – ambazo ndizo makazi ya walalahoi hao, kuliko kule ambako kuna maghorofa ya kila aina, ambako rangi nyeupe si aghalabu kuziona kwa wingi, zikiwamo zile za Wachina, Wafaransa, Wa Afrika Kusini, Wamarekani, na aghalabu akina Bwana Kubwa fulani wenzetu “wa hapa hapa”! Mitaa hiyo ya “uzunguni” ukipiga mbiu ya “Mwiziiii!” watu watakupita na kukutazama, huku wakitazamana na kusema: “Jamani, hebu mwoneeni huruma huyu, kachanganyikiwa haswa! Sijui tumpeleke Mirembe?” Kumbe kweli umeporwa, tena fedha zako nyingi tu, na tapeli aliyekubuhu, ambaye anaishi kwenye hayo hayo maghorofa, wewe ukadhani ukienda huko kudai haki yako – tangu lini Kaizari akamsikiliza mlalahoi? – kwa “wenye nazo” utaipata! Thubutu! Haya, tuendelee… maana naona natoka nje ya mada, kidogo…

Mhe. Waziri Mkuu, wananchi wamebaini kwamba ni vigumu anayekwapua Shilingi Bilioni kadhaa kwenda jela, kuliko yule anayetuhumiwa wizi wa kuku kuhukumiwa kifo cha papo kwa papo na wananchi hao wenye hasira. Sawa na ile kauli ya kale, kwamba ni vigumu tajiri kwenda mbinguni kuliko …. Ah, Mtoto wa Mkulima, jazia mwenyewe hapo. Mie simo!

Wananchi wamebaini kwamba, haki haipatikani tena Mahakamani, kwani imenadiwa kwa wenye “nguvu ya pesa”; kwa hiyo, wajane watapoteza haki yao ya kufungua na kusimamia mirathi ya waume zao, ili kulinda maslahi ya watoto wao, kwani ndugu wa marehemu waume zao, ndio watakaochukua kila kitu na kuwaacha wakiteseka na watoto wao. Watauza zile nyumba za urithi kwa “wenye nazo”, ambao kutwa wanazikodolea kwa uchu, kwani wanajua kwamba kule “uswazi” ni rahisi sana kuporomosha maghorofa bila kuzingatia kanuni za usalama wakati wa ujenzi – Ebo! Kwani wanaoshi “uswazi” wanastahili usalama wa makazi yao? Uliona wapi? – hivyo ni rahisi sana kuporomosha maghorofa yale, bila hata kuwa na nondo za milimeta 35 (nadhani hiki ndicho kiwango cha chini kabisa kinachostahili, la sivyo yule mhandisi amenipotosha!), sembuse zege “iliyotulia”! Halafu watakuja wale wa “maje…”, enhee, wale wale, kuja kuwatimua nje ya nyumba zao, wakikodi “watoto wa vijiweni” kuja kusaidia zoezi, nao hao wana lao, ndani ya nusu saa nyumba imesafishwa, nyeupe, na mwenye uwezo wa “kujisevia” anachokitaka anaishia nazo anakokujua yeye, mama mwenye nyumba wakati huo yuko kazini… ndiye mjane na msimamizi halali wa mali za marehemu, lakini Baba Mdogo yeye anaona bora nyumba iuzwe, haki itadaiwa kwa Mungu… alikuwa akitamani sana mali za kaka yake, sasa, ilhali hayupo, watoto watajua wenyewe pa kwenda… nyumba imeuzwa, shauri (si kesi) la mirathi bado halijaiva mahakamani, na wenye kuidai nyumba yao wameshaitwaa, kinyume cha sheria. Mhe. Hakimu kwa kuwa “kapozwa” kwa kitu kidogo, hana ubavu wa kuwaita waliojitwalia mali zile, hata kama ni wazi kwamba “mahakama imedharauliwa”… kwa Kizungu tunaita “contempt of court”. Hujui maana yake? Unaishi wapi? Mbagala? Ahaaa! Basi, siku ukiitwa mahakamani ukatoe ushahidi, usiende, ndipo utajua nini maana yake, sawa?

Mhe. Waziri Mkuu, wananchi wamebaini kwamba ni rahisi kwa mlalahoi kukamatwa kwa “mtego” wa Shilingi Milioni Mbili kuliko “kigogo” mwenye “strong room” nyumbani kwake, iliyosheheni mamilioni ya kila sarafu kubwa duniani, kukamatwa na kuhojiwa na TAKUKURU, akiulizwa: “Umezipataje?” Kwanza watu wa TAKUKURU wakifika pale hukaribishwa mezani kwenye “chai nzito” iliyosheheni kila aina ya vikorombwezo, kuanzia “bacon” hadi “scrambled eggs” – samahani, bado sijajua tafsiri halisi ya maneno haya – na wakishamaliza wanaitwa ofisini (Of course, kuna ofisi ya nyumbani! We vipi? Khaaa!) na hapo kila mmoja anapewa bahasha yake ya rangi ya kahawia. Anaambiwa asihesabie hapo kwani anaweza kupata mshtuko, ikawa kesi nyingine ya kuita ambulensi… Kalaghabahoooo!

