Bajeti ya Serikali 2021/2022 ni Trilioni 36.33, Bodaboda na Madiwani Waneemeka, Barabara hadi Vijijini, Miradi kuendelea, Watanzania Kufunga Mkanda

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,797
11,959
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Nchemba leo Juni 10, 2021 katika Bunge la Tanzania jijini Dodoma saa 10:00 jioni anawasilisha Bajeti Kuu ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

Hii inakuwa bajeti ya kwanza kwa serikali ya awamu ya Sita na Waziri Mwigulu ameiita Bajeti ya Kimkakati.




======

HOTUBA YA WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO, MHESHIMIWA DKT. MWIGULU LAMECK NCHEMBA MADELU (MB), AKIWASILISHA BUNGENI MAPENDEKEZO YA SERIKALI KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA 2021/22
10 Juni 2021


1623403889714.png


Mheshimiwa Spika, hotuba hii inawasilisha Bajeti ya kwanza ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yenye Dira na Mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Sita ya “Kudumisha mazuri ya Awamu zilizopita, Kuyaendeleza mema yaliyopo na Kuleta mengine mapya. Hivyo, makadirio ya bajeti ya Serikali kwa mwaka 2021/22 yameandaliwa kwa kuzingatia nyaraka na miongozo mbalimbali ikiwemo: Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26 ambao umeandaliwa kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025; Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 - 2025; Dira ya Maendeleo ya Afrika Mashariki 2050; Ajenda ya Maendeleo ya Afrika 2063; Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030; Mwongozo wa Ushirikiano wa Maendeleo; na makubaliano mengine ya kikanda na kimataifa ambayo Tanzania imeyaridhia. Aidha, Bajeti imezingatia kikamilifu maeneo ya kipaumbele yaliyoainishwa katika Hotuba ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati akilihutubia Bunge hili tarehe 22 Aprili 2021.

TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2020/21

Mwenendo wa Mapato

Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya mwaka 2020/21, Serikali ilipanga kukusanya jumla ya shilingi trilioni 34.88 kutoka katika vyanzo vyote vya ndani na nje. Hadi Aprili, 2021 shilingi trilioni 24.53 zimekusanywa sawa na asilimia 86.1 ya lengo la kipindi hicho. Mchanganuo ni kama ifuatavyo:

Mapato yaliyokusanywa kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yalifikia shilingi trilioni 14.54, sawa na asilimia 86.9;

Mapato yasiyo ya Kodi yalifikia shilingi trilioni 1.80, sawa na asilimia 78.5 ya lengo;

Mapato yanayotokana na vyanzo vya ndani vya Mamlaka za Serikali za Mitaa yalifikia shilingi bilioni 607.4 sawa na asilimia 88.5 ya lengo;

Misaada na mikopo nafuu iliyopokelewa ilikuwa shilingi trilioni 1.89 sawa na asilimia 70.4 ya lengo;

Mikopo ya ndani ikijumuisha mikopo ya kulipa dhamana za Serikali zilizoiva ilifikia shilingi trilioni 3.99, sawa na asilimia 95.7 ya lengo; na

Mikopo ya nje yenye masharti ya kibiashara ilifikia shilingi trilioni 1.68 sawa na asilimia 88.1 ya lengo.

Mheshimiwa Spika, mlipuko wa UVIKO-19 umesababisha kutofikiwa kwa baadhi ya malengo ya makusanyo ya mapato ya ndani hususan kwa sekta za utalii, usafiri wa anga na uingizaji wa bidhaa kutoka nje. Aidha, baadhi ya mashirika na taasisi zimeathiriwa na UVIKO-19 na hivyo kupungua kwa michango na gawio kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali. Mathalani, mapato ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania yameathiriwa kufuatia kuporomoka kwa shughuli za utalii kulikosababishwa na kusambaa kwa UVIKO-19 katika nchi zinazoleta watalii wengi nchini.

Mheshimiwa Spika, misaada na mikopo nafuu iliyopokelewa hadi Aprili 2021 ni shilingi trilion 1.89 ikilinganishwa na shilingi trilion 1.82 mwaka 2019/20. Pamoja na athari za mlipuko wa UVIKO -19, misaada na mikopo nafuu iliongezeka kwa asilimia 3.84 ikilinganishwa na kiasi kilichopokelewa katika kipindi kama hicho mwaka 2019/20. Serikali itaendelea kuimarisha ushirikiano na Washirika wa Maendeleo ili kuwezesha upatikanaji wa misaada na mikopo nafuu katika kuchangia bajeti ya Serikali.


Mwenendo wa Matumizi

Mheshimiwa Spika, makadirio ya matumizi kwa mwaka 2020/21 yalikuwa shilingi trilioni 34.88 ambapo shilingi trilioni 22.10 ni matumizi ya kawaida na shilingi trilioni 12.78 ni matumizi ya maendeleo. Katika kipindi cha Julai 2020 hadi Aprili 2021, jumla ya shilingi trilioni 24.74 zimetolewa sawa na asilimia 86.8 ya lengo. Kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni 17.42 zilikuwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida ambazo zinajumuisha shilingi trilioni 6.09 kwa ajili ya mishahara, shilingi trilioni 4.49 Matumizi Mengineyo na shilingi trilioni 6.84 kugharamia deni la Serikali.

Mheshimiwa Spika,
hadi Aprili 2021, jumla ya shilingi trilioni 7.32 sawa na asilimia 74.1 ya lengo zimetolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambapo shilingi trilioni 6.24 ni fedha za ndani sawa na asilimia 79.7 ya lengo na shilingi trilioni 1.08 ni fedha za nje sawa na asilimia 52.8 ya lengo.

Mheshimiwa Spika,
katika utekelezaji wa Bajeti ya Serikali kwa kipindi cha Julai 2020 hadi Aprili 2021, Serikali iliendelea kutoa fedha kwa ajili ya kugharamia maeneo ya vipaumbele yaliyoainishwa kwenye bajeti kama ifuatavyo:


Ulipaji wa deni la Serikali kwa wakati shilingi trilioni 6.84;

Ulipaji wa mishahara ya watumishi kwa wakati shilingi trilioni 6.09;

Miradi ya kuzalisha, kusafirisha na kusambaza umeme ikiwemo mradi wa kufua umeme wa maji wa Julius Nyerere; na mradi wa kusambaza umeme vijijini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) shilingi trilioni 1.02;

  1. Ujenzi na ukarabati wa Reli ikiwemo ujenzi wa Reli kwa Kiwango cha Kimataifa shilingi trilioni 1.49;
  2. Ujenzi wa barabara, madaraja, na viwanja vya ndege shilingi trilioni 1.15;
  3. Ulipaji wa madeni yaliyohakikiwa ya Watumishi, Wazabuni na Watoa Huduma, Wakandarasi na Washauri Elekezi shilingi bilioni 965.1;
  4. Mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, elimumsingi bila ada, uimarishaji wa vyuo vya VETA, kukuza ujuzi kwa vijana na ujenzi wa miundombinu ya elimu shilingi bilioni 406.6;
  5. Ununuzi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi pamoja na ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya afya shilingi bilioni 265.8; na
  6. Miradi ya maji mijini na vijijini shilingi bilioni 207.5.

SERA ZA BAJETI KWA MWAKA 2021/22

Shabaha za Uchumi Jumla

Mheshimiwa Spika, makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka 2021/22, yameandaliwa kwa kuzingatia misingi (assumptions) pamoja na shabaha mahsusi za uchumi jumla. Malengo na shabaha za uchumi jumla ni kama ifuatavyo:

  1. Kuongeza kasi ya ukuaji wa Pato Halisi la Taifa kufikia asilimia 5.6 mwaka 2021 na kuendelea kukua kwa wastani wa asilimia 6.2 ifikapo mwaka 2023;
  2. Kuendelea kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei na kuhakikisha kuwa unabaki kwenye wigo wa tarakimu moja kati ya wastani wa asilimia 3.0 – 5.0 kwa mwaka 2021/22;
  3. Mapato ya ndani (ikijumuisha mapato ya Halmashauri) kufikia asilimia 15.9 ya Pato la Taifa mwaka 2021/22;
  4. Mapato ya kodi kufikia asilimia 13.5 ya Pato la Taifa mwaka 2021/22 kutoka matarajio ya asilimia 12.9 mwaka 2020/21;
  5. Kuhakikisha kuwa nakisi ya bajeti (ikijumuisha misaada) haizidi asilimia 3.0 kuendana na makubaliano ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki;
  6. Kuwa na akiba ya fedha za kigeni kwa kiwango cha kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne (4.0); na
  7. Kuhakikisha kuwa viashiria vya ustawi wa jamii vinaimarika.
Maeneo ya Kipaumbele kwa Mwaka 2021/22

Mheshimiwa Spika, Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2021/22 ni ya kwanza katika utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26 wenye dhima ya

Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu
. Bajeti hii itajielekeza katika utekelezaji wa vipaumbele vilivyoainishwa katika maeneo matano (5) ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2021/22. Maeneo hayo ni: Kuchochea uchumi shindani na shirikishi; kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma ili kuongeza thamani ya mazao ya kilimo; kukuza uwekezaji na biashara; kuchochea maendeleo ya watu; na kuendeleza rasilimali watu.

