BAADA YA Azimio la Zanzibar la mwaka 1992: CAMAETEC: Mkombozi wa mkulima kijijini, mjini

nngu007

JF-Expert Member
Aug 2, 2010
15,862
5,797
*Imevumbua trekta ndogo inayofanya kazi nyingi kwa wakati mmoja
Na Arodia Peter, Dar es Salaam


KUPITIA Azimio la Zanzibar la mwaka 1992 Tanzania ilibadili sera yake ya ujamaa na kujitegemea na kuingia sera mpya ya soko huria ili kuendana na matakwa ya kiuchumi ya sera za nchi za Magharibi.

Sera hii ndiyo chimbuko la kuuzwa kwa viwanda na mashirika ambayo yalianzishwa kwa nguvu kubwa na Rais wa awamu ya kwanza, Mwalimu Julius Nyerere.

Kilimo ambacho kinatajwa kuwa uti wa mgongo wa taifa kilitiliwa mkazo na Serikali ya Mwalimu Nyerere hadi kuanzisha Kiwanda cha Kutengeneza zana za Kilimo- Ubungo Farm Implements (UFI) kilichopo eneo la Ubungo Dar es Salaam .

Kiwanda hiki kilikuwa kinatengeneza zana zote za kilimo yakiwamo shoka, koleo, nyundo, matoroli jembe la mkono, jembe la kukokotwa na wanyamakazi. Kiwanda hiki kilitoa ajira kwa Watanzania wengi hivyo kuondoa umasikini wa kipato kwa wakati huo.

Ni bahati mbaya kwamba kiwanda hiki licha ya kubinafsishwa, hakikuzalishi tena zana hizi na haijulikani ni nini kinazalishwa katika kiwanda hicho. Zana za kilimo nyingi hivi sasa zinaagizwa kutoka nje ya nchi.

Hata hivyo zana hizo zinazoagizwa na wafanyabiashara hazikidhi mahitaji ya kilimo hasa maeneo ya vijijini. Serikali kwa kutambua tatizo hilo ilianzisha kituo cha CAMARTEC kilichoko jijini Arusha ili kiweze kuchochea utengenezaji wa zana za kilimo na teknolojia nyingine kwa ajili ya wakulima wa vijijini.

CAMARTEC ni Taasisi ya Utafiti na Uendelezaji wa Teknolojia zinazohitajika katika sekta ya kilimo na maendeleo vijijini. Kituo
hiki kipo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara na kilianzishwa mwaka 1982.

Katika ripoti iliyosomwa na Mkurugenzi Mkuu wa CAMARTEC, Evarist Ngw'andu, kwa Kamati ya Bunge ya Viwanda na Biashara hivi majuzi amesema majukumu ya kituo hicho ni kubuni, kuunda, kutengeneza na kueneza zana mbalimbali zikiwamo teknolojia za kilimo, ugavimaji, ujenzi wa nyumba zenye gharama nafuu.

Teknolojia nyingine ni zile za usindikaji mazao, uhifadhi nafaka, usafirishaji vijijini na nishati jadidifu. Utafiti na maendeleo ya teknolojia.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa hadi sasa CAMARTEC imeweza kuunda trekta dogo (Small mult-role tractor) linaloweza kufanya kazi mbalimbali kama vile kulima, kupalilia, kusafirisha mizigo, kuendesha mashine za kufua umeme, mashine za kusukuma pampu za maji, kusaga nafaka na kadhalika. Trekta hili lina uwezo wa kufanya kazi mwaka mzima bila kupumzika tofauti na zingine.

Kituo kimefanikiwa kuunda trekta hilo aina ya CAMARTEC Fastrucktor au CFT-221KK kupitia uzalishaji wa mlolongo kwa ushirikiano na mtaalamu kutoka RGS Development ya Uingereza ambaye anatoa ushauri wa kiufundi.

Hadi sasa trekta sita zimekamilika na nne kati ya hizo zimefanyiwa majaribio kwenye mikoa ya Pwani na Morogoro kwa lengo la kuthibitisha ufanisi wake kwenye hali halisi shambani na kupata maoni ya watumiaji.

Tayari zimeonesha ufanisi mzuri katika kazi zilizokusudiwa. Kituo kimeandaa mpango wa biashara wa kuzalisha trekta hizo na zana zake nchini katika siku za karibuni.