Mhe. Waziri Mkuu, wananchi wamebaini kwamba ni rahisi kwa mtuhumiwa “mwenye nguvu ya pesa” kuachiwa dakika chache baada ya kufikishwa kituo cha polisi, au hata kutoroshwa na askari polisi, kisha kutokomea kusikojulikana, kuliko mlalahoi mwenzao, ambaye atafanyiwa kila aina ya maovu na kisha ndugu zake “kukamuliwa” pesa nyingi ili ndugu yao apate dhamana, ambayo ni haki yake!

Mhe. Waziri Mkuu, jambo hili ndilo linalowafanya wananchi wazidi kukosa imani na Jeshi la Polisi kila uchao, wakifikia uamuzi wa kuvamia vituo vya polisi ili “kuwahukumu” watuhumiwa wao wenyewe, pindi wanaposhindwa, huchukua hatua za kuvichoma moto na kuviteketeza vituo hivyo. Unakumbuka yaliyotokea Hedaru?!

Mhe. Waziri Mkuu, kama kweli Serikali ya CCM ingekuwa inazingatia “miiko” ya utawala bora, wale waliokwapua mabilioni ya shilingi Benki Kuu kupitia Akaunti za Madeni ya Nje (EPA) wasingeambiwa “warudishe pesa”, bali, wangekamatwa wote na kufikishwa mahakamani, kisha kuhukumiwa vifungo vya jela pamoja na kazi nzito. Mhe. Waziri Mkuu, kati ya watuhumiwa zaidi ya mia moja, waliofikishwa mahakamani hawafiki ishirini! Je, ina maana wale waliorudisha pesa sio wezi kama hao “dagaa” waliokamatwa na kupelekwa mahakamani, huku “mapapa” wakiendelea kutesa na kurandaranda na “mavogue” mitaani kutwa, huku wakiendelea “kuwachakachua” mabinti wa kilalahoi wanaotoka Tandale kwa Mtogole?

Mhe. Waziri Mkuu, Serikali ya CCM imeshindwa – na hili ni dhahiri kabisa – kusimamia utawala bora, kiasi kwamba, haki inakosekana na wananchi wanazidi kuteseka chini ya utawala dhalimu unaochangiwa na matumizi mabaya ya viongozi wa Serikali. Gazeti la “Mtanzania”, toleo la Jumapili, Juni 20, 2010, ukurasa wa 6, lilichapisha barua ya malalamiko ya mwananchi – Damas Bugwainwe – yenye kichwa cha habari “Katibu Mtendaji Kata huyu ni hatari”, akizungumzia vitendo vya udhalilishaji na matumizi mabaya ya madaraka ya “mtumishi wa umma” huyo anayewatesa wananchi – umma – aliotumwa kwao kuwatumikia! Mhe. Waziri Mkuu, ulikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), malalamiko ya aina hii uliyapata kila mara… hayakuisha wakati wako, hakika bado hayakuisha wakati wa aliyekuwa mrithi wako, Celina Kombani, na sasa mrithi wake … hata jina sijalijua, hakika hayataisha!

Mhe. Waziri Mkuu, zilitokea tuhuma nzito – tena mpya – za ufisadi wa matumizi mabaya ya rasilmali fedha, kwenye shirika la umma, Mamlaka ya Bandari Tanzania; magazeti mawili, “Mtanzania” na “Mzalendo” (hili linamilikiwa na chama chako, CCM), toleo la Jumapili, Juni 20, 2010, yote yalitoa taarifa kuhusu malipo yasiyoeleweka kwa “watumishi” kumi na wawili (12) wa Mamlaka ya Bandari kulipwa kiasi cha Shilingi Bilioni 1.22 katika kipindi cha miaka tatu tu! Taarifa hizo ziliwakilishwa na aliyekuwa Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani wa Ofisi ya Rais, Menejimenti na Utumishi wa Umma na Tume ya Utumishi wa Umma, Mhe. Grace Kiwelu (Viti Maalum-CHADEMA), alipokuwa akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2010/2011, Jumamosi, Juni 19, 2010. Kwa mujibu wa magazeti hayo mawili, msingi wa taarifa hiyo ni maelezo ya uchunguzi wa Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG). Hizi ni tuhuma nzito dhidi ya TPA, zilizothibitishwa na Serikali yako… kamwe, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali hawezi kusema uongo! Je, hili nalo umeliona? Umelifanyia kazi?

Kuhusu utawala bora… naishia hapa… lakini nimeeleweka.

DEMOKRASIA: Mhe. Waziri Mkuu, ufanisi wa demokrasia – haswa ikizingatiwa kwamba demokrasia hujenga nchi yenye amani, inayowawezesha wananchi wake kufanya maamuzi sahihi kwa mustakabali wao – “umezikwa rasmi” hivi sasa nchini Tanzania. Tumebakiwa na “demokrasia kiinimacho”, ambayo imejenga mazingira ya kuwapo kwa “nguvu ya pesa” ndani ya Chama Tawala, CCM.