Mheshimiwa Spika, ili kuwa na uchumi shindani na shirikishi, Serikali itajielekeza katika kugharamia miradi ambayo itajikita katika: Kujenga jamii yenye uwezo wa kushindana kikanda na kimataifa; kusimamia utulivu wa viashiria vya uchumi jumla; kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji; kuchochea uvumbuzi na uhawilishaji wa teknolojia kutoka nje; na kuendeleza miundombinu na huduma za reli, barabara za kufungua fursa za kiuchumi, kuunganisha nchi jirani, kupunguza msongamano mijini na barabara za vijijini, madaraja, usafiri wa majini na angani, mageuzi ya TEHAMA pamoja na kutekeleza mradi wa Tanzania ya Kidijitali, nishati, bandari na viwanja vya ndege. Eneo hili limetengewa jumla ya shilingi trilioni 7.44 ikijumuisha shilingi trilioni 3.13 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kielelezo.

Mheshimiwa Spika
, miradi mingine ya kielelezo itakayotekelezwa ni: Kuboresha Shirika la Ndege Tanzania (ATCL); Makaa ya Mawe - Mchuchuma na Chuma – Liganga ikijumuisha ujenzi wa reli ya kiwango cha Kimataifa (Standard Gauge Railway) kutoka Mtwara hadi Mbamba Bay na matawi ya Mchuchuma na Liganga; Bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima (Uganda) hadi Tanga (Tanzania); Mradi wa Kuchakata Gesi Asilia kuwa Kimiminika (LNG) – Lindi; Mradi wa Kufua Umeme wa Maji - Ruhudji MW 358; Mradi wa Kufua Umeme wa Maji - Rumakali MW 222; Uchimbaji wa madini ya Nickel; Ujenzi wa Madaraja Makubwa na Barabara za Juu za Daraja la Kigongo - Busisi (Mwanza), Tanzanite (Dar es Salaam) na Interchange ya Kamata (Dar es Salaam); Bandari ya Uvuvi (Mbegani) na Ununuzi wa Meli za Uvuvi; Kiwanda cha Sukari Mkulazi; Utafutaji wa mafuta katika vitalu vya Eyasi Wembere na Mnazi Bay North; Mradi wa Magadi Soda – Engaruka; Kuongeza Rasilimali Watu yenye Ujuzi Adimu na Maalumu (Ujuzi wa Kati na Wabobezi) kwa Maendeleo ya Viwanda na Ustawi wa Jamii; na kuendeleza Kanda Maalumu za Kiuchumi.

Mheshimiwa Spika, ili kuchochea maendeleo ya watu, miradi itakayotekelezwa italenga kuboresha maisha ya watu kwa kuimarisha upatikanaji wa huduma za jamii ikiwemo elimu na mafunzo kwa ujumla, afya na ustawi wa jamii, huduma za maji na usafi wa mazingira na kinga ya jamii ikijumuisha Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kupitia TASAF. Aidha, Serikali itaendelea kupanga, kupima na kumilikisha ardhi mijini na vijijini, kusimamia na kuendeleza rasilimali za maji; na kuendelea na utekelezaji wa programu za kulinda mazingira na kuhimili mabadiliko ya tabianchi. Jumla ya shilingi trilioni 4.43 zimetengwa.

Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kuendeleza rasilimali watu, Serikali itagharamia programu inayolenga kuendeleza maarifa na ujuzi wa rasimali watu katika ngazi zote za elimu ikiwemo kuweka mazingira wezeshi kwa vijana kujiajiri. Aidha, Serikali itaendelea kuboresha viwango vya utoaji wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi pamoja na ujuzi adimu kwa lengo la kuongeza tija na ushindani wa wananchi katika kutumia rasimali zilizopo nchini ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Jumla ya shilingi bilioni 50.5 zimetengwa.

Mheshimiwa Spika, pamoja na miradi ya kielelezo, Serikali itatekeleza miradi mingine ya uboreshaji wa miundombinu ambayo itagharamiwa na mikopo yenye masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia. Miradi hiyo ni Mradi wa Kuendeleza Jiji la Dar es Salaam Awamu ya Pili (DMDP II) wa kukabiliana na mafuriko kwenye Bonde la Mto Msimbazi utakaogharimu dola za Marekani milioni 120. Mradi huu utahusisha ujenzi wa daraja katika eneo la Jangwani, na upanuzi na ujenzi wa kingo za mto Msimbazi. Mradi wa pili unahusisha uboreshaji wa barabara za kukuza fursa shirikishi za kijamii na kiuchumi ambapo Benki ya Dunia itatoa dola za Marekani milioni 300 na mchango wa Serikali ni dola za Marekani milioni 50. Mradi huu unalenga kuboresha barabara za vijijini katika maeneo yenye tija kubwa ya uzalishaji wa mazao ya kilimo.



Maeneo Mengine Muhimu

Maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi Mwaka 2022

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inajiandaa kufanya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu SURA 351. Kama mojawapo ya maandalizi ya utekelezaji wa Sensa ya Mwaka 2022 Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa upande wa Tanzania Bara na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Zanzibar imekamilisha kuandaa Kitabu cha Mkakati wa Usimamizi na Utekelezaji wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka, 2022. Kitabu hiki kinaainisha namna ya usimamizi na utekelezaji wa zoezi zima la Sensa, gharama ya kufanya Sensa pamoja na muundo wa Sensa utakavyokuwa katika ngazi zote za kiutawala.

Mheshimiwa Spika,
jumla ya shilingi bilioni 328.2 zinatarajiwa kutumika kugharamia sensa ya mwaka 2022. Kwa mara ya kwanza katika historia ya Sensa nchini, Sensa ya Mwaka 2022 itatumia teknolojia ya vishikwambi (tablets) katika utengaji wa maeneo ya kijiografia na ukusanyaji wa takwimu uwandani. Matumizi ya teknolojia hii yana manufaa makubwa, hasa katika kupunguza gharama na muda wa kukusanya na kuchakata takwimu, hali inayowezesha kutoa matokeo ya Sensa ndani ya muda mfupi.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ni jukumu la kila mtu, natoa wito kwa kamati zote za Sensa, Wakuu wa Mikoa na Wilaya zote, Waheshimiwa Wabunge pamoja na wananchi wote kwa ujumla kuhakikisha wanatoa ushirikiano wa kutosha katika maandalizi ya Sensa na wajitokeze wote siku ya kuhesabu watu. Lengo ni kuhakikisha Watu waliolala nchini usiku wa kuamkia siku ya Sensa (usiku wa sensa) wanahesabiwa na kuchukuliwa taarifa zao za kiuchumi, kijamii, mazingira na makazi wanayoishi na mengine mengi kwa ajili ya kupanga mipango endelevu ya maendeleo ya wananchi.


Maslahi ya Wafanyakazi

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua na kuthamini mchango wa watumishi wa umma na wa sekta binafsi katika kukuza Pato la Taifa. Kwa kutambua hilo, Serikali itachukua hatua mbalimbali za kuboresha maslahi ya wafanyakazi kama ifuatavyo:

Kupunguza kiwango cha chini cha kutoza kodi ya mapato ya ajira (PAYE) kutoka asilimia 9 hadi asilimia 8. Hatua hii ni mwendelezo wa juhudi za Serikali za kupunguza mzigo wa kodi kwa wafanyakazi, ambapo kiwango hicho kimepunguzwa kutoka asilimia 11 mwaka 2015/16 hadi asilimia 8 itakayoanza kutekezwa mwaka 2021/22;

Kufuta tozo ya asilimia 6 iliyokuwa ikitozwa kwa ajili ya kulinda thamani ya mkopo wa elimu ya juu (Value Retention Fee) kwa wanufaika; na Kutenga jumla ya shilingi bilioni 449 kwa ajili ya kuwapandisha vyeo watumishi 92,619.


Maslahi ya Madiwani, Maafisa Tarafa na Watendaji wa Kata

Mheshimiwa Spika, Madiwani wenzetu wanafanya kazi nzuri sana za kusimamia shughuli za maendeleo kwenye kata zetu. Hawa ni wabunge wakaazi wa kwenye kata zetu ambao kila siku wako na wananchi wetu kwenye kusimamia shughuli za maendeleo. Hata hivyo, katika baadhi ya halmashauri madiwani wamekuwa wakikopwa posho zao, na wengine hufikia hatua ya kupiga magoti kwa wakurugenzi watendaji ili walipwe. Hali hii imekuwa ikipunguza ufanisi katika halmashauri zetu kwa madiwani wengi kufanya maamuzi yanayopendekezwa na wakurugenzi watendaji hata kama hayana maslahi kwa Taifa ili waweze kulipwa posho zao. Jambo hili limeongelewa kwa hisia kali sana na Waheshimiwa Wabunge hapa bungeni. Waheshimiwa Wabunge na Waheshimiwa Madiwani, napenda niwaeleze kuwa MAMA YETU amesikia kilio chenu na alinielekeza mimi pamoja na Waziri wa TAMISEMI kulitafutia ufumbuzi suala hili.

