BAK
JF-Expert Member
- Feb 11, 2007
- 124,789
- 288,009
Date::3/17/2009
Baada ya tamko la polisi majambazi wapora Sh40m kweupe Dar
Festo Polea na Hidaya Kivatwa
Mwananchi
Baada ya tamko la polisi majambazi wapora Sh40m kweupe Dar
Festo Polea na Hidaya Kivatwa
Mwananchi
Siku moja baada ya Kamanda wa Polisi wa Kanda ya Dar es salaam, Suleiman Kova kutangaza kuunda kikosi cha kupambana na uhalifu wa aina zote, watu watatu, wakiwa na silaha, jana walipora zaidi ya Sh40 milioni kwenye duka maarufu la Kariakoo Barzaar na kutoweka nazo.
Kova alikuwa ametangaza kuunda kikosi maalum cha askari ambao wamepewa mafunzo maalum ya kupambana na uhalifu, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu Mizengo Pinda, aliyetaka wahalifu katika soko la Kariakoo, stendi ya Ubungo na sehemu nyingine washughulikiwe na jana majambazi hao walifanya uporaji huo kwenye maeneo hayo ya Kariakoo.
Majira ya saa 3:45, majambazi hayo manne yalimvamia mhasibu wa duka hilo la Kariakoo Barzaar Ltd, Kishori Sheti na kufanikiwa kupora fedha taslimu karibu Sh 40 milioni na kusababisha kizaazaa kwenye Mtaa wa Swahili na Narung'ombe, eneo lenye watu wengi.
Mara baada ya kupora, wamiliki wa duka hilo walijaribu kulifukuza gari lililowabeba majambazi hao wakati wakitimka, tukio lililoonekana kama maigizo.
Watu walioshuhudia tukio hilo walisema kuwa, majambazi hao waliokuwa wakitumia gari aina ya Toyota Corolla iliyokuwa na namba T429 AAT walimshambulia mhasibu huyo mara baada ya kushuka kwenye gari akitokea katika duka lao jingine lililo Mtaa wa Livingstone na Maina akiwa amebeba begi lililokuwa na fedha zilizoporwa.
Kwa mujibu wa mashuhuda, kabla mhasibu huyo mwenye asili ya Kiasia hajafika dukani, alivamiwa na watu watatu. Watu wawili kati yao, walijaribu kuvuta begi hilo, huku mwingine aliyesalia akimtishia kwa bastola.
Tukio hilo mfano wa sinema liliendelea kwa dakika kadhaa ndipo mlinzi wa mhasibu huyo aliyefahamika kwa jina la Joseph Hassan, aliyekuwa amebaki ndani ya gari ambalo 'bosi' wake alishuka, alitoka na kupiga risasi hewani.
Baada ya kusikia mlio wa risasi majambazi hao nao walijibu mashambulizi kwa kupiga risasi mbili hewani kwa lengo la kumtisha mlinzi huyo na kufanikiwa kupora begi hilo na kuingia kwenye gari lao na baadaye kutoweka, wakimuacha mlinzi huyo akipiga risasi kuelekea kwenye gari la majambazi hao na kupasua kioo cha nyuma cha gari hilo.
Hata hivyo, juhudi za mlinzi huyo kuokoa fedha hizo ziligonga mwamba na majambazi hao kufanikiwa kutoroka huku wakifyatua risasi hewani wakati wakifuatwa na wafanyabiashara hao waliokuwa na gari aina ya Toyota Double Cabin.
Mkurugenzi wa Kariakoo Barzaar, Nurdin Abdallah alisema gari hilo lilifanikiwa kutoroka, lakini wakiwa katika juhudi za kulisaka ghafla walisimamishwa na gari la polisi ambao walihofia kuwa ni majambazi.
Tulishangaa kusimamishwa ghafla na polisi wakitushuku sisi ndio majambazi na baada ya kutoa maelezo walituachia, lakini wakati huo wezi wale walishatuacha mbali hivyo hatukuweza kuwaona tena, alisema mkurugenzi huyo akionekana kushtushwa na tabia hiyo ya polisi kutojiunga nao kwenye msako.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, Faustine Shilogile alikiri kutokea kwa uporaji huo na kuongeza kuwa gari lililotumiwa na majambazi hao pamoja na watu wawili wanaoshukiwa kuwa walihusika kwenye uporaji huo, wameshakamatwa.
Ni mapema mno kutaja majina ya watuhumiwa hao kwa kuwa ndiyo kwanza tumeanza kuwahoji ili kufanikisha kuwapata watuhumiwa wengine waliohusika, alisema Kamanda Shilogile.
Kamanda Shilogile alisema inasadikiwa kuwa risasi iliyopasua kioo cha gari la majambazi hao, ilimjeruhi mtu mmoja aliyekuwa ndani.
Alisema licha ya kukamatwa kwa watu hao wawili wanaoendelea kuhojiwa na polisi, watu wengine watatu waliokuwepo katika duka hilo ambao wanahisiwa kuhusika katika kupanga tukio hilo la uporaji, wanashikiliwa na polisi.
Tunawashikilia pia watu watatu kutoka katika duka hilo ambao nao huenda wamehusika kwa namna moja au nyingine kufanya mipango iliyofanikisha uporaji huo, kwa kuwa hakuna mtu anayejua kuwa wakati huo jamaa hao walikuwa na fedha isipokuwa watu wa ndani humo. Hivyo nao tunawahoji, alisema Kamanda Shilogile.
Matukio ya ujambazi yalishamiri mwanzoni mwa mwaka 2006 kiasi cha serikali kuamua kuchukua hatua madhubuti za kuukomesha, ikiwa ni pamoja na kuwaweka chini ya ulinzi maalum baadhi ya watu waliohisiwa kuwa wanafadhili wahalifu hao.
Hatua hizo zilisaidia kupunguza kwa ujambazi, lakini kuanzia mwishoni mwa mwaka jana vitendo vya uhalifu huo vilianza kurejea na wakati fulani majambazi walidiriki kupora mchana kwenye masoko ya mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Katika hatua nyingine, Kamanda Shilogile aliwataka wafanyabiashara na wananchi kutumia jeshi la polisi wakati wanapotaka kusafirisha fedha zao na kuachana na kujiamini kupita kiasi.
Msijiamini... tumieni polisi wetu kwani tulishatoa wito huo wa kutumia polisi wetu katika harakati za kusafirisha fedha, lakini hadi leo watu wengine hawatumii. Wanajiamini wakati majambazi wana silaha za moto ambazo zinawafanikishia uhalifu kama huo wakati wowote, alisema.