Mhe. Waziri Mkuu, Serikali ya CCM imetunga na kupitisha Sheria ya Matumizi ya Uchaguzi ya mwaka 2010 (The Electoral Expenses Act of 2010), ambayo imelenga kudhibiti vitendo vya rushwa wakati wa kampeni za chaguzi mbali mbali hapa nchini, lakini wote tunatambua kwamba tatizo la rushwa wakati wa uchaguzi, kimsingi na kwa kiwango kikubwa, tena cha kutisha, liko ndani ya CCM, wala si kwa vyama vya upinzani! Haiwezekani vyama hivyo viwe vimeanzishwa kupinga mambo yote yatokanayo na ufisadi – ikiwemo rushwa – kisha navyo viwe vimeiga mkumbo huo. Hicho kitakuwa ni kichekesho, dhihaka na kejeli kwa Watanzania!

Mhe. Waziri Mkuu, wengi tumesema kwamba Sheria ya Matumizi ya Uchaguzi ya mwaka 2010 haina nia wala lengo la kudhibiti ulaji rushwa wakati wa uchaguzi, bali, ni sheria iliyopitishwa kuikandamiza na kuikaba kabali, kama si kuizika kabisa demokrasia nchini humu. Hali hii tayari imeanza kujidhihirisha, kwani licha ya tuhuma nyingi zilizopelekwa TAKUKURU, dhidi ya wagombea wa CCM kulalamikiwa kutoa rushwa na kufanya kampeni kabla ya muda wake, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Edward Hosea, amedai kwamba yeye na “vijana” wake walikusanya ushahidi kabla ya kuwapeleka watuhumiwa wote mahakamani. Mhe. Waziri Mkuu, wakati naandika makala haya nilikuwa nina hakika – kwa asilimia mia moja – kwamba hakuna yeyote atakayepelekwa mahakamani, kwani, haiwezekani kwa Mkurugenzi wa TAKUKURU, Edward Hosea, ambaye ni kiongozi aliyeteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, ambaye ndiye Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, kuwaadhibu makada wa CCM! Tusidanganyane! Hili haliwezekani!

Mhe. Waziri Mkuu, kwa upande wa demokrasia, “nguvu ya dola” itaendelea kutumika kuwatisha wananchi waipigie kura CCM. Tayari tumepata taarifa kwamba kuna baadhi ya vyombo hivi vya dola vilitumika kuwatisha wananchi kwamba wasipoichagua tena CCM “wataadhibiwa”. Pia, nguvu nyingi ilitumika kuwatisha wananchi kwa nia ya kujenga imani kwamba, mbadala wa CCM ni vita na ukosefu wa amani. Watanzania – kwa uwingi wao – ni waoga na wapenda amani. Kwa vitisho hivyo, wataendelea kuichagua CCM.

Demokrasia? Demokrasia gani? Hakuna demokrasia Tanzania!


UCHUMI: Mhe. Waziri Mkuu, Serikali ya CCM imebuni dhana ya “Kilimo Kwanza”. Kwenye bajeti ya Serikali Kuu ya mwaka 2010/2011, Waziri wa Fedha amedai kwamba bajeti hiyo imezingatia dhana hiyo ya “Kilimo Kwanza” kwa kuondoa ushuru kwenye vifungashio, yaani, paketi za juisi na maziwa. Paketi hizi ni zile zinazotokana na karatasi. Lakini cha kushangaza ni kwamba, hakuna kiwanda hata kimoja hapa nchi kinachotumia paketi za karatasi kusindika bidhaa za maziwa, kinachomilikiwa na Watanzania wazawa. Kiwanda pekee kinachosindika maziwa kwa kutumia paketi za karatasi maalum ni kile cha “Brookside”, kilichopo Jijini Arusha, ambacho kinamilikiwa na raia wa Kenya, na, cha kusikitisha zaidi, kiwango kikubwa (takriban asilimia tisini – 90%) ya maziwa yote yanayosindikwa kwenye kiwanda hicho hupelekwa nchini Kenya, huku Watanzania huambulia kiwango kidogo tu cha maziwa hayo. Awali, kiwanda hicho kilikuwa mkombozi kwa wakulima wanaofuga ng’ombe wa maziwa, hususan wale wa Sanya Juu, Wilaya ya Hai, Mkoa wa Kilimanjaro, ambao ndio wanaozalisha kiwango kikubwa cha maziwa kwenye Kanda ya Kaskazini Mashariki. Lakini sasa, kiwanda hicho kinaagiza maziwa kutoka nchini Kenya, jambo ambalo linapoteza maana halisi ya dhana hiyo ya “Kilimo Kwanza”.

Kwa kuwa wakati naandika makala haya Kampuni ya Maziwa ya Tanga ilikuwa bado haijaingia rasmi kwenye mchakato huu, wa kufungasha maziwa kwenye paketi za karatasi, napenda kuipongeza kampuni hiyo kwa ujasiri wake huo na ninaziomba kampuni nyingine, kama vile ASAS Dairies, kuiga mfano huo. Ni dhahiri kwamba sasa ushindani una nafasi kubwa hapa nchini, lakini Serikali izingatie kwamba, kimsingi, dhana ya “Kilimo Kwanza” HAITEKELEZEKI!

