Balile: DPP, IGP, DCI lifutieni taifa aibu kesi ya Mbowe

issenye

JF-Expert Member
Feb 2, 2011
3,780
5,204
Na Deodatus Balile

Imenichukua muda kuandika makala hii. Ninafahamu kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, anashitakiwa kwa tuhuma za kufadhili ugaidi kwa Sh 600,000. Anashitakiwa pia kwa tuhuma za kupanga njama za kulipua vituo vya mafuta katika miji ya Arusha, Mwanza na Dar es Salaam mwaka 2020.

Kubwa zaidi, anatajwa kuwa alitaka kumdhuru Lengai ole Sabaya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mwaka jana. Sabaya yuko mahakamani anashitakiwa kwa wizi wa kutumia silaha na matumizi mabaya ya madaraka.

Sitanii, ninafahamu kuna kundi halijakata tamaa. Kila nikiandika ukweli, husambaza taarifa kuwa mimi ni mwanaharakati. Ninadhani katika eneo hili kuna kutojitambua. Kuna tofauti kati ya harakati na uandishi wa habari.

Mwandishi wa habari anasimamia ukweli, ukweli mtupu. Hafanyi kampeni katika jambo analoliandika, bali yeye anaeleza ukweli wa kinachoendelea na kuuonyesha umma ni wapi kuna tundu lizibwe.

Ninafahamu kesi ikiwa mahakamani kifungu cha 114(1)(d) cha Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 kinazuia kuijadili, kwa kueleza nani anashinda na nani anashindwa.

Hilo ni jukumu la mahakama, nami sitaingia huko. Ni kwa msingi huo, hata washitakiwa wengine anaoshitakiwa nao Mbowe wala siwataji. Mimi ninalo jambo moja la kitaifa. Sura ya nchi yetu kimataifa.

Ninaomba kwa unyenyekevu mkubwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini, Sylvester A. Mwakitalu, Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Simon Sirro na Mkurugenzi wa Upelelezi, DCI Kamishna Camillius Wambura mnisikilize kidogo. Rais wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan, anaandaa filamu yenye lengo la kuitangaza Tanzania nje ya nchi.

Sitanii, uamuzi wa Rais Samia kuandaa filamu ni wa msingi na wa kuungwa mkono. Yapo mataifa ambayo kamwe hayaifahamu Tanzania. Sisi tuliopata fursa ya kusafiri nje ya nchi, unakuwa kama Washington, ukimwambia Mzungu unatoka Tanzania, anakuuliza: “Tasmania?” Tasmania ni kisiwa cha nchini Australia chenye ukubwa wa kilomita za mraba 90,758. Kina wakaazi 541,000 na kimezungukwa na visiswa vidogo 1,000. Kisiwa hiki ni cha 26 kwa ukubwa duniani. Kinavutia watalii wengi.

Ni nadra sana kukutana na mtu nje ya nchi, tena wakati mwingine wasomi waliobobea wakiifahamu Tanzania.

Uamuzi wa Rais Samia kuitangaza nchi yetu kupitia utalii ni wa kwanza kufanywa na Rais binafsi, bila kutegemea wasaidizi au wageni maarufu kutoka nje ya nchi ndio watangaze utalii wetu. Utalii unakadiriwa kuingiza dola bilioni mbili hapa nchini.

Nchi ya Misri yenye vivutio vichache ukilinganisha na sisi wanaingiza dola bilioni 12 kwa mwaka. Kwa uhalisia, bajeti ya Tanzania ni dola bilioni 14.

Tukiitangaza nchi yetu vizuri, tuna uwezekano wa kupata dola bilioni 15 kama mchezo kutoka kwenye utalii. Ni bahati mbaya, ninasema ni bahati mbaya juhudi hizi anazofanya Rais Samia zinavutwa miguu na uamuzi usio sahihi wa baadhi ya watendaji katika vyombo vya dola.

