Bajeti: Kambi ya Upinzani imewasilisha bungeni bajeti mbadala ya TSh29.9 trilioni

HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KATIKA WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO, MHESHIMIWA HALIMA JAMES MDEE (MB), AKIWASILISHA BUNGENI MAONI YA KAMBI RASMI YA UPINZANI KUHUSU HALI YA UCHUMI WA TAIFA, MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA SERIKALI KWA MWAKA WA FEDHA 2017/18
Inatolewa chini ya Kanuni ya 99(9) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016
_________________________
1. UTANGULIZI

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika Wizara ya Fedha na Mipango, Mheshimiwa Halima James Mdee (Mb), naomba kuwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu Hali ya Uchumi wa Taifa, Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/18.
Mheshimiwa Spika, kabla sijatoa maoni hayo, napenda kutumia fursa hii, kipekee kutoa pole nyingi kwa CHADEMA FAMILY, kwa kuondokewa na mmoja wa waasisi wa CHADEMA, Mzee Philemo Ndesamburo, aliyefariki dunia tarehe 31 Mei, 2017 huko Moshi, Kilimanjaro na hatimaye kupumzishwa katika nyumba yake ya milele tarehe 6 Juni, 2017. Marehemu Mzee Philemon Ndesamburo licha ya kuwa mwasisi wa CHADEMA, lakini pia alijitoa kwa hali na mali kukifadhili na kukilea Chama cha Demokrasia na Maendeleo na kukifikisha hapa kilipo leo. Mafanikio tuliyo na yo leo kama chama, na kama wabunge wa CHADEMA na viongozi wa chama kwa ngazi mbali mbali, na mafanikio tuliyo nayo leo, katika siasa za vyama vingi hapa nchini, kwa sehemu fulani yanatokana na juhudi za Mzee wetu huyu.

Mheshimiwa Spika, Taifa limempoteza mwanamageuzi wa karne, aliyekuwa tayari kupoteza maisha yake, kwa ajili ya mabadiliko ya kweli ya kisiasa, kiuchumi na kijamii katika Taifa letu. Kama chama, tutamkubuka kwa kuyaenzi yale yote aliyoyaasisi kwa mustakabali mwema wa chama chetu na Taifa kwa jumla. Hakika ni vigumu kuziba pengo aliloliacha. Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi, AMINA.

Mheshimiwa Spika, baada ya salama hizo za rambi rambi, naomba nitambue mchango uliotukuka wa Mhe. Halima James Mdee (Mb) ambaye ndiye Waziri Kivuli mwenye dhamana ya kuisimamia Serikali katika masuala ya Fedha na Mipango, kwa kufanya kazi usiku na mchana kufanya tafiti na uchambuzi wa nyaraka mbalimbali na kupata takwimu ambazo zimejenga msingi wa hotuba hii kwa zaidi ya asilimia 90.

Mheshimiwa Spika, tofauti na nchi zilizoendelea ambapo watu wenye upeo na weledi wa kufanya kazi namna hii huenziwa na kujengewa mazingira mazuri ya kuwa bora zaidi, katika nchi zinazoendelea watu wa aina hii hukumbana na madhila mengi ikiwa ni pamoja na kuwekwa kizuizini kwa sababu tu ya ujasiri wao wa kuisimamia na kuikosoa Serikali tena katika misingi ya kikatiba na kisheria.

Mheshimiwa Spika, wakati Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Mheshimiwa Freeman Mbowe (Mb) anahitimisha hotuba yake kuhusu Bajeti ya Serikali hapa Bungeni tarehe 6 Aprili, 2017 alisema kwamba: “… ili maendeleo ya kiuchumi yaweze kumfikia kila mwananchi ni lazima uchumi huo uwe shirikishi. Uchumi huo hauwezi kuwa shirikishi ikiwa tunabaguana kwa misingi ya tofauti za kisiasa au tofauti nyinginezo. Uchumi wa nchi yetu hauwezi kujengwa na kundi moja la jamii na kulibagua linguine. Hali kadhalika uchumi wa nchi yetu hautajengwa na chama kimoja cha siasa kwa kukibagua kingine au kuchochea migogoro ndani ya vyama vingine.