Mhe. Waziri Mkuu, nikiwa mdau wa kilimo na uchumi, nimeshangazwa kuona kwamba vifungashio mbali mbali vinavyotumia mali ghafi za chupa, kusindika bidhaa za mazao yanayotokana na kilimo ambavyo vinatoka nje ya nchi, na baadhi hapa nchini, kama vile mvinyo unaotengenezwa na ndizi; juisi inayotokana na maua ya rosella; pamoja na jam, asali, na kadhalika, havikuondolewa ushuru! Aidha, vifungashio vya plastiki na makopo, vinavyofungashia bidhaa zitokanazo na nyanya, kama vile tomato puree, tomato paste, tomato sauce, tomato juice, tomato ketchup, na kadhalika, havikuondolewa ushuru! Zaid, vifungashio vya paketi za karatasi, “aluminium foil”, makopo, na kadhalika, vinavyotumika katika kuhifadhia mbegu za mazao mbali mbali, navyo havikuondolewa ushuru! Mhe. Waziri Mkuu, hii kweli ni dhana ya “Kilimo Kwanza”?

Mhe. Waziri Mkuu, bajeti ya Serikali ya mwaka 2010-11 iliwakumbuka wadau wa sekta ya kilimo cha bustani kwa kuondoa ushuru kwenye uwekezaji wa nyumba maalum za kuzalishia maua, yaani, “green houses”, lakini bajeti iliwasahau wakulima wa mikataba wanaozalisha mbegu za mboga na mazao ya maua, ambao wanahitaji fedha kwa ajili ya kuwekeza kwenye mifereji ya maji kwa matumizi ya kilimo cha umwagiliaji; miundo mbinu kama vile barabara zinazopitika kila wakati, hata kama ni za changarawe; fedha kwa ajili ya kujenga shule, zahanati, vituo vya afya au hospitali kwa ajili ya wananchi waliopo kwenye sehemu wanazoishi, wengi wao wakiwa ni wafanyakazi katika miradi hiyo pamoja na familia zao; na pia, kuweka fungu la uwezeshaji kupitia mikopo nafuu kwa ajili ya kujikimu, kupitia vikundi vya SACCOS na kadhalika! Bado tutasema kwamba bajeti hiyo ni ya “Kilimo Kwanza”?

Mhe. Waziri Mkuu, kiwango kikubwa cha Watanzania, hususan wale wanaoishi vijijini, kutokana na umaskini wao, wamelazimika kuyakimbia makazi yao na kuhamia sehemu za karibu na barabara kuu. Hali hii inajidhihirisha kutokana na ujenzi holela wa nyumba ambazo zinazojengwa kwa kusindika udongo ambazo hazifai kwa matumizi ya binadam, tena mara nyingi zinazojengwa kwenye eneo la hifadhi ya barabara kuu, pasi na Serikali kutoa tamko lolote au kuchukua hatua yoyote ile ya kisheria, mpaka pale ambapo inabidi barabara hizo kuu kuhitaji kupanuliwa, na hapo Serikali hulazimika kuwalipa fidia watu hao ambao wanakuwa wameishi barabarani miaka kadhaa! Lakini cha ajabu na kuikitisha sana, Mhe. Waziri Mkuu, hakuna mtu yeyote kwenye Serikali yako ambaye ameona kwamba hili ni tatizo, hususan ikizingatiwa kwamba, hivi sasa, wageni wengi kutoka nje ya nchi wanapendelea zaidi usafiri wa mabasi – luxury… Marcopolo, Yutong, Irizar, n.k. – kwa kuwa, hata wao huko nje wana hali mbaya ya kiuchumi na usafiri huu ni wa gharama nafuu kwao, kuliko kupanda ndege, hata wakiwa hapa nchini. Tunasahau kwamba wanapokuwa njiani hupenda kupiga picha, wakirudi nyumbani kwao wawaoneshe wenzao kwamba: Hii ndiyo Tanzania ya sasa!

Mhe. Waziri Mkuu, hivi Ofisi yako haioni kwamba uhamiaji huu holela wa wananchi kukimbilia barabarani, tena kwenye Eneo la Hifadhi ya Barabara Kuu, na kujenga nyumba hizi za “tembe”, sio tu ni kurudisha nyuma harakati zote za kimaendeleo, bali pia, ni kujenga picha potofu mbele ya wageni wetu, kwamba kweli Tanzania ni nchi masikini, tena masikini sana? Je, Mhe. Waziri Mkuu, huoni kwamba hili ni tatizo kubwa, kwani wanapozidi kuitangaza nchi yetu kuwa masikini, tena masikini sana, huoni kwamba mafanikio yaliyofikiwa yanaonekana ni kidogo, kwani kama unavyojua, vyombo vya habari vya nchi za magharibi hupenda kukuza sana dhana hii kwamba Afrika ni bara masikini, wakati si kweli? Mhe. Waziri Mkuu, NINAKATAA nchi yangu Tanzania kuitwa MASIKINI! Hata kidogo, Mhe. Waziri Mkuu, Tanzania SIO masikini!

Mhe. Waziri Mkuu, kama watu hawa wangekuwa na “maisha bora”, wasingelazimika kuyakimbia makazi yao vijijini na kuhamia kwenye maeneo ya hifadhi ya barabara kuu, ambapo sio tu kwamba kuwapo kwao kwenye sehemu hizo kunahatarisha maisha yao, kwani wengi wao hugongwa na magari yanayoacha njia, wengi wao wakiwa usingizini usiku au hata mchana, lakini pia, sehemu hizo, kimsingi, hazina huduma muhimu za kijamii, kama vile maji, hospitali, shule na hata umeme!

