barafu
JF-Expert Member
- Apr 28, 2013
- 6,739
- 32,863
Katika miaka ya mwisho wa 70 na miaka ya 80 nilikuwa Mlezi (Patron) wa African Sports Club, Tanga. Nikiwa kiongozi nilijitahidi sana kuijenga timu ya mpira ya Sports na tulipata matokeo mazuri na ya kujivunia.
Wanakimanomano waliogopwa na timu maarufu kama Yanga na Simba, mbali na watani wetu -Coastal Union. Ukweli ni kwamba timu za Sports na Coastal Union si tu ziliunda kikosi kikubwa cha timu ya Taifa Stars kwa miaka mingi, lakini pia zilichangamsha jiji la Tanga na kuvutia vijana wengi chipukizi na mahiri wa kucheza mpira wa miguu kutoka pande zote za Tanzania.
Hivyo ni jambo la kusikitisha sana hii leo kuona timu tatu za mpira toka Tanga zikishushwa daraja kwa mpigo. Msemo wa miaka ya karibuni, 'Tanga kunani' ni muhimu katika kuchunguza hali inayojitokeza katika fani ya mpira wa miguu kwetu Tanga.
Hivi karibuni niliandika makala katika gazeti la Guardian nikilalama kuhusu kufifia kwa jiji la Tanga. Hakika ufikapo mjini Tanga huwezi kutoshikwa na huzuni kwanini Taifa letu au niseme Serikali yetu iuachie mji huu wa kihistoria ufikie hatua ya vijana kuukimbia.
Upole wa wenyeji na ushwari wa Tanga hautoshelezi kimaendeleo. Sishangazwi na hata kuzuka hivi karibuni kwa umjahidina na hata ugaidi katika maeneo ya Jiji la Tanga. Ni matokeo ya vijana kukosa mwelekeo katika mazingira magumu ya ukosefu wa ajira.
Katika miaka ya mwishoni mwa 60 na miaka yote ya 70 hadi katikati ya miaka ya 80 Tanga ilikuwa ni eneo lenye makampuni mengi ya Umma na binafsi, tena maarufu nchini. Na Bandari ya Tanga pamoja na reli vilichangia kutoa ajir anyingi kwa vijana .
Timu za mpira za African Sports, Coastal Union na Bandari ziliweza kuwa na wachezaji mpira wa miguu wenye ajira katika makampuni haya. Na hawa vijana walipewa nafasi ya kuimarisha na kukuza vipaji vyao kupitia misaada mingi kutoka kwenye makampuni na mashirika bila kujali kutokuwepo kazini mara kwa mara. Ilikuwa nia aina kubwa ya 'corporate social responsibility' kwa vyombo hivi.
Leo Tanga haina tena mashirika ya umma. Makampuni binafi ya nguo na mafuta ya kupikia yamefunga kutokana na kipindi kigumu kilichopitiwa baada ya Serikali kufungua milango kiholela ya bidhaa kutoka nje kati ya mwaka 1986 na 1995. Ubinafsishaji uliyofuatia haukuzalia matunda yoyote kwa Tanga.Kiwanda cha Sementi alhamdullillahi ni mkombozi kikifuatiwa na Tanga Fresh xha Maziwa na Pembe kinachotengeneza unga.
Hamisi Kindoroko naye kasaidia kujenga hoteli ya kisasa -Tanga Beach Resort. Athi River Mining wanakamilisha kiwanda kipya cha sementi. Labda Tanga itaibuka tena katika miaka mitano ijayo ukifikiria pia bonba la mafuta toka Uganda kuishia Tanga bandarini. Tusubiri kuibuka tena kwa African Sports na Coastal Union ambazo ni timu za watu. Mgambo ni timu ya Jeshi. Nashangaa kushuka kwake daraja!
Lakini kwa miaka mingi Tanga imekuwa ni kama mtoto yatima katika mageuzi ya uchumi. Uyatima huu pia umekumba fani ya mpira wa miguu. Mnauliza, 'Tanga kunani'? Jibu mnalo. Si jibu kutoka kwa wana Tanga peke yao.
Taifa zima na Serikali wanalo jibu. Kamahatua madhubuti hazitachukuliwa kwa haraka, basi Mwenyezi Mungu atunusuru na janga ninalohisi linajengeka taratibu na mbalo sote tunaweza tukalijutia.
Imeandikwa na Balozi Mwapachu