Mheshimiwa Spika,
napendekeza kuanzia mwaka 2021/22, Serikali Kuu ianze kulipa posho za kila mwezi za Waheshimiwa Madiwani moja kwa moja tena kwenye akaunti zao kwa Halmashauri zote zenye uwezo mdogo kimapato. Halmashauri 16 zenye uwezo mkubwa wa kimapato (Daraja A) zitaendelea kutumia mapato yake ya ndani kulipa posho za Madiwani kupitia kwenye akaunti zao.

Mheshimiwa Spika,
Maafisa Tarafa ni viunganishi muhimu wa ngazi za kata na Wilaya zetu ambapo wengi wao hufanya kazi nzuri sana ya kusimamia utekelezaji wa maelekezo ya Serikali katika maeneo yao. Kwa kutambua umuhimu wao, Serikali ya CCM iliwapatia pikipiki viongozi hawa ili waweze kufanya kazi zao vizuri.


Hata hivyo, wengi wao wanashindwa kugharamia ununuzi wa mafuta na matengenezo ya vitendea kazi hivi na kulazimika kuwachangisha wananchi na hata wengine kuomba msaada kwa wadau mbalimbali. Hali hii inapunguza sana ufanisi katika Tarafa zetu. Kupitia hotuba hii, napenda niwajulishe Maafisa Tarafa wote nchini kuwa MAMA YETU amesikia kilio chenu. Hivyo, napendekeza kuanzia mwaka 2021/22, Serikali Kuu ianze kulipa posho ya shilingi 100,000/= kwa mwezi kwa kila Afisa Tarafa ili waweze kumudu gharama za mafuta na matengenezo ya pikipiki.

Mheshimiwa Spika, Watendaji Kata ndio wasimamizi wa kazi za sekta zote na ni watendaji wakuu kwenye kata. Wengi wao wanafanya kazi katika mazingira magumu ili kufanikisha shughuli za maendeleo katika kata zetu ikiwemo kusimamia ukusanyaji wa mapato na masuala ya usalama. Idadi kubwa ya watendaji hawa hutumia mishahara yao kufanya kazi mbalimbali ikiwemo ufutiliaji wa mapato ya Serikali kwa kukodi pikipiki ili kufanikisha shughuli zilizopo. Kwa ujumla wanafanya kazi nzuri sana ya kusimamia shughuli za maendeleo kwenye kata zetu. Jambo hili limeongelewa kwa hisia kali sana na Mheshimiwa Rose Busiga, Mbunge wa Viti Maalum (Geita), ambaye ni mtendaji wa kata mstaafu na kuungwa mkono na wabunge wengi hapa bungeni. Waheshimiwa wabunge, MAMA YETU amesikia kilio hiki na kutuelekeza kulitafutia ufumbuzi suala hili. Hivyo, napendekeza kuanzia mwaka 2021/22, Serikali kuanza kulipa posho ya shilingi 100,000/= kwa mwezi kwa kila Mtendaji Kata kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri yaliyokuwa yakitumika kulipa madiwani.

Madeni ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii

Mheshimiwa Spika, wastaafu wetu walilitumikia Taifa hili kwa uzalendo, uadilifu na bidii kubwa sana. Hatuwezi kuhesabu mafanikio ya nchi yetu bila kutaja mchango wa wazee hawa. Kumekuwepo na changamoto za muda mrefu za ulipaji wa mafao yao kutokana na ufanisi mdogo wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii katika kuhudumia wastaafu wetu. Hali hiyo kwenye mifuko yetu imechangiwa, pamoja na mambo mengine, na uwepo wa madeni ambayo mifuko inaidai Serikali na hivyo kusababisha wastaafu wetu kukosa au kusubiri kwa muda mrefu ili kulipwa mafao yao. Jambo hili pia limejadiliwa kwa hisia kali na Waheshimiwa Wabunge hapa bungeni. Wazee wetu hawa hupata shida sana, ambapo baadhi yao hufadhiliwa malazi kwa kulala misikitini na makanisani na wengine hutegemea wahisani kuhudumia familia zao kinyume na mchango walioutoa katika ujenzi wa nchi hii. MAMA YETU amesikia kilio cha wazee hawa na kutuelekeza Wizara ya Fedha na Mipango kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu kukamilisha zoezi la kitaalamu ili kujua hali halisi ya madeni na namna bora ya kulipa madeni hayo.

Mheshimiwa Spika, napendekeza kulipa madeni yanayodaiwa na mifuko kwa kutenga fedha kwenye bajeti na kutumia utaratibu wa kutoa hatifungani maalum isiyo taslimu (Non-cash Special Bond) zitakazoiva kwa nyakati tofauti kuanzia miaka miwili hadi 25. Utaratibu wa hatifungani una faida mbalimbali zikiwemo: kuipa Serikali nafasi ya kibajeti ya kuendelea kutekeleza miradi mingine ya maendeleo; kuiwezesha Serikali kuyatambua madeni hayo kwenye kanzidata ya madeni; na kuzuia madeni hayo kuendelea kuongezeka kulingana na tathmini ya thamani ya madai (actuarial valuation). Aidha, utaratibu huo utaboresha mizania ya hesabu na mtiririko wa mapato yanayotokana na riba ya hatifungani hizo kwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Hatua hii inakwenda kumaliza kabisa tatizo hilo la wazee wetu kudai haki yao kwa damu na machozi yaliyodumu kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Spika
, Serikali imepokea malalamiko kuhusu kucheleweshwa kwa michango ya watumishi kupelekwa kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii na baadhi ya ofisi za Serikali kutopeleka kabisa michango hiyo. Jambo hili limekuwa likisababisha usumbufu kwa watumishi punde wanapostaafu. Hivyo, napendekeza kulipa michango hiyo moja kwa moja kutokea Hazina kwa taasisi zote ambazo watumishi wanalipwa na Hazina. Taasisi ambazo zinalipa watumishi kutokana na vyanzo vyao vya mapato zitaendelea kupeleka michango ya watumishi wao kwa ufuatiliaji wa karibu wa Serikali. Serikali itafanya uhakiki na kulipa madeni ya michango ambayo haijawasilishwa kwenye mifuko hadi sasa.


Jeshi la Polisi

Mheshimiwa Spika, katika jeshi la polisi kwa askari wapiganaji, kuna utaratibu wa wapiganaji kufanya kazi kwa mikataba ya muda mfupi kwa miaka 12 kabla hawajapata ajira za kudumu. Jambo hili huwasababishia wapatapo mkataba wa kudumu wawe wamechelewa kwa miaka 12 ikilinganishwa na mtumishi mwingine aliyeingia pamoja kazini katika idara nyingine. Jambo hili linamadhara hasi katika itifaki ya utumishi na mafao ya mpiganaji anapostaafu. Hiki kimekuwa kilio cha muda mrefu cha askari wa Jeshi la Polisi. Kutokana na changamoto hiyo, MAMA YETU amesikia kilio cha askari hao na alituelekeza tukae na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ili kutafuta suluhisho la jambo hili. Napendekeza kuanzia mwaka 2021/22 askari wa Jeshi la Polisi wataingia mkataba wa kipindi cha miaka 6 na kuingia katika ajira ya kudumu.

Kodi ya Majengo

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na changamoto kubwa katika ukusanyaji wa kodi ya majengo, hali iliyosababisha Serikali kubadili njia za ukusanyaji mara kwa mara. Kabla ya mwaka 2017/18, Serikali za Mitaa zilikuwa na jukumu la kukusanya mapato hayo lakini hazikufanya vizuri. Kuanzia mwaka 2017/18, Serikali ilitumia Mamlaka ya Mapato kukusanya kodi hiyo, ambapo pia haikufanya vizuri. Ukusanyaji wa kodi hii kwa kutumia Serikali za Mitaa au TRA umekuwa ukitumia njia za kizamani ambazo zinahusisha watu kusafiri, kupanga foleni na kukusanya fedha taslimu (cash). Utaratibu huu unatumia gharama kubwa, muda na ni hatarishi kwa mapato. Katika kuhakikisha kodi hii inafikia malengo, Serikali imeandaa utaratibu mzuri wa kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa kodi ya majengo.