Mshikamano wa kitaifa ni muhimu sana katika kujenga uchumi ulio imara. Ndoto ya kufikia uchumi wa viwanda haiwezi kufikiwa tukiwa na msigano wa namna hii”. Aidha, aliongeza pia kwamba: “kutofautiana kifikra ni afya ya akili, na ili uvumbuzi utokee lazima kuwe na fikra mbadala – ‘alternative thinking’ Nilidhani kuwa Serikali na Chama cha Mapinduzi wangetambua kuwa uwepo wa watu wenye fikra mbadala katika taifa hili ni tuna na zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu; lakini badala yake Serikali wameona kuwa uwepo wa watu hao ni kama mwiba na kikwazo.”

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapenda kunukuu maneno ya Kitabu cha mwasisi wa Taifa la Afrika ya Kusini Hayati Nelson Mandela “No Easy Walk To Freedom” kama maneno ya faraja kwa Wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni waliopatwa na madhila mbalimbali kwa nyakati tofauti ikiwa ni pamoja na kufungiwa kuhudhuria vikao vya bunge au kuadhibiwa kwa namna nyingine yoyote ile, wakati wakitekeleza majukumu yao ya kibunge, kwamba wasifadhaike; kwa kuwa imewapasa kupitia njia hiyo, ili kufikia lengo lililo kubwa zaidi la kutwaa madaraka ya dola kwa njia ya kidemokrasia.

Mheshimiwa Spika, baada ya utangulizi huo, sasa naomba nitoe Bashraff ya Bajeti ya Serikali iliyowasilisha mbele ya Bunge lako kwa ajili ya kupata idhini ya Bunge.

Mheshimiwa Spika, kwa heshima kubwa, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapenda kuungana na waheshimiwa Wabunge ambao kwa umoja wao walisema kuwa bajeti hii haijawahi kutokea katika historia ya hivi karibuni ya bajeti za Serikali. Kambi Rasmi ya Upinzani inakiri kwamba ni kweli haijawaji kutokea bajeti ya namna hii na kwamba bajeti hii imevunja rekodi kwa sababu zifuatazo:-

1. Bajeti hii ni bajeti ambayo takwimu za vitabu vyake vya mapato na matumizi (Volume I, II, III &IV) zinatofautiana sana, na pia sura ya bajeti iliyosomwa na Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango inatofautiana pia na vitabu hivyo. Wakati kitabu cha Mapato ya Serikali kinaonyesha kuwa Serikali kwa mwaka wa fedha 2017/18 itakusanya jumla ya shilingi trilioni 23.9; kitabu cha Matumizi ya Serikali kinaonyesha kuwa Serikali inakusudia kutumia jumla ya shilingi trilioni 26.9 ikiwa ni ongezeko la matumizi ya shilingi trilioni 3 ambayo vyanzo vyake havijaonyeshwa kwenye kitabu cha mapato.

Wakati huo huo, sura ya bajeti iliyosomwa na Waziri wa Fedha na Mipango inaonyesha kuwa bajeti ya Serikali kwa maana ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2017/18 ni kiasi cha shilingi trilioni 31.7 – kiasi ambacho hakionekani popote katika vitabu vya mapato na matumizi ya Serikali. Hali kadhalika kwa mujibu wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Mikaka Mitano tarakimu hii ya shilingi trilioni 31.7 inaonekana kwamba ni makisio ya bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2018/19. Hivyo, sasa hivi tunatekeleza mapendekezo ya Mpango kwa mwaka wa fedha 2018/19 na sio 2017/18. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inakiri kabisa kwamba haijawahi kutokea!!!


2. Hii ni bajeti ambayo imedhamiria kuuwa kabisa dhana ya ugatuaji madaraka kwa Serikali za Mitaa (D by D) kwa kuziondolea Serikali za Mitaa madaraka yake ya kisheria ya kukusanya kodi ya Majengo, Kodi ya Mabango na Ushuru wa huduma mijini (City Service Levy) kwa malengo ya kujiendesha, na kurudisha madaraka hayo ya ukusanyaji kodi hizo Serikali Kuu kupitia TRA. Hii inadhihirisha kwamba yote yaliyofanywa na Serikali za CCM zilizopita na gharama zote zilizotumika kuimarisha madaraka kwenye Serikali za mitaa yailikuwa hayana maana yoyote. Kambi Rasmi ya Upinzani inakiri kwamba haijapata kutokea bajeti ya Serikali yenye lengo la kuuwa Serikali za Mitaa kwa kuzipunguzia madaraka na kuziondolea vyanzo vyake vya mapato.

