Elections 2010 Barua kwa mjomba kuhusu uchaguzi

Anold

JF-Expert Member
Jul 15, 2010
1,456
612
Mjomba mpendwa salaam,

Mimatumaini yangu kuwa unaendelea vizuri wewe pamoja na wote hapo ulipo.

Dhumuni la barua hii ni kutoa pole kwako kutokana na mikikimikiki ya uchaguzi, kwakweli kilikuwa kipindi kigumu kwako pamoja na familia yako kutokana na ukweli kuwa muda wote ulikuwa kwenye kampeni, ukijitahidi kueleza yale mambo muhimu ambayo kama wapiga kura wangekuchagua ungeweza kuyafuatilia na kusaidia kubadilisha maisha ya wapiga kura wako ambao miaka nendarudi viongozi waliowahi kushika nafasi za uongozi hawakuweza kufanya cha ajabu kutokana na sababu mbalimbali ambazo nyingi wanazijua wao japo nakiri zipo za msingi.

Nilipatwa na mshangao mkubwa yalipotangazwa matokeo kuwa hukuambulia nafasi hii muhimu pamoja na ukweli kuwa ulikuwa unaungwa mkono na watu wengi, pamoja na ukweli kuwa sera zako zingesaidia sana maendeleo ya haraka katika eneo letu, kimsingi kitondi hicho mimi binafsi kiliniudhi na kunikatisha tamaa sana kiasi ambacho ilifikia mahali kidogo potelea mbali nivunje hata hiyo amani tuliyokuwa nayo muda mrefu. Pamoja na ukweli kuwa mimi nimeumia lakini naamini wewe ndiyo umeumia kwa kiasi kikubwa, na hii inatokana na ukweli kuwa kuna maeneo kadhaa ambayo nasikia kura zako zilikuwa zimempita mgombea mwenzako lakini kwa mshangao wakati wa kutangazwa matokeo yeye ndiye alikuwa na mshindi kwa kura za kishindo.
Mjomba mimi binafsi pamoja na rafiki zangu ambao tulikuwa tukikuunga mkono tumeumia sana pia tunakupa pole kwa matokeo haya ambayo naamini yemekuumiza sana na ninaimani unafikiria mengi ya kufanya ili kuhakikisha kuwa haki yako inapatikana.

Mjomba hivi najuzi nilisikia kuwa ili kuonyesha hisia zako kuhusiana na zoezi zima la uchaguzi lilivyoendeshwa, ulilazimika kususia hotuba iliyokuwa inatolewa na mkuu wa nchi, mjomba kwa hili siwezi kukulaumu kwani naamini kuwa katika medani za kisiasa hili linakubalika ila tatizo ni kwamba kutokana na uchanga na ugeni wa uelewa wa siasa, jambo hilo limetafsiriwa vibaya na nasikia umeeleweka vibaya sana kiasi kwamba sasa hivi kuna mpango unaandaliwa ili kukuadhibu kwa hatua ile uliyochukua kwani ilitafsiriwa kuwa ni aibu na ni dosari kwa nchi yetu ambayo haijawahi kupatwa na tukio kama lile.
Kimsingi na kwa maoni yangu nafikiri huna sababu ya kuadhibiwa maana ni haki yako kuonyesha hisia zako kwa njia ya kistarabu, naita njia ya kistarabu kwani kuna mwaka mmoja huko ulaya waziri mkuu aliwahi kupigwa na mayai viza na watu waliokuwa wakimpinga, naamini hiyo njia ya namna hiyo pamoja na nyingine zinazoweza kuhatarisha amani na umoja hizo mjomba kamwe hutazitumia.

Mjomba kwa kuwa uchaguzi umekwisha na mambo inavyoelekea yanaenda, nakushauri kwa sasa uelekeze nguvu zako kuhakikisha kuwa hii katiba iliyopo inafanyiwa marekebisho makubwa, nasema hivi kwakuwa inavyoelekea kama katiba hii haitarekebishwa nakuhakikishia mjomba hutakaa ushinde kwa nafasi uliyogombea labda ugombee nafasi nyingine na si hilo tu imebainika wazi kuwa katiba hii inamapungufu mengi na bila wewe kutia juhudi ili baadhi ya mambo na taratibu zibadilishwe au ziondolewe mjomba usahau kushinda.