Kodi ya Wajasiliamali

Mheshimiwa Spika, wafanyabiashara na watoa huduma wadogo nchini wameendelea kutambulika kupitia vitambulisho vya wajasiriamali. Tangu kuanza kwa zoezi la utoaji wa vitambulisho vya wafanyabiashara na watoa huduma wadogo nchini, jumla ya vitambulisho 2,335,711 vimegawiwa ambavyo vimewezesha kukusanya jumla ya shilingi bilioni 46.71. Lengo ni kuendelea kuwatambua wafanyabiashara wadogo na kuwawekea mazingira rafiki ya ufanyaji biashara. Katika mwaka 2020/21, Serikali imefanya maboresho ya vitambulisho hivyo kwa kuweka picha na jina la mjasiriamali ili kuongeza udhibiti na kufungua fursa kwa wajasiriamali kuweza kutumia vitambulisho hivyo kupata huduma za kibenki na bima ya afya. Ofisi ya Rais TAMISEMI itaendelea na uratibu wa kugawa vitambulisho hivi kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania ambayo ndiyo yenye mfumo wa kusajili wafanyabiashara hao, kuchapisha vitambulisho na kuwapatia Halmashauri husika kwa ajili ya kugawa.

A. Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA 148

Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA 148 kama ifuatavyo:

Kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye vyumba vya ubaridi (cold rooms) vinavyotambuliwa kwa H.S Code 9406.10.10 na 9406.9010. Lengo la msamaha huu ni kuwapunguzia gharama wazalishaji wa mbogamboga na maua nchini ili kuchochea kilimo cha kisasa;

Kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye madini (precious metals) na makinikia yatakayoingizwa nchini kwa ajili ya kuchenjuliwa, kuongezewa thamani na kuuzwa kwenye masoko ya madini yanayotambulika nchini. Lengo la pendekezo hili ni kuviwezesha viwanda vya uchenjuaji vilivyoanzishwa nchini kupata malighafi ya kutosha kwa ajili ya uchakataji na hatimaye kuongeza ajira na mapato ya Serikali;

Kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye huduma za bima ya mifugo. Lengo la marekebisho haya ni kuchochea shughuli za ufugaji nchini;

Kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye bidhaa na huduma zitakazoingizwa au kununuliwa hapa nchini kwa ajili ya kutekeleza mradi wa mafuta ghafi (EACOP). Lengo la marekebisho haya ni kutoa unafuu wa kodi katika utekelezaji wa miradi tajwa;

Kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye mafuta ghafi yanayotambulika kwa H.S Code 2709.00.00 kwa lengo la kutoa unafuu kwa mlaji ikiwemo Kampuni ya uendeshaji wa bomba la mafuta (EACOP);

Kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye Nyasi Bandia zinazotambulika kwa HS Code 5703.30.00 na 5703.20.00 kwa ajili ya Viwanja vya Mpira vilivyoko kwenye Majiji. Msamaha huo utahusisha ridhaa kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania. Lengo la hatua hii ni kuendeleza michezo na kukuza vipaji nchini;

Kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye kadi za kutengeneza vitambulisho vya taifa zinazotambulika kwa H.S Code 3921.11.90.00 na malighafi nyingine za kutengeneza kadi hizo zinazotambulika kwa H.S Code 3921.11.90.00 zitakazoingizwa nchini na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA). Lengo la pendekezo hili ni kupunguza gharama za kutengeneza Vitambulisho vya Taifa na kuharakisha upatikanaji wake;

Kumekwepo na ukiritimba katika kupokea fedha za misaada kwenye miradi ya maendeleo kwa hitaji la kisheria la kusubiri idhini ya Baraza la Mawaziri likae ili kuidhinisha misamaha. Napendekeza Kutoa msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa Taasisi zisizo za kiserikali (NGO’s), kwenye bidhaa na huduma zitakazotumika kwenye miradi inayotekelezwa na taasisi husika. Aidha, taasisi zitakazonufaika na msamaha huo ni zile ambazo zina mikataba na Serikali yenye kipengele kinachotoa msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani;

Sekta ya mawasiliano imekuwa ikikua vizuri na kuwa kiungo muhimu cha kuongeza wigo wa wananchi ambao wako kwenye ulimwengu wa kidijitali na kwenye sekta ya fedha (Financial

Inclusion).
Napendekeza kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye simu janja za mkononi (smart phones) HS Code 8517.12.00, vishikwambi (Tablets) HS Code 8471.30.00 au 8517.12.00 na modemu (modems) HS Code 8517.62.00 au 8517.69.00. Lengo la hatua hii ni kuhamasisha matumizi ya huduma za mawasiliano ili kufikia lengo la asilimia 80 ya watumiaji wa intaneti ifikapo mwaka 2025 kutoka asilimia 46 iliyopo sasa;

Kufuta msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye mikebe inayotumika kuhifadhia maziwa inayotambuliwa kwa H.S Code 7310.29.20 ambayo kwa sasa haitumiki kwa ajili ya kazi hiyo na badala yake napendekeza kutoa msamaha wa kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye mikebe ya kubebea maziwa inayotambulika kwa H.S Code 7310.29.90, 7310.10.00 na 7612.90.90. Lengo la Pendekezo hili ni kuwapunguzia gharama wazalishaji na kuchochea ukuaji wa sekta ya maziwa nchini;

Kufuta msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye taa zinazotumia umeme wa jua zinazotambulika kwa H.S. Code 85.13 na 94.05. Lengo la pendekezo hili ni kuwianisha msamaha huu sambamba na msamaha unaotolewa chini ya Sheria ya Ushuru wa Forodha ambayo inasamehe Kodi kwenye vifaa vinavyotumika kuzalisha nishati ya umeme wa jua pekee na kurahisisha usimamizi wake. Aidha, pendekezo hili linalenga kuweka usawa katika ulipaji kodi kwa watumiaji wa taa zinazotumia nishati za aina zote;

Kutoza Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa kiwango cha asilimia sifuri kwenye huduma ya usafirishaji na huduma zinazohusiana na usafirishaji wa mafuta ghafi kupitia bomba linalojengwa kwa pamoja baina ya Serikali ya Tanzania na Uganda (EACOP). Lengo la pendekezo hili ni kuwezesha huduma tajwa kutekelezwa bila kodi sanjari na uzoefu wa kimataifa kwa bidhaa zilizopita hapa kwenda nchi jirani au ng’ambo;

Kuzitambua bidhaa za mtaji zilizomo kwenye Sura ya 84, 85 na 90 ya Kitabu cha Ushuru wa Pamoja wa Forodha wa Afrika Mashariki kuwa bidhaa za mtaji zitakazostahili kupata kivutio cha ahirisho la malipo ya VAT. Lengo la pendekezo hili ni kuwianisha maana ya bidhaa za mtaji kwenye Sheria za kodi na kuziba mianya ya upotevu wa mapato ya Serikali kwenye kifungu tajwa;

Kubadilisha utaratibu wa kutoa msamaha kwenye miradi ya Serikali inayogharamiwa na fedha za serikali na fedha za wafadhili ambapo mnufaika wa msamaha huo atawasilisha maombi kwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania badala ya utaratibu wa kuwasilisha kwa Waziri wa Fedha kwa ajili ya kupata ridhaa na kutoa Tangazo la Serikali (GN) kwa kila mradi. Utaratibu huu utarahisisha na kuharakisha utoaji wa misamaha badala ya utaratibu wa sasa kutokana na TRA kuwa na ofisi kwa kila mkoa nchini kote ambazo zinaweza kupokea, kuchambua na kusimamia matumizi sahihi ya misamaha; na

Kuhusu Zanzibar, napendekeza kufanya marekebisho ya Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani ili kurudisha utaratibu wa kurejesha VAT kwa bidhaa zinazonunuliwa Tanzania Bara na kutumika Tanzania Zanzibar. Hii inatokana na mfumo wa kutoza VAT kwa kiwango cha asilimia sifuri kwa bidhaa za viwandani pekee kutowanufaisha wafanyabiashara wa Zanzibar wanaonunua bidhaa na kutozwa VAT Tanzania Bara na kutozwa tena VAT bidhaa hizo zinapopelekwa Zanzibar. Aidha, inapendekezwa marejesho ya VAT yatakayofanyika kwa bidhaa zinazotoka Tanzania Bara kwenda Zanzibar yafanyike pia kwa bidhaa zitakazotoka Zanzibar kwenda Tanzania Bara sambamba na marekebisho ya vifungu husika vya Sheria za VAT kwa pande zote mbili za muungano. Ili kuwa na ufanisi wa marejesho, maboresho ya mifumo yatafanyika ili isomane baina ya Tanzania Bara na Zanzibar. Kutokana na utaratibu huu, kiwango cha asilimia sifuri ya Kodi ya Ongezeko la Thamani kilichokuwa kinatozwa bidhaa hizo kitasitishwa.

Hatua zote za Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa ujumla zinatarajiwa kupunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 55,499.97.


Sheria ya Ushuru wa Bidhaa

Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa kifungu cha 124(2) cha Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, marekebisho ya viwango maalumu vya ushuru wa bidhaa (specific duty rates) kwa bidhaa zote zisizo za petroli yanaweza kufanyika kila mwaka ili kuvihuisha na mfumuko wa bei na viashiria vingine vya uchumi jumla. Hata hivyo, kutokana na biashara za bidhaa hizi kuzorota kutokana na athari za kiuchumi zilizosababishwa na ugonjwa wa UVIKO-19, napendekeza kutofanya mabadiliko ya viwango maalumu vya ushuru wa bidhaa kwa bidhaa zote zisizo za petroli isipokuwa vinywaji vikali na bia zitakazotengenezwa kwa kutumia shayiri iliyozalishwa hapa nchini.