Mifano hai ya magari makubwa, kama vile malori ya mizigo na mabasi kuacha njia na kuhamia pembezoni, kwenye eneo la hifadhi ya barabara kuu, na kisha kuzigonga nyumba zinazojengwa kwenye maeneo hayo, ambapo watu wengi hupoteza maisha, ni mingi sana. Mwaka 2010, mapema, kwenye eneo la Michungwani, lori moja la mizigo liliacha njia, mchana kweupe, na kuiparamia nyumba iliyojengwa kwenye enel la hifadhi ya barabara kuu, ambapo ilikuwa takriban saa saba mchana, ndani ya nyumba hiyo, wakazi wake walikuwa wakipata chakula cha mchana. Inasadikika takriban watu watatu walipoteza maisha yao, lakini cha ajabu na kusikitisha ni kwamba, wananchi, badala ya kutambua kwamba tukio hilo lilikuwa ni ajali na bahati mbaya, na kimsingi, kama nyumba hiyo isingejengwa kwenye eneo hilo, pasingetokea maafa yeyote, wananchi hao waliamua kuchukua sheria mikononi mwao na kuifunga barabara, huku wakisambaza kila aina ya miti, mawe, na kadhalika, barabarani, na kufanya kila aina ya fujo. Magari mengi madogo yalipasuliwa vioo vyake yalipojaribu kupita pembezoni hapo, huku waliokuwamo ndani wakijeruhiwa kwa kukatwa na chupa, na mabasi mengi ya abiria yalilazimika kusubiri zaidi ya saa tano, hadi askari polisi kutoka Polisi Mkoa Tanga walipofika eneo hilo kwenda kuwatuliza wananchi hao waliopandwa na hasira. Mhe. Waziri Mkuu, unajua kilichojiri baada ya tukio hilo? Hebu tembelea eneo hilo ghafla, ujionee mwenyewe. Kwanza, pamewekwa matuta – yale ya migongo mingi mikubwa – kwenye pande zote mbili za barabara, lakini, pili, nyumba ziko vile vile, hata zile zilizopo kwenye eneo la hifadhi ya barabara kuu, na nyingine mbili au tatu, mpya, zimejengwa!


ELIMU, AFYA, MIUNDOMBINU, MAWASILIANO, MAZINGIRA: Mhe. Waziri Mkuu, mengi yamesemwa kuhusu haya, kwa hiyo ninaona nisipoteze muda wangu na wako, kwani nitakuwa ninatia chumvi, nami sikukusudia kufanya hilo.


Mhe. Waziri Mkuu, Tanzania ya leo ni nchi ambayo inakimbiwa na vijana wake, wengi wao wakiwa wasomi, ambao wanaamini kwamba wanaweza kuwa na maisha bora zaidi wakiwa nje ya nchi yao, ama barani Ulaya au Marekani, kuliko “kusotea maisha magumu” hapa nchini. Wengi wa hawa ni vijana waliohitimu vyuo vikuu, au ambao wamehitimu Kidato cha Sita, na kujikuta hawana matumaini yoyote yale ya maisha, kwani wanajikuta katika mazingira magumu pindi wanapojaribu kutafuta ajira.

Mazingira ya kupata ajira ya uhakika, bila ya kuwa na mtu wa “kukushika mkono”, kwa sasa hapa nchini ni magumu sana. Nafasi zote “nzuri” za ajira hutwaliwa na vijana wanaotoka kwenye familia “za wakubwa”, na nyingine hutwaliwa na wageni kutoka Ulaya au hata nchi jirani. Hakuna “uzalendo” kwenye soko la ajira. Mhe. Waziri Mkuu, vijana wasomi wamekimbia nchi yao, wameona ni bora kuishi hata kwa kufanya kazi hotelini, kufagia vyoo, kulea vikongwe, na ajira nyingine ambazo wenyeji wa huko Ulaya na Marekani wanaona ni za “kudhalilisha”, lakini vijana wetu hawa – mimi nawaita wakimbizi wa kiuchumi – wana malengo yao. Wanajua kwamba “watasota” kwa miaka kadhaa, lakini baadaye “wataibuka” baada ya kujiendeleza kielimu na kupata ajira nzuri zaidi, nafasi ambayo wanaona hawataipata hapa nchini, kwani kwa wenzetu, huhitaji kupata “Godfather” au “Godmother” wa kukushika mkono na kukupeleka kwenye ofisi nyeti, ama Serikalini au kwenye sekta binafsi. Kwenye soko la ajira la Ulaya na Marekani, “kinachoongea” ni elimu yako!

Mhe. Waziri Mkuu, Serikali ya CCM hivi leo imekosa sifa zake nzuri mbele ya Watanzania walio wengi. Ukweli – ambao CCM haitaki kuusikia – ni kwamba, CCM “haiuziki” kwa Watanzania; wamekosa imani nayo, pia, wamekosa imani kwa viongozi wake.

Ndani ya Chama Cha Mapinduzi kuna matabaka mawili – watawala na watawaliwa. Kuna viongozi wa ngazi za juu – makada – ambao wanaona kwamba wao peke yao ndio wenye haki ya kupata nafasi hizo, pindi wanapoondoka wanawarithisha watoto wao nafasi hizo. Utata mkubwa uliojitokeza hivi karibuni ni ushahidi kamili juu ya hili!