3. Hii ni bajeti ambayo kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania inawalipisha watanzania maskini wasio na uwezo wa kumiliki magari kodi ya ada ya mwaka ya leseni za magari (Annual Motor Vehicle Licence Fee) kwa kuihamishia kodi hiyo kwenye ushuru wa bidhaa za mafuta ya petrol, dizeli na mafuta ya taa ambapo athari zake ni kupanda kwa gharama za maisha kwa wananchi masikini. Ieleweke kupanda kwa bei ya mafuta kutasababisha kupanda kwa nauli katika sekta ya usafirishaji jambo litakalosababisha kupanda kwa bei za vyakula, kupanda kwa bei za kusaga na kukoboa nafaka kwa kutumia mashine zinazotumia petrol au dizeli kwa wananchi waishio vijijini, kupanda bei kwa pembe jeo za kilimo, kushindwa kupata nishaati ya mwanga kwa wananchi waishi vijijini kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta ya taa nk. Kwa maneno mengine bajeti hii imelenga kuwabebesha wananchi masikini mzigo wa kodi kwa matumizi ya anasa ya watu wa tabaka la kati na juu wenye uwezo mkubwa kifedha wa kuweza kumiliki magari na vitu vingine vya thamani kubwa. Katika hili, Kambi Rasmi ya Upinzani inakiri kabisa kwamba haijawahi kutokea bajeti ya namna hiyo ya kuwanyonya masikini na kuwaneemesha matajiri. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani haijawahi kuona chombo chochote cha moto cha usafiri wa barabarani kinachotumia mafuta ya taa.

4. Hii ni bajeti ambayo kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania Serikali itatoza kodi ya shilingi elfu kumi (10,000/=) kwa nyumba zote katika halmashauri zote nchini ambazo hazijafanyiwa uthamini zikiwemo nyumba za tembe na tope kwa wananchi masikini waishio vijijini. (Hii iko katika ukurasa wa 48 kipengele cha iii cha hotuba ya Bajeti 2017/18) Badala ya Serikali kupunguza kodi kwenye vifaa vya ujenzi ili wananchi wa vijijini waweza kuwa na nyumba bora zenye staha, na badala ya Serikali kufanya uthamini wa ardhi na nyumba za wananchi masikini waishio vijijini ili waweze kupata hati miliki itakayoongeza thamani ya ardhi na nyumba zao ili waweze kutumia hati hizo kupata mikopo itakayoboresha maisha yao; bado Serikali imeendelea kuwabamiza kodi katika ufukara na uduni wao. Haya ni mastaajabu!!!, na hakika Kambi Rasmi ya Upinzani haijawahi kuona bajeti ya namna hii.

5. Hii ni bajeti ambayo imeendelea kupandisha kodi kwenye bidhaa ambazo uzalishaji wake hutumia malighafi inayozalishwa ndani ya nchi kama vile shayiri, zabibu, tumbaku n.k, jambo ambalo ni dhahiri litapunguza bei za mazao hayo, na hivyo kupunguza kipato cha wakulima wa mazao hayo. Kwa maneno mengine, bajeti hii haimjali mwananchi masikini ambaye ndiye mzalishaji wa malighafi hizo.

6. Hii ni bajeti ambayo imejinasibu kama bajeti ya uchumi wa viwanda wakati haijaonyesha popote mkakati wa kuongeza uzalishaji wa nishati ya umeme ambayo ndiyo msingi wa uzalishaji viwandani.

7. Hii ni bajeti ambayo haijataja popote itaongeza ajira kiasi gani kwa watanzania na wala haijasema itapunguza umasikni wa watanzania wa kiwango gani kwa mwaka wa fedha 2017/18. Aidha, ni bajeti ambayo haikuzungumzia popote utekelezaji wa ahadi ya Serikali ya kutoa shilingi milioni 50 kwa kila kijiji.