Mheshimiwa Spika,
napendekeza pia kufanya marekebisho ya Ushuru wa bidhaa kwenye bidhaa zifuatazo:

Kupunguza Ushuru wa Bidhaa kwenye bia zinazotengenezwa kwa kutumia shayiri iliyozalishwa hapa nchini kutoka shilingi 765 kwa lita za sasa hadi shilingi 620 kwa lita. Lengo la mapendekezo haya ni kuchochea kilimo cha shayiri hapa nchini;

Kuanza kutoza Ushuru wa bidhaa wa asilimia 10 kwenye nyuzi na kamba za plastiki (synthetic fibres) zinazoingizwa kutoka nje ya nchi au kuzalishwa hapa nchini zinazotambuliwa kwa heading 55.11 na 56.07 isipokuwa zile zinazotumika kwenye Uvuvi (HS Code 5607.50.00). Lengo la marekebisho haya ni kulinda mazingira na kuchochea uzalishaji na matumizi ya bidhaa za katani. Hatua hii inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa shilingi milioni 2,644; na

Kuanzisha tozo ya ushuru wa bidhaa kwa kiwango cha asilimia 10 kwenye pikipiki zilizotumika kwa zaidi ya miaka 3 zinazoingizwa nchini zinazotambuliwa kwa HS Code 8711. Lengo la marekebisho haya ni kudhibiti uingizaji wa pikipiki chakavu na kulinda mazingira. Hatua hii inatarajiwa kuongeza ya mapato ya Serikali kwa shilingi milioni 263.7.

Hatua za kutoza Ushuru wa Bidhaa kwenye bidhaa zisizo za petroli kwa ujumla wake zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 2,907.7.


F. Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa

Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya Marekebisho kwenye Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa kama ifuatavyo:

Kubainisha mazingira ambayo Kampuni iliyolipa tozo ya huduma haitawajibika kulipa tozo ya uzalishaji. Marekebisho hayo yanalenga kutatua mgongano uliojitokeza kwenye kutafsiri kifungu husika; na

Kupunguza ada za matangazo kama ifuatavyo:

Mabango yanayowaka kutoka shilingi 18,000 hadi shilingi 13,000;

Mabango yasiyowaka kutoka shilingi 15,000 hadi shilingi 10,000;

Matangazo ya ukutani kutoka shilingi 15,000 hadi shilingi 10,000;

Matangazo ya kielectroniki kutoka shilingi 20,000 hadi shilingi 10,000;

Matangazo kwenye magari kutoka shilingi 15,000 hadi shillingi 10,000 kwa watangazaji wanaotangaza bidhaa za watu wengine;

Matangazo ya muda mfupi/promosheni kwa siku kutoka shilingi 55,000 hadi shilingi 50,000; na Kila mabango 100 ya promosheni ya kwanza au sehemu ya fungu la mabango 100 ya kwanza kutoka shilingi 100,000 hadi shilingi 50,000.

Ada zote hizi zinatozwa kwa futi za mraba. Kushushwa kwa ada hizi kutapunguza gharama za kutangaza biashara nchini na hatimaye kukuza ushindani kwenye biashara.


G. Sheria ya Kodi ya Majengo, SURA 289

Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya kodi ya majengo, SURA 289 ili ukusanyaji wa kodi ya majengo ufanyike kwa kutumia mfumo wa ununuzi na utumiaji wa umeme kupitia mashine za LUKU. Kila mita ya umeme ina uhusiano na mmiliki wa jengo au mtumiaji wa mita, na kwa kuwa Sheria ya Kodi ya Majengo inataka kodi hiyo ikusanywe kwa mmiliki au mtumiaji wa jengo, hivyo, napendekeza kodi ya majengo ya kiwango cha shilingi 1,000/= kwa mwezi kwenye nyumba za kawaida zenye mita moja na itakatwa kwenye ununuzi wa umeme (LUKU). Aidha, napendekeza kiwango cha shilingi 5,000/= kwa mwezi kwa kila ghorofa au apartment zenye mita moja na itakatwa kwenye ununuzi wa umeme (LUKU). Serikali itaweka utaratibu kwenye nyumba za kawaida na za ghorofa zinazochangia mita moja na zinazotumia mita zaidi ya moja.

H. Sheria ya Ardhi, SURA 113

Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho ya Sheria ya Ardhi, SURA ya 113 na Kanuni zake za mwaka 2001 kwa kupunguza tozo ya mbele (premium) inayotozwa wakati wa umilikishaji wa ardhi kama ifuatavyo:

Kupunguza tozo kutoka asilimia 2.5 hadi asilimia 0.5 kwa umiliki mpya wa ardhi; na Kupunguza tozo kutoka asilimia 1 hadi asilimia 0.5 kwa urasimishaji.

Lengo la pendekezo hili ni kuhamasisha wamiliki wa ardhi kukamilisha taratibu za kupata hatimiliki na kufanikisha sehemu kubwa ya ardhi kuandikishwa na kupunguza migogoro. Hatua za kufanya marekebisho ya Sheria ya Ardhi kwa ujumla wake zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 9,000.


I. Sheria ya Ushuru wa Stempu, SURA 189

Mheshimiwa Spika, napendekeza kuifanyia Marekebisho Sheria ya Ushuru wa Stempu kwa lengo la kuhuisha viwango vilivyopo sambamba na mfumuko wa bei kwa kuwa viwango hivyo ni vya muda mrefu tangu mwaka 2006. Marekebisho hayo ni kama ifuatavyo:

Ushuru wa Stempu kutoka shilingi 500 hadi shilingi 2,000;

Ushuru wa Stempu kwenye Katiba za Makampuni kutoka shilingi 5,000 hadi shilingi 10,000;

Ushuru wa Stempu kwenye nyaraka za Ubia ambazo mtaji wake unazidi shilingi 100,000 lakini hauzidi shilingi 1,000,000 kutoka shilingi 2,000 hadi shilingi 5,000;

Ushuru wa Stempu kwenye nyaraka za Ubia ambazo mtaji wake unazidi shilingi 1,000,000 kutoka shilingi 5,000 hadi shilingi 10,000; na

Ushuru wa Stempu kwenye nyaraka za kumaliza ubia kutoka shilingi 1,000 hadi 10,000.

Hatua za kufanya marekebisho ya Sheria ya Ushuru wa Stempu kwa ujumla wake zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 2,500.89.


K. Sheria ya Michezo ya Kubatisha, SURA 41

Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya mabadiliko ya Sheria ya Michezo ya Kubahatisha kama ifuatavyo:

(i) Kupunguza kiwango cha kodi kwenye zawadi ya ushindi (Gaming tax on Winnings) kutoka asilimia 20 hadi asilimia 15 kwenye Michezo ya kubahatisha ya ubashiri wa matokeo ya michezo (Sports betting);

Kuongeza kiwango cha Kodi katika michezo ya kubahatisha ya ubashiri wa matokeo ya michezo (sports betting) kwa mapato ghafi (Gross Gaming Revenue - GGR) kutoka asilimia 25 ya mauzo ghafi hadi asilimia 30 ya mauzo ghafi. Ongezeko la asilimia 5 litapelekwa kwenye Mfuko wa Maendeleo ya Michezo kwa ajili ya kuendeleza michezo nchini;

Kutoza kodi ya michezo ya kubahatisha kwa asilimia 10 ya mapato ghafi kwenye michezo ya kubahatisha inayoendeshwa kwa kompyuta (Virtual Games); na

Kutoza Kodi ya michezo ya kubahatisha kwa asilimia 10 ya mapato ghafi kwenye michezo ya kubahatisha iliyo chini ya majaribio.

Lengo la hatua hizi ni kuleta usawa wa utozaji kodi katika michezo ya kubahatisha. Hatua hizi za marekebisho ya michezo ya kubahatisha zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 14,925.38.


L. Sheria ya Ukaguzi wa Umma, SURA 418

Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya Marekebisho kwenye Sheria ya Ukaguzi wa Umma, SURA 418 kama ifuatavyo;

Kumwezesha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuwa na uwezo wa kisheria wa kukagua mashirika yaliyoanzishwa chini ya Sheria ya Makampuni ambayo Serikali ina umiliki wa hisa ili kumwezesha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu kukagua mashirika/makampuni hayo. Kwa sasa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali anakagua mashirika/makampuni hayo bila kuwa na nguvu za kisheria, hali inayoweza kuleta mgogoro wa kisheria; na

Kumwezesha Waziri mwenye dhamana ya Fedha kuwasilisha Bungeni majibu kuhusu taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwenye kikao kinachofuata cha Bunge baada ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuwasilisha taarifa yake badala ya utaratibu wa sasa ambapo taarifa zote huwasilishwa kwa pamoja katika kikao kimoja cha Bunge.