Mifano hai ipo mingi sana; January Makamba, mtoto wa Katibu Mkuu wa CCM, Mhe. Luteni Kanali Mstaafu Yussuf Makamba, alitangaza nia ya kugombea Ubunge kwenye Jimbo mojawapo mkoani Tanga, aligombea, na alishinda uchaguzi huo, hivi sasa ni Mbunge, kama sikosei, jimbo ni Bumbuli.

Ridhwani Kikwete, mtoto wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, ni Kamanda wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) kupitia CCM Wilaya ya Bagamoyo, huku kukiwa na tetesi kwamba huenda atatangaza nia ya kugombea nafasi mojawapo ya uongozi kupitia kura za wananchi, hapo baadaye.

Victor Kinjekitile Ngombale Mwiru, mtoto wa kada maarufu na mwenye nguvu, Mhe. Ngombale Mwiru, tayari ni Kamanda wa UVCC, Kata ya Kijitonyama, na kuna tetesi kwamba atatangaza nia ya kugombea mojawapo ya nafasi za uongozi kupitia kura za wananchi, hapo baadaye.

Mwisho, lakini si mwisho kwa umuhimu, kwamba Kippi Warioba, mtoto wa Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Jaji Lusinde Warioba, aliyekuwa Diwani wa Kata ya Mikocheni, Wilaya ya Kinondoni, aligombea nafasi ya Ubunge kwenye Jimbo la Uchaguzi la Kawe, Wilaya ya Kinondoni. Hata hivyo, hakuweka wazi uamuzi wake huo mapema kutokana na kuhofia “mbinu” zake za ushindi kubainika mapema, kwani inadaiwa kwamba Jimbo la Uchaguzi la Kawe ni mojawapo ya majimbo “magumu” kwa wanachama wa CCM na pia kwa wale wa vyama vya upinzani. Kwa bahati mbaya kwake, hakusinda uchaguzi huo kutokana na madai ya kuwapo kwa ufisadi wakati wa zoezi la kura za maoni kuwapata wagombea wa CCM; wananchi, wakazi wa Jimbo la Kawe, wana-CCM, waliomtaka Kippi Warioba awe mgombea wao, walisikika wakidai kwa nguvu zao zote kwamba wanamtaka Kippi (licha ya kwamba ni mtoto wa mkubwa, labda pengine ukweli ni kwamba aliwajibika ipasavyo wakati alipokuwa diwani wa Kata ya Mikocheni…), na walidai kwamba, iwapo Kippi Warioba hatachaguliwa na kupitishwa kuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Kawe, basi, kura zao zingehamia kwenye upinzani, hususan, CHADEMA. Hicho ndicho kilichotokea… Mhe. Halima Mdee hivi sasa ndiye Mbunge wa Jimbo la Uchaguzi la Kawe, kupitia CHADEMA.

Mhe. Waziri Mkuu, waliotajwa hapo juu, wote ni watoto wa viongozi – makada – wa ngazi za juu za uongozi kwenye Chama Cha Mapinduzi. Hawa ndio “warithi” wa himaya zao; usultani kupitia dhana ya demokrasia, ndani ya Chama Cha Mapinduzi.

Mhe. Waziri Mkuu, wanachama wengine, kama vile dada yangu Shy-Rose Bhanji, Naibu Kamanda wa UVCCM, Kata ya Kijitonyama, ambaye ni msomi aliyebobea kwenye fani ya uandishi wa habari, na dada yangu Jane Mihanji, ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), ambaye naye pia ni msomi aliyebobea kwenye fani ya uandishi wa habari, ni mojawapo ya viongozi mahiri wanaotarajiwa kushika nafasi mbali mbali za kuwaongoza wananchi wa Tanzania, na hawa ni wale wenye “wito halisi”, ambao hawana “Godfather” au “Godmother” kwenye CCM wa kuwarithisha nafasi zao. Hawa wana wito, ni tarajio la wanachama “wa tabaka la chini” ndani ya CCM. Hakika bado wana nafasi kubwa za kushika wadhifa huo kutokana na ukweli kwamba WANASTAHILI! Haitarajiwi kwamba watahamia kwenye chama kingine zaidi ya CCM, lakini, Mhe. Waziri Mkuu, napenda kutoa angalizo, ambalo ni kama ifuatavyo: Shy-Rose Bhanji na Jane Mihanji ni mfano tu wa viongozi bora vijana waliopo ndani ya CCM, lakini, Mhe. Waziri Mkuu, Chama Cha Mapinduzi kisiwachoshe vijana kama hawa wenye nia, ari na nguvu ya kutaka kuongoza ndani ya CCM, kwani, nao pia wanastahili kupata nafasi hiyo kutokana na ukweli kwamba, mosi, wameitumikia kwa dhati CCM kwa muda mrefu, na pili, kama wawakilishi wa wananchi wa “tabaka la chini”, wasikatishwe tamaa na hatimaye kuihama CCM, na wanapohama, hakika, wale wote wanaowasikiliza watahama pamoja nao. CCM itabaki yatima. Hicho ndicho mnachokitaka?

