Baraka Shamte, Mtoto wa Waziri Mkuu wa Kwanza wa Zanzibar Sheikh Mohamed Shamte

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,841
30,168
BARAKA SHAMTE MTOTO WA WAZIRI MKUU WA KWANZA WA ZANZIBAR SHEIKH MOHAMED SHAMTE

Kama isingekuwa kushiriki kama Mtafiti Msaidizi wa Dr. Harith Ghassany wakati anatafiti kitabu chake ‘’Kwaheri Ukoloni Kwaheri Uhuru,’’ labda nisingejua mengi katika historia ya Zanzibar na labda nisingemjua Baraka Shamte.

Siku moja niko Jamia Mosque, Nairobi nimemaliza kusali L’Asr navaa viatu natoka msikitini akaingia mtu tukatazamana.

Yeye alikuwa kachelewa kama mimi.

Moyo ukanistuka.

Moyo umenistuka kwa kuwa sura yake ilikuwa imeshahabiana sana na sura ya Sheikh Mohamed Shamte Waziri Mkuu wa kwanza wa Zanzibar ilipopata uhuru mwaka wa 1963

Sikustahamili nikamtolea salamu kisha nikamuuliza, ‘’Wewe una udugu na Sheikh Mohamed Shamte?’’

Jibu alilonipa lilinifanye nicheke kwani alininambia, ‘’Mimi ndiye Shamte mwenyewe.’’

Kwa mazungumzo mafupi tu tukawa yeye kanijua na mimi nimemjua kwani ndugu zake wengi walikuwa nawafahamu ila Baraka Shamte.

‘’Vipi Sheikh Mohamed humjui Baraka Shamte huyu ndugu yangu mtu maarufu sana katika siasa za Zanzibar.’’

Hakika Baraka Shamte alikuwa mtu maarufu lakini mimi sikumfahamu

Nilikuja kumjua Baraka Shamte miaka mingi baadae mwaka wa 1995 niko Zanzibar wakati wa uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi nimekaa na wenzangu Malindi pembeni ya mgahawa maarufu unaoitwa ‘’Passing Show.’’

Ilikuwa baada ya kura kumalizika kupigwa na kuhesabiwa lakini matokeo hayatolewi kwa muda uliostahili na tetesi zikawa zimezagaa mjini kuwa Seif Shariff Hamad amemwangusha Komando Salmin Amour

Zanzibar asubuhi ile ilikuwa imechangamka sana watu wameweka vigenge vigenge vidogo vidogo vya watu wawili wawili, watatu watatu hakuna mazungumzo ila mazungumzo ya uchaguzi na tetesi za kushindwa kwa Komando na CCM.

Nikiwa hapa Malindi ndipo nilipoonyeshwa Baraka Shamte akipita lakini kapita kimya, kimya na wanaomjua wakachukua ile kama ishara ya kuthibitisha kuwa mambo kwa upande wa Salmin Amour na CCM Zanzibar si mazuri.

Mimi nikipima upepo akili yangu inanieleza kuwa CCM imeshindwa uchaguzi wa rais kwa jinsi nilivyowaona wafuasi wa CCM walivyokuwa wamenyongea.

Siku nzima ikapita hakuna matokeo ya kura za rais na hii ndiyo imekuwa kama sehemu ya chaguzi zote za rais Zanzibar.

Matokeo hayatoki kwa muda unaotakiwa.

Asubuhi siku ya pili nimefika tena kijiweni.

Haukupita muda akapita Baraka Shamte kavaa rangi za chama chake huku akipiga kelele, ‘’We have won the election we are going to form the government.’’

‘’Tumeshinda uchaguzi tutaunda serikali,’’ hizi ndizo zilikuwa kelele za Baraka Shamte.

Baraka Shamte ilikuwa kama vile sasa yeye anawafahamisha Wazanzibari matokeo ya uchaguzi ule wa rais wa mwaka wa 1995.

Sikusubiri tena haraka nikakata tiketi nikarudi Dar es Salaam.

Sifa ya Sheikh Mohamed Shamte, Waziri Mkuu wa Zanzibar aliyepinduliwa mwaka wa 1964, ni kuwa Allah alimjalia kupata watoto wengi na wenye akili sana na baadhi yao niliwafamu kwa karibu na hakuna hata mmoja alikuwa katika siasa ila Baraka Shamte.