N. Sheria ya Usajili wa Magari, SURA 124

Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Usajili wa Magari SURA 124, kwa kupunguza ada ya usajili wa magari kwa namba binafsi kutoka shillingi 10,000,000 hadi shillingi 5,000,000 kila baada ya miaka mitatu. Lengo la hatua hii ni kuwezesha wamiliki wa magari kuchagua namba binafsi ya usajili wa gari kwa gharama nafuu na hivyo kuongeza mapato ya Serikali kwa kuwa kiwango cha sasa hakina mwitikio mzuri.

Hatua hizi za marekebisho ya Sheria ya Usajili wa Magari inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 270.


O. Sheria ya Usalama Barabarani, SURA 168

Mheshimiwa Spika, vijana wengi wamejiajiri kwenye sekta ndogo ya kuendesha bajaji na pikipiki zikijulikana kama bodaboda. Hata hivyo, Vijana hawa hupata usumbufu mkubwa wa kulipa faini kutoka kwenye vipato vyao pale panapotokea uvunjaji wa Sheria ya Usalama Barabarani umefanywa na abiria wao. Hali hii imekuwa ikisababisha baadhi yao kushindwa kulipa faini na hivyo kuzitelekeza pikipiki zao kwenye vituo vya polisi. Mheshimiwa Rais alielekeza jeshi la Polisi kujikita kwenye kutoa elimu kuhusu usalama barabarani badala ya kuwekeza kwenye makosa na kugeuza faini kuwa chanzo cha mapato. Hivyo basi, napendekeza kupunguza adhabu zinazotolewa chini ya Sheria ya Usalama Barabarani SURA
kwa makosa ya Pikipiki na Bajaji kutoka shilingi 30,000 za sasa hadi shilingi 10,000 kwa kosa moja. Lengo la hatua hii ni kuweka adhabu kwa kuzingatia uwezo wa kulipa. Aidha, adhabu kwa makosa mengine ya vyombo vya moto zinazotolewa kwa mujibu wa Sheria zinaendelea kubaki kama ilivyo sasa.


P. Sheria ya Raia wa Kigeni (Uratibu wa Ajira), Na. 1 ya mwaka 2015

Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho ya Sheria ya Raia wa Kigeni (Uratibu wa Ajira), Na. 1 ya 2015 kama ifuatavyo:

Kuweka adhabu ya kiasi cha shilingi 500,000/= kwa kila mwezi kwa mwajiri aliyeajiri raia wa kigeni na kushindwa kuwasilisha ritani za kila mwezi zenye taarifa za raia wa kigeni aliowaajiri ikiwemo taarifa zao za mishahara kwa Kamishna wa Kazi. Lengo la pendekezo hili ni kuhimiza uwajibikaji wa hiari;

Kuweka adhabu ya kifungo cha miezi 12 au faini ya shilingi millioni kumi (10) au vyote kwa mwajiri aliyeajiri raia wa kigeni na kushindwa kuwasilisha ritani za mwezi zenye taarifa za raia wa kigeni aliowaajiri ikiwemo taarifa zao za mishahara kwa Kamisha wa kazi. Lengo la pendekezo hili ni kuhimiza uwajibikaji wa hiari.


x. Utoaji Leseni za Bima kwa Makampuni

Napendekeza kubadili utaratibu wa sasa wa makampuni ya bima kulazimika kuomba leseni upya kila mwaka na badala yake makampuni yanayofanya vizuri yawe na leseni ya kudumu, na makampuni yalioko kwenye hali ya uangalizi yapewe leseni na miaka mitatu huku yakiwa kwenye uangalizi na yakiimarika na kufanya vizuri yaingie kwenye leseni za kudumu. Taratibu za ufuatiliaji na malipo ya kila mwaka yaendelee kama ilivyo sasa. Lengo ni kupunguza ukiritimba.

Maeneo Mahususi

Barabara za Mijini na Vijijini

Mheshimiwa Spika, hali ya barabara vijijini hairidhishi ambapo bado vipo vijiji ambavyo havina barabara kabisa. Barabara nyingi zinazosimamiwa na TARURA zina hali mbaya. Kwa sasa mtandao wa barabara zilizo chini ya TARURA una urefu usiopungua kilomita 108,946.2 ambazo zinaunganisha maeneo mbalimbali ya mijini na vijijini. Hadi Desemba 2020, mtandao wa barabara zilizo chini ya TARURA wenye kiwango cha lami ulifikia kilometa 2,250.69, sawa na asilimia 2.1 tu, changarawe kilometa 27,809.26 (asilimia 25.6) na udongo kilometa 78,886.25 (asilimia 72.4).

Mheshimiwa Spika,
hali hii ya barabara ina madhara makubwa sana kwa jamii yetu kwani baadhi ya akina mama wajawazito wanapoteza maisha kwa kuchelewa kufika kwenye vituo vya afya. Aidha, wapo wengine ambao wanajifungulia njiani kutokana na kuchelewa kufika kwenye vituo vya afya. Vilevile, wapo baadhi ya wanafunzi wanaosombwa na maji na kufariki kutokana na ubovu wa miundombinu ya barabara, hususan katika maeneo ya vijijini. Kadhalika, bado kuna changamoto ya usafirishaji wa mazao na bidhaa kutoka au kwenda barabara kuu katika baadhi ya maeneo. Serikali imeona ipo haja ya kutafuta vyanzo vipya vya mapato kuongezea katika mgawo wa sasa kupitia Mfuko wa Barabara ili kufanikisha ugharamiaji wa mtandao wa barabara hizo.


Upatikanaji wa Maji Safi na Salama Mijini na Vijijini

Mheshimiwa Spika, hali ya upatikanaji wa maji safi na salama mijini na vijijini bado hairidhishi. Maji hayana mbadala, maji ni uhai, maji ni maisha kwa viumbe hai vyote. Bado vipo vijiji ambavyo havina kisima hata kimoja cha maji safi na salama na badala yake hutumia maji ya mapalio, maji ya madimbwi, maji ya mito wanayochangia na wanyama. Tanzania ina vyanzo vikubwa na vya uhakika vya maji ikiwa ni pamoja na Ziwa Tanganyika, Ziwa Victoria, Ziwa Nyasa, Ziwa Rukwa, Ziwa Chala, Mto Kiwira, Ruvu, Rufiji na Ruvuma pamoja na mingine. Aidha, kuna uwezekano wa kutumia mabwawa makubwa kama ya Kidunda, Ndembela na Farkwa kama yangekamilika lakini utekelezaji wake haujaanza pamoja na fidia kutolewa na Serikali kutokana na uhaba wa fedha. Ipo miradi mingi katika mikoa ya Iringa, Kagera, Kigoma, Kilimanjaro, Lindi, Mara, Mbeya, Mtwara, Mwanza, Njombe, Rukwa, Ruvuma, Shinyanga, Simiyu, Singida, Songwe, Tabora, Tanga na Simiyu inayotakiwa kutekelezwa katika mwaka 2021/22, lakini haikuwa katika bajeti. Mikoa mingine ambayo sikuitaja hapa iko kwenye bajeti ya Wizara husika.

Mheshimiwa Spika, hali ya ukosefu wa maji safi na salama ina madhara makubwa sana kwa jamii yetu. Serikali imedhamiria kuhakikisha kuwa inampa nafuu mwanamke katika kufanya shughuli zake za kiuchumi, lengo likiwa ni kumtua mama ndoo kichwani na kuondoa changamoto mbalimbali zinazowakumba akina mama na mabinti katika harakati za kutafuta maji. Aidha, kuna baadhi ya wanafunzi wanakosa masomo na kuharibu maisha yao kutokana na uhaba wa maji katika maeneo yao. Hivyo, Serikali imeona ipo haja ya kuongeza fedha za kugharamia miradi ya maji kwa kubuni vyanzo mbadala vya mapato kwa ajili ya kugharamia miradi ya maji hususan katika maeneo ambayo yana uhaba mkubwa wa maji.


Afya na Bima ya Afya kwa Wote

Mheshimiwa Spika, Sekta ya Afya ni sekta muhimu katika ustawi wa jamii yetu na ni moja ya mahitaji muhimu sana katika maisha ya sasa ya mwanadamu. Serikali ya CCM imefanya kazi kubwa sana katika sekta hii, ingawa bado kuna kazi kubwa ya kufanya kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu na mabadiliko ya hali za kiafya kwenye kizazi cha leo. Aidha, wananchi katika maeneo mbalimbali wametumia nguvu kubwa katika kutafuta ufumbuzi wa masuala ya upatikanaji wa huduma za afya kwa kujenga maboma karibu na maeneo yao. Majengo yaliojengwa kwa nguvu za wananchi yamekaa kwa muda mrefu, kati ya miaka mitano (5) hadi 15. Hadi kufikia Juni 2021, kuna jumla ya maboma 8,004 ya zahanati ambayo yapo katika mikoa mbalimbali nchini na yapo katika hatua mbalimbali za kukamilishwa. Vilevile, yapo maboma kwenye ngazi ya vituo vya afya zaidi ya 1,500 ambayo yametumia nguvu ya wananchi na yanahitaji kukamilishwa. Serikali itaendelea na jitihada za kutafuta fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa maboma hayo pamoja na kuajiri wataalamu wa afya na kuimarisha upatikanaji wa dawa, vitendanishi, vifaa na vifaa tiba.