Mhe. Waziri Mkuu, ninaandika ninachokiona, kilichopo. Kama kuna anayebisha kwamba ndani ya CCM hakuna matabaka, namwomba anipe ushahidi wake, wa kina. Tusidanganyane, hata kwenye CCM hakuna demokrasia ya kweli.

Mhe. Waziri Mkuu, umewataka wanachama wa vyama vya upinzani kuwa wakweli kuhusu kile kilichofanywa na Serikali ya CCM, kuanzia Tanganyika ilipopata Uhuru mwaka 1961 hadi sasa.

Kama ni Uhuru wa bendera na sarafu, kweli, hivyo vipo. Lakini hadi leo, bajeti bado inategemea – kwa kiwango kikubwa – misaada kutoka kwa “wajomba” wafadhili wa nje. Hivi sasa, “wajomba” hao wameanza kutuchoka. Hatuna vyanzo mbadala vya mapato, na kila tunaposhauriwa, tunafanya kinyume na ushauri huo. Tunawaachia wageni waigeuze nchi yetu kuwa “Shamba la Bibi”; kwenye sekta ya madini, tunaambulia asilimi tatu tu ya mrahaba! Pale ambapo kuna wachimbaji wadogo wadogo, anapokuja mwekezaji “mwenye nguvu ya pesa”, wachimbaji hao wanakiona “kiama” kabla ya siku zao.

Vyombo vya dola – dola yao wenyewe – ndivyo hutumika kuwachomea nyumba zao, kuwapiga risasi, kuwasweka rumande, ili mradi wachoke na wahame sehemu hizo pasi na kulipwa fidia stahiki! Kwenye sekta ya uvuvi, “wawekezaji” hao wanatoroka na mamia ya tani ya shehena za samaki wa bei mbaya – jodari na kadhalika – ambao wanawauza huko kwao na kujipatia faida lukuki! Wananchi wanakamuliwa “damu” kwenye soda, vileo, sigara na kodi za magari! Migogoro ya ardhi haikomi – rejea makala ya kaka yangu, “Kamanda” Manyerere Jackton, kuhusu ufisadi wa “mavuvuzela” wa Wizara ya Ardhi, huko Kwembe Kati, Wilaya ya Kinondoni, Mkoa wa Dar es Salaam, toleo la “Mtanzania”, Juni 20, 2010! Najua uliisoma, lakini, leo, naomba uirejee.

Wanakijiji wanakimbilia mijini; shule hazina walimu, zahanati hazina madaktari wala wauguzi, mashamba hayalimwi kutokana na kukosekana miundombinu ya umwagiliaji, misitu inafyekwa – tena na wahamiaji haramu – wanaofanya biashara haramu ya uchomaji mkaa, masoko yanakimbiwa na wakulima na wachuuzi kutokana na Watendaji wa Kata kutoza ushuru mkubwa kuliko mapato yao! Mhe. Waziri Mkuu, nina hakika umeshapata habari za ufisadi kwenye vocha za pembejeo za kilimo!

Sasa ni kipi Serikali ya CCM inachojivunia kwa madai imewaletea Watanzania “maendeleo” kwenye nchi yao? Ni maendeleo gani hayo ambapo asilimia themanini (80%) ya raia waliopo mahabusu na gerezani ni wanyonge, wasio na hatia, waliobambikiwa kesi na maafande, kwa kukosa ‘vijisenti’ vya kuwahonga ili wawarudishie uhuru wao, baada ya maafande hao waliotupa jalalani viapo vyao vya “kuwalinda raia na mali zao”?

Ni maendeleo gani hayo ambapo wafanyabiashara wadogo wadogo wanabambikiwa viwango vikubwa vya kodi na maofisa wabadhirifu wa TRA, huku wafanyabiashara wakubwa, tena wa nchi za kigeni, ama wanatorosha rasilmali zetu nje ya nchi bila kulipia kodi (k.m. nyara mbali mbali, vito vya madini, n.k.) na wengine wanaingiza makontena yaliyosheheni bidhaa mbali mbali, na wengine wanaingiza magari bila kulipia kodi?