Ujenzi wa nyumba zenye gharama nafuu
Ngw'andu anaeleza kuwa kutokana na gharama kubwa ya malighafi za ujenzi kituo kimefanya utafiti wa ujenzi wa nyumba zenye gharama nafuu kwa kutumia teknolojia ya udongo-saruji ili watu wengi waweze kuitumia.

Anasema, kazi iliyofanyika ni kujumuisha dhana ya kufungamana (interlocking) kwenye muundo wa awali wa mashine ya kutengeneza matofali ya udongo–saruji (soil-cement blocks).

"Mashine hii ilifanyiwa usanifu na kutengenezwa. Hadi sasa tumeweza kukamilisha mashine zipatazo nane, lengo likiwa ni kupata matofali yanayoweza kutumika kujenga nyumba zenye gharama nafuu" anasema.

Pia imebuniwa mashine ya kutengeneza vigae vya saruji vyenye uwezo wa vigae 80 kwa siku na inafaaa katika kutoa ajira kwa vijana vijijini na mijini.

Usindikaji wa mazao
Mojawapo ya juhudi za kituo hiki kuchukua teknolojia kutoka nchi za nje na kuziboresha au kuunda upya kuendana na hali ya mahitaji ya humu nchini.

Mfano mzuri ni wa mashine ya kuchambua mbegu za nyanya iliyoundwa nchini Korea na kutumiwa na Kituo cha Kimataifa cha Uzalishaji Mbegu cha Tengeru (AVRDC).

Katika utafiti wake, CAMATERC iligundua kwamba mashine hiyo ingeweza kutengenezwa kirahisi nchini kwa kubadilisha na kuboresha baadhi ya sehemu zake.

Katika kazi hiyo, kituo kililenga kuboresha mfumo endeshi wa kutafiti matumizi ya malighafi mbadala kwa kupunguza ukubwa wa chekecheke za kukamulia na kutumia pampu ya nguvu ndogo zaidi bila kuathiri ufanisi wake.

Mashine ya kupukuchua mahindi
Katika kazi hii kituo kililenga kupata muundo wa mashine ya kupukuchua mahindi ulioboreshwa.

Mashine hii imeundwa kwa mfumo ambao itaweza kutembezwa na kupukuchua katika maeneo mbalimbali shambani na mkulima ataweza kupata mazao bora kutokana na upukuchuaji ulio bora hivyo kuongeza ajira kwa wakulima na wajasiliamali wengine.

Jiko la kupikia (biogesi)
CAMARTEC tayari imeweza kuunda jiko hilo kwa kutumia aina ya vyuma vinavyopatikana kwa urahisi katika maeneo mengi nchini. Tayari jiko limefanyiwa majaribio ya awali na matokeo yake ni mazuri zaidi kuliko ya jiko liloagizwa nje ya nchi.

Ili kuhawilisha teknolojia, kituo kimeendesha mafunzo yanayohusu uundwaji wa jiko hilo kwa wajasiliamali kadhaa na wale waliofuzu wameweza kuchukua nafasi ya kuzalisha majiko hayo kibiashara katika maeneo mbalimbali nchini.

Changamoto
Licha ya juhudi zinazofanywa, CAMARTEC inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo uwezeshwaji mdogo wa kifedha kutoka serikalini kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu yake ya msingi.

Upungufu wa vitendea kazi, wataalamu na mafunzo kwa wataalamu, uwezo mdogo kwa wananchi wa vijijini kununua na kuzitumia teknolojia zinazoendelea kuenezwa na CAMARTEC.

Kituo hicho kinakabiliwa na tatizo la kasi ndogo ya uhawilishaji wa teknolojia zilizothibitishwa kwa matumizi, kupanda kwa gharama za malighafi hasa vyuma, na uwezo mdogo wa sekta binafsi kuchukua teknolojia za CAMARTEC kuzizalisha kibiashara.

Kwa mfumo wa kodi wa sasa, CAMARTEC na watengenezaji wa zana za kilimo nchini wanalipa kodi kwa malighafi inayotengeneza zana zilizobuniwa na CAMARTEC hivyo gharama ya zana hizo kuwa kubwa kuliko zilizoingizwa kutoka nje.

Hili linatakiwa kufanyiwa kazi ili kuongeza idadi ya zana zilizotengenezwa nchini kutokana na bei kushuka.

 
Back
Top Bottom