Mheshimiwa Spika, kuna mradi mkubwa wa bima kwa wote (Universal Health Care) unaolenga kuwafikia watanzania wote. Tanzania ina jumla ya kaya milioni 12.827, ambapo asilimia 20 ya kaya hizo inakadiriwa kuwa ni kaya zisizokuwa na uwezo. Katika kufanikisha utekelezaji wa dhana ya bima ya afya kwa wananchi wote, Serikali itahitaji zaidi ya shilingi bilioni 149 katika mwaka wa kwanza kwa ajili ya kaya zisizo na uwezo. Kiasi hicho cha fedha kitaendelea kuongezwa kila mwaka ili ifikapo mwaka 2034/35, wananchi wote wawe wamefikiwa na bima ya afya. Serikali imeendelea kuboresha na kusogeza huduma za afya karibu na wananchi ambapo vituo vya kutolea huduma za afya kwa ngazi mbalimbali vimeendelea kujengwa ili bima ya Afya iweze kutumika na kuwanufaisha wananchi wote.


Elimu

Mheshimiwa Spika, kuhusu sekta ya elimu kuna kazi kubwa bado iko mbele yetu. Bado kuna shule ambazo zina wanafunzi wengi kuliko idadi ya madarasa na zipo zinazogawa mikondo ili wanafunzi wengine wasome asubuhi na wengine wasome mchana. Hali hii inapunguza muda wa wanafunzi kusoma. Zipo shule ambazo kwenye darasa moja wanaweka uzio wa ubao kutenganisha ili chumba kimoja wasome wanafunzi wa madaraja mawili. Aidha, zipo shule ambazo miundombinu yake imechakaa sana kiasi cha kutishia usalama wa watoto na walimu wetu. Yapo pia madarasa yaliyoezekwa kwa nyasi na yana sakafu ya vumbi. Kadhalika, mwaka ujao utakuwa wa kwanza wa kupokea wanafunzi kidato cha kwanza waliodahiliwa darasa la kwanza kwa mpango wa elimumsingi bila ada. Jambo hili lisipoangaliwa mapema litakuja kusababisha wanafunzi kuchaguliwa kujiunga kidato cha kwanza na kukosa pa kwenda hadi miundombinu ijengwe kwa zimamoto. Kwa hatua ya maendeleo nchi yetu iliyofikia katika sekta mbalimbali, hali hii haipendezi na haitakiwi kuendelea. Kujenga miundombinu ya shule zetu kwa kusubiri irushwe kwenye mitandao ya kijamii ndio tuone inatutia aibu, au kusubiri watoto wakose pa kwenda au wakose pa kukaa ndipo tukimbizane na kufukuzana, ni ishara ya kutopanga vizuri. Hili tusingependa liendelee kuwepo.

Mheshimiwa Spika, kila mwaka kuna wanafunzi kati ya asilimia 15 - 20 wanatoka kwenye mfumo wa elimu kwa kutoendelea na kidato cha kwanza kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo kupata ujauzito, utoro na hali ngumu ya maisha. Ukosefu wa mpango wa kugharamia mahitaji ya sekta ya elimu ndiyo chanzo cha tatizo hili.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa elimu ya juu, zaidi ya wanafunzi 11,000 wenye sifa za kujiunga na vyuo vikuu ambao tayari walishapata udahili katika vyuo mbalimbali walikosa mikopo. Naongelea mkopo, sio fedha ya bure, bali ni mkopo ambao ataurejesha. Katika jamii nyingi za kitanzania, mtoto akikosa mkopo huku akiwaona wenzake wanaendelea, inamfadhaisha sana. Ni mfadhaiko kwake na familia nzima. Kwa hatua ya maendeleo ambayo nchi yetu imepata katika sekta mbalimbali hali hii haipendezi na haitakiwi kuendelea. Serikali inakusudia kuchukua hatua za kuhakikisha kuwa inaongeza bajeti ya mikopo ya elimu ya juu ili kuwanufaisha vijana wote wenye sifa za kupata mkopo.


U. Tarehe ya Kuanza Kutekeleza Hatua Mpya za Kodi

Mheshimiwa Spika, hatua hizi za kikodi zinazopendekezwa zitaanza kutekelezwa tarehe 1 Julai, 2021, isipokuwa pale itakapoelezwa vinginevyo. Aidha, Marekebisho hayo yataainishwa katika Muswada wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2021 na Matangazo ya Serikali (Government Notices).

SURA YA BAJETI KWA MWAKA 2021/22

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia shabaha, malengo pamoja na sera za bajeti kwa mwaka 2021/22, Sura ya Bajeti inaonesha kuwa jumla ya shilingi trilioni 36.33 zinatarajiwa kukusanywa na kutumika. Mapato ya ndani yanatarajiwa kuwa shilingi trilioni 26.03, sawa na asilimia 71.7 ya bajeti yote. Kati ya mapato hayo, mapato ya kodi ni shilingi trilioni 22.18, sawa na asilimia 13.5 ya Pato la Taifa. Aidha, Serikali inalenga kukusanya mapato yasiyo ya kodi ya shilingi trilioni 2.99 na mapato kutoka vyanzo vya Halmashauri shilingi bilioni 863.9.

Mheshimiwa Spika
, Washirika wa Maendeleo wanatarajia kuchangia misaada na mikopo nafuu yenye jumla ya shilingi trilioni 2.96, sawa na asilimia 8.1 ya bajeti yote. Kiasi hicho kinajumuisha fedha za miradi ya maendeleo shilingi trilioni 2.67 na Mifuko ya Pamoja ya Kisekta shilingi bilioni 282.3. Napenda kuwashukuru Washirika wa Maendeleo kwa kuendelea kutoa fedha za misaada na mikopo nafuu ili kufanikisha miradi na programu mbalimbali za maendeleo zitakazotekelezwa katika bajeti ya mwaka 2021/22.

Mheshimiwa Spika,
kipekee ningependa kuwatambua Washirika wetu wa Maendeleo kama ifuatavyo: Serikali za Canada, China, Denmark, Finland, India, Ireland, Italia, Korea ya Kusini, Japan,Ufaransa, Ujerumani, Norway, Poland, Ubelgiji, Uholanzi, Uswisi, Uingereza, Sweden na Marekani. Vilevile, kuna Mashirika ya Kimataifa ambayo ni Benki ya Maendeleo ya Afrika, Benki ya Dunia, Benki ya Kiarabu kwa Maendeleo ya Kiuchumi katika Afrika, Mfuko wa Abu Dhabi, Mfuko wa Kuwait, Mfuko wa kimataifa wa kusaidia mapambano dhidi ya virusi vya Ukimwi, kifua kikuu na malaria, Umoja wa Ulaya, Benki ya Uwekezaji ya Ulaya, Umoja wa mataifa na mashirika yote yaliyopo chini yake, Mfuko wa OPEC kwa Maendeleo ya Kimataifa, Mfuko wa Mazingira, pamoja na Shirikisho la GAVI. Ninapenda pia kuyatambua Mashirika yasiyo ya Kiserikali ya ndani na nje pamoja na mashirika ya ufadhili - philanthropies kwa misaada yao kwenye sekta mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, Serikali inatarajia kukopa shilingi trilioni 7.34 kutoka soko la ndani na nje kwa masharti ya kibiashara. Kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni 4.99 ni mikopo ya ndani ambayo inajumuisha shilingi trilioni 3.15 kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za Serikali zinazoiva na shilingi trilioni 1.84 kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo. Aidha, shilingi trilioni 2.35 zinatarajiwa kukopwa kutoka soko la nje kwa lengo la kuongeza kasi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Spika
, kwa mwaka 2021/22, Serikali inapanga kutumia jumla ya shilingi trilioni 36.33 kwa matumizi ya kawaida na maendeleo. Kati ya fedha hizo, shilingi trilioni 23.0 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi trilioni 13.33 kwa ajili ya matumizi ya maendeleo. Fedha zilizotengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida zinajumuisha shilingi trilioni 10.66 kwa ajili ya ulipaji wa deni la Serikali, shilingi trilioni 8.15 kwa ajili ya mishahara na shilingi trilioni 4.19 kwa ajili ya matumizi mengineyo. Aidha, Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 200.0 kwa ajili ya kulipa madeni yaliyohakikiwa ya watumishi, wazabuni na watoa huduma.