Mheshimiwa Spika, wahenga walisema,“ukistaajabu ya Musa, utaona ya Firauni. Maajabu ya bajeti hii ni mengi lakini itoshe kusema tu kwamba “ukiwa mwongo, basi uwe pia na kumbukumbu nzuri” Waheshimiwa wabunge na hata wananchi wanaweza kusahau mengine, lakini hili la ahadi ya shilingi milioni 50 kwa kila kijiji ni mapema mno kuweza kulisahau. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutolea maelezo ahadi hii ya shilingi milioni 50 kwa kila kijiji ili wananchi wajue kama wamekopwa fedha hii au wamedhulumiwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hayo machache, waliosema kwamba bajeti hii haijawahi kutokea walikuwa sahihi, na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inawaunga mkono.

Mheshimiwa Spika, tofauti na bajeti mbadala za Kambi Rasmi ya Upinzani zilizopita ambazo ziliweka msisitizo katika Ukuaji wa Uchumi Vijijini (Rural Growth) safari hii bajeti mbadala ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imebeba kauli mbiu ya Ukuaji Shirikishi wa Uchumi (Inclusive Economic Growth) ambapo watu wote wanatakiwa kushiriki katika kujenga uchumi katika mazingira yao na pia ukuaji wa uchumi unatakiwa uwaguse watu wote katika tabaka zote.

Mheshimiwa Spika, wakati Kiongozi wa Upinzani Bungeni akiwasilisha hotuba yake kuhusu bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu hapa Bungeni tarehe 6 Aprili, 2017, alisema kwamba: “tangu Serikali hii ya awamu ya tano iingie madarakani imekuwa ikijigamba kuwa uchumi wa nchi unakuwa kwa kasi ikilinganishwa na serikali za awamu zilizotangulia, lakini kumekuwa na kilio kikuu kwa upande wa wananchi kuhusu hali ya maisha kuendelea kuwa ngumu kuliko wakati wowote katika historia ya nchi yetu”. Aidha, alisema kwamba: “kilio hiki cha wananchi kinamaanisha kwamba ukuaji wa uchumi unaohubiriwa na Serikali haujawafikia wananchi ambao ndio wadau wakubwa wa nchi hii”.

Mheshimiwa Spika, Kiongozi wa Upinzani alinukuu maneno ya Wanazuoni wa uchumi wanaosema kwamba “Growth is inclusive when it takes place in the sectors in which the poor work (e.g. agriculture); occurs in places where the poor live (e.g. undeveloped areas with few resources); uses the factors of production that the poor possess (e.g. unskilled labour); and reduces the prices of consumption items that the poor consume (e.g. food, fuel and clothing).”

Mheshimiwa Spika, kwa tafsiri isiyo rasmi ni kwamba ukuaji wa uchumi unakuwa shirikishi unapotokea kwenye sekta ambazo watu maskini wanafanya kazi kama vile kilimo; unatokea katika maeneo ambayo watu masikini wanaishi kwa mfano maeneo ambayo hayajaendelea na yasiyo na rasilimali; unatumia nyenzo za uzalishaji ambazo watu masikini wanazo kwa mfano nguvukazi isiyo ya kitaalamu; na unapunguza bei za bidhaa ambazo watu masikini wanatumia kwa mfano chakula, mafuta na nguo.

Mheshimiwa Spika, kwa muktadha huo, ukipima hali ya Tanzania utaona kwamba uchumi wetu sio shirikishi kwa kuwa ukuaji wake hautokei katika sekta ambazo watu masikini wanafanya kazi au maeneo ambayo watu masikini wanaishi. Aidha, ukuaji wa uchumi wetu hautumii nyenzo za uzalishaji ambazo watu masikini wanazo na pia ukuaji huo haujapunguza bei za bidhaa ambazo watu masikini wanatumia. Kimsingi bajeti hii ambayo imeshabikiwa kwamba haijawahi kutokea, iko kinyume kabisa na mahitaji hayo ya ukuaji shirikishi wa uchumi.


2. MWENENDO WA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA SERIKALI KWA MIAKA MTATU ILIYOPITA 2014/15 – 2016/17

Mheshimiwa Spika, wahenga wetu walishasema kwamba “Sikio la kufa halisikii dawa” Nimeanza na methali hiyo, kwa kuwa, kwa miaka yote ya uhai wa Bunge la Kumi na mpaka bunge hili la kumi na moja, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imekuwa ikiishauri Serikali kubana matumizi kwa kupunguza bajeti ya matumizi kawaida yasiyo ya lazima na kuelekeza fedha hizo kwenye miradi ya maendeleo, lakini kinyume chake Serikali hii ya CCM imeendelea kuongeza bajeti matumizi ya kawaida hata kwa matumizi yasiyo ya lazima na kupunguza bajeti ya maendeleo.

Mheshimiwa Spika, ili kuthibitisha jambo hili, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imefanya tathmini ndogo ya utekelezaji wa bajeti ya Serikali kwa maana ya matumizi ya kawadia na matumizi ya maendeleo kwa miaka mitatu mfululizo iliyopita na kubaini kwamba utekelezaji wa bajeti ya Serikali umeweka matumizi ya kawaida kama kipaumbele kuliko bajeti ya maendeleo ambayo ndiyo dira ya ujenzi wa uchumi katika nchi yetu. Kwa mfano mwaka 2014/15 utekelezaji wa bajeti ya maendeleo ulikuwa ni asilimia 40, mwaka 2015/16 asilimia 31.24 na mwaka 2016/17 asilimia 35.26. Ukitafuta wastani wa utekelezaji wa bajeti ya maendeleo kwa kutumia takwimu hizi kwa miaka tajwa utakuta kwamba utekelezaji wa bajeti ya maendeleo kwa miaka hiyo haujawahi kuzidi asilimia 40.

Mheshimiwa Spika, wakati utekelezaji wa bajeti ya maendeleo uko chini ya wastani, utekelezaji wa bajeti ya matumizi ya kawaida yakiwemo matumizi yasiyo ya lazima umebaki kuwa juu. Kwa mfano kwa mwaka wa fedha 2014/15 matumizi ya kawaida yaikuwa ni asilimia 91, mwaka 2015/16 asilimia 81 na mwaka 2016/17 asilimia 68.7. Ukitafuta wastani kwa kutumia takwimu hizi kwa miaka tajwa utakuta bajeti ya matumizi ya kawaida imekuwa ikitekelezwa kwa kwa takriban asilimia 80.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inapenda kuweka rekodi sawa kwamba; utekelezaji wa asilimia 68.7 wa bajeti ya matumizi ya kawaida kwa mwaka wa fedha 2016/17, haumaanishi kwamba Serikali imebana matumizi bali imegoma kutoa fedha ambazo zilikuwa zimepangwa kutumiwa na kwa maana hiyo, fedha hizo zinabaki kuwa ni deni la Serikali. Kwa maneno mengine matumizi ya kawaida bado yako juu ukilinganisha na matumizi ya maendeleo.

Mheshimiwa Spika, mwenendo huu wa kutumia mapato yetu kwa matumizi ya kawaida kwa takriban asilimia 80 na kutoa fedha kiduchu kwa ajili ya miradi ya maendeleo ambazo nazo hazitolewi kwa wakati, kunaifanya nchi yetu kuwa na uchumi wa ‘mchumia tumbo’ – yaani hand to mouth economy.

3. TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MAENDELEO KWA MWAKA WA FEDHA 2016/17

Mheshimiwa Spika, tarehe 31 Mei, 2017 wakati nawasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu bajeti ya Wizara ya Fedha, nilieleza kwa kirefu jinsi ambavyo Serikali hii ya CCM imekuwa ikipuuza utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambayo ndiyo msingi wa uchumi wa wananchi kwa kutotoa fedha za utekelezaji wa miradi hiyo. Katika maelezo yangu nilitaja Wizara 10 za mfano kuonyesha tofauti ya fedha zilizoidhinishwa na Bunge na fedha halisi zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa bado Serikali haijatoa sababu za msingi za utekelezaji duni namna hii wa bajeti ya maendeleo, nitarudia sehemu hiyo, ili kwa mara nyingine kuipa Serikali nafasi ya kuwaeleza wananchi ina lengo gani hasa kwa kutotekeleza bajeti ya maendeleo kwa takriba asilimia 70.
Mheshimiwa Spika, Wizara nilizozitolea mfano kwa kutopatiwa fedha za maendeleo kwa ukamilifu wake katika mwaka wa fedha 2016/17 ilikuwa ni kama ifuatavyo:

i. Ofisi ya Makamu wa Rais ( Mazingira)
Mheshimiwa Spika, nilieleza kuwa, kati ya shilingi bilioni 10.9 za miradi ya Maendeleo zilizoidhinishwa na Bunge katika ofisi hii, ni shilingi bilioni 1.2 tu sawa na asilimia 11.3 ya fedha ya fedha hizo zilizotolewa na hazina kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo. Kwa maneno mengine bajeti ya Maendeleo ya Ofisi ya Makamu wa Rais – Mazingira haikutekelezwa kwa asilimia 88.7.

Mheshimiwa Spika, nilitoa angalizo kwamba, fedha hizi ndizo hutumika kupambana na uharibifu wa mazingira yetu ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi ambayo yamekuwa na athari kubwa sana kwa wananchi kama vile ukame, mafuriko, magonjwa ya mlipuko, njaa nk na kwamba kitendo cha Serikali kutotoa fedha hizo maana yake ni kubariki athari mbaya zinazotokana na uharibifu wa mazingira ziendelee kuwaangamiza wananchi.

ii. Tume ya Kudhibiti Ukimwi :

Mheshimiwa Spika, Kati ya shilingi bilioni 10.1 za miradi ya maendeleo zilizoidhinishwa na Bunge, ni shilingi bilioni 2.7 tu sawa na asilimia 27 ya bajeti ndio zimetolewa. Nilieleza kwamba tafsiri ya kutotekeleza bajeti hiyo kwa asilimaia 73, maana yake ni kwamba; vita dhidi ya maambukizi ya UKIMWI hapa nchini si kipaumbele tena cha Serikali hii ya awamu ya tano.
iii. Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi:

Mheshimiwa Spika, nilieleza pia kwamba, kati ya shilingi bilioni 897.6 zilizoidhinishwa na Bunge kwa ajili ya miradi ya maendeleo, ni shilingi bilioni 500.4 sawa na asilimia 55 ndizo ambazo zilikuwa zimetolewa hadi kufikia Machi, 2017. Hata hivyo, mchanganuo wa fedha hizo ni kwamba, shilingi bilioni 427 (asilimia 48) zilikuwa ni kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu na shilingi bilioni 470 (asilimia52) zilikuwa ni kwa ajili ya kugharamia miradi halisi ya maendeleo.

Mheshimiwa Spika, fedha za maendeleo katika sekta ya elimu zinaonekana kuwa nyingi kwa kuwa zimechanganywa pamoja na fedha za mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inashauri kwmba; ni muhimu tukatenganisha kati ya miradi ‘halisi ya maendeleo’ na ‘ Mikopo ya wanafunzi’ ili kuweza kupata picha halisi ya nini hasa kinakwenda kutumika kutatua changamoto za uboreshaji/ upanuzi/ujenzi wa miundombinu na shughuliza utafiti katika sekta hiyo.

Mheshimiwa Spika, tukija kwenye miradi halisi ya maendeleo, kati ya miradi 16 ambayo ilitengewa fedha katika mwaka wa fedha 2016/17 Kamati ya Bunge ya Maendelelo na Huduma za Jamii ilifanya ukaguzi wa miradi 5 tu sawa na na 12% ya miradi yote. Kati ya miradi hiyo mitano , ni miwili tu iliyopatiwa fedha! Tena kwa kiwango kidogo sana. Ifuatayo ni Hali halisi ya miradi mitano iliyokaguliwa :

 Mradi wa upanuzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) – Mradi namba 6361. Bunge liliidhinisha shilingi bilioni 4, hakuna fedha yoyote iliyopelekwa
 Mradi wa ukarabati wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam (Mradi namba 6350).

Bunge iliidhinisha shilingi bilioni 9.4, hakuna fedha yoote iliyopelekwa
 Mradi wa Hospitali ya Mloganzila (Namba ya Mradi 6364).Chuo kiliomba shilingi 14,549,727,933 (BN. 14.5) hakuna fedha iliyopelekwa mpaka 13/Mei /2017 wakati wa hotuba ya bajeti ya wizara ya elimu inasomwa.

 Mradi wa Mfuko wa Utafiti na Maendeleo wa COSTECH (Namba ya Mradi 6345. Katika Malengo ambayo nchi nchi imejiwekea , ni kutenga 1% ya Pato la Taifa. Hata hivyo, mfuko huu ulitengewa kiasi cha shilingi bilioni 12.8 tu sawa na 0.012% ya pato la Taifa . Pamoja na udogo huo , kiasi kilichotolewa ni shilingi bilioni 4.07 tu (sawa na 31.7%).

Kati ya hizo fedha Mfuko mkuu wa hazina uliotakiwa kutoa bilioni 8 ilitoa shilingi bilioni 1.5 tu na TCRA iliyotakiwa kutoa shilingi bilioni 4.8 ilitoa shilingi bilioni 2.57 tu.

 Mradi wa ujenzi wa DIT teaching Tower (Namba ya Mradi 4384). Mradi huu una umri wa miaka 11 (2006- 2017)…bado unasuasua, hakuna pesa na Matokeo yake gharama za mradi zimeongezeka toka bilioni 5 mpaka bilioni 9.

iv. Wizara ya Maji
 Tume ya Taifa ya umwagiliaji- Fungu 05:

Mheshimiwa Spika, katika sekta ya Maji, kati ya shilingi bilioni 35.3 za miradi ya maendeleo zilizodhinishwa na Bunge, ni shilingi bilioni 2.9 tu sawa na asilimia 8.4 zilizotolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo. Kwa upande wa usambazaji wa maji ,mijini na vijijini kati ya shilingi bilioni 915.1 zilizotengwa, zilizotolewa ni shilingi bilioni 181.2 sawa na 19.8% ya fedha zote za miradi ya Maendeleo ndizo zilizotolewa.

Mheshimiwa Spika, nilisema na narudia tena kusema kwamba; utekelezaji duni namna hii wa bajeti ya maendeleo katika sekta ya maji ni matusi kwa watanzania ambao uhaba wa maji umewafanya waishi kama wanyama; na kwamba; ule usemi wa Serikali wa kumtua mama ndoo ya maji, kwa mazingira haya ni dhihaka na ni ulaghai kwa akina mama wote wa nchi hii ambao wanaendelea kusota na kukumbana na kila aina ya kadhia katika kutafuta maji.

Aidha, niliitahadharisha Serikali Ikumbuke kwamba, hawa kina mama inaowafanyia mzaha kaatika suala la maji ndio mtaji mkubwa wa kura waliyoipa ushindi, na sasa imeshindwa kutumiza ahadi yake ya kuwatuma ndoo za maji kichwani, kwa kushindwa kutekeleza bajeti ya maendeleo iliyodhinishwa na Bunge.

v. Wizara ya Viwanda na Biashara:

Mheshimiwa Spika, Kati ya shilingi bilioni 42.1 zilizotengwa, wizara ilipokea shilingi bilioni 7.6 tu sawa na 18.6%. Nileeleza wazi na ninarudia tena kwamba; kwa utekelezaji huo wa bajeti, ni aibu kwa Serikali kutumia Kauli mbiu ya ‘Tanzania ya Viwanda’ kama kampeni ya kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia viwanda.

vi. Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa:

Mheshimiwa Spika, nilieleza pia kwamba, pamoja na unyeti wa Wizara hii, bado ilikumbwa na janga hili la kutopewa fedha za maendeleo. Moja ya mradi muhimu sana katika wizara hii ni mradi wa Defence Scheme ( mradi namba 6103) ambao unatekelezwa chini ya Kifungu namba 2002- Military Research and Development Fungu 57. Mradi huu, ulitengewa jumla ya shilingi bilioni 151.1. lakini Mpaka mwezi Machi,2017 wizara ilikuwa imepokea shilingi bilioni 30 tu sawa na 20% tu! Mbali na mradi tajwa hapo juu kwa mujibu wa Taarifa ya Kamati ya kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje Ulinzi na Usalama fedha za miradi ya maendeleo ziliwasilishwa ni 14.5% tu, yaani Bunge liliidhinisha shilingi bilioni 230, pesa zilizotolewa hadi Machi 2017 ni shilingi bilioni 33.9. Halafu tunaitangazia dunia kwamba tuna lengo la kuwa na jeshi dogo la kisasa lenye weledi, wakati Serikali haitoi fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo ambapo kupitia miradi
 
Hmm! Ngoja tuhamishe kwanza channel zetu kutoka kwenye ripoti ya makinikia ndio tutaweza kuelewa kilichomo kwenye hii bajeti mbadala...
 
Mmmh watu wako kwenye makinikia sijui Kama wataisoma.. summarize bana makene
 
Ngoja nipige kazi baadae jioni nitaipitia neno kwa neno, maana hii kazi ya kusifia sifia hata ujinga tumechoka
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom