''Bara Mtateseka Sana Kwa Sababu Hamtaki Kutujua Wazanzibari''

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,854
30,201
"BARA MTATESEKA SANA KWA SABABU HAMTAKI KUTUJUA WAZANZIBARI"

Ilikuwa wiki ya pili tu baada ya uchaguzi wa Rais Zanzibar baina ya Maalim Seif na Dr. Ali Mohamed Shein.

Mwaka ni 2010.

Kumbukumbu ya "siege," yaani kupigwa tepe Bwawani Hotel palipokuwa panatolewa matokeo ya uchaguzi na ZEC kila mtu anakumbuka.

Vijana wa CUF waliudhibiti uwanja ule barabara hakiingii wala kutoka kitu.

Vijana wanasubiri matokeo ya uchaguzi na taarifa za kuaminika zilikuwa zile zile za kila uchaguzi wa Rais Zanzibar.

Lakini safari hii hali ilikuwa tofauti kwani Zanzibar ilikuwa kwenye maridhiano.
Kulikuwa na mategemeo makubwa kuwa hali siasa nayo itageuka na kuwa bora.

Kama si busara ya Maalim Seif damu ingemwagika na wala Maalim Seif asingekabidhiwa madaraka.

Hili lingetokea kuna watu wangesema Maalim kawtoa kikoa watoto wa wenzie.
Jana Khamis Abdulla Ameir katembelewa nyumbani kwake na Rais wa Zanzibar Dr. Hussein Ali Mwinyi.

Khamis Abdulla Ameir kachukua fursa hii kumkabidhi Rais wa Zanzibar kitabu chake maarufu, "Maisha Yangu Miaka Minane Ndani ya Baraza la Mapinduzi Khaini au Mhanga wa Mapinduzi?"

Video hii imenikumbusha ile "siege," ya Bwawani iliyomalizika kwa salama sana kupita kiasi.

Wiki ile ile rafiki yangu mmoja mtu mkubwa katika uongozi na siasa za Zanzibar akanikaribisha nyumbani kwake Zanzibar tukawa tumebarizi kwenye bustani yake tunazungumza kuhusu uchaguzi wa Zanzibar uliomalizika juma lililopita.

Sahib yangu huyu ambae kwa hakika ni kaka yangu akanipa kisa cha Rais mmoja wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambae katika mkutano wa hadhara aliwashambulia wanasiasa wa zamani wa Hizbu ambao yeye aliwaona maadui wa mapinduzi.

Meza Kuu ilikuwa kimya kwa kutahayari ingawa katika meza kuu ile walikuwapo watu wanaopendezewa na mashambulizi kama yale ''ala,'' Kisonge.

Lakini kwa pale katika mkutano ule unaohutubiwa na Rais wa Jamhuru ya Tanzania hali ya siku ile haikuwa rafiki kwa makombora kama yale.

Nitasimama hapa twende "fast forward," jioni yake kwenye dhifa ya chakula cha jioni.

Kwenye hafla ile rafiki yangu huyu akamwambia Rais wa Muungano kuwa mchana ule hotuba yake imepeleka majonzi nyumbani kwa Rais mwenzake Zanzibar.

Akamaliza kwa kumwambia Rais wa Muungano kuwa, "Bara mtateseka sana kwa sababu hamtaki kutujua Wazanzibari."

Hii video ya Rais wa Zanzibar Dr. Hussein Ali Mwinyi kumtembelea Khamis Abdulla Ameir nyumbani kwake imebeba ujumbe mzito sana.

Kitulize kichwa chako chambua.
Nakuhakikishia utauona udugu wa Wazanzibari.

Tuliza kichwa chako mtafute nani mtu baki baina ya hawa watu hawa.
Hakika pale hakuna mtu baki.

Allah ndivyo alivyowajaalia Wazanzibari kuwa daima wawe ndugu.

 
Back
Top Bottom