Tetesi: Baraza la Ulamaa lilimpa masharti Mufti Mkuu, Amuondoe Alhad Mussa, Aondoke yeye au Waondoke wote wawili

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,373
8,108
Baada ya kutafutwa Sheikh Alhad na kumweleza tuhuma mbalimbali zilizoelekezwa kwake, ikiwemo kupendelewa na Mufti Zubeir kutokana na ukaribu wao wa kifamilia, kuingilia majukumu ya Baraza la Ulamaa ambapo alisema leo atalitolea ufafanuzi jambo lake.

“Leo nitazungumza pale Karimejee hall, karibu sana upate elimu ya mambo haya,” alisema.

Jitihada za Mwananchi kumpata Mufti Zubeir kujibu tuhuma zinazoelekezwa kwake za kumpendelea Sheikh Alhad ziligonga mwamba.

Aidha, taarifa ambazo gazeti hili limezipata ni kwamba, baadhi ya mambo yanayotajwa dhidi yake ni vita ya umufti ndani ya baraza hilo ambapo baadhi ya viongozi walishamuona Sheikh Alhad ana nguvu kubwa na ushawishi kwenye jamii.

“Hili la Sheikh Alhad kuwa na nguvu kubwa na kukubalika mbele za watu na makundi mbalimbali kuna baadhi ya viongozi ndani ya Bakwata walikuwa hawalipendi na walimuona amekuwa maarufu hata kuliko wao na masheikh wengine.

“Lakini walisahau uchapakazi wake na ubunifu katika kufanya shughuli za kidini na kuwatumikia Waislamu ndizo zimemfikisha hapo, sasa badala waige mazuri yake, wamekaa kumtengenezea fitna, majungu na kuhakikisha wanamundoa katika nafasi hiyo,” kilisema chanzo hicho.

Mwingine alibainisha ukaribu wa kifamilia kati ya Mufti Zubeir, ulimfanya aogopeke na hata tuhuma zilizokuwa zikielekezwa kwake hazikufanyiwa kazi.

“Kilichofanyika sasa ni kutumia nafasi ya mgogoro wa ndoa ya Dk Mwaka kumshughulikia kwa kuwa huko nyuma hawakuwa na sababu wala vithibitisho ambavyo wangeweza kumuengua katika nafasi hiyo,” kiliendelea kueleza chanzo chetu

“Ni kutokana na ukaribu huo wa Sheikh Alhad na Mufti wa kifamilia, Baraza la Ulamaa katika sakata hilo lilimpa masharti matatu.

“Masharti hayo moja aamue kumuondoa Sheikh Alhad, aondoke yeye au wawaondoe wote,” kilieleza chanzo chetu

Kwa taratibu, Baraza la Ulamaa lina uwezo wa kumwondoa Mufti.

Sababu nyingine inayotajwa kuwa nyuma ya pazia ya sakata hili ni Masheikh wa Baraza la Habari la Kiislamu Tanzania (Bahakita), siku moja baada ya Baraza la Ulamaa kutangaza kubatilisha uamuzi wa Sheikh Alhad na kamati yake wa kuvunja ndoa ya Dk Mwaka, wao walijitokeza kumtetea Sheikh huyo, jambo lililotafsiriwa kuwa huenda ni mkakati ulioratibiwa kwa lengo la kulishambulia baraza hilo na kumkinga yeye (Alhad).

Hata hivyo, pia kitendo cha Sheikh Alhad kuzungumzia sakata hilo kwa nyakati tofauti wakati Baraza la Ulamaa likiwa linashughulikia mgogoro huo ambapo akiwa Chanika alilalamika kuiona barua ya baraza hilo kumuonya kupitia mitandao huku mwenyewe ikiwa haijamfikia.

Barua hiyo, ilimuonya Sheikh Alhad kutoligeuza Baraza la Masheikh ambapo yeye ndiyo mwenyekiti wake kuwa mahakama ya Kadhi.

Akilalamikia hilo, Sheikh Alhad alisema

“nasikitika barua hiyo sikuipata na hivyo kulazimika kupita katika mapito hayohayo iliyopitia huko mitandaoni.

“Kwani mimi kama Sheikh wa mkoa ukiacha na vyeo vyangu vingine, nina nguvu zangu na nina heshima yangu kubwa na siamini kama Baraza la Ulamaa linaweza kunionya katika sura ile.

“Badala yake naweza kuonywa na Mufti ambaye ndiye Mwenyekiti wa Baraza la Maulamaa, lakini siwezi kuonywa na mtu tu ambaye anaweza kujiandikia barua akajiita ni Katibu wa Baraza la Ulamaa lakini katika sura ambayo siyo ya kuridhisha,” alisema Alhad akiwa Chanika.

Hata hivyo, alisema katika utendaji kazi Baraza la Ulamaa linaweza kumuita kiongozi wake yeyote ambaye wataona ameenda ndivyo sivyo, badala ya kuandikiana barua na kwenda katika mitandao kwa lengo la kuvunjiana heshima au kumdogosha mtu fulani.

Akizungumzia uamuzi wa kumuondoa Sheikh Alhad, Katibu wa Bahkita, Said Mwaipopo, alisema katika uamuzi walitegemea Baraza la Ulamaa lingeanika makosa ya Sheikh Alhad.

Hata hivyo, alisema kama walitumia kigezo cha mgogoro wa Dk Mwaka, basi watakuwa wamelivua nguo baraza hilo na viongozi wake hawapaswi kuendelea na nafasi zao kwa kuwa wanaendeshwa na mtu badala ya kuendeshwa na katiba ya Bakwata iliyoliunda.