Miaka mingi ilipita kufikia siku nilipokutana na Baraka Shamte uso kwa uso katika mahojiano ya kipindi cha televisheni, ‘’Walioacha Alama Katika Historia ya Tanzania.’’

Jana yake nilikuwa nimefanya kipindi cha mazungumzo na vijana wa Kizanzibari katika hoteli moja mjini.

Jioni ile nikapokea simu kutoka kwa rafiki yangu mtu mkubwa sana katika serikali ya mapinduzi akaniambia iweje nafika Zanzibar kwenye himaya yake nafanya mahojiano na Wanzibari bila ya kumtaarifu yeye.

Nilijiuliza imekuwaje kajua kuhusu mahojiano yale?

Au Zanzibar imekuwa ‘’Police State?’’

Nikajirudi mwenyewe na kujicheka nikijiambia wasiwasi wangu ni kwa sababu ya kusoma sana vitabu vya ‘’espionage,’’ kiasi naanza kuogopa hata kivuli changu mwenyewe.

Huyu bwana nilikutananae mara ya kwanza Dar es Salaam kwenye mgahawa maarufu wakati wa uchaguzi wa 2000 na tukaingia katika mazungumzo makali baina yetu kuhusu siasa na historia ya Zanzibar bila mimi kumjua hata jina na tukiwa na hadhira kama ya meza tatu zilizounganishwa watu wakitusikiliza.

Ulikuwa mjadala mkali lakini wa kistaarabu na mwisho wa mazungumzo huyu bwana akataka kunijua nani mimi kwani aliniambia kuwa amependa sana mazungumzo yangu.

Urafiki wetu leo umekuwa udugu.

Ndugu yangu huyu akaniambia kuwa ikiwa nataka kuzungumza na kiongozi yeyote wa Zanzibar nimfahamishe atanipangia miadi.

Hivi ndivyo nilivyokutana na Baraka Shamte na akaniomba nifanye kipindi chetu nyumbani kwake.

Ikawa Baraka Shamte kanipa heshima kubwa.

Nilikusudia kufanya kipindi cha nusu saa lakini hazikutosha tulifanya kipindi cha saa nzima.

Katika watu wote niliopata kuwahoji faragha au kwa ajili ya kurusha hewani Baraka Shamte ni habari nyingine inayojitosheleza.

Waingereza wanasema, ‘’There is no dull moment.’’

Hatumwi mtoto dukani.

Kipindi hiki: ‘’Walioacha Alama Katika Historia ya Tanzania – Baraka Shamte,’’ mimi nimekipata jina langu mwenyewe makhsusi na huwaeleza rafiki zangu na wakacheka sana, jina la kipindi hiki nimekiita: ‘’Mazugumzo baina ya ‘’Wendawazimu’’ Wawili.’’

Ukweli ni kuwa nilimkamia Baraka Shamte kwani nilikuwa nimefanya utafiti wa kutosha kuhusu yeye mwenyewe kama mtoto wa Waziri Mkuu Sheikh Mohamed Shamte kiongozi wa Zanzibar ambae serikali yake ilipinduliwa na tayari nilikuwa naijua historia ya baba yake.

Nilikuwa na mengi ya kutosha kuhusu Sheikh Mohamed Shamte wakati nilipokuwa Mtafiti Msaidizi wa Dr. Harith Ghassany wakati anatatafiti historia ya Zanzibar.

Katika sehemu ya pili ya kipindi ndipo nilipofungua silaha zangu zote na nilianza na ‘’Kilemba cha Kiomani,’’ alichokuwa akifunga baba yake Waziri Mkuu Sheikh Mohamed Shamte.

Nilipata kumsikia Baraka Shamte akikisanifu ‘’Kilemba cha Kiomani’’ na kushangazwa kina uhusiano gani na Mzanzibari.

Sikuwa namkatisha nikimpa nafasi ya kutosha azungumze kwani nilitaka watazamaji wangu wastarehe na Baraka Shamte.