Sitanii, nimeomba kwa unyenyekevu mkubwa DPP, IGP na DCI mniazime masikio. Kuna makosa tunayafanya, sina uhakika kama ni kwa bahati mbaya au makusudi.

Hili neno ugaidi ni neno baya na la hatari sana katika masikio ya watalii, jumuiya ya wafanyabiashara na wasafiri wa kawaida. Yaliyotokea Septemba 11, 2001 nchini Marekani, bila kusahau ya Agosti 7, 1998 kwa Tanzania na Kenya ni somo kuu la ubaya wa neno gaidi.

Tanzania inapaswa kuwa ya mwisho kumfungulia mtu kesi ya ugaidi au kumtaja mtu kuwa ni gaidi. DCI ameiambia dunia Hamza Mohamed aliyeua askari watatu na mlinzi wa kampuni binafsi alikuwa gaidi. Inawezekana alikuwa mgonjwa wa akili tu. Neno kama hili halipaswi kutamkwa kamwe kutoka vinywani mwa vyombo vya dola. Mbowe anashitakiwa kwa kufadhili ugaidi, tena kwa Sh 600,000!!! Ugaidi kwa Sh 600,000? Let us be serious.

Sitanii, wanaotafuta nafasi ya kulichafua taifa letu mbele ya jamii ya kimataifa wanakusanya hizi kauli na kueleza kuwa Tanzania kuna ugaidi. Nilisema nitaizungumzia kesi ya Mbowe kwa picha pana. Kila Mbowe anapopelekwa mahakamani, vyombo vya habari vya kimataifa vinaimulika Tanzania na kuhakikisha neno ‘ugaidi’ linatajwa.

Sisi tunaweza kuwa na malalamiko yetu dhidi ya Mbowe. Tena wengine nikizungumza nao wanasema Mbowe alitaka kumshinikiza Rais Samia kwa matamko juu ya Katiba mpya, na milele Rais hashinikizwi. Tunaweza kujikuta katika ‘kujimwambafai’ tunalichafua taifa letu kwa kiwango cha kutisha. Ninashawishika kusema hapa tulipofika tufunge breki.

Tufunge breki tuchague mkondo wa mazungumzo badala ya mabavu. Rwanda na Burundi walipigana kwa mtutu, ila mwisho wa siku walikuja AICC Arusha wakafanya mazungumzo na wakaafikiana.

Ninaomba kusema si kila tatizo la kisiasa tutalitatua kwa kukamata watu na kuwafikisha mahakamani. Kwa kufanya hivyo, tutajikuta tunamchafua Rais aliyeko madarakani na nchi kwa ujumla.

Sitanii, kwa hatua iliyofikiwa DPP nikuombe utumie busara ya Mfalme Suleiman katika kubaini mtoto ni wa nani.

Mama mmoja alisema mtoto auawe, akatwe vipande viwili kila anayedai ni wake apewe kipande akazike. Aliyekuwa mama wa kweli akasema ni bora mama wa kusingizia amchukue huyo mtoto angalau atakuwa anamwona, anampungia mkono akiwa hai. Mfalme Suleiman kwa kauli hizo mbili akabaini mama halisi wa mtoto.

DPP wakati umefika utumie Kifungu cha 91 cha Sheria ya Mwenendo wa Mashitaka (CPA) kuondoa kesi ya Mbowe mahakamani. IGP na DCI niwaombe sana neno ugaidi msilitumie tena, linachafua sura ya Tanzania. Mbowe ni Mtanzania. Zungumzeni naye, mwelezeni umuhimu wa uzalendo kwa taifa letu.

Lakini pia msikilize na kesi zake za kuvunjiwa ukumbi wa Bilcanas. Msumeno ukate pande zote. Ninarudia, si kila kesi ya kisiasa tutaimaliza kwa kuifikisha mahakamani. Tuvuke huu msitari unaoleta sura ya ubabe. Mungu ibariki Tanzania.
 
Kibatala anawavua nguo huko!

