Balali atoweka
2008-05-08 10:36:59
Na Mashaka Mgeta
Gavana wa zamani wa Benki Kuu ya Tanzania aliyefukuzwa kazi, Dk. Daudi Balali, ametoweka nchini Marekani, na serikali haijui mahali alipo.
Jitihada za serikali, kupitia kwa Waziri wa Fedha na Mambo ya Uchumi, Bw. Mustapha Mkulo, kumsaka Bw. Balali anayehusishwa katika kashfa ya ufisadi kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) katika jiji la Washington nchini humo hivi karibuni, hazikufanikiwa.
``Awali tuliambiwa kwamba Balali alikuwa anatibiwa Marekani, lakini nilipokuwa huko (Marekani) hivi karibuni, nilimtafuta sana katika jiji la Washington, hakuonekana... Hatujui yupo wapi,`` alisema Bw. Mkulo, wakati akihojiwa na Nipashe jijini Dar es Salaam jana.
Hata hivyo, habari za awali zilisema kwamba Balali anatibiwa katika jiji la Boston.
Alisema timu iliyoundwa na Rais Jakaya, ikiwa inaongozwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bw. Johnson Mwanyika, inaendelea kushirikiana na vyombo vya dola, kushughulikia masuala yote yanayomhusu Gavana huyo wa zamani wa Benki Kuu.
Pia, Bw. Mkulo, alisema kwa upande mwingine, serikali imewekeza nguvu zake kuhakikisha fedha zinazodaiwa kutokana na kashfa ya EPA zinarejeshwa.
Kwa mujibu wa Bw. Mkulo, kuna mafanikio makubwa katika kuzirejesha fedha hizo, ingawa hakutaja kiasi kilichopatikana hadi kufikia jana
alipohojiwa na gazeti hili.
``Kuhusu kiasi kilichopatikana, hilo siwezi kulizungumzia lakini ninachoweza kusema ni kwamba, kuna mafanikio makubwa kuhusu kurejeshwa kwa fedha zilizofujwa kwenye EPA,``alisema.
Aidha, Bw. Mkulo, ameshindwa kuelezea athari za kiuchumi zinazotokana na baadhi ya Watanzania, kujilimbikizia mabilioni ya fedha nje ya nchi.
Alifikia hatua hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu matokeo ya ukamilishaji wa makadirio mapya ya takwimu za pato la Taifa kwa bei za mwaka 2001 kwa Tanzania Bara.
Alisema fedha zinazohifadhiwa na Watanzania nje, zinawekwa na wananchi wanaoishi ughaibuni, viongozi wa serikali na watu wengine wanaposafiri na kuamua kuwaachia ndugu zao, hususan wanaotoka huko, na wenye fedha zilizopatikana kwa njia haramu.
Hivi sasa kuna tuhuma zinazoelekezwa kwa aliyekuwa Waziri wa Miundombinu, Bw. Andrew Chenge, kujilimbikizia takribani Dola 1,000,000 za Marekani huko Jersey nchini Uingereza.
Ingawa Bw. Mkulo hakutaka kugusia fedha hizo, alisema kutokana na asili yake, ni vigumu kubaini kiasi cha fedha zilizohifadhiwa nje.
Hata hivyo, alisema serikali inawashawishi Watanzania wanaoishi nje, kuweka fedha zao kwenye benki za hapa nchini, ili kusaidia kuinua pato la Taifa.
Alisema uhifadhi wa fedha za wananchi wanaoishi nje ya mataifa yao, ulileta mafanikio katika nchi kama Pakistan na Philippines.
Bw. Mkulo, alitoa mfano kuwa Pakistan inapata Dola bilioni 4 za Marekani kwa mwaka, wakati Philippines ina utaratibu wa kuwatambua watu wake wanaofanya kazi nje, na kuingiza fedha zao katika akaunti zilizopo nchini humo, zinazolipwa kupitia Benki Kuu ya nchi hiyo.
Alisema kwa upande wake, Tanzania inaendeleza jitihada za kutafuta vyanzo vya fedha zilizopatikana kupitia njia zisizo halali.
``Vyombo vya dola vinashughulikia suala hilo, kwa kushirikiana na polisi wa kimataifa, Interpol,`` alisema.