Nikamvusha Baraka Shamte Bahari ya Hindi hadi Dar es Salaam wakati baba yake Sheikh Mohamed Shamte yuko Ukonga Prison, Dar es Salaam kifungoni baada ya serikali yake kupinduliwa.

Nikamtoa Ukonga Prison nikamrejesha Kariakoo ambako baba yake aliishi baada ya kutoka kifungoni.

Nilihitimisha kwa kumuuliza kama aliweza kumwangalia baba yake machoni alipotoka jela akiwa hana ‘’Kilemba cha Kiomani,’’ wala juba, mtu mzima amedhofu kwa shida za kuwa kifungoni.

Nikamuuliza yeye kama mwanamapinduzi alitegemea yale yaliyoifika Zanzibar baada ya mapinduzi na kama walifanya mapinduzi yale ili iwe vile?

Baraka Shamte si mjinga si mtu wa kulishwa maneno na mtu mwingine.

Baraka Shamte si mtu wa kwenda kuuliza nijibu nini?

Baraka Shamte ana akili yake mwenyewe na anaitumia vizuri anapokutana na ‘’wendawazimu,’’ kama mimi.

Majibu yake hayakuwa yale niyasikiayo siku zote kwa wenzangu na mie.

Tulipomaliza mahojiano yetu sote tulikuwa taaban lakini naamini mwenzangu alichoka zaidi yangu na cha kushangaza ni kuwa hata mpiga picha wangu tukiwa ndani ya gari yetu tunarudi hoteli aliniambia, ‘’Nafurahi kukurekodi kwani maswali yako yananifurahisha sana hata sijui wapi unayatoa."
 

Attachments

  • MOHAMED SHAMTE NA MKEWE.jpg
    MOHAMED SHAMTE NA MKEWE.jpg
    29.8 KB · Views: 17
  • BARAKA SHAMTE.jpg
    BARAKA SHAMTE.jpg
    43.5 KB · Views: 19
Kuna muda huwa najawa na huzni sana najiuliza "hivi sheikh Mohammed ikitokea siku hatuko nawe duniani una vijana wako uliowarithisha hii historia? Kwa mara ya kwanza kukuona na kukufaham ilikuwa 2009 nikiwa mwanafunzi Minaki sekondari tulikuwa na semina kwa shule za kiislam maeneo ya chamazi kule tangu hapo nikaanza kukufatilia leo tupo kesho hatupo sawa maandiko yako yapo video zipo YouTube ila mwanangu au mjukuu wangu hatapata ladha niliyoipata mimi niliyekushuhudia kwa macho yangu basi apate japo robo yake kwa kuonana na mwanafunzi wako Allah akupe umri mrefu wenye faida in Shaa Allah!
 
Kuna muda huwa najawa na huzni sana najiuliza "hivi sheikh Mohammed ikitokea siku hatuko nawe duniani una vijana wako uliowarithisha hii historia? Kwa mara ya kwanza kukuona na kukufaham ilikuwa 2009 nikiwa mwanafunzi Minaki sekondari tulikuwa na semina kwa shule za kiislam maeneo ya chamazi kule tangu hapo nikaanza kukufatilia leo tupo kesho hatupo sawa maandiko yako yapo video zipo YouTube ila mwanangu au mjukuu wangu hatapata ladha niliyoipata mimi niliyekushuhudia kwa macho yangu basi apate japo robo yake kwa kuonana na mwanafunzi wako Allah akupe umri mrefu wenye faida in Shaa Allah!
Namkubali sana huyu mtaalamu kwa historia adhimu hata na hivyo kuna kuna vitu visivyokua na mbadala ama spair part they live once and only....Nishawahi kumuuliza swali kama hilo ya kwamba mpaka wa sasa walau ameweza kutengeneza copy yake? Kwa maana ya mtu wakuendeleza chochote anachokifanya kwa sasa hata baada ya uhai wake? Nampongeza walau kwa kuandika kwenye servers za jamiforum kuna wengine wanauwezo wa kuandika lakini hawapendi kufanya hivyo kwa Furaha yao binafsi na ni sahihi kabisa.

Sent from my HUAWEI TIT-U02 using JamiiForums mobile app
 
Back
Top Bottom