Kibatala: umesikia Mashahidi wa serikali wanasema waliwakamata mkiwa mnakula?

Shahidi: Ndiyo

Kibatala: Utakubaliana na mimi kama mlienda kula bila shaka ulikuwa na pesa, Je umesikia hapa mahakamani wamezungumzia kuhusu Pesa ulizokuwa unataka kununulia chakula?

Shahidi: Hapana
 
Mkuu umeandika kiuzalendo sana.hakika Kuna watu kwa makusudi au kwa bahati mbaya hawajui Kama wanalialibia taifa.kesi ya mboe italeta majibu mabaya Sana huko mbeleni Kama watawala bado watatia pamba masikioni
 
Kingai ni hatari sana kwneye hii sekta ya kuchukua pesa ya watuhumiwa
Kibatala anawavua nguo huko!

Kibatala: umesikia Mashahidi wa serikali wanasema waliwakamata mkiwa mnakula?

Shahidi: Ndiyo

Kibatala: Utakubaliana na mimi kama mlienda kula bila shaka ulikuwa na pesa, Je umesikia hapa mahakamani wamezungumzia kuhusu Pesa ulizokuwa unataka kununulia chakula?

Shahidi: Hapana
 
Kuna member mmoja kwenye ile thread ya kesi ya Mbowe kaandika point ya maana sana; kwamba Jeshi la Polisi ni chombo kinachohusika na haki za wananchi moja kwa moja; is there any oversight body to oversee Police Force? Hakipo!

Yaani wao Polisi wamekabidhiwa mamlaka yote kuhusu haki za wananchi na hakuna chombo huru kinacho-monitor matendo yao? Wanaweza kujifanyia wapendavyo na kuripoti UONGO? Hii haikubaliki; kama taasisi kama TRA, PPRA, LATRA, n.k. ambazo zina oversight bodies kuhakikisha haki inatendeka sembuse polisi wanaohusika na MAISHA ya wananchi? Tena polisi wenyewe ndio hawa wanaoweza kutumika na wanasiasa! Hii ni hatari sana! Katiba Mpya isisahau hili.
 
Na mimi sitanii, nasema hivi, sehemu pekee ya kumsafisha au kumuacha na uchafu ndugu Freeman vivyo hivyo kwa serikali ni Mahakamani tu. Kumshawishi mwendesha mashtaka aifute kesi wakati ameishaueleza umma ana ushahidi ni kuficha uchafu unukao ili uvune uyoga mweupe.

Pia kisingizio cha kibebeo cha filamu ya utalii kwa kutangaza nchi huku tukihatarisha mwenendo wetu wa kujisafisha kuwa ama hatuna uchafu ama tunao uchafu sasa tunausafisha kwa kutumia vyombo muhimu vya kufanya jambo hili la kusafisha halikubaliki.

Tuiamini mahakama kuwa inamudu kulifanyia kazi jambo hili kwa ufanisi wa hali ya juu.

Ndugu, Balile, mwanasheria msomi na mwandishi wa habari. Mimi hapa
, raia kindakindaki wa Tanzania, sitanii.
 
Kitu cha kwanza mtalii akitaka kuweka mguu Tanzania anaenda google anaangalia terrorism in Tanzania, akiona tuu kesi kama za kina mbowe, Hamza au ule utekaji kama wa kina Moe amemaliza haihitaji maelezo zaidi, tunaojua ni kazi chafu tuu ya wajinga wachache kama kina siro na wapuuzi wenzake
 
Umeongea vyema kabisa. Ila kuna shida kubwa sana ndani ya kichwa cha Siro. Hata ukiangalia alivyo ongea kwamba polisi hawana sheria inayo wazuia kuingilia mikutano ya vyama vya siasa, utaona uso wake una aibu. Lakini amesha amua ana fanya. Kwa sheria gani? Jilo analijua yeye. Ila kwa kweli polisi imelipaka taifa matope.
 
Back
Top Bottom