Bado ninakukumbuka Sasha!

Tony Laurent

JF-Expert Member
Jan 5, 2011
4,726
5,442


Baada ya kupiga funda mbili za kinywaji kilichopo mbele yangu, nainua macho taratibu kuangalia uelekeo wa mlango wa kuingilia ndani ya eneo/ ukumbi nilimo. Ghafla namwona dada mmoja mrefu wastani, rangi yake maji ya kunde, akiwa amevalia gauni rangi ya samawati (blue) akiingia kwa madaha na kujiamini ndani ya ukumbi huu. Nywele zake zilikuwa ndefu kiasi, akiwa amezinyoa kwa mtindo wa panki kwa mbali...... mkononi alikuwa kashikilia mkoba mdogo rangi ya samawati, rangi sawa na gauni alilovaa. Miguuni kavalia viatu vya rangi ya samawati vikiwa na visigino virefu wastani.

Wakati akiwa anaendeea kutembea kuelekea eneo/ meza iliyokuwa wazi mara macho yetu yanakutana. Nilijikuta nimetabasamu, sijui hata hilo tabasamu lilitokaje tokaje, kwa kuwa sina kawaida ya kutabasamu mara kwa mara. Hufanya hivyo tu ninapokuwa kwenye sehemu ya kazi kwa ajili ya kuwavutia na kujenga mazingira rafiki kwa wageni/wateja.

Sipo peke yangu ninayemtupia huyu mrembo jicho ( langu lilikuwa la kuibia), bali karibia wanaume wote walimtupia jicho. Wengi wakimtazama kwa matamanio. Wengine walimsindikiza kwa macho hadi alipofika na kuketi sehemu aliyoona inamfaa.

Mimi nina utamaduni wa kila ninapoingia kwenye ukumbi au bar au mgahawa hupendelea kukaa sehemu ambayo inatazama mlango ili niwe kwenye nafasi nzuri ya kumwona kila anayeingia. Sababu ya kufanya hivyo- hiyo ni simulizi ya wakati mwingie.

Niliendelea kupata kinywaji changu taratibu, huku kichwani nikiwa na mawazo tele! Mawazo yaliyotokana na changamoto mabalimbali za kimaisha.

Zimepita takribani dakika 20, tangu mrembo huyu aingie hili eneo, nami nikiwa nizama kwenye lindi la mawazo, mara ghafla naona mtu ananishika bega na kunimbia, "Samahani kaka, mambo? naona kama una mawazo sana! Nashituka kidogo, na kuinua kichwa changu kumtazama huyu kiumbe anayenishika bega,.. kumbe ni yule mrembo akiwa amesimama pembeni yangu akinitazama kwa kwa huruma. "

Ooh! Karibu na samahani sikukuona wakati unafika hapa mezani kwangu" Ninajibu kinyonge kiasi.
" Usijali" Mrembo anajibu.. na anaendelea... " Nilifika nikakusalimia nikaona upo kimya na ukionekana umezama kwenye lindi la mawazo ,ndio nikakugusa bega"

"Daa! Samahani dada sikukusikia kabisa. Dunia hii ina mambo mengi sana. Ila usijali kuhusu mawazo yangu. Karibu uketi" Najikaza kujibu huku nikimsogezea kiti ali akae.
" Asante kaka" anajibu akiwa anaketi mbele yangu na usoni akiachia na tabasamu mwanana! Na anaendelea. Naitwa Sasha mimi ni mgeni hapa mjini. Kuna rafiki yangu alitakiwa kuja kunipokea, lakini amenipigia kuwa atachelewa kidogo hivyo amenielekeza nije hapa kwa muda atakuja kunipitia. Na humu ndani nimekuona wewe umekaa peke yako na muda mwingi umejiinaamia nikaona nije nijumuike na wewe kwa muda wakati namsubiria mwenyeji wangu"

" Mimi naitwa Tony. Karibu sana hapa Bongo" Najibu huku nikijitahidi kuonyesha utulivu wa hali ya juu.

Nanyoosha mkono wangu na yeye ananyoosha wake. Tunashikana kama ishara ya kusalimiana. Nautingisha mkono wake kidogo na kumkaribisha kwa mara nyingine tena na kwamba ajisikie huru...............


SIJUI NIANDIKE MWISHO AU NIANDIKE ITAENDELEA? 😊😊

Jamani nilikuwa najaribu kuandika hadithi........, sijui kama nimepatia kwa huo mwanzo tu? Naomba mwongozo kwa wabobezi wa eneo hili.

Nitarudi baadae kuja kusoma komenti zenu......
Asanteni
 
Back
Top Bottom