Mheshimiwa Spika
, jumla ya shilingi trilioni 13.33 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya maendeleo, sawa na asilimia


ya bajeti yote. Kati ya kiasi hicho, fedha za ndani ni shilingi trilioni 10.37 na fedha za nje shilingi trilioni 2.96. Aidha, fedha za maendeleo zinajumuisha, shilingi trilioni 1.19 kwa ajili ya miradi ya reli ikiwemo ujenzi wa Reli ya Kati kwa Kiwango cha Kimataifa; shilingi trilioni 2.08 kwa ajili ya miradi ya barabara, ujenzi wa madaraja, na viwanja vya ndege; shilingi trilioni 2.34 kwa ajili ya miradi ya kuzalisha, kusafirisha na kusambaza umeme ikiwemo mradi wa kufua umeme wa maji wa Julius Nyerere; shilingi bilioni 589.4 kwa ajili ya miradi ya maji mijini na vijijini; shilingi bilioni 233.3 kwa ajili ya ununuzi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi; shilingi bilioni 500 ni kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu; shilingi bilioni 215.6 kwa ajili ya maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022; na shilingi bilioni 312.1 kwa ajili ya elimumsingi bila ada. Aidha, Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 400.0 kwa ajili ya kulipa madeni yaliyohakikiwa ya miradi ya maendeleo.

HITIMISHO

Mheshimiwa Spika, ninapoelekea mwisho wa hotuba hii, napenda kumshukuru kwa dhati “MAMA YETU” kwa kuniamini na kuniteua kuwa Waziri wa Fedha na Mipango. Ninamuahidi Mheshimiwa Rais, Waheshimiwa wabunge na Watanzania wote kwamba, nitaibeba dhamana hii kwa uadilifu, weledi na uwezo wangu wote na ninamuomba Mwenyezi Mungu anijalie afya njema, hekima na busara katika kutekeleza majukumu hayo. Naomba nielezee masuala machache muhimu kabla ya kuhitimisha hotuba hii.

Mheshimiwa Spika,
kwanza natoa pongezi kwa “MAMA YETU” kwa matumaini makubwa aliyowapa watanzania. “MAMA YETU” ameonesha ni Kiongozi Makini, ni Kiongozi Shupavu, ni Kiongozi Mchapa Kazi, ni Kiongozi Mwadilifu, ni Kiongozi Msikivu, ni Kiongozi aliye na dira thabiti na maono ya kuendelea kuiletea nchi yetu maendeleo makubwa. Ameweka wazi kuwa hataki kodi ya dhuluma, hataki kuendesha Serikali kwa mapato ya dhuluma, ameweka wazi kusimama imara kwenye masuala ya mapato na matumizi ya Serikali, ameweka wazi kuwa atakuwa imara kwenye vita dhidi ya rushwa.


Mheshimiwa Spika, kwa kauli hizo “MAMA YETU” ameonesha kuwa, kukaa kwake katika nafasi mbalimbali katika Serikali za awamu mbalimbali SMT na SMZ kumemfanya awe kiongozi aliyeandaliwa na KUIVA na aliye tayari kuiongoza nchi kwa ufanisi mkubwa. Itakumbukwa mbali na nafasi zingine nyingi alizoshika katika miaka yake takribani ishirini Serikalini, MAMA YETU amekuwa Waziri katika Awamu ya Nne na amekuwa Makamu wa Rais katika Awamu ya Tano. “Kuna style za uongozi amejifunza”.

Mheshimiwa Spika
“kuna style za uongozi amejifunza” kupitia Awamu hizo alikopewa nafasi kuhudumu katika nafasi mbalimbali. “MAMA YETU” alikuwa Waziri katika awamu ya nne iliyokuwa ikiongozwa na Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete. Mheshimiwa Kikwete alikuwa Mzalendo wa kweli, alikuwa na maono (Visionary Leader), alikuwa mwalimu, alikuwa mzazi, alikuwa mlezi na kiongozi, alikuwa rahim sana, alikuwa mvumilivu sana aliyeamini kwenye Mifumo, Taasisi na Utendaji wa Kitaasisi. Hii naweza kuifananisha kama “Refa kwenye mchezo” wa mpira wa miguu, ambaye anachezesha mechi zake akiwa na “kadi ya njano tu”, kadi nyekundu anaiacha nyumbani. Ukicheza rafu mara ya kwanza anakuonya kwa kukuelekeza, ukicheza rafu mara ya pili anakupa kadi ya njano, ukikosea anakupa kadi ya njano tena na alipotakiwa kutoa kadi nyekundu mara nyingi alionya kwa mdomo, kwa kuwa kadi nyekundu alikuwa anaiacha nyumbani. Rais Kikwete aliamini sana kwenye Mifumo na Utendaji wa Kitaasisi. Kwa mtazamo wangu, jinsi “MAMA YETU” alivyoanza ni dhahiri amepata funzo kwenye awamu hiyo ikiwemo funzo la Uzalendo, maono na kuamini kwenye Mifumo, Taasisi na Utendaji wa Kitaasisi”, na hapa naweza kusema ameichukua “kadi ya njano”, anayo na ameanza kutumia kama mnavyoona.

Mheshimiwa Spika, “MAMA YETU” alikuwa Makamu wa Rais katika awamu ya tano iliyokuwa ikiongozwa na Hayati Rais Dkt. John Pombe Magufuli. Rais Magufuli alikuwa mzalendo wa kweli, alikuwa na Maono (Visionary Leader), alijitoa kwa nguvu zote (Dedicated), alikuwa na uthubutu sana, mtu wa vitendo sana na muumini wa matokeo na kuchukua hatua za papo kwa papo. Kama refa wa mchezo wa mpira wa miguu, alikuwa akienda kuchezesha Mechi zake akiwa na “kadi nyekundu tu”, kadi ya njano alikuwa anaiacha nyumbani. Ukicheza rafu mara ya kwanza tu anakupa kadi nyekundu, wakati mwingine hata asipoiona rafu yeye, mchezaji au shabiki akisema ameona rafu anakupa kadi Nyekundu (no nonsense), hata mimi mwenyewe niliwahi kutembelewa na kadi nyekundu nikakosa michezo kadhaa. Hayati Dkt. Magufuli aliamini kwenye nidhamu ya hali ya juu ya mchezo. “MAMA YETU” alikuwa Line one na Mheshimiwa Majaliwa akiwa Line two. Hivyo, “MAMA YETU” amepata mafunzo kwenye awamu hiyo ya Uzalendo, Uthubutu, mtu wa vitendo kuamini kwenye matokeo na nidhamu kazini na ameichukua “kadi nyekundu”.

Mheshimiwa Spika “kuna style za uongozi amejifunza”.

“MAMA YETU” anazo kadi zote, “kadi ya njano” na “kadi nyekundu”. MAMA YETU” ni Mzalendo wa kweli, ni Mwadilifu sana, ana Uthubutu, ana Maono, anaamini kwenye Mifumo, Taasisi na Utendaji wa Kitaasisi”, hataki maneno anataka vitendo. Nitoe rai kwa watumishi wote wa umma na watanzania kwa ujumla tuchape kazi kwa bidii, kwa uadilifu na uzalendo mkubwa. Kwa watumishi wa umma tusimamie matumizi ya fedha za walipa kodi kwa uadilifu mkubwa na kwa watanzania tulipe kodi bila shuruti. Tabia moja ya refa asiyependa kuonea upande wowote, huwa hawezi kupendelea upande wowote. Kwenye michezo ya mieleka huwa mnapewa tahadhari ya don’t try this at home, kwenye maslahi ya nchi wanaotaka kumjaribu MAMA YETU nawaonya

Don’t try at all”. Tujiepushe na kadi Nyekundu.


Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais amenituma niwahakikishie watanzania kupitia hotuba hii kuwa, tunaendelea kuijenga nchi, tunaendelea kuijenga nchi, ije mvua, lije jua, tunaendelea kuijenga nchi, uwe usiku au mchana, tunaendelea kuijenga nchi. Hakuna mradi hata mmoja utakaokwama, wala hakuna Sekta ya maendeleo itakayozorota.

“KAZI INAENDELEA.”

Mheshimiwa Spika
, naomba kutoa hoja.

Kusoma Hotuba Neno kwa Neno. Fungua HAPA
 

Attachments

  • BAJETI_YA_SERIKALI_2021_22_09_JUNE_2021_REVISED_1_FINAL_FINAL_9.pdf
    1.4 MB · Views: 56
Tuone Bajeti ikigusa maisha ya watu moja kwa moja. Tumechoka kuona raia waliovaa nguo zlizochoka,zimechanika, wakishinda uwanja wa ndege, njaa zikiwapiga kuja kupokea ndege mpya. Huku wakienda kwenye maflyover kupiga mapicha ya kuwatumia ndugu zao vijijini.
 
Kima cha chini cha mshahara kimepanda ??? Retention fee 6% waondoe yote tusiione kabisa na tutaendelea kulipa 30,000 kama kawaida hadi tuzeeke.
 
Back
Top Bottom