Ni maendeleo gani ambapo raia asiye na hatia anapigwa na “watu wenye hasira” mpaka anazimia, na hapo ndipo unapokuwa mwisho wa uhai wake kwani huishia kuchomwa moto, mara nyingi askari polisi wakichekelea kwamba “kibaka sugu” amekomeshwa? Kuna ushahidi wowote kwamba anayeuwawa – tena kwa tuhuma tu, za wizi wa kuku, simu za mkononi, mikoba ya akinamama, n.k. – anastahili adhabu hiyo kubwa? I wapi haki yake ya kuishi, kama ilivyoainishwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania? Iweje leo, “wananchi wenye hasira” wakiuke katiba kwa kuutoa uhai wa mtu ambaye, mosi, hajakamatwa na kufikishwa polisi, na pili, hajashtakiwa kwa tuhuma zinazomkabili kama ilivyoainishwa kisheria, iki afikishwe mahakamani kujibu tuhuma hizo kwenye mwendendo halali wa kesi inayoendeshwa kisheria?
Ni maendeleo gani ambapo leo, wastani wa bei ya mafuta ya petroli ni Shilingi Elfu Mbili na Ushee kwa lita, na dizeli haiko mbali sana na bei hiyo, huku kilo moja ya nyama ya ngombe ikiwa wastani wa Shilingi Elfu TANO?! Ni maendeleo gani hayo unayoyadai yameletwa na CCM huku leo kilo moja ya maharage ni wastani wa Shilingi Elfu Mbili, huku kilo moja ya sukari ni Shilingi Elfu MBILI, kilo moja ya mchele ni Shilingi Elfu Moja na Mia Tano, na chumvi ni Shilingi Mia Tatu kwa paketi ndogo zisizofika hata robo kilo? Kuku mzima, ukienda sokoni – yule wa kisasa – utamnunua sio chini ya Shilingi Elfu Saba, na yule wa kienyeji ni Shilingi Elfu Kumi! Bado unadai Serikali ya CCM IMELETA MAENDELEO? Maendeleo gani wakati hali ya kimaisha inazidi kuwa mbaya, nauli za daladala sasa ni Shilingi Mia Tatu kwa kila safari isiyozidi kilometa hamsini, unataka kusema hawa wananchi, wanaosafiri takriban siku 25 kwa wiki, watapata wapi Shilingi Mia Sita kwa siku, kwa nauli ya kwenda na kurudi “vibaruani” – sio kazini, kwani kazi ni ajira, yenye mshahara unaoeleweka, na pensheni pia wanalipwa, lakini hadi leo, tunafikia miaka 50 ya “uhuru”, watu wanatumikishwa kama watumwa kwenye viwanda, ilhali wanalipwa kwa ujira wa siku moja… nikikutajia ni kiasi gani utasema ninatania, hivi, Mhe. Waziri Mkuu, ni mtu gani leo ataweza kuishi kwa ujira wa Shilingi Elfu Mbili kwa siku? Baada ya kuzitaja gharama zote hapo juu, za mahitaji MUHIMU ya maisha ya binadam – sijataja gharama za kununua vocha za simu, kwani hizo, kwa wengi, bado ni anasa – zikiwa zimepanda maradufu, kwa muda mchache wa miaka kumi tu?

Mhe. Waziri Mkuu, mimi na wenzangu wengi, bado hatujayaona maendeleo hayo yanayozungumziwa. Ni afadhali miaka ya 1970, ambapo Tanzania ilikuwa mbele kwa maendeleo MARA ISHIRINI kuliko sasa! Lakini kitendo chako cha kusimama leo, na kusema Serikali ya CCM imeleta maendeleo, ni kutowatendea haki Watanzania. Tuombe radhi! Tuombe radhi upesi!

Mwaka 2011, Tanzania inatimiza miaka hamsini ya uhuru. Mimi natamka rasmi kwamba, mwaka 2011, Chama Cha Mapinduzi kinaadhimisha miaka hamsini ya kuujenga na kuuimarisha umaskini nchini Tanzania!

Mungu Ibariki Tanzania!


Mwandishi wa makala haya ni mchumi, mchambuzi wa masuala ya kijamii na kisiasa, ni mjasiriamali na pia mwanataaluma kwenye teknolojia ya habari na mawasiliano. Anapatikana kupitia ujumbe binafsi ndani ya JF.
 

politiki

JF-Expert Member
Sep 2, 2010
2,376
1,250
Good analysis mwana haki,
NINGEPENDA NIONGEZEE HAPO FACTS MBILI NDANI YA MIAKA HAMSINI YA UHURU WA NCHI YETU.
BAADA YA MIAKA HAMSINI YA UHURU NI ASILIMIA 14% YA WATANZANIA WOTE NDIO WANA UMEME TENA USIO WA UHAKIKA.
NI ASILIMIA 12% YA WATANZANIA WOTE WENYE KUPATA MAJI YA KUNYWA YA BOMBANI . HIZI NI FACTS NA SIYO NGONJERA ZAKE
ALIZOZITOA BUNGENI. HUWEZI KUZUNGUMZIA MAENDELEO BILA KUZUNGUMZIA HAYA MAENEO MAWILI KWA MAANA NI MUHIMU SANA
KWENYE NCHI YEYOTE ILE DUNIANI.
 

Gad ONEYA

JF-Expert Member
Oct 26, 2010
2,633
1,195
Sishangai hata akilaumu wanaokosoa chama na serikali, mtu mwenyewe hajui kwa nini wananchi ni maskini wakati takwimu alizopewa mezani kwake zinaonysha uchumi wa nchi unakuwa!
 

GJ Mwanakatwe

JF-Expert Member
Mar 26, 2011
241
0
Unajua wakati mwingine mtu ukiwa madarakani unakuwa kama kipofu. Tunapozungumzia maendeleo ndani ya miaka hamsini ya uhuru kwamba hakuna haina maana kwamba hakuna kilichofanyika, la hasha, bali ina maanisha kwamba maendeleo yaliyopo ni madogo mno ukilinganisha na umri wa uhuru wa miaka hamsini.Hayo wanayoona kwamba ni maendeleo ilikuwa yawepo ndani ya miaka mitano ya uhuru yaani mwaka 66. Inakuwaje miaka hamsini ya uhuru nchi haina umeme wa uhakika na wa kutosha? haina maji safi ya kunywa,barabara hazina rami nk? Mbona Singapore walikuwa kama sisi wakati tunapata uhuru lakini leo wanamaendeleo makubwa wakati hawana resources hata moja ?
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom