Barua ya Kichungaji Kutoka kwa Askofu Renatus Nkwande Kuhusu Maandalizi ya Sinodi ya 16 ya Maaskofu Katoliki itakayohitimishwa Roma 2023

Mama Amon

JF-Expert Member
Mar 30, 2018
2,021
2,478
1640184714140.png

A
skofu Mkuu Renatus Leonard Nkwande, wa Jimbo Kuu la Mwanza, nchini Tanzania

Usuli

Ifuatayo ni Barua ya Kichungaji kuhusu Maadhimisho ya Sinodi ya 16 ya Maaskofu Katoliki.

Sinodi hii, inanogeshwa na kauli mbiu isemayo, “Kwa ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.”

Maadhimisho ya Sinodi yameanza kwa kuwashirikisha waumini walei katika ngazi ya Jumuiya Ndogo Ndogo kwenye Makanisa mahalia duniani kote.

Tayari kuna dodoso limeandaliwa na linaendelea kujibiwa na waumini kupitia Jumuiya Ndogo Ndogo.

Askofu Mkuu Renatus Leonard Nkwande, wa Jimbo Kuu la Mwanza, nchini Tanzania, anaitaja Sinodi kama nyenzo ya kuwawezesha waumini kujitambua kama familia ya Mungu inayojali na kuwajibika, kujadiliana na kushiriki katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani. Endelea kujisomea....

Maudhui ya Barua

Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu yananogeshwa na kauli mbiu: “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Maadhimisho haya yamegawanyika katika awamu kuu tatu kuanzia Mwezi Oktoba 2021 hadi Oktoba 2023.

Awamu ya kwanza ni kwa ajili ya Makanisa mahalia pamoja na taasisi zote zinazoendeshwa na kusimamiwa na Kanisa Katoliki ni kuanzia tarehe 10 Mwezi Oktoba 2021 hadi tarehe 15 Agosti 2022.

Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande, wa Jimbo kuu la Mwanza ameandika Barua ya Kichungaji kuhusu maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu katika Ngazi ya Kijimbo inayoongozwa na kauli mbiu “Mimi ni njia, na ukweli na uhai” (Yohane 14:6).

Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande anagusia maadhimisho ya Sinodi ya Kwanza ya Jimbo Kuu la Mwanza ambayo imewawezesha kujitambua kama familia ya Mungu inayojali na kuwajibika; inayojikusanya pamoja, “Shikome” ili kujadiliana katika ukweli na uwazi, tayari kushiriki katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu kwa kujikita katika uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Sinodi ni Kipindi cha kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikilizana, lakini zaidi kusikiliza Neno la Mungu na Roho Mtakatifu ambaye ndiye mtendaji mkuu wa maadhimisho ya Sinodi.

Askofu mkuu Nkwande amemteua Padre Gregory Kiloma awe mratibu mkuu wa shughuli zote za adhimisho hili katika ngazi ya Kijimbo kwa kumkabidhi Biblia na Mshumaa wenye mwanga ili Kristo Yesu ambaye ni njia, na ukweli na uhai aongoze shughuli yote hii!

Wapendwa Waamini Walei, Watawa, Mapadre na wote wenye mapenzi mema. Tumsifu Yesu Kristo! “Mimi ni njia, na ukweli na uhai” (Yohane 14:16).

Napenda nichukue nafasi hii kuwafikishia ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kuwa Kanisa zima linaalikwa kutembea pamoja na hivyo lifanye Sinodi kiulimwengu kuanzia tarehe 10 Oktoba 2021, siku ambayo yeye alifanya uzinduzi rasmi kwa ngazi ya kijimbo. Hitimisho la Sinodi hii linatarajiwa kuwa Oktoba 2023.

Nia ya Baba Mtakatifu ni kulitaka Kanisa lote kufanya tafakari ya kina zaidi juu ya tabia yake halisi ya kisinodi inayotokana na mwaliko na maisha ya ubatizo.

Kwa njia ya ubatizo tunafanyika wafuasi katika Kristo aliyejifunua kwetu akisema: “Mimi ni njia, na ukweli na uhai” (Yohane14:16).

Kwa hiyo, sinodi kimsingi ni mwaliko wa kutembea pamoja katika Imani tukiuendea utakatifu na ukamilifu.

Ukristo ni maisha ya ufuasi, yaani kutembea pamoja katika njia, ambayo ni Kristo mwenyewe. Ni katika njia hii pia tunajifunza ukweli wa Mungu unaotufanya huru na kutupatia uzima wa milele.

Ni bahati njema kwamba tabia ya kisinodi si jambo geni kwa jimbo letu sasa. Miaka Ishirini (20) iliyopita, Askofu Mkuu wa Mwanza nyakati hizo, Mhashamu Anthony Petro Mayala, aliitisha Sinodi ya Kwanza ya Jimbo.

Nia yake ilikuwa ni kutualika waamini wote kutwaa tabia ya Kanisa ya kisinodi, na hivyo tutembee pamoja katika Imani tukiziendea changamoto za wakati ule na kuzikabili kwa kutengeneza mazingira mazuri ya kuishi maisha ya wito wetu wakikristo na kuinjilisha.

Bila shaka matunda ya Sinodi hiyo ya kwanza katika Jimbo letu tunayaona bayana. Pamoja na mambo mengine mengi, Sinodi Mwanza imetupatia fursa ya kuyafanya upya maisha yetu tukijitambua kama familia ya Mungu Baba na Mwana na Roho Mtakatifu inayojali na kuwajibika. Hii imekuwa njonzi na dira yetu.