Kabla sijasahau nimesikia kuwa unampango pia wa kuitisha maandamano ili kujaribu kuwaeleza wananchi kilichotokea kwa hili sina cha kushauri ila nataka nikuhakikishie kuwa wananchi wengi ni waelewa na wameshajua kila kitu kilichotokea kiasi kuwa wameamua kunyamaza na kutulia kuendelea na shughuli zao kwani watanzania waliowengi hawataki matatizo ndio maana hata haki zao huamua kizinunua Polisi au Mahakamani ili kurahisisha mambo, ni vigumu sana kukubaliana na hili lakini mjomba naomba ulipokee si kwa kutoa au kupokea chochote ila kwa kuelekeza nguvu zako katika kushinikiza mabadiliko ya sheria mbalimbali kandamizi.

Mjomba ni bahati mbaya sana kuwa hukuwepo wakati mkuu wa chi anahutubia Bunge, ila kuna neno ambalo mtoa hotuba alilisema ambalo mimi binafsi sikubaliani nalo kuwa kuna mpasuko wa kidini katika nchi hii, kwa kweli sidhani kuwa nchi yetu tumefikia huko, ni bahati mbaya sana kuwa hata vijana wako walisusia hotuba hiyo kiasi ambacho wakati wa kujadili hotuba hiyo hawataweza kuomba mwongozo wa spika ili dini hiyo ibainishwe waziwazi. Mimi nimeshangaa sana maana mimi binafsi nilimchaguwa kiongozi ambaye sio wa dini yangu sasa ungekuwepo kwenye mjadala huo ungesaidia sana kushinikiza itajwe hiyo dini inayosemekana kuwa inachochea mgawanyiko ili tuisute hadharani,
Mjomba miezi kadhaa ijayo kutakuwa na vikao vya bunge najua fika kuwa wewe hutakuwepo, ila vijana wako tunawategemea sana wajenge hoja zenye kupeleka taifa hili mbele, tumechelewa sana kupiga hatua za kimaendeleo kutokana na sababu ambazo nyingi hazina msingi kwa hali hii mjomba uwaambie kabisa hao rafiki zako watakaokuwakilisha na kuwakilishwa wapiga kura wao kuwa nchi yetu kwa sasa haina muda wa kupoteza hivyo yote yafanyike ila hili la kutatua kero mbalimbali liwe la msingi na lipewe kipaumbele.

Kuna tetesi mjomba kuwa kuna mkakati unapangwa ili kuendea meza ya maridhiano ili umtambue raisi aliye madarakani, naamini utatumia busara zako kulimaliza hili, ila mjomba kuna kitu muhimu ambacho lazima ukielewe kuwa chama chako kipindi hiki kipo peke yake maana wenzako mliokuwa pamoja walikwenda kwenye vikao kama hivyo kilichotokea ni kuunda muafaka wa mashaka mpaka sasa hivi pamoja na kupongezwa sana lakini wao sio chama cha upinzani hivyo hawawezi kukosoa serikali hivyo ujue wazi kuwa sasa hivi wewe mjomba na chama chako ndiyo tegemeo, sasa pamoja na maridhiano au muafaka ila lazima utambue nafasi yako ili watanzania wasije wakakushangaa kama wenzako tunavyowashangaa. Sasa mjomba kama utaitwa wewe nenda tena mpende tu mgombea mwenzako aliyeshinda maana tatizo sio yeye ni mfumo uliopo hivyo mjulishe wazi kuwa huna ubaya naye bali mfumo uliopo haufai kwa sasa, naamini kwa uungwana wake atakuelewa tu mjomba.

Ninamengi sana ya kukueleza mjomba ila kwa leo ngoja niishie hapa, ni salimie sana shangazi na wote wenye nia njema katika taifa hili. Nimatumaini yangu kuwa barua hii utaipata na utaifanyia kazi.
Samahani sana nimeandika kwa haraka kiasi ambacho kuna vimakosamakosa ila naamini utaielewa.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Similar Discussions

0 Reactions
Reply
Top Bottom