Kuhusu tuhuma za kuwa walijitokeza kumtetea Sheikh Alhad, alikanusha hilo na kueleza Sheikh huyo hana uwezo wa kuwatuma kwa kuwa hajawaajiri, bali walizungumza kama waumini wengine wa Kiislamu ambao hawakupendezwa na hatua hiyo.

Naye Imamu wa msikiti wa Wamwela Mbagala, Yusufu Kabundula, alisema hatua iliyochukuliwa dhidi ya Sheikh Alhad ni sahihi, kutokana na mamlaka iliyofanya hivyo kuwa juu yake kisheria kwa kuona alichokifanya ndivyo sivyo.


Mrithi wake afunguka

Jana, Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, ambaye ni Imamu Mkuu wa Msikiti wa Kichangani Magomeni, Walid Alhad Omar, alitoa ujumbe kwa waumini wote na Watanzania kumuombea dua kwa majukumu mapya aliyopewa.

Ombi hilo alilitoa jana kwenye swala ya Ijumaa aliyokuwa akiiongoza iliyofanyika katika Msikiti wa Kichangani.

“Nimeteuliwa, ni maamuzi na mapenzi ya Mungu, kwa hiyo nawaomba waumini na Waislamu wote na Watanzania mniombee dua nikayafanye vyema majukumu mapya,” alisema Sheikh huyo.

Mara baada ya kumalizika kwa swala hiyo iliyokusanya waumini wengi kulikuwa na hafla maalumu ya kumpongeza kwa uteuzi huo ambapo waumini wote walikuwa wanampa mkono kama ishara ya kumtakia mema katika majukumu yake. Baada ya kuisha tukio hilo lilofanyika ndani ya msikiti, Sheikh huyo alitoka nje ya msikiti kuwasalimia kinamama waliokuja kuswali na kupiga nao picha ya pamoja, huku kina mama hao wakitoa maneno ya shukrani kwake.

Hata hivyo Mwananchi, lilipomfuata azungumzie uteuzi huo, Sheikh huyo mteule alisema “Siwezi kuzungumza kwa sasa, nasubiria niapishwe kwanza ndipo nitawaita na kuzungumza na kujibu maswali yenu yote,” alisema Sheikh Walid, alipoulizwa na gazeti hili anazungumziaje nafasi hiyo


Waumini watoa neno

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, waumini wa msikiti huo walisema elimu aliyonayo, busara na hekima zake anastahili kushika wadhifa huo na kutekeleza majukumu yake kwa weledi.

Jamhuri Kihwelu, aliyewahi kuwa kocha wa Timu ya Taifa, Serengeti Boys, amesema kuteuliwa kwake siyo jambo lililozuka tu, ilipangwa na Mungu.

“Lakini amini aliyetoka hakuwa mbaya isipokuwa Mungu aliona wakati wake wa kuondoka umefika na kuingia mwingine kwangu. Waislamu tumepata mtu mzuri wa kushika madaraka,” alisema.

Alimmwagia sifa kuwa ni mtu mzuri katika kutoa ushauri, msheshi na ni mkarimu wa kupenda watu kwenda kuswali kwenye msikiti wake na wanamtakia mema asiwe na kiburi awaongoze kwa busara Waislamu wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Amis Rajabu Mzee wa Msikiti wa Kichangani amesema Sheikh huyo ni msikivu na anapenda kuwasilikiza wote, lakini pia kiongozi mwenye dira za maendeleo.

“Tumeanza naye tangu umeanza huu msikiti, tuko naye amesimamia tumejenga msikiti huu pamoja na kujenga shule wanayosoma wanafunzi wetu, ni mtu sahihi kwa wana Dar es Salaam,” alisema.


Kuhusu Sheikh Alhad

Alikuwa akishikilia nafasi mbalimbali za kidini na kijamii na kuhudhuria makongamano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa pamoja na kutoa mchango katika ustawi wa jamii.

Amekuwa ni mmoja wa viongozi wa kidini nchini anayeshikilia bendera katika kuimarisha misingi ya amani, vilevile amekuwa akihimiza kuhusu uzalendo, utaifa na maridhiano baina ya Watanzania.

Ukiacha cheo cha Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, pia ni mwanzilishi na Mwenyekiti wa kamati za amani na jumuiya za maridhiano Tanzania.

Nafasi nyingine ni pamoja na mwenyekiti wa kamati za viongozi wa dini, kamati za kupambana na dawa za kulevya na mwenyekiti wa walimu wanaosomesha Quruani Tanzania, mhadhiri na imamu wa msikiti wa Majumwaa Dar es Salaam.

Aidha, Julai 2018 Alhad Mussa alipewa shahada na pongezi kwa kujitolea kufanikisha semina ya malezi na mabadiliko ya elimu iliyotolewa na Bakwata, hata hivyo Novemba 2018 alipewa tuzo kwa akitambuliwa kazi alizozifanya ndani ya Taasisi hiyo kwa kipindi cha miaka kumi.

Mwaka 2019 alipewa cheti cha heshima kwa kutambua mchango wake katika kufanikisha shughuli za Chama cha Mapinduzi (CCM) kilichotolewa na umoja wa vijana wa chama hicho.

MWANANCHI
 
Mbona mnajitahidi kumtetea huyu sheikh wa mchongo?
Aende kule kwa rafiki zake mashia wakampe ulaji
 
Hapo MaCCM yamekaa pembeni yanawagombanisha na kuwagonganisha vichwa kwa kutumia Kipande Cha mkate.

Yanagongana vichwa Kama mazuzu.
 

Attachments

  • images.jpeg
    images.jpeg
    61.2 KB · Views: 8
Bakwata ni muflisi ktk nchi hii. Hawana kitu cha maana cha kuonesha na kuwa mfano bora wa kiongozi.
 
Back
Top Bottom