Hata leo tunapoalikwa na Baba Mtakatifu kufanya Sinodi, ni lazima tuendelee “kujali na kuwajibika” kama wanafamilia wa Jimbo Kuu la Mwanza.

Tunaalikwa tujikusanye pamoja (Shikome) ili kufanya mazungumzano katika roho na tabia ya kisinodi.

Ni wakati unaompendeza Mungu (Kairos) kwamba tujadili mema na mahangaiko ya ulimwengu huu ili tuone ni kwa namna ipi Kanisa kama familia ya Mungu ni usharika mtakatifu unaomhusisha kila mbatizwa, na kwa kweli watu wote wenye mapenzi mema, katika kuiishi na kuitangaza habari njema ya wokovu.

Ni katika mwono huu Baba Mtakatifu Francisko amechagua mada hii: “For a Synodal Church: Communion, Participation and Mission.”

Anamaanisha kuwa kwa Kanisa la kisinodi: sote tuwe na umoja, ushiriki na utume kwa ajili ya sinodi ambayo tayari ameizindua hapo tarehe 10 Oktoba 2021.

Tunaalikwa kama Kanisa tusiwe watazamaji. Tuimarishe tabia yetu ya kujali na kuwajibika kwa kuwa washiriki wa ujenzi wa ufalme wa Mungu. Tufanye hivi tukiwa pamoja kama kanisa na kila mmoja ashiriki kwa uwezo na karama aliyopewa na Mungu kuieneza Injili kwa Mataifa yote.

Waamini, ni vyema tukatafakari kama kweli ule wito wa kumfuasa Kristo unaotutaka kuiishi na kuihubiri injili tumeutekeleza (tumeutimiza)! Wote wamekuwa wafuasi wa Kristo? Wangapi hawajawa? Wangapi wanaacha na kuondoka? Umefanya nini hapo ulipo ili kukabiliana na hali hii?

Tuzitafakari pia changamoto za leo ikiwa ni pamoja na: umaskini, ulegevu na utepetevu katika Imani, ukosefu wa maadili na mila potovu, magonjwa na uharibifu wa mazingira.

Kama familia, Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo (JNNK), Parokia na Jimbo tumefanya nini ili kuzikabili changamoto hizi?

Matendo ya kila mmoja wetu: Je, baba, mama, watoto na vijana, waamini na Wachungaji, tumekuwa kweli chumvi na mwanga katika jamii ya leo kama ubatizo unavyotutaka?

Yapo mengi tunayoweza kujiuliza na kwa “umoja wetu kama familia ya Mungu” tunaweza kuyatolea majibu.

Tumealikwa rasmi na Baba Mtakatifu kuianza rasmi hii safari ya kutembea pamoja katika Imani ngazi ya Jimbo tangu tarehe 17 Oktoba 2021. Hata hivyo sisi kama Jimbo tumejipangia tufungue tukio hili muhimu leo tarehe 07 Novemba 2021 hapa Kawekamo.

Kama mlivyotangaziwa na kusomewa barua yangu hii ya kichungaji maparokiani, nazidi kuwaalika Wachungaji Mapadre, Viongozi walei wote na waumini wote tuwe WASIKIVU ili Roho wa Mungu aongee nasi kupitia wenzetu.

Tusipuuze ushiriki wa yeyote. Kanisa hili ni letu sote na kila mmoja amepewa fursa na Mwenyezi ya kujenga. Tukubali na kupokea changamoto toka kwa wengine bila jaziba na bila kujenga chuki. Kanisa limejengwa litajengwa na wenye Moyo.

Nawakumbusha kuwa katika ngazi ya Jimbo, mchakato wa Sinodi ngazi ya Jimbo unaishia 15 Agosti 2022.

Hivyo muda wetu ni mfupi lazima tufanye kazi. Tujibu maswali toka katika dodoso la Roma kabla ya tarehe 20 Februari 2022.

Tarehe 25 Februari 2022 majibu na maoni yote toka kwa waumini yawe yameletwa ofisi ya Askofu Mkuu.

Taasisi zetu, mashule, seminari, chuo kikuu na vyuo vingine vifanye hivyo pia. Naagiza pia makundi mbali kama WAWATA, VIWAWA, UWAKA, Moyo Mtakatifu wa Yesu na vyama vyote vya kitume Kijimbo vijibu na kutoa maoni yao.

Namuomba Katibu Mtendaji wa Idara ya utume wa Walei afuatilie kwa karibu na kukusanya nyaraka zote zitakazopatikana na mazungumzano.

Kwa kuwa Askofu hawezi kufanya mambo yote yeye mwenyewe, ninamteua Padre Gregory Kiloma awe mratibu mkuu wa shughuli zote za adhimisho hili na ninamkalisha kwenye kigoda ishara ya kumkabidhi usimamizi wa mazungumzano haya kama ilivyokuwa ikifanyika enzi na enzi katika jadi ya wakazi wa Mwanza wakati mkuu wa kaya anapoongea na familia yake ‘hashikome’.

Aidha sisi kama Jumuiya ya waumini tunaouendea utakatifu kwa njia ya Kristo Bwana aliyefanyika Mwili kwa mazungumzano kati yake na Mungu Baba, ninamkabidhi Padre Gregory Kiloma, Biblia na mshumaa wenye mwanga ili Kristo ambaye ni njia, na ukweli na uhai” (Yohane 14:16) aongoze shughuli yote hii.

Nawatakia kila jema.

+Renatus Leonard Nkwande.


Askofu Mkuu wa Jimbo kuu la Mwanza.
 
Back
Top Bottom