Baraza letu la wawakilishi - Zanzibar

CoolGuy

New Member
Jun 7, 2011
2
0
Utangulizi

Mimi mwandishi wa warka huu ni mshabiki wa siasa za Zanzibar ambako nimezaliwa, nimekulia, na naishi. Nimeamua kutoa maoni yangu mapema ili kuepuka wengine kuja kutukosoa na kuwapa mwanya wa kutudhihaki kwa jambo husika ninalotaka kulitolea indhari.

Nikiri kuwa kwa muda mrefu nimekuwa nikitaka kuandika kuhusu jambo hili, ila huwa najizuia kwa kuhofia kusibiwa na mambo kadhaa yasiyofaa, kama vile kuambiwa ‘ya siasa waachie wana siasa’, au kifikiriwa kuwa nakosoa kwa niaba ya Wapinzani kwa vile hawamo kwenye Baraza, na hatimaye kupachikwa nembo ya Upinzani, n.k.

Warka huu unazungumzia mambo mawili ambayo nahisi yakirekebishwa yatanyanyua zaidi hadhi ya Baraza, nayo ni:

(1) Khulka na Muonekano wa Wawakilishi kwenye Baraza
(2) Utendaji wa kiufundi kwa vipindi vya televesheni vya Baraza la Wawakilishi

Khulka na Muonekano wa Wawakilishi kwenye Baraza

Kinachokwaza ni khulka wanazoonesha baadhi ya Wawakilishi wetu wakiwa kwenye Vikao vya Baraza, ambavyo hurushwa mubashara au vinginevyo na vyombo vyetu vya habari, hasa Televesheni. Kwa bahati nzuri, matangazo hayo yanasambaa kote duniani kutokana na kuimarika kwa uwezo wa vyombo hivyo.

Binafsi nahisi Waheshimiwa Wawakilishi wetu wanapaswa kuepuka baadhi ya mambo ili kutoa picha kuwa ni Wawakilishi makini wa Baraza makini, kuwa wao ni watu wazima waliojikita kiukweli (wapo serious) katika kutekeleza wajibu wao. Mambo hayo ni:

Kufanyiana dhihaka zilizokithiri

Kuitana majina ya masikhara na utani, ambayo yanaleta picha ya “utoto” kwenye chombo kinachotakiwa kuonekana ni makini na kimepevuka.

Kadhalika kupeana vyeo wasivyokuwa navyo, kama vile “Profesa” n.k. au Mwakilishi kutoa kauli Barazani kuwa Waziri Fulani ni dada yake, kwakuwa tu majina ya wazee wao yamefanana, ilhali si kweli. Hali hii hupelelekea wananchi wa kawaida kuamini kuwa wahusika wana sifa hizo, huku sisi tuwajuao tukikirihishwa na dhihaka zilizokithiri.

Naamini kuwa mambo hayo yakiepukwa, Wazanzibari wengi watavutiwa zaidi na kutizama Baraza lao la Wawakilishi, hata kama Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nalo litakuwapo mtandaoni wakati huo.

Utendaji wa kiufundi kwa vipindi vya Baraza la Wawakilishi

Hili nalo lina sura tatu, lakini kubwa linahusiana na mkanganyiko baina ya mtangazaji wa televesheni na timu ya urushaji matangazo inayokuwa ndani ya Baraza la Wawakilishi.

Adha hutokea pale mtangazaji anapokariri neno kwa neno, suali la Mwakilishi linalotaka kujibiwa wakati huo, huku mchakato wa kulijibu ukiendelea sawia ndani ya Baraza. Sauti kutoka vyanzo viwili hivyo huchanganyika na kutufanya sisi wasikilizaji kutokuelewa nini kinasemwa.

Tatizo hili halijitokezi kwenye Bunge la Muungano, hivyo nashauri Zanzibar Broadcasting Corporation (ZBC) kuutizama na ikiwezekana kuiga utaratibu wa Tanzania Broadcasting Corporation (TBC), ili kuondoa kero hii.

Jengine katika sehemu ya ufundi ni pale sauti inaposita kusikika kabisa kwa zaidi ya nusu saa huku kipindi kikiendelea, au picha kuondoka kabisa na tukawachwa tukitizama kioo cheusi kwa muda kama huo. Huwa najiuliza iwapo mafundi mitambo hawana njia, kifaa au namna yoyote inayoweza kubainisha kasoro hiyo?

La mwisho katika matatizo ya ufundi ni kipindi kukatika ghafla bila ya taarifa, watizamaji tukawekewa nyimbo au kasida kwa muda mrefu, na baadae kipindi husika kikarejeshwa kikiwa kimeshaendelea na kufikia mbali, na hayo yote yanafanyika bila watizamaji kujulishwa au kuombwa radhi baada ya kutokea.

Hitimisho
Natamani Warka huu uchukuliwe kuwa ni uamsho kwa wahusika waliopo na wajao (wake up call), na si lawama kwa wahusika waliopo. Waheshimiwa Wawakilishi wetu wakumbuke kuwa hakuna binaadam mkamilifu, na kuwa akukosoaye anakupenda maana anaamini kuwa unastahiki na una uwezo wa kujirekebisha ili uwe mbora zaidi ya ulivyo sasa.

Kwa upande wa changamoto za kiufundi, nataraji kuwa wahusika watachukua jitihada za kuondoa kero husika, ili wao, vyombo vyetu vya habari na Baraza letu la Wawakilishi lipige hatua zaidi na kuwa mfano wa kuigwa na wengine.
 
Back
Top Bottom