Babu Loliondo Kafichua Ubinafsi wa Wanasiasa na Viongozi Wetu

Mbunge

Senior Member
Aug 7, 2008
104
10
MARA kadhaa niliamini kuwa ninafanya makosa kuwafikiria watu wetu wana ubinafsi zaidi kuliko watu wengine.
Ninapoona mtu kwenye gari la kubeba watu wanane anapita peke yake na mke wake pengine na katoto kamoja; au nilipoona nyumbani kwa mwanasheria Manjonjo kuna magari 6 binafsi achilia mbali yale ya shirika au serikali; nilipoona ghorofa liko kando ya mbavu za mbwa ya babu aliyeuza kiwanja kilichojengwa ghorofa kule Lushoto; nilipoona wake wa viongozi wana nguo kiasi ambacho hawajui ziko ngapi achilia mbali peya za viatu; nilipoona wakwe na watoto wa wakubwa wanapelekwa nje kusoma na kwenda kununua nguo; nilipoona tajiri yangu anajenga mahekalu Dar, kwao na kwenye miji anayoipenda ndani na nje ya nchi; nilipoona wakubwa wakiugua wanakwenda kutibiwa nje na mwisho nilipoona matajiri na wakubwa wanazikwa kwenye makaburi ya kulipia na daima masafi na hakuna wauza bangi au wafanya ngono humo au wachawi wanaowanga usiku -kamwe sikuuelewa ubinafsi ni kitu gani !
Tukio lililonisaidia kugutuka na kutoka usingizini ni pale wakubwa walipokuwa wakiwanyang'anya wadogo nafasi ya kunywa kikombe cha dawa ya babu kule Samunge, Sale, Loliondo wilayani Ngorongoro.
Hawa watu kwa sababu ya vyeo na utajiri zao mimi niliamini sikuzote wana afya tena zaidi ya afya. Sasa walipotangulia kwanza wao wanywe kikombe huku wagonjwa hoi wakiachwa nyuma sikuamini macho yangu. Niliouona ubinafsi mkongwe, ulio na mgongo mchafu na unaoteleza kama wa mamba; nikaiona tamaa ya kuishi hata kama huwatendei watu mambo ya maana; nikaona uroho na uchu wa ukubwa unavyojiingiza na kumdhalilisha kikongwe wa watu akakosa sauti ya kuukemea; nikaona tadi na inda ya wale tunaowaita ndio majemadari wetu wa kututoa toka kwenye umaskini, ujinga na maradhi. Na jinsi walivyokuwa wanamnyenyekea babu ili wapate kwanza wao kikombe cha dawa nikatambua kumbe na wao si lolote na si chochote. Somo ambalo hawalijui, hawalishiki na wala hawatalishika. Wao na mahekalu yao wanakwenda kwenye kibanda cha udongo kilichoezekwa nusu kwa bati na nusu kwa majani!
Hawakujiuliza kwanini wengine wamekwenda wakarudi maiti; kwanini wengine wanaitumia nafasi hiyo kuwanyonya wengine; kwanini kijiji hicho na mtu huyo akachaguliwa kuwa hapo alipo; kwanini wageni wanakuja na watakuja; na nini wao kama viongozi wanaweza wakakifanya na pale Samunge na jirani zake fumba na kufumbua umaskini ukakimbia nakutoweka milele ?

Na kubwa zaidi hawakuweza kamwe kujiuliza MBONA SISI KAMA VIONGOZI TUMESHINDWA KABISA KUWAPA WANANCHI MATUMAINI ? LAKINI SISI NDIO TUMEKUWA WA KWANZA KUKIMBILIA MATUMAINI YA UHAI MPYA TOKA KWA BABU LOLIONDO?

Na somo Muumba alilotaka walifahamu na walielewe kwa salama na faida yao wenyewe, yaani, unyenyekevu na kutambua kwamba sisi hapa duniani ni wapita njia tu na faida kubwa kwetu ni kuwatendea wengine yale tunayoyataka na tunayoyapenda sisi wenyewe sina uhakika kama kuna aliyejifunza!
Wasalaam,
Mjukuu wa Babu
 
Back
Top Bottom