BAE yakubali kufanya biashara na Tanzania; imekubali kuiuzia Tanzania kifaa kipya cha rada

nngu007

JF-Expert Member
Aug 2, 2010
15,862
5,797
[h=2][/h]ALHAMISI, AGOSTI 30, 2012 05:16 NA BENJAMIN MASESE, DAR ES SALAAM

KAMPUNI ya BAE System ya Uingereza, imekubali kuiuzia Tanzania kifaa kipya cha rada ya kuongozea ndege iliyoharibika hivi karibuni. Taarifa za kampuni hiyo kukubali kufanya biashara na Tanzania zimekuja baada ya kuwepo taarifa, kwamba kampuni hiyo haiko tayari kufanya biashara na Tanzania, ingawa ndiyo iliyoiuzia rada hiyo wakati wa awamu ya tatu ya utawala wa Rais Benjamin Mkapa.

Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Mhandisi Fadhili Manongi, alisema kuwa Agosti 20 mwaka huu, alipokea barua kutoka Kampuni ya BAE ikiwaahidi kuwauzia kifaa kiitwacho Power Supply Unit, kilichokuwa kimeharibika.

Alisema kifaa hicho ambacho ni kwa ajili ya rada hiyo ya kuongozea ndege katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere Dar es Salaam, kinanunuliwa kwa gharama ya pauni 9,000 za Uingereza.

Mhandisi Manongi alisema kutokana na barua hiyo kuwahakikishia kuuziwa kifaa hicho, tayari mipango ya manunuzi inaendelea ili kifaa hicho kiweze kununuliwa na kuletwa nchini haraka.

“Kifaa cha rada kilichokuwa kimeharibika pale uwanja wa ndege tulikipeleka Afrika Kusini ambapo Kampuni ya Tellumat imeweza kukitengeneza kwa gharama ya Dola za Marekani 2,516 na kimerejeshwa nchini na kufungwa.

“Hivi sasa hali ya uongozaji ndege imerejea kama ilivyokuwa awali na tunaendelea kusubiri taratibu za ununuzi wa kifaa kipya kutoka Kampuni ya BAE, napenda kuwahakikishia Watanzania wote, kwamba anga ya Tanzania ni shwari.

“Unajua watu wengi hawafahamu rada yetu inaongoza ndege hadi nje ya nchi, rada hii inaongoza ndege za Burundi na Rwanda ambapo sasa ufanisi katika kazi umeongezeka na hakuna athari zilizojitokeza wakati kifaa hicho kikiwa kibovu,” alisema.

Manongi alisema Tanzania na Uingereza zina uhusiano mzuri, licha ya kuwapo mvutano wa urudishaji wa chenji ya rada hiyo baada ya kubainika taratibu na sheria hazikufuatwa katika ununuzi, hali iliyosababisha Serikali ya Uingereza kuitaka Tanzania kuwafikisha waliohusika mahakamani.

Alisema kwamba, wakati kifaa hicho kilipokuwa kimeharibika, wafanyakazi wa TCAA walikuwa makini kuongoza na kuhakikisha abiria wanakuwa salama katika safari zao, ikiwa ni pamoja na kufanya uchunguzi wa ndege mara kwa mara.

Aliongeza kwamba kuharibika kwa kifaa hicho kumetoa somo kwa TCAA kujiandaa kuwa na akiba ya vifaa vya rada, ili kuwa na uhakika katika shughuli zao.

Wakati huo huo, alisema kutokana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia duniani, kuna haja kwa Serikali ya Tanzania kuwaongezea masilahi marubani ili kuendana na soko la ajira yao.

“Tatizo lipo, viwanda vimeongezeka, nchi zinakua, ndege zinaongezeka na marubani wamekuwa wakitafutwa kulingana na umuhimu wao.

“Kwa maana hiyo, ili kukabiliana na changamoto za ajira hiyo, tunapaswa kuwa na mshahara unaolingana na wengine, vinginevyo marubani watatukimbia ili wakaajiriwe kwingine.

“Hapa kwetu kuna marubani na wahandisi wapatao 500, wakati mahitaji halisi ni 800, hivyo kuna haja ya kuwaboreshea masilahi marubani wetu, kwani waliopo wengi ni wazee na hii ilisababishwa na Serikali kusitisha masomo yao katika miaka ya 80,” alisema.

Agosti 17, mwaka huu, Mhandisi Manongi alitoa taarifa kwenye vyombo vya habari, kwamba kifaa cha Power Supply Unit cha rada iliyoko JNIA, kimeharibika na kwamba wakati huo ndege zilikuwa zinaongozwa kwa simu na redio.

Rada hiyo ilinunuliwa kutoka Kampuni ya BAE kwa pauni za Uingereza milioni 29.5, sawa na Sh bilioni 70 za Tanzania. Hata hivyo ilibainika kwamba, mchakato uliotumika kuinunua haukuzingatia taratibu na sheria, kitendo kilichosababisha mvutano kati ya Serikali ya Tanzania na kampuni hiyo.

 
Serikali yetu ilivyo dhaifu bado itafanya tena biashara na hii kampuni.
 
